杏MAP导航

Tafuta

Thamani ya Sakramenti ya Ubatizo. Thamani ya Sakramenti ya Ubatizo.  (? Antonio Gravante - www.studio-fotograv.com)

Dominika ya 21 Mwaka C:Ubatizo na Ufalme wa Mbinguni!

Ubatizo unatufanya wakristo na washirika wa taifa la Mungu.Lakini ili tuweze kustahilishwa kuuridhi uzima wa milele,tunapaswa kuuishi ukristo wetu vizuri kwa kuzishika na kuziishi amri za Mungu,kuishuhudia imani yetu kwa maneno na matendo, tukimtumainia na kumtegemea Mungu katika yote.

Na Padre Paschal Ighondo –Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 21 ya mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya Dominika hii yanatukumbusha ukuu na thamani ya sakramenti ya ubatizo, msingi wa maisha yote ya kikristo, lango la kuingilia uzima katika Roho, na mlango wa sakramenti zote (KKK1213). Ni sakramenti ya kwanza kati ya sakramenti tatu za kutuingiza katika ukristo – ubatizo, Kipaimara na Ekaristi Takatifu (KKK 1212). Ubatizo unatufanya wakristo na washirika wa taifa la Mungu. Lakini ili tuweze kustahilishwa kuuridhi uzima wa milele, tunapaswa kuuishi ukristo wetu vizuri kwa kuzishika na kuziishi amri za Mungu, kuishuhudia imani yetu kwa maneno na matendo, tukimtumainia na kumtegemea Mungu katika yote. Ni katika tumaini hili wimbo wa mwanzo unasema hivi; “Ee Bwana, utege sikio lako unijibu. Wewe uliye Mungu wangu, umwokoe mtumishi wako anayekutumaini. Wewe, Bwana, unifadhili, maana nakulilia wewe mchana kutwa” (Zab. 86:1-2). Na mama kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu, wewe waiunganisha mioyo ya waamini katika nia moja. Uwawezeshe watu wako wapende hayo unayoamuru, na kutamani hayo unayoahidi, ili katika ulimwengu huu geugeu, mioyo yetu iwe huko kunako furaha za kweli”.

Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Isaya (Isa 66:18-21). Somo hili linabeba ujumbe wa matumaini na faraja kwa mataifa yote. Mungu anaahidi kuwakusanya watu wa mataifa yote na lugha zote, waliowahi kuisikia sauti yake na ambao hawajawahi kuisikia wala kuona utukufu wake kwa kuwa Yeye ni Mungu wa watu wote na anaahidi kuchagua makuhani hata kutoka kwa mataifa ya kipagani. Hivyo Israeli anatakiwa kutambua kuwa kule kuwa taifa teule sio kwa sababu ya ubora wake bali ni upendeleo kutoka kwa Mungu kwa maandalizi ya kumpokea Mwokozi Yesu Kristo, ambaye ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma duniani akazaliwa na Bikira Maria chini ya sheria, kusudi awakomboe wote waliokuwa chini ya sheria, na kuwapa hali ya kuwa wana wa Mungu kwa neema zake. “Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo” (Yn 1:17 ). Kristo Yesu ndiye njia, ukweli na uzima (Yn 14:6). Nasi tukiishi kadiri ya mafundisho yake tutastahilishwa kuushiriki uzima wa milele. Ni katika muktadha huu wimbo wa katikati unasema; “Enendeni ulimwenguni mwote, Mkaihubiri Injili. Aleluya. Enyi mataifa yote, msifuni Bwana, Enyi watu wote, mhimidini, maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu, na uaminifu wa Bwana ni wa milele” (Mk. 16:15; Zab. 116).

Somo la pili ni la waraka kwa Waebrania (Ebr 12:5-7, 11-13). Ujumbe mahususi wa somo hili umejikita katika umuhimu na dhamani ya fadhila ya uvumilivu katika kupambana na nyakati ngumu na magumu yake katika maisha, ikiwa ni pamoja na kuishuhudia imani yetu ya kikristo kwa maneno na matendo. Fadhila hii inatuimarisha katika nyakati za mateso na madhulumu, tusikate tamaa bali tupige moyo konde tusonge mbele, huku tukimtumainia Mungu, ambaye wakati mwingine anayaruhusu magumu na majaribu yatupate ili tuweze kukua na kukomaa katika imani na fadhila zingine. Ni katika muktadha huu tunaaswa kwa kauli hii; “Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, wala usizimie moyo ukikemewa naye; maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi. Naye humpiga kila mwana amkubaliye. Kila adhabu wakati wake huonekana kuwa si kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani”. Hata Kristo Yesu amekuwa sababu ya wokovu wetu kwa kupitia majaribu magumu na mateso mengi. “Ingawa alikuwa Mwana, alijifunza utii kutokana na mateso aliyoyapata, akiisha kukamilishwa, akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wote wanaomtii” (Ebr. 5:8-9). Basi nasi tujifunze kuvumilia mateso na mahangaiko ya kimaisha katika kuishuhudia imani yetu, ili tupate kibali machoni pa Mungu na kushirikishwa uzima wa milele.

Injili ni ilivyoandikwa na Luka (Lk 13:22-30). Ujumbe mahususi ni kuwa si juu yetu kujua wangapi wataokoka, wajibu wetu ni kufanya juhudi ili tuokoke. Sisi tuliohubiriwa Injili baada ya Wayahudi kuikataa, tusipookoka ni kosa letu kwa kutojitayarisha vema hapa duniani kupata ukamilifu wa wokovu mbinguni. Kumbe kusikiliza mahubiri na mafundisho ya Kanisa, kushiriki sadaka ya Misa Takatifu na kupokea Ekaristi Takatifu, hakutoshi kwa ajili ya kuurithi ufalme wa mbinguni. Watakaoingia mbinguni ni wale walioishi amri ya mapendo, waliofanya yale aliyoyaamuru Yesu Kristo. Nasi tujitahidi kufanya hivyo ili tupate kustahilishwa kuingia katika uzima wa milele. Tunakumbushwa kuwa kule kubatizwa na kuwa wana wa Mungu, wateule wake, sio tiketi ya kuingia mbingu bali kule kujibidisha kuishi kadiri ya maagizo yake. Kristo Yesu anasisitiza kuwa; “watakuja watu toka mashariki na magharibi, na toka kaskazini na kusini, nao wataketi chakulani katika ufalme wa Mungu”. Huu ni mwangwi wa utabiri wa Nabii Isaya na ahadi ya Mungu katika somo la kwanza aliposema; “wakati unakuja nitakapokusanya mataifa yote na lugha zote; nao watakuja, nao watauona utukufu wangu, nitawatuma hao waliookoka kwa mataifa, wauhubiri utukufu wangu”.

Tumeumbwa kwa mfano na sura ya Mungu
Tumeumbwa kwa mfano na sura ya Mungu

Utabiri huu unaweka wazi kuwa sote tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, sote tunaitwa kuwa watakatifu, sote tunaitwa kushiriki furaha ya uzima wa milele, kwa sharti la kuzishika na kuziishi amri za Mungu. Bila kuishi maisha ya kumtukuza na kumsifu Mungu, bila kuwa na muunganiko na Mungu wetu aliyemtakatifu, hatuwezi kuuona utukufu wake katika maisha yajayo. Na huku ndiko kuingia katika mlango ulio mwembamba, kuishi kadiri ya amri za Mungu. Kumbe katika kuuridhi ufalme wa mbinguni haitoshi kuwa mingoni mwa Taifa teule la Israeli, wala kule kubatizwa na kuitwa mkristo haitoshi kuuridhi ufalme wa mbinguni. Bali yatupasa kuiishi Imani yetu, kuwa kweli mashahidi wa Kristo kwa watu wote. Ushuhuda wa kiimani sio jambo rahisi, yahitaji kujitoa sadaka, kuvumilia mateso na mahangaiko yake. Ndiyo maana Yesu anasema; “Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze”. Kuna uwezekano kuwa tumebatizwa, na tunaitwa wakristo, lakini kama hatuuishi ukristo wetu, tusije kushangaa siku ya mwisho wa maisha yetu Bwana atakapomtuma mjumbe wake kutuita, kila mmoja kwa mda na nafasi yake yakasikika maneno haya; “siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu. Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno”.

Ni wazi ubatizo ni mlango wa sakramenti zingine zote, ubatizo ni sakramenti inayotuingiza katika ukristo, ni sakramenti inayotuondolea dhambi ya asili na adhabu zake zote. Ni kwa njia ya ubatizo tunazaliwa upya, tunakuwa watoto wa Mungu na wa Kanisa. Ubatizo unatupa uwezo wa kufa kwetu kuhusu dhambi na kuzaliwa tena katika maisha mapya. Kwa ubatizo tunashirikishwa Fumbo la Pasaka, fumbo la ukombozi wetu. Ubatizo hutuwezesha kuingia kwa namna ya pekee katika ushirika wa Utatu Mtakatifu, kwani hutufanya kuwa watoto wa Baba, warithi pamoja na Kristo, na kuwa hekalu la Roho mtakatifu (KKK 1263). Ubatizo unatushirikisha ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo. Hii ndiyo maana ya “alama ya kiroho isiyofutika” tunayopata katika sakramenti hii. Lakini licha ya haya yote, bado tuna wajibu wa kuishi kweli kama Watoto wa Mungu, tuna wajibu wa kuishi kama watoto wa Kanisa. Na wakati mwingine tunapaswa kwenda kinyume na fikra za kiulimwengu huu, kuishi kinyume na mtazamo wa wana wa ulimwengu huu, kujinyima kwa ajili ya wengine, kuachana na tamaa za kidunia na kuyakaza macho yetu kuelekea mbinguni. Huu ni mlango mwembamba.

Basi tumwombe Mungu atujalie neema na baraka zake tuwe kweli watoto wake, tuuishi kweli ukristo wetu, ili mwisho wa siku ukifika tuweze kuokolewa na kuingia katika ufalme wa uzima wa milele mbinguni kama wana wateule wa Mungu. Ni katika tumaini hili mama kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi: “Ee Bwana, wewe umetufanya kuwa wanao kwa sadaka yako moja. Utujalie kwa wema baraka za umoja na amani katika Kanisa lako”. Antifona ya komunio inasisitiza kusema; “Bwana asema: Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho” (Yn. 6:54. Na Sala baada ya komunyo inayohitimisha maadhimisho haya inasema; “Ee Bwana, tunakuomba dawa ya rehema yako ituponye kabisa. Utukamilishe kwa wema wako na kutuhifadhi hivi hata tuweze kukupendeza katika mambo yote”.

Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari ya Juma la 21 la Mwaka C
22 Agosti 2025, 09:30