Tafakari Dominika 17 ya Mwaka C wa Kanisa: Sala:Ibada na Uchaji!
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya Neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican leo ni Dominika ya 17 mwaka C. Kila mwaka Kanisa Katoliki Kiulimwengu huadhimisha siku ya Wazee Ulimwenguni kila ifikapo Dominika ya nne ya Mwezi Julai. Siku hii ilianzishwa na Papa Francisko mnamo 2021 kwa lengo la kutambua mchango mkubwa wa kizazi cha wazee katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Baraza la Kipapa kwa ajili ya Walei, Familia na Maisha, katika mwaka huu 2025, lilichapisha kauli mbiu inayoongoza Siku V ya Wazee Ulimwenguni itakayoadhimisha tarehe 27 Julai 2025. Katika taarifa hiyo inabainisha kuwa: “Baba Mtakatifu Leo XIV alichagua mada ya maadhimisho hayo isemayo “Heri ambaye hajapoteza matumaini yake” (Sir 14:2). Maneno haya, yaliyotolewa katika kitabu cha Sira, yanaonesha baraka za wazee na kuonesha katika tumaini lililowekwa kwa Bwana katika njia ya Mkristo na kupatanishwa na uzee. Katika ujumbe wake kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Tano ya Wazee Duniani itakayoadhimishwa tarehe 27 Julai 2025, Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa wito wa matumaini kwa wazee kote ulimwenguni, akisisitiza umuhimu wao kama mashuhuda wa imani, hekima na upendo. Kauli mbiu ya mwaka huu ni: “Heri wale ambao hawajapoteza tumaini” (rej. Sir 14:2).
Masomo ya Dominika ya 17 ya Mwaka C wa Kanisa yanatufundisha nguvu ya sala, si tu kama ibada ya kidini, bali kama njia ya matumaini na mabadiliko ya maisha. Katika dunia yenye huzuni nyingi, mateso, na kutokujua kesho, tunahitaji kurejea kwenye chanzo halisi cha tumaini: mawasiliano hai na Mungu ndio sala. Abrahamu anathubutu kuingia kwenye mazungumzo ya kina na Mungu. Anaomba msamaha kwa ajili ya Sodoma, akijadiliana kama rafiki na Mungu. Katika dunia yenye “Sodoma” nyingi za kisasa (vita, uonevu, mmomonyoko wa maadili), watu wa Mungu wanaitwa kuwa sauti ya maombezi. “Tumaini halikai kimya linazungumza kwa sala yenye huruma kwa wengine.” Dominika hii imepambwa na dhamira ya nguvu ya sala na maombi, kwamba Yeye aliye Baba na mpaji wa yote yaliyo mema, hachoki kuwasikiliza wale wanaomuomba kwa moyo, roho, akili na sauti… tumtukuze kwa kuwa anasikia, tumuabudu kwa kuwa anatujibu, tumsifu na kumuadhimisha milele. Mtume Paulo anafundisha kuwa tumefufuliwa pamoja na Kristo. Dhambi zetu zimesamehewa – agano jipya limetangazwa. Baba Mtakatifu Leo anahimiza tutazame mbele kwa macho ya neema, si macho ya hukumu. Kwa kuwa tumesamehewa, basi tunapaswa kueneza msamaha, na kujenga jamii mpya yenye matumaini ya kweli. Yesu anawafundisha wanafunzi wake kusali: “Baba yetu…” Kisha anawahimiza kuomba bila kuchoka: “Ombeni, nanyi mtapewa...” Katika ulimwengu wa ukataji tamaa, sala si tukio la kubembeleza, bali ni kitendo cha matumaini. Kama watoto tunavyomwendea baba yao, vivyo hivyo waamini wanamwendea Mungu kama chanzo cha kila zawadi njema. “Sala ni pumzi ya tumaini; bila sala, tumaini hufa.” Tunayo mengi ya kumwambia katika kuomba kwetu kwa ajili yetu na wenzetu, wazima na wafu… SALA YA BABA YETU ni msingi wa hayo yote, ni sala kamili kuliko zote sababu imefundishwa na Kristo mwenyewe na ikisemwa kwa roho ya uchaji na moyo wa ibada inakuwa mbele za Mungu harufu nzuri ya manukato ikitustahilia mema yote mbele zake.
UFAFANUZI: Kristo Yesu amesema “Msalipo semeni” BABA YETU… Huyo pekee tunayemuomba, kumuabudu, kumshukuru na kumtukuza ni BABA YETU, hili tumefunuliwa na Kristo mwenyewe, katika Yeye sote tumepata kuwapo, kama Baba anatutunza na mkononi mwake tunao usalama… Historia imeanzia kwake, kwake tunaelekea na kwake tu upo ukamilifu wetu, ndani ya Baba huyu lipo pumziko, raha na heri ya milele… “A-metuumba bila sisi lakini Hawezi kutukomboa bila sisi” (Mt. Augustino), Yeye anapotunyeshea neema ya msaada sisi tujibidishe kumsikiliza na kumtii kwa moyo wote. ULIYE MBINGUNI… ‘Mungu wetu yupo mbinguni, hufanya chochote apendacho (Zab 115:3), maisha yetu ni safari kuelekea Yerusalem mpya, mbinguni kwa Baba. Mbingu ni moyo wa wenye haki ambamo Mungu anakaa kama hekalu lake. Katika Kristo mbingu na nchi zimepatanishwa, kwa msalaba na ufufuko wake anatuwezesha kupanda huko pamoja naye. tuombe neema ya kutamani kufika mbinguni, tuvumilie magumu ya njiani na neema ya Baba itusaidie. JINA LAKO LITUKUZWE… Hilo ni Jina takatifu na la kuogopwa (Zab 111:9), lisitajwe kiholela au katika shuhuda na viapo viovu, kulitukuza Jina la Baba ni kutenda kwa namna iliyo takatifu. Tusali ombi hili kwa unyenyekevu tukikumbuka kuwa nyimbo zetu za sifa hazimzidishii Mungu chochote bali zinatufaa wenyewe kwa wokovu, katika yote tunayofikiri na kutenda, katika kufaulu na kuanguka, tusijitukuze wenyewe, Jina tukufu la Bwana litukuzwe sasa na hata milele, amina. UFALME WAKO UFIKE… ni hamu yetu kwamba Mungu atawale ndani yetu sote, hapa tunafanywa washiriki ili enzi, utawala, milki, ukuu na mamlaka vilivyo mali ya Mungu vifike kote hadi miisho ya ulimwengu. Ufalme huu upo mbele yetu, tumeupewa na Kristo wake aliyetwaa mwili, akafa na kufufuka. Ni ufalme wa haki, amani, furaha na upendo. katika Ekaristi tunaonjeshwa hapa duniani sherehe isiyo na mwisho ya ufalme wa mbinguni. Ni moyo ulio safi tu ndio unaweza sema “ufalme wako uje.” tuombe neema ya kuuishi ufalme wa Mungu na kufanya toba kwa nyakati zile tulizokumbatia ufalme mwingine.
UTAKALO LIFANYIKE… tunaposali tuwe tayari kupokea tunachojaliwa hata kama ni tofauti na matazamio yetu ya kibinadamu sababu Yeye anajua kilicho bora na tunachohitaji kuliko sisi, tuzoee kupokea majaliwa yake hasa magumu na mazito ya maisha. Analotaka tufanye basi tulitende, tusiwe vikwazo kwa mapenzi yake na kwa wenzetu. Baba yetu ni mwema na alitakalo daima ni zuri kwa ajili yetu, katika mapenzi yake tunapata utakaso na yeyote anayefanya mapenzi ya Mungu huyo Mungu humsikia. Kama vile Kristo alivyotimiza mapenzi ya Baba nasi atusaidie tulitimize lile atakalo Mungu: kumjua, kumpenda, kumtumikia ili tufike kwake. DUNIANI KAMA MBINGUNI… hili ni la pekee kabisa, kwamba utakatifu ule, shangwe ile, uzuri ule, furaha ile ya kimbingu ionekane hapa duniani kwa njia ya Ukristo wetu! Dunia iwe mbingu ndogo, paradiso ing’aayo. Tumshukuru Mungu kwa ajili ya wote wanaojitahidi kuifanya dunia yetu ifanane na mbingu kwa sala, kazi na sera nzuri ili sayari hii iliyo nyumba yetu sote iwe mahali pazuri kwa wote… Na sisi tunaoigeuza gehenna kwa dhambi Mungu mwema atuhurumie na kutusamehe. UTUPE LEO MKATE WETU WA KILA SIKU… uzima, afya, riziki, amani na mahitaji yetu yote ni majaliwa ya Mungu kwetu! Ombi hili linaakisi tumaini la watoto wanaotegemea mema kutoka kwa Baba yao. Yeye anabariki kazi na juhudi za akili, kifua na mikono yetu. Tunapoomba na kujaliwa “mkate” wetu wa kila siku tutekeleze pia wajibu wetu kwa ndugu zetu wahitaji… wapo wanaohitaji mkate kama riziki, mkate wa haki na mahusiano mema, tujifunze “fadhila ya kugawana” mema ya kimwili na ya kiroho si kwa kulazimishwa bali kwa upendo. Tunapokea mkate huu kwa njia ya “sala na kazi” (Mt. Benedikto) hivi tusali kama kila kitu kinamtegemea Mungu na tufanye kazi kama vile kila kitu kinatutegemea sisi, tushukuru pia kwa mapaji tunayojaliwa (KKK 2834.) UTUSAMEHE MAKOSA YETU KAMA TUNAVYOWASAMEHE WALE WALIOTUKOSEA… hapa tunaungama kwamba “sote tumetenda dhambi na kupungukiwa utukufu wa Mungu” (Rum 3:23), hayupo yeyote awezaye simama na kusema ni mtakatifu, tunahitaji huruma na msamaha kutoka Kwake. Msamaha wa Mungu hauwezi penya mioyo yetu pindi hatujawasamehe wenzetu, msamaha ni kilele cha upendo na kumpenda Mungu kunaanza na kumpenda jirani. Mzigo wa kinyongo ni mzito mno, msamaha unaleta wepesi na kurudisha ndani mwetu ukawaida wa maisha.
USITUACHE KATIKA KISHAWISHI… “majaribu hayana budi kuja” (Lk 17:1a) lakini “Mungu ni mwaminifu hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo, lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili” (1Kor 10:13), tusikimbie magumu, tusikwepe mateso, neema ya Mungu itusaidie kushindana mpaka mwisho na kushinda, SALA ndio silaha pekee dhidi ya vishawishi, tusali bila kuchoka… vishawishi vituimarishe tuufikie ukomavu wa imani yetu. tunapoomba neema hii, sisi wenyewe tusiwe vishawishi na tusiwaingize wenzetu katika majaribu, wakishindwa kustahimili tukawaangusha adhabu yetu itakuwa kubwa (Lk 17:2). LAKINI UTUOPOE MAOVUNI… maovu hayo ni nafsi, shetani, yule mwovu, mwongo na baba wa uongo (KKK 2851-52), kwa ombi hili MUngu atuepushe na mwovu huyu na maovu yote yaliyopo, yaliyopita na yajayo, atuondolee dhiki zote na kutukinga na watu wabaya, atujalie kwa wema amani maishani mwetu… nasi tusiwatendee wenzetu maovu, bali tuione sura ya Mungu katika wote tunaokutana nao. Mungu ameisikiliza sala ya Ibrahim katika somo I (Mwz 18:20-32), anatusamehe makosa yote na kufuta mashtaka yetu kadiri ya somo II (Kol 2:12-14), amesema katika Injili ya leo “ombeni nanyi mtapewa, tafuteni nanyi mtaona” (Lk 11:9) basi na tuombe, sala yetu daima imuelekee Baba yetu wa mbinguni, katika Roho Mtakatifu, kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Leo Yesu anatufundisha kusema, “Baba yetu…” Katika maneno haya machache kuna utambulisho wetu, tumaini letu, na uhusiano wetu wa milele. Kama Abrahamu, simama mbele za Mungu kwa ajili ya wengine. Kama Paulo, kaa na Kristo hata katikati ya mateso. Kama Maria na wanafunzi, omba na uamini, hata majibu yawe kimya. Katika mwaka huu wa Jubilei ya Matumaini, tufufue moyo wa sala, tusamehe wengine, na tusimame kama mashuhuda imani na matumaini kwa njia ya sala, ushuhuda, na uaminifu kwa Mungu. “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona...” (Lk 11:9). Amina.