Dominika ya XXII Mwaka C:“Ufanyapo chakula cha mchana au cha jioni usiwaite… wenye mali”
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya neno la Mungu kutoka hapa radio vatican leo Dominika ya 22 Mwaka C Katika kuelekea kilele cha Jubilei ya Matumaini, Kanisa linatualika kuishi kama watu wa tumaini – si tumaini lisilo na msingi, bali tumaini linalochipuka kutoka kwa maisha yenye mizizi ya kiroho, Unyenyekevu, Huduma kwa wasio na sauti, Maisha ya jumuiya yenye huruma na ukarimu. Mara nyingi utasikia watu kwenye maukio yao au sherehe zao wanapanga namna zitakavyokuwa au wangependa ziwe. “Tungependa ndoa yetu iwe ndogo tu, watu wachache wa karibu, jioni na kila kitu kiishie hapa nyumbani”, ilikuwa hamu ya Bwana na Bibi harusi watarajiwa, wee! wazazi na ndugu zao hawakuelewa kabisa jambo hilo, walijibu mengi na mojawapo lilikuwa “Sisi tumechangia harusi nyingi sana, lazima na sisi tuchangiwe msitutanie kabisa!.. halafu nyinyi pia ni wachangiaji wazuri kwa wenzenu, lazima na wao wawachangie hivi mtake msitake sherehe lazima iwe kubwa na reception kubwa ukumbin.” Papa Leo XIV, katika ujumbe wake kwa maandalizi ya Jubilei hii, amesisitiza: “Tumaini la Kikristo ni mti unaomea ardhini mwa unyenyekevu na kunyunyiziwa na maji ya huruma.”
Somo la I – Yoshua bin Sira 3:17–20, 28–29: Maisha ya kiroho yanaanza na moyo unyenyekevu. “Kadiri ulivyo mkuu, jinyenyekeze zaidi, nawe utapendelewa mbele za Bwana.” Maji ya hekima hayaingii kwenye udongo mgumu wa kiburi. Kujiona mdogo mbele ya Mungu huleta baraka; mnyenyekevu husikiliza, hufundishika, na hudumu kwa upendo. Huu ni ukweli kwa tulio wengi, kutenda matendo mazuri si kwa sababu tunafanya fadhili au kwa sababu tunampenda na kumjali tunayemualika, bali kwa sababu tunakopesha na tungependa kulipwa tuwapo na jambo letu… kwa sababu hiyo, shughuli zetu zimekuwa na ubaguzi na mialiko imezingatia sana vigezo duni vya kibinadamu… Kristo amewataja rafiki, ndugu, jamaa na jirani “wenye mali” ili na wao watualike siku moja… Tunatamani kujilinganisha nao katika siku zao bora tukijiweka katikati yao na kujipambanua kwenye madaraja yao ndio maana hata pakuketi ni lazima iwe “high table” waliko “wakubwa” hao, tuketi nao hotelini, tule nao mbuzi choma na kunywa nao wine…
Jambo hili limepelekea kujibembeleza, kusifu kwa daima hata kusikostahili,(kule Tanzania kuna msemo wanaitwa chawa) kuunga mkono lolote hata kama sio jema na ikibidi hata kuonea watu au kufanya lolote hata la aibu kiasi gani ili kubaki kwenye viti vya mbele… lakini hapo ‘high table’ ni pakuu mno na kwa hakika hapatustahili tulio wengi na hivi tunatumia nguvu nyingi mno kujihalalisha, Yesu amesema ni aibu kuambiwa ‘mpishe huyu’, tujizoeshe basi kuketi sehemu yetu na hiyo itutoshe. Lakini huku chini ndiko kwenye furaha, ndiko kwenye usingizi mzuri na nadra sana kuugua vidonda vya tumboni, shida za moyo na za msongo wa mawazo sababu hakuna mambo mengi… na hawa ambao tunadhani hawatufai na hivi hatuwakumbuki kwenye shughuli zetu ndio wenzetu hasa, ndio wanaoshika chepeo na jembe kuchimba makaburi yetu ili tupate maziko ya heshima… Kristo amewataja masikini, vilema, viwete na vipofu… najaribu kuwaona wapiga picha/shooting wa shughuli yenye watu hawa, hakika yake hawataipenda buruji iliyojinasihi masikini kama hawa, wanakamati pia, nao waalikwa wengine wataondoka wakisonya… Tunalosahau ni kuwa hawa wanawakilisha aina ya watu wanaopenda,
Somo la II Waebrania 12:18–24: Tofauti kati ya Mlima Sinai (hofu na giza) na Mlima Sayuni (furaha na huruma). Wakristo wamekaribishwa katika mji wa Mungu aliye hai – si kwa hofu, bali kwa tumaini na uaminifu. Tumaini letu liko katika neema ya Mungu, si vitisho. Tumeitwa kwenye karamu ya furaha ya mbinguni – kwa wanyenyekevu na wenye moyo wa ushirika.
Yesu anafundisha kwa mfano, “Usikae mahali pa mbele…” bali sehemu ya mwisho – na mwenyeji atakupandisha, Waalike maskini, viwete, vipofu – ambao hawana cha kukulipa. Huko ndiko “kulipwa kwako kutakuwa katika ufufuo wa wenye haki.” Ukarimu wa kweli ni ule usiotegemea faida, bali huruma. Heshima ya kweli hutoka kwa Mungu, si kwa wanadamu au watawa wa dunia. Katika jamii ya sasa, Heshima ya kijamii hutegemea cheo, mali, au followers wa mtandaoni. Ukubwa hupimwa kwa majukwaa, si moyo. Upendo unakuwa wa masharti: “Nitakusaidia kama utanisaidia.” kujali na kusamehe kwa dhati kwani hawana matarajio makubwa maishani mwao yenye kuwapa kiburi na dharau kwa yeyote, wanajua mahitaji ya kila mmoja wao, wanapeana moyo na faraja katika daraja lao na sala zao nyonge hufika na kusikika upesi zaidi mbele ya Kiti cha enzi… kwa macho yetu hawafai tena wamestahili viti vya nyuma katika sherehe lakini mbele ya Mungu ni matajiri wakubwa na furaha yao haikomi kifuani pa Ibrahim (Lk 16:19-31. Kumbuka Mwenyezi Mungu haumbi ‘vinyago’ bali anaumba watu wema na wazuri kabisa licha ya tofauti zao za rangi, lugha, tamaduni, nguvu, uwezo na udhaifu wao… wote ni Mungu!
Katika mwanga wa Jubilei ya Matumaini, ujumbe wa Dominika hii ni wito wa kutengeneza, karamu ya kiroho, fungua maisha yako kwa maskini wa kimwili na kiroho. Uongozi wa unyenyekevu: Hasa kwa vijana, toa huduma, si majigambo. Tumaini linalogusa maisha ya wengine: Fanya matendo yasiyoonekana na watu – lakini yanayogusa moyo wa Mungu. Tafuta kufanya wema bila kutarajia malipo. Omba neema ya kuacha sifa ya dunia ili uvae taji la mbinguni. Tuombe neema ya kuliishi vema Neno la Mungu ambalo leo limefunganishwa katika fadhila ya unyenyekevu na kujishusha… Yoshua bin Sira katika hekima yake (3:17-20, 28-29) anatuasa kuwa hata tukipata mafanikio kiasi gani tuendelee katika unyenyekevu, tusimdharau au kumshusha yeyote, tusitamani heshima kupita ile ya utu tulioumbwa nao… unyenyekevu ni dada ya ukweli, nao ni adui wa kiburi aliye kaka wa uongo… Waalikeni hata watu wasio wa familia kwenye sherehe zenu – hasa waliosahaulika. Jifunzeni kuishi kwa unyenyekevu wa Kristo, si mashindano yasiyo na heshima. Jenga mtandao wa upendo, si wa sifa binafsi. Tumia teknolojia kueneza ujumbe wa huruma, si majigambo au ubaguzi.
Mtakatifu Augustino ambaye leo ni Kumbukumbu yake anasema ‘unyenyekevu ndio fadhila muhimu kuliko zote, ya pili pia ni unyenyekevu na hata ya tatu inabaki kuwa ni unyenyekevu’… wengi tunaeleza unyenyekevu kama ni 'mmoja kuchukua nafasi anayostahili' lakini Kristo leo amesema unyenyekevu ni 'kuchukua nafasi ya chini' Yeye mwenyewe akiwa mfano (Filp 2:5-11)… Unyenyekevu ni vita dhidi ya “kujiona” (egoism) yaani kuwa na kichwa kikubwaaa na kineneee kwenye mwili mkondefuuu na mdhaifuuu... kirusi cha “kujiona” ni kibaya na cha hatari kuliko virusi wote unaowafahamu… katika unyenyekevu tunajipatia kibali machoni pa BWANA na hivi kustahilishwa, linavyosema somo II (Ebr 12:18-19, 22-24), kuufikilia mlima Sayuni na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni na kuwa miongoni mwa mkutano ule mkuu na Kanisa la wazaliwa wa kwanza. Yesu anatufundisha: “Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, na ajidhiliye atakwezwa.” (Lk 14:11) Katika muktadha wa Jubilei ya Matumaini, Dominika hii ni kioo cha matumaini ya kweli Tumaini linaanza pale tunapojinyenyekeza na kumjali mwingine asiye na sauti. Ndipo Mungu hutuinua kwa heshima ya milele.