杏MAP导航

Tafuta

Masomo ya dominika hii yanatuasa na kutukumbusha wajibu wetu wa kutumia mali na vitu vya dunia hii kwa sifa na utukufu wa Mungu ili tustahilishwe kuurithi ufalme wa mbinguni. Masomo ya dominika hii yanatuasa na kutukumbusha wajibu wetu wa kutumia mali na vitu vya dunia hii kwa sifa na utukufu wa Mungu ili tustahilishwe kuurithi ufalme wa mbinguni.   (AFP or licensors)

Tafakari Dominika 18 Mwaka C wa Kanisa: Utu na Uhai wa Binadamu

Wajibu wetu wa kutumia mali na vitu vya dunia hii kwa sifa na utukufu wa Mungu ili tustahilishwe kuurithi ufalme wa mbinguni. Msisitizo ni kuwa thamani ya maisha ya mwanadamu haiko katika vitu bali kwa Mungu aliyemuumba kwa sura na mfano wake mwenyewe (Mw.1:27). Hivyo ni katika kuishi kadiri ya amri za Mungu, mwanadamu anatambua thamani ya maisha yake, umuhimu wa kumtegemea Mungu, kuutumainia na kuukimbilia msaada wake katika safari yake!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 18 ya mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatuasa na kutukumbusha wajibu wetu wa kutumia mali na vitu vya dunia hii kwa sifa na utukufu wa Mungu ili tustahilishwe kuurithi ufalme wa mbinguni. Msisitizo ni kuwa thamani ya maisha ya mwanadamu haiko katika vitu bali kwa Mungu aliyemuumba kwa sura na mfano wake mwenyewe (Mw.1:27). Hivyo ni katika kuishi kadiri ya amri na maagizo yake Mungu, mwanadamu anatambua thamani ya maisha yake, umuhimu wa kumtegemea Mungu, kuutumainia na kuukimbilia msaada wake katika safari ya maisha yake kuelekea Mbinguni. Ni katika muktadha huu wimbo wa mwanzo unaofungua maadhimisho ya dominika hii unasema hivi; “Ee Mungu, uniokoe, ee Bwana, unisaidie hima. Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu, ee Bwana, usikawie” (Zab. 70: 1, 5). Naye mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Bwana, uwe nasi watumishi wako, utukirimie mema yako yasiyo na mwisho sisi tuombao. Uyatengeneze na kutuhifadhia mema hayo, kwa vile tunaona fahari kwamba wewe ndiwe mwumba na mfalme wetu."

Busara na hekima ya mkulima mpumbavu!
Busara na hekima ya mkulima mpumbavu!

Somo la kwanza ni la Kitabu cha Mhubiri (Mh 1:2; 2:21-23). Ujumbe msingi katika somo hili ni huu: kwa mwanadamu mambo yote ya kidunia anayohangaika nayo yanakoma kwa kifo chake na ya ulimwengu ujao ambayo hayajui huanza. Kwa kuwa ni Mungu peke yake anayejua yote. Basi yampasa mwanadamu amtegemee Mungu katika yote kwa maana bila Yeye yote ni ubatili, ni utupu, ni bure, ni udanganyifu, tena ni uupuzi, ni kukimbiza upepo tu: “Hekima yake na upumbavu ni ubatili” (1:12-18; 2:12-16); “Anasa ni ubatili” (2:1-11); “Kutaabika ni ubatili” (2:17-26); “Uonevu, taabu na uadui ni ubatili (4:1-12); nayo “maendeleo na utajiri ni ubatili (4:13-16; 5:7-6:12). Kumbe, hekima, elimu, maarifa, mamlaka, uwezo, utajiri, na ushawishi, vyote hivi vina thamani na umuhimu kwa wakati na mahali muafaka katika maisha ya mwanadamu, lakini si vya kudumu, vinakoma kwa kifo, na haviyapi maisha yake thamani, hadhi, wala maana. Ndiyo maana mzaburi anasema hivi; “Binadamu hatadumu katika fahari yake…atakapokufa hatachukua chochote, utukufu wake hautashuka kaburini pamoja naye, makaburi yatakuwa maskani yake milele” (zab 149). Kama hali ndivyo ilivyo, tufanye nini basi? Mzaburi katika wimbo wa katikati anatuambia hivi; “Njoni, tumwimbie Bwana, tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu. Tuje mbele zake kwa shukrani, tumfanyie shangwe kwa zaburi. Njoni, tuabudu, tusujudu, tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba. Kwa maana ndiye Mungu wetu, na sisi tu watu wa malisho yake, na kondoo za mkono wake. Ingekuwa heri leo msikie sauti yake! Msifanye migumu mioyo yenu; Kama vile huko Meriba, kama siku ya Masa jangwani. Hapo waliponijaribu baba zenu, wakanipima, wakayaona matendo yangu” (Zab. 94 : 1-2, 6-9). Nasi tukimtumainia Mungu, yote tuyafanyayo atayapa maana katika maisha ya sasa hapa duniani na katika maisha ya milele mbinguni, maana Yeye ni muweza wa yote.

Jiwekeeni hazina mbinguni
Jiwekeeni hazina mbinguni   (ANSA)

Somo la Pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai (Kol 3:1-5; 9-11). Ujumbe mahususi katika somo hili ni huu; kwa sakramenti ya ubatizo tumekufa kuhusu dhambi katika Kristo na tumefufuka naye, tukapata uzima mpya. Basi sasa tuishi kadiri ya uzima mpya. Tuifishe hali ya dhambi ndani yetu, tukiyatafuta yaliyo juu, Kristo aliko, na siyo yaliyo katika nchi. Hii haina maana kuwa maisha ya hapa duniani hayana maana na tusihangaike nayo. La hasha. Tunachoambiwa ni kuepuka maisha ya dhambi, maisha ya kumchukiza Mungu. Hili linafanyika kwa kuuvua utu wa kale, pamoja na matendo yake, kuvifisha viungo vyetu vinavyoweza kutuingiza katika dhambi za uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya na ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, na ulafi (Gal 5:20-21); na kujibidisha katika kuuvaa utu mpya katika Kristo kwa njia ya Roho Mtakatifu ili tuweze kuzaa matunda ya kiroho ambayo ni “upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, na kiasi (Gal. 5:22-23).

Maisha, utu na heshima na binadamu ni zaidi ya fedha na mali
Maisha, utu na heshima na binadamu ni zaidi ya fedha na mali   (AFP or licensors)

Injili ni ilivyoandikwa na Luka (Lk 12: 13-21). Ujumbe mkuu katika sehemu hii ya Injili ni huu; wingi wa mali anazojilimbikizia mwanadamu haumhakikishii wokovu wa maisha yake, kwa maani si wingi wa vitu unaomuhesabia haki mbele za Mungu, bali ni matendo mema. Zaidi sana uhai wa kila mwanadamu upo mikononi mwa Mungu na sio katika vitu. Hivyo tujitahidi kuishi vyema hapa duniani, tukivitumia vizuri tulivyojaliwa na Mungu ili mwisho wake ukifika tukashirikishwe na ya mbinguni aliko Mungu Baba yetu. Daima tukumbuke kuwa; “Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, dunia na wote wakaao ndani yake” (Zab 24:1). Mungu kwa upendo wake anatujalia tuvitumie kwa sifa na utukufu wake, na baada ya maisha yetu hapa duniani tutapaswa kutoa hesabu yake. Tukivitumia vizuri vitu tulivyojaliwa Mungu atatuambia; “Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache …. ingia katika furaha ya Bwana wako” (Mt 25:21.) Kumbe basi, kuwa na mali nyingi si vibaya na wala sio dhambi, maana vyote viliumbwa kwa ajili ya mwanadamu ili kwayo aishi vyema na kumtukuza Mungu muumba wake. Yesu anatoa fundisho hili baada ya mtu mmoja kumwomba amsaidie kutatua mgogoro wa kugawana mali ya urithi na ndugu yake. Katika kufikisha huu ujumbe Yesu anasimulia simulizi la mkulima mpumbavu aliyeweka tumaini lake lote katika mavuno mengi aliyojipatia, akajikinai, akamsahau Mungu na watu wengine hata kujiseme nafsini mwake; “Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia; Mpumbavu wewe, usiku huu wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?” Hii inatufundisha kuwa mali nyingi inaleta kiburi na kumfanya mtu amsahau Mungu muumba wake na lengo la maisha yake. Kiburi hiki kinamfanya awadharau wengine. Hivyo kiburi na dharau ndizo sababu ya hukumu aliyoipokea.

Wakulima, mahujaji wa imani na matumaini
Wakulima, mahujaji wa imani na matumaini

Lakini pia hata asiye na mali anaweza kumuacha Mungu akajiingiza katika utafutaji wa mali kwa shauku kubwa hata kwa njia na namna mbaya na zisizo halali, ikiwemo kudhulumu uhai wa wengine. Katika hili Mtume Paulo anatoa maonyo haya; “Lakini wale watu wanaotamani kuwa na mali kwa haraka haraka, huanguka kwenye majaribu na wamenaswa na tamaa nyingi za kipumbavu, zenye kudhuru, zinazowazamisha katika uharibifu na maangamizi. Kwa maana kupenda fedha kwa kupindukia ndiyo shina moja la maovu ya kila namna. Baadhi ya watu wakitamani fedha, wameiacha amani na kujichoma wenyewe kwa maumivu mengi” (1Tim. 6:9-10). Basi, tuzingatie ushauri huu; Lakini utauwa na kuridhika ni faida kubwa. Kwa kuwa hatukuja humu duniani na kitu cho chote, wala hatuwezi kutoka humu na kitu. Lakini kama tuna chakula, mavazi, na malazi turidhike navyo (1Tim. 6:6-8.) Tukumbuke kuwa maisha ni zaidi ya pesa, maisha ni zaidi ya mali, maisha ni zaidi ya madaraka, maisha ni zaidi ya fahari, na maisha ni zaidi ya tamaa za mwili. Na kwa kuwa muda wetu wa kuishi hapa duniani, miili yetu, uzuri wetu, nguvu zetu, akili zetu, nafasi zetu, mahusiano yetu na mali zetu zote, ni zawadi toka kwa Mungu, ametukabidhi tuvitunze na kuvitumia kwa sifa na utukufu wake na kujitakatifuza kwetu.

Tumieni vyema mali ya dunia
Tumieni vyema mali ya dunia   (AFP or licensors)

Basi tuzingatie ushauri huu; “Lakini wewe, mtu wa Mungu…Fuata haki, utauwa, imani, upendo, saburi na upole. Pigana vile vita vizuri vya imani…shika uzima wa milele…mbele za Mungu avipaye vitu vyote uhai na mbele za Kristo Yesu…” (1Tim. 6:11-14). Nanyi matajiri msijivunie, wala msiweke tumaini lenu katika mali ambayo si ya hakika, bali wekeni tumaini lenu katika Mungu ambaye amewapatia vitu vyote kwa wingi ili mvifurahie kwa kuwatendea mema wengine kwa ukarimu. Kwa njia hii mtajiwekea hazina kama msingi kwa ajili ya wakati ujao na hivyo mtajipatia uzima wa milele mbinguni (1Tim. 6.17-19). Basi tumwombe Mungu, aliyetupa mamlaka juu ya mali na vitu vya dunia hii, atujalie hekima na busara tuvitumie vyema alivyotujalia kwa riziki ya dunia hii, na hivi lengo lake la kutuumba, yaani kumjua, kumpenda, kumtumikia na mwisho kufika kwake mbinguni, liweze kutimia ndani mwetu. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, tafadhali uzitakatifuze dhabihu hizi kwa wema wako. Uikubali sadaka hii ya roho zetu, na kutufanya sisi wenyewe tuwe kwako sadaka ya milele”. Na katika sala baada ya komunyo anapohitimisha maadhimisho ya dominika hii anasali hivi; “Ee Bwana, utulinde daima na popote sisi uliotutia nguvu kwa chakula cha mbinguni. Utufadhili siku zote ili tustahili ukombozi wa milele”. Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari D 18
30 Julai 2025, 14:36