Dominika ya 22 Mwaka C:Jivikeni unyenyekevu&acheni kiburi na majivuno
Na Padre Paschal Ighondo –Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 22 ya mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe wa masomo ya Dominika hii umejikita katika fadhila ya unyenyekevu ambayo kwayo mtu hujitambua kuwa hajitoshelezi, na hivyo kutambua thamani na uhitaji wa binadamu mwenzake na Mungu aliye ukamilifu wote kwa maisha yake. Kwa njia hiyo tunaaswa kuachana na kiburi na majivuno, na kujivika unyenyekevu, ili kutambua uwepo wa Mungu na nguvu zake na kumtumaini Yeye, Naye kila tumwitapo ataitika na kutuokoa na taabu zetu zote. Ni katika muktadha huu wimbo wa mwanzo unasema hivi; “Ee Bwana, unifadhili, maana nakulilia wewe mchana kutwa. Kwa maana wewe, Bwana, u mwema, umekuwa tayari kusamehe, na mwingi wa fadhili kwa watu wote wakuitao” (Zab. 86: 3, 5). Na mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali; “Ee Mungu uliye na uwezo na nguvu, uliye na kila kitu kilicho chema, ututilie mioyoni mwetu upendo wa jina lako. Uyakuze ndani yetu yale yaliyo mema kwa kutuongezea uchaji; uyalinde kwa tunza yako yale uliyoyakuza”.
Somo la kwanza ni la kitabu cha Yoshua bini Sira (YbS 3:17-20, 28-29). Katika somo hili tunaaswa kuwa tukifanikiwa katika maisha tusijae kiburi, bali tujivike unyenyekevu. Tukifanya hivyo tutapendwa na watu na kupata kibali machoni pa Bwana na kujuzwa siri zake. Kwa maana fadhila ya unyenyekevu inatusaidia kujua kuwa yote tuliyonayo yanatoka kwa Mungu na ndiye ukamilifu wote. Basi tujiepushe na kiburi kwa maana kinaleta maanguko na kuangamia kwa mtu. Yoshua bini Sira anasema kuwa mateso ya mwenye kiburi hayana matibabu na msiba wake hauleti kupona. Lakini moyo wa busara utatambua mithali na sikio sikivu, ni tamaa ya mtaalamu (YbS 3:28-29). Basi tujivike unyenyekevu, tumtumainie Mungu aliye ngao na nguvu yetu, naye atatuokoa na kila ovu, na kutustahilisha kuingia katika uzima wa milele mbinguni. Ni katika muktadha huu wimbo wa katikati unasema hivi; “Wenye haki watafurahi na kuushangilia uso wa Mungu; Naam, watapiga kelele kwa furaha. Mwimbieni Mungu, lisifuni jina lake, furahini katika Bwana, shangilieni mbele zake. Yeye ni Baba wa yatima na mwamuzi wa wajane. Mungu katika kao lake takatifu, huwakalisha wapweke nyumbani, huwatoa wafungwa wakae hali ya kufanikiwa. Ee Mungu, ulinyesha mvua ya neema, urithi wako ulipochoka uliutia nguvu. Ee Mungu, kwa wema wako uliwahifadhi walioonewa” (Zab. 68: 3-6, 9-10).
Somo la pili ni la waraka kwa Waebrania (Ebr 12:18-19, 22-24). Sehemu hii ya somo hili ni wosia kwa Wayahudi walioongokea Ukristo, lakini kwa sababu ya mateso na madhulumu walianza kuwa na wasi wasi na imani yao ya kikristo, hata wengine walianza kukata tamaa na kutamani kuruidia imani yao ya zamani. Hivyo wanaaswa wajipe moyo, wabaki imara katika imani yao, wasonge mbele mpaka wauifikie “mlima Sayuni, mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu ya mbinguni”, iliko furaha ya kweli isiyo na ukomo, aliko Kristo Yesu Mkombozi wetu, aliyetufunulia uwepo wa Mungu katikati yetu. Kristo Yesu kwa unyenyekevu na utii hata mauti ya msalaba, amekuwa ukamilifu wa Agano alilofanya Mungu na Babu zao na kuwapa Amri zake. Na kila anayebatizwa na kumfuata, anashirikishwa maisha ya Kimungu na heri ya Watakatifu kwa Agano hilo. Nasi tusirudi kamwe nyuma na kuiacha imani yetu kwa sababu yoyote ile, hata ikiwa ni kuteseka na kudhulumiwa kwa ajili yake, kwani ndiyo ufunuo kamili wa Mungu kwetu kwa njia ya Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu, aliye njia ya kwenda mbinguni na mlango wa kuingia katika uzima wa milele.
Injili ni ilivyoandikwa na Luka (Lk 14:1, 7-14). Ujumbe mahususi ni huu; tukitaka kuufaidi ufalme wa Mungu, lazima tuwe watii na kujivika fadhila ya unyenyekevu, na kumtegemea Mungu; “Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa”. Katika utii na unyenyekevu tuwasaidie wahitaji – maskini, vilema, viwete na vipofu – kwa upendo, na kwa kuwa wao hawana uwezo wa kutulipa, tunakuwa na heri na baraka katika ufufuo wa wenye haki, kustahilishwa kuingia katika ufalme wa mbinguni. Zaidi sana fadhila ya unyenyekevu, inatusaidia kutambua hali yetu ya dhambi, umaskini wetu wa kiroho, uhitaji wetu wa wengine, unyonge wetu, madhaifu na mapungufu yetu, na kwamba hatuustahili Ufalme wa Mungu. Lakini Mungu kwa upendo na huruma yake kwa kuangalia unyenyekevu wetu anatustahilisha kuupokea uzima wa milele (rej. KKK 2546, 2559, 2631, 2713). Lakini tunaposema fadhila ya unyeyekevu maana yake ni nini hasa? Kwanza kabisa fadhila ni mazoea na mwelekeo thabiti wa kufanya mema. Mtakatifu Thomaso wa Akwino anasema; “Fadhila ni tabia ya kudumu ya akili, dhamira au vionjo, ambayo kwayo mtu aweza kutenda analotakiwa kimaadili katika nafasi fulani, au kutenda kwa njia sahihi, yaani akiwa na msukuma wa kufaa”. Hivyo fadhila hutusaidia kutenda mema kwa wepesi, kwa urahisi, kwa kudumu na kwa furaha. Kuwa mwenye fadhila humaanisha kujisahau mwenyewe kwa ajili ya upendo wa Mungu unaojimimina kwetu. Ni kuiga upendo wa Kristo, kujikana nafsi na kuwa mwanga wa upendo kwa Mungu na jirani (rej KKK 1803-1811).
Ili kudumu kuwa mkristu mwema, lazima kuamua kwa makusudi kujijengea mazoea mema yanayoendana na imani ili kujijengea tabia njema, mwenendo safi na adilifu. Mtume Paulo anasema; “Ndugu zangu jazeni fikira zenu kwa mambo mema na yanayostahili kusifiwa, mambo ya kweli, bora, haki, safi, ya kupendeza na ya heshima” (Fil. 4:8). Mazoea yanayoendana na Injili huitwa fadhila. Hivyo unyenyekevu unajengwa kwa matendo mema madogo madogo ya kila siku. Unyenyekevu unampa mtu uwezo na utayari wa kujitafakari kila mara ili kujua vipawa vyake na kuvitumia vyema, kujua na kufahamu udhaifu wake, kukubali kukosolewa na kujirekebisha anapokuwa amekosea. Ni katika muktadha huu unyenyekevu unakuwa ni mama ya fadhila zingine, na humfanya mtu kuwaheshimu wengine na kumtegemea Mungu, na hivyo kupata kibali cha kukwezwa; “kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa” (Lk 14:11).
Kinyume cha unyenyekevu ni kiburi kinachomfanya mtu kupenda makuu, ufahari, kujikweza, kujiona bora kuliko wengine, kutokuwa tayari kuwa chini ya mamlaka yoyote ile, daima anajiona mkamilifu na kila analofanya ni kwa nguvu na uweza wake, hivyo anajisifu yeye mwenyewe daima (rej. (Rm 1:29-32; Yak 4:6; Lk 18:11-12). Ni katika mazingira haya kiburi kinakuwa mzizi mkuu wa dhambi, kwani mwenye kiburi ukaidi haumuachi, hawathamini wengine, hujiona anajua yote, yeye ndiye kipimo cha ukweli, hivyo hawezi kutii sheria yoyote. Jamii yenye kiburi, inajiona kuwa inajitosheleza katika yote, inamwondoa Mungu kama chanzo cha ukweli wote, na hivyo inajifanya yenyewe mizani ya maadili. Jamii yenye kiburi haitambui kuwa furaha ya kweli ni kumwona Mungu, watu wake daima wanaitafuta furaha ndani mwao, kwa ajili ya hiyo hawawezi kutenda mema kwa sababu imeondoa chanzo cha mema. Jamii ya namna hii haiwezi kuwa na furaha, watu wake daima wanaishi katika kilindi cha huzuni (rej. KKK 1866, 2094, 2317,2540, 2728).
Basi tumwombe Mungu atujalie fadhila ya unyenyekevu ili kwayo tuweze kutambua ukuu wake na kumtegemea yeye, ili atuinue wakati ufaao na zaidi kutuingiza katika maisha ya umilele mbinguni. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, sadaka tutoayo ituletee daima baraka yako, ili jambo linalotendwa kwa fumbo, likamilishwe ndani yetu kwa nguvu ya sadaka hii”. Na katika sala baada ya komunyo mama Kanisa anapohitimisha maadhimisho ya dominika hii anasali; “Ee Bwana, sisi tuliolishwa Mkate Mtakatifu tunakuomba sana, ili Chakula hicho cha mapendo kitutie nguvu moyoni, hata tuvutwe kuwatumikia jirani zetu kwa ajili yako”. Tukifanya hivyo nafsi zetu zitatulia kama anavyoshuhudia Mtakatifu Agostino baada ya kuikosa furaha ya kweli katika viumbe na kumwongokea Mungu akisema; “Ee Mungu umetuumba kwa ajili yako na roho zetu hazitatulia kamwe mpaka pale zitakapotulia ndani mwako.” Na hili ndilo tumaini letu.