杏MAP导航

Tafuta

Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatutafakarisha juu ya, “NGUVU YA SALA” Bwana wetu Yesu Kristo mara nyingi katika maandiko Matakatifu alisali, alidumu daima katika muunganiko na Baba yake wa mbinguni. Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatutafakarisha juu ya, “NGUVU YA SALA” Bwana wetu Yesu Kristo mara nyingi katika maandiko Matakatifu alisali, alidumu daima katika muunganiko na Baba yake wa mbinguni.  

Tafakari Dominika ya 17 Mwaka C wa Kanisa: Nguvu ya Sala!

Maadhimisho ya Siku ya Tano yaBibi, Babu na Wazee Duniani inaadhimishwa tarehe 27 Julai 2025, Papa Leo XIV ametoa wito wa matumaini kwa wazee kote ulimwenguni, akisisitiza umuhimu wao kama mashuhuda wa imani, hekima na upendo. Kauli mbiu ya mwaka huu ni: “Heri wale ambao hawajapoteza tumaini” (rej. Sir 14:2). Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatutafakarisha juu ya, “NGUVU YA SALA” Bwana wetu Yesu Kristo mara nyingi alikuwa anasali!

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya 17 ya mwaka C wa Kanisa. Ibada na heshima kwa watakatifu Joakim na Anna ni mwendelezo wa Ibada kwa Bikira Maria na hatimaye, Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Ni nafasi muafaka ya kutafakari changamoto, fursa na matatizo yaliyopo na kuendelea kuyafanyia kazi na hatimaye, kuyapatia majibu muafaka kwa mwanga wa tunu msingi za Kiinjili na kiutu. Wazazi na walezi warithishe imani hii kwa njia ya maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu; kwa kutambua na kuenzi kweli msingi za maisha kadiri ya upendo na mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu; watoto wasaidiwe kupata mwanga na ufunuo wa Mungu katika hija ya maisha yao. Wazee ni amana na utajiri wa jamii; wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo mizizi ya jamii; mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya ni imani na mang’amuzi ya maisha. Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yatakuwa yanakaribiana sana na Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria. Siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani ni matunda yanayobubujika kutoka katika Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” uliozinduliwa rasmi tarehe 19 Machi 2021 na ukahitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kumi ya Familia Duniani hapo tarehe 26 Juni, 2022 kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu.” Siku ya Mababu, Mabibi na Wazee ni muda wa kuserebuka, kutoa faraja na kuonesha upendo kwa wazee, ili kujenga na kudumisha: Umoja, udugu, upendo na faraja tunu msingi katika maisha ya kijamii. Ni muda kwa waamini kujifunza sanaa ya kupenda na kupendwa na katika muktadha huu, wazee wanaweza kuwa magwiji kwa vijana wa kizazi kipya!

Siku ya Tano ya Bibi, Babu na Wazee Kwa Mwaka 2025
Siku ya Tano ya Bibi, Babu na Wazee Kwa Mwaka 2025   (ANSA)

Ndoto, kumbukumbu na sala ni kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati pamoja na waja wake. Wazee wawe ni wadau katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji katika maisha na utume wa Kanisa. Kila mwaka Kanisa Katoliki Kiulimwengu huadhimisha siku ya Wazee Ulimwenguni kila ifikapo Dominika ya nne ya Mwezi Julai. Siku hii ilianzishwa na Papa Francisko mnamo 2021 kwa lengo la kutambua mchango mkubwa wa kizazi cha wazee katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Baraza la Kipapa kwa ajili ya Walei, Familia na Maisha, katika mwaka huu 2025, lilichapisha kauli mbiu inayoongoza Siku V ya Wazee Ulimwenguni itakayoadhimisha tarehe 27 Julai 2025. Katika taarifa hiyo inabainisha kuwa: “Baba Mtakatifu Leo XIV alichagua mada ya maadhimisho hayo isemayo “Heri ambaye hajapoteza matumaini yake” (Sir 14:2). Maneno haya, yaliyotolewa katika kitabu cha Sira, yanaonesha baraka za wazee na kuonesha katika tumaini lililowekwa kwa Bwana katika njia ya Mkristo na kupatanishwa na uzee. Katika ujumbe wake kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Tano ya Wazee Duniani itakayoadhimishwa tarehe 27 Julai 2025, Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa wito wa matumaini kwa wazee kote ulimwenguni, akisisitiza umuhimu wao kama mashuhuda wa imani, hekima na upendo. Kauli mbiu ya mwaka huu ni: “Heri wale ambao hawajapoteza tumaini” (rej. Sir 14:2).

Siku ya Wazee Duniani 2025
Siku ya Wazee Duniani 2025   (AFP or licensors)

Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatutafakarisha juu ya, “NGUVU YA SALA” Bwana wetu Yesu Kristo mara nyingi katika maandiko Matakatifu alisali, alidumu daima katika muunganiko na Baba yake wa mbinguni. Anawafundisha wanafunzi wake hali kadhalika namna ya kusali (Lk 11:1-13) akisisitiza hasa udumifu (persistence) na Imani katika kusali. Mungu mwenye huruma anatupenda, anatuhurumia, anatusikia na anafahamu mahitaji yetu yote hata kabla hatujamwomba. Katika somo la kwanza (Mwa 18:20-32) tunaona Imani na udumifu wa Ibrahimu katika kusali na kuomba si kwa ajili yake tu bali kwa ajili ya watu waovu wa Sodoma. Kwa njia ya udumifu na Imani yake katika kuomba, Mwenyezi Mungu anaahidi kutokuungamiza mji wa Sodoma iwapo wapo huko wachache wanaomcha Mungu. Ni Nguvu ya sala, nguvu ya maombi. Mzaburi katika wimbo wa katikati (Zab138:1-3,6-9) anamshukuru Mungu kwa kuwa alimjibu sala na maombi yake siku ile aliyomwita, akamfariji nafsi na kumtia nguvu. Hii ni nguvu ya sala, na Imani thabiti na udumifu katika kuomba, tena kuomba bila kuchoka. Mtume Paulo katika somo la pili (Kol 2:12-14) anatufundisha nguvu ya sadaka ya Kristo, ambaye ni mwombezi na mpatanishi wetu kwa Mungu, kwamba hapo Mwanzo tulikua tumekufa lakini kwa njia ya sadaka yake sisi sote tumefufuliwa na tu hai tena. Kristo anatuombea sisi kwa Baba, ndiye kuhani mkuu anayetufaa sana, anayechukuana nasi katika udhaifu wetu.

Udumifu wa imani katika sala
Udumifu wa imani katika sala   (Vatican Media)

Somo la Kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Mwanzo 18:20-32. Hii ni sala ya Ibrahimu ambaye anauombea mji Sodoma, ambao Mungu alipanga kuungamiza. Sodoma ulikua ni moja kati ya miji mitano katika bonde la Mto Yordani (Mwa 13:10-13). Watu wa mji huu walikua ni wabaya, wenye kufanya dhambi nyingi sana juu ya Bwana (Mwa 13:13). Katika mji huu aliishi Lutu binamu yake na Ibrahimu (Mwa 13:8-10). Ibrahimu katika sala yake anamwomba Mungu asiwaharibu wenye haki pamoja na waovu. Hapa tunapata fundisho kubwa juu ya haki na huruma ya Mungu (God’s justice balanced with his mercy), kwamba, Mwenyezi Mungu hawaangamizi wenye haki pamoja na waovu, na wakati huo huo anatoa muda na nafasi kwa ajili ya waovu vile vile kufanya toba ili wasiangamizwe na gadhabu ya Mungu. Ibrahimu akitambua haki na huruma ya Mungu, anasali kwa Imani na udumifu ili Mungu asiwaangamize wenye haki pamoja na waovu na atoe muda zaidi iwapo wapo watakaotaka wongofu. Mwenyezi Mungu hatimaye alisikiliza sala ya Ibrahimu, akitoa muda na nafasi ya kutubu kwa watu wa mji wa Sodoma, na ikiwa wangepatikana hata watu 10 tu wenye haki basi asingeuteketeza mji wa Sodoma.    Ndugu zangu katika somo hili la kwanza tuna mambo matano ya kujifunza. Kwanza: Mungu ni Mwenye haki na huruma kuu (God’s Justice and Mercifulness) Katika somo hili la kwanza, Mwenyezi Mungu anapanga kuungamiza mji wa Sodoma kwa kuwa watu wa mji ule walikua ni wabaya na wenye kufanya dhambi na uovu mwingi mbele za Bwana (Mwa 13:13). Kwa njia ya sala na maombi ya Ibrahimu, Mwenyezi Mungu anatoa muda na nafasi zaidi kwa watu wa mji huo waweze kuacha uovu na kuiepuka gadhabu ya Bwana. Kwa haki walistahili kuangamizwa mara moja lakini kwa kuwa Mungu ni mwingi wa huruma anatoa muda na nafasi ya kutubu, kwa ajili ya wenye haki wachache aliahidi kutokuungamiza mji wa Sodoma. Ndugu mpendwa, Mungu wetu ni Mungu mwenye haki, lakini pia ni mwingi wa huruma. Mzaburi anauliza katika Zaburi ya 130:3-4, “Bwana kama wewe ungehesabu maovu yetu, Ee Bwana nani angesimama? Lakini kwako kuna msamaha ili wewe uogopwe. Sisi sote kwa haki ilitupasa kufa kwa sababu ya dhambi na kosa la wazazi wetu wa kwanza, Adamu na Eva. Lakini Mungu wetu kwa sababu ya huruma yake, akalikumbuka Agano alilofanya na Ibrahimu na uzao wao hata milele, akatuletea mkombozi, Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa sababu ya mwenye haki mmoja, Bwana wetu Yesu Kristo, sisi sote tukapata ukombozi wa milele kutoka katika dhambi na mauti. Mtakatifu Thomasi wa Akwino anatufundisha kuwa, Mungu ni mwenye haki, lakini katika Huruma yake kuu, anatoa neema na msamaha pale ambao kwa haki tulistahili adhabu “God is perfectly just, but in his divine Mercy offers grace and forgiveness where strict justice would demand punishement” Huruma sio kinyume na haki bali inakwenda mbali zaidi ya haki kwa kuponya na kurejesha upya uhusiano zaidi ya kulipa fidia ya kile kilichokua kinapaswa kulipiwa.

Hayati Papa Francisko akisali mbele ya Picha ya Bikira Maria Afya ya Warumi
Hayati Papa Francisko akisali mbele ya Picha ya Bikira Maria Afya ya Warumi   (Vatican Media)

Hivyo ndugu wapendwa, Mwenyezi Mungu anatupa nafasi kila siku ya kufanya mabadiliko.  Hakuna kuchelewa kwa Mungu kwa kuwa kila sekunde aliyonipa na aliyokupa ni ya thamani katika kuuchuchumilia Utakatifu wetu. Tutumie vyema fursa na nafasi alizotupa Mungu za kuutafuta Utakatifu. Kwa njia ya Mama Kanisa tunapata nafasi ya kuipokea huruma kubwa ya Mungu wetu ambaye anataka sisi sote tuupate uzima wa milele. Usiogope kuungama kwa sababu dhambi na uovu wako ni mkubwa, usiogope kwenda mbele za Mungu kwa kuwa unajiona hustahili, bali jipe moyo na utumaini katika huruma ya Mungu isiyo na mipaka. Pili: Kwa njia ya sala tunaingia katika mazungumzo na Mungu (Prayer is a dialogue not just a monologue). Sala ni mawasiliano (communication) kati yetu sisi na Mungu, tukimshukuru, kumtukuza, kumwabudu, kumsifu, kutubu na kuomba msamaha kwa makosa yetu na ya wengine na kumwomba kwa ajili ya mahitaji yetu mbalimbali ya kimwili na kiroho na yale ya ndugu na Jirani zetu. Abrahamu anazungumza moja kwa moja na Mungu, analeta maombi yake mbele za Mungu. Mung anatupokea kama tulivyo, anatupa nafasi ya kuzungumza naye kila wakati. Ndugu mpendwa, Mungu anashuka na kusema nasi. Mungu hayupo mbali nasi bali yupo karibu kabisa na sisi. Kama alivyoshuka na kusema na Ibrahimu na kufunua kwake mpango wake, ndivyo anavyoshuka Mungu kwangu na kwako kila mara tunapomwalika katika sala na anafunua ulio mpango wake katika maisha ya kila mmoja wetu. Katika adhimisho la Ekaristi Takatifu, kwa njia ya Roho Mtakatifu, Yesu anashuka kati yetu, anasema nasi katika Sakramenti Takatifu ya Altare. Anabaki nasi kila siku katika Tabernaklo ili na hapo tunapat nafasi kila mmoja wetu kuzungumza naye. Jenga urafiki na Yesu, mpokee anapokuja kwako, ana neno nawe, fungua moyo wako, mpe muda wako. Zungumza na Yesu kirafiki kabisa, yeye ni kaka yetu mkubwa, ni ndugu yetu kabisa. Kila siku jitahidi ndugu mpendwa kutenga muda wa kuzungumza na Mungu. Mwalike Mungu aseme na familia yako, aseme na watoto wako, aseme juu ya changamoto zako mbalimbali unazopitia, aseme na ndugu na jamaa zako, aseme na marafiki zako, aseme na wale wote waliokata tamaa kabisa, aseme na waregevu waliokana imani yao nk.

Sala ya Baba Yetu ni muhtasari wa Injili
Sala ya Baba Yetu ni muhtasari wa Injili   (Vatican Media)

Tatu: Mwenyezi Mungu anafikika, anatuvumilia (God is approachable and patient). Ibrahimu anazungumza na Mungu kwa ujasiri lakini kwa unyenyekevu mkubwa. Anatambua udogo na unyenyekevu wake mbele za Mungu. Akiisha kumwomba na kumsihi Bwana mara kadhaa, anasema, “Basi nimeshika kusema na Bwana, nami ni mavumbi na majivu tu” Alijiona hastahili mbele za Bwana, lakini bado aliendelea kusali na kumsihi Mungu, kwa kuwa Mungu anafikika, na anatuvumilia. Ndugu mpendwa, Ibrahimu anatufundisha kuwa tunaweza kwenda daima mbele za Mungu kwa ujasiri bila woga lakini kwa unyenyekevu na ibada. Tunatambua nguvu, uweza, mamlaka, utukufu na enzi vya Mungu wetu, Mungu ambaye yu daima karibu nasi, Mungu anayefikika. Ndugu mpendwa, tuwapo mbele za Mungu tunapaswa kukiri unyonge na udhaifu wetu mbele zake. Mungu ni Mtakatifu sana na sisi tu dhaifu daima mbele zake, tu wadogo, wanyonge na wanyenyekevu. Tukitambua udogo na unyenyekevu wetu tutakua tayari kwa moyo mnyofu kumtegemea Mungu Baba yetu kwa kila jambo. Tutatambua kuwa bila Mungu hatuwezi kufanya jambo lolote jema, na hatuwezi kufanikiwa katika yale yote ambayo tunayafanya. Tutaanza daima na Mungu katika kila jambo tutakalotenda, tutaanza siku yetu na Mungu, tutaanza kazi zetu na Mungu, tutamaliza hali kadhalika na Mungu. Tunapaswa kila siku kuwa katika muunganiko wa kuduma na Mungu wetu katika sala na hapo atatujibu sala na maombi yetu. Tunapaswa kuwa kama watoto wadogo ambao daima imani na tumaini lao ni kwa wazazi wao. Tumshirikishe Mungu mambo yetu, changamoto zetu, furaha zetu, kufanikiwa kwetu, kushinda na kuinuka kwetu, tumshirikishe maisha yetu yote.

Muhimu: Kudumu katika sala, kiini cha imani
Muhimu: Kudumu katika sala, kiini cha imani   (Vatican Media)

Nne: Nguvu ya maombezi, kusali kwa ajili ya wengine (Intessesory power of prayer). Ibrahimu anatufundisha juu ya wajibu wetu wa kusali kwa ajili ya kuwaombea wengine. Yeye hakusali kwa ajili yake na familia yake tu, bali anasali kwa ajili ya wakosefu, anaomba huruma ya Mungu kwa ajili ya wenye dhambi ili Mungu awarehemu na kuwaepusha na hukumu na gadhabu yake watu wa mji wa Sodoma. Sala ya kweli inawajumuisha wengine, sio sala ya kichoyo bali ni sala inayowakumbuka wengine pia. Ndugu mpendwa, sala zetu hazipaswi kuwa za kichoyo na ubinafsi bali tunapaswa kusali na kuombea pia wengine. Tunapaswa kuomba huruma ya Mungu kwa ajili yetu sisi na kwa ajili ya wongofu wa wengine. Tunapaswa kusali kwa ajili ya mahitaji yetu ya kiroho na kimwili na kwa ajili ya mahitaji ya wengine pia. Omba kwa ajili ya waliokata tamaa, omba kwa ajili ya umoja katika familia zenye mpasuko, omba kwa ajili ya wagonjwa waliopo hospitalini na majumbani, omba kwa ajili ya haki, amani, uwajibikaji katika taifa letu, omba kwa ajili ya Watoto wa wengine ambao pengine wametafuta ajira kwa muda mrefu bila mafanikio, omba kwa ajili ya miito mitakatifu katika kanisa, omba kwa ajili ya biashara zako na za wengine pia. Sala ina nguvu, na Mungu wetu anasikia sala zetu kila mara tunapoomba kwa moyo mnyofu na tunapoomba kwa ajili ya wengine.Tano: Imani na Udumifu katika kusali (faith and persistence in prayer). Ibrahimu anatufundisha juu ya kusali kwa Imani thabiti na udumifu. Katika mazungumzo yake na Mungu, alimwomba Mungu asiwaangamize wenye haki pamoja na waovu. Na kwa nia hiyo alisali na kusisitiza na hatimaye Mungu akamwahidi kuwa hata wangepatikana wenye haki kumi asingeuharibu mji wa Sodoma. Alisali, akasisitiza juu ya nia yake mbele za Mungu mara sita mfululizo na Mungu hakumkemea wala hakumkaripia. Ndugu mpendwa, Yesu aliwafundisha mitume wake mara kadhaa juu ya udumifu na katika somo la Injili katika dominika hii ya 17 amesisitiza juu ya udumifu na imani thabiti katika kusali. Tunapaswa kusali daima bila kuchoka. Kristo ameshatupa moyo kwamba; “Ombeni nanyi mtapata, tafutaeni nanyi mtaona, bisheni nanyi mtafunguliwa. Omba ndugu mpendwa katika hali zote. Usichoke katika kusali na kuomba. Usikate tamaa hata kama majibu ya sala zako yatachelewa. Mungu anatujibu muda na wakati wake, subiri kwa matumaini wakati wa Mungu. Mwombe Mungu akupe uvumilivu, utambue kuwa yeye anajua ni wakati gani atatujibu sala na maombi yetu. 

Sala ya Baba Yetu ni Muhtasari wa Injili na kiini cha imani
Sala ya Baba Yetu ni Muhtasari wa Injili na kiini cha imani   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Wimbo wa katikati ni kutoka katika Zaburi ya 138:1-3, 6-9. Zaburi ya 138:1-3, 6-9 Ni moja kati zaburi za kusifu na kushukuru (Praise and thanksgiving) ya Mfalme Daudi. Daudi anaimba na kumshukuru Mungu. Kwa nini Daudi anasali zaburi hii ya kumshukuru na kumsifu Mungu? Sababu ya Daudi kusali Zaburi hii inatupa nasi sababu kwa nini tunapaswa kusali na kumshukuru Mungu kila mara tunapozungumza na Mungu. Kwanza: Daudi anamshukuru Mungu kwa sababu ya upendo na uaminifu wake. Anamshukuru Mungu kwa kuwa kwa sababu ya upendo uaminifu wake. Upendo na uaminifu ya Mungu wetu havibadiliki, vyadumu milele na milele. Licha ya dhambi na udhaifu wetu bado Mungu anaendelea kutupenda, anaendelea kutuhurumia na kutupa nafasi tena ya kuanza upya, akitumiminia wingi wa neema na baraka zake. Pili: Anamshukuru Mungu kwa kuwa ni yeye peke yake anayestahili sifa na utukufu wote. Mzaburi anatambua nafasi ya Mungu, Mungu mwenye nguvu, Mungu mkuu na mtukufu anayestahili utukufu na sifa mbele ya miungu yote. Hivyo Mungu pekee ndiye astahiliye kusifiwa na kutukuzwa milele. Utambuzi huu wa mzaburi juu ya nafasi ya Mungu, ndiyo wapaswa kuwa mtazamo wetu kila mara tunaposali mbele za Mungu. Tunapaswa kutambua nafasi ya Mungu katika maisha yetu ya kila siku, kwamba ndiye Baba yetu, ndiye Mungu wetu, ndiye Mfalme wetu, ndiye aliye juu ya miungu yote. Tatu: Anamshukuru Mungu kwa sababu ya ulinzi nyakati za mateso. Mzaburi anakiri kwamba alipokwenda katika shida Mwenyezi Mungu alimuhuisha, akanyoosha mkono wake juu ya hasira ya adui zake. Ndugu mpendwa kila mmoja anafahamu jinsi gani Mwenyezi Mungu alivyomlinda na kumwokoa katika hatari mbalimbali za roho na za mwili. Ametuokoa katika hajali mbalimbali, ametukinga dhidi ya magonjwa, ametukinga dhidi ya mitego na hila za mwovu shetani. Mshukuru Mungu nyakati zote alizokukinga na endelea kutumaini ulinzi wake. Nne: Anamshukuru Mungu kwa kuwa hayupo mbali nasi bali yupo katikati yetu. Mzaburi anashukuru Mungu kwa kuwa ijapokuwa yu juu sana bado amemwona myenyekevu. Tunaposali tunajinyenyekesha mbele za Mungu ambaye kwa mapendo na unyenyekevu mkubwa amekuja kwetu, ametwaa hali yetu, ametushirikisha Umungu wake, amekaa kati yetu.

Mungu ni Mwenye haki na huruma kuu
Mungu ni Mwenye haki na huruma kuu   (ED Wien)

Somo la Injili: Ni Injili ya Luka 11:1-13. Somo la Injili Takatifu kutoka Injili ya Luka, Bwana wetu Yesu Kristo anawafundisha wanafunzi wake kusali. Kristo kwa nyakati mbalimbali alisali, aliunganika na Baba yake wa Mbinguni muda wote katika sala. Kabla ya kufanya jambo lolote kubwa, Bwana wetu Yesu Kristo alisali. Na hapa alipokwisha kumaliza kusali, mmoja wa wanafunzi wake anamwomba awafundishe kusali kama vile Yohane alivyowafundisha wanafunzi wake kusali. Yesu anawafundisha Mitume wake SALA YA BWANA. Mtakatifu Thomas wa Aquino anatufundisha kuwa, “Sala ya Bwana ni muhtasari wa Injili yote. Kwa kuwa Bwana, baada ya kufundisha namna ya kusali, alisema mahali pengine, Ombeni nanyi mtapewa. Na kwa kuwa kila mmoja aja haja zake binafsi, basi sala hii ya kawaida na inayofaa hutumika pamoja. Kwa sababu haijalishi ni hitaji gani la mtu binafsi, tunalieleza kwa maneno ya sala hii tukimgeukia Baba ajuaye yote.” Kumbe, Sala ya Bwana ni Sala yenye nguvu. Si tu maneno, bali ni mchoro wa moyo wa Mungu unaochorwa katika roho ya kila anayeomba.  Ni kama ramani ya mbinguni ambapo kila mstari unatuvusha hatua moja karibu na moyo wa Baba. Katika ulimwengu uliojaa kila aina ya kelele, sala hii ni kama tulizo la roho, daima ikitufundisha kupumua ndani ya mapenzi ya Mungu, tukikumbuka kwamba kabla hatujafungua midomo yetu, yeye tayari anajua kilichopo moyoni mwetu. Katika somo hili la Injili dominika ya leo tuna mafundisho mawili makubwa ya kujifunza. Kwanza: Kristo anawafundisha Mitume wake sala ya Bwana. Bwana wetu Yesu Kristo katika kujibu ombi la mmoja wa wanafunzi wake aliyeomba awafundishe kusali, anawafundisha sala ya Bwana ambayo ndani mwake ina maomb yafuatayo; Kwanza: Baba yetu uliye Mbinguni. Kristo aliwafundisha Mitume wake kwamba, msalipo semeni, “Baba yetu uliye Mbinguni” Ombi hili la kwanza katika sala ya Bwana latukumbusha juu ya kiini cha Imani yetu, kwamba Mungu ni Baba yetu wa mbinguni. Ni sala inayotuunganisha sisi sote kama Watoto wa Mungu, kama ndugu kwa kuwa Baba yetu ni mmoja aliye Mbinguni. Yatukumbusha kuwa sala ya Bwana ni sala inayowajumuisha wote, si sala ya kibinafsi, si sala ya kichoyo, ndiyo sababu Yesu hasemi Baba yangu uliye mbinguni bali Baba yetu uliye Mbinguni. Sala hii yatukumbusha juu ya wajibu wetu wa kuikiri Imani yetu kwa Mungu mmoja, katika nafsi tatu, yaani Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Tunamtambua na kumkiri kama Muumba wetu. Pia tunaalikwa kudumu katika umoja, kwa kuwa sote tu Watoto wa Baba mmoja hakupaswi kuwe na mwanya wowote wa utengano. Tusali ili sote tuwe na umoja kama Baba yetu wa mbinguni alivyo katika umoja. Tuombee umoja katika familia zetu, umoja katika kanisa, umoja katika nchi yetu. Tusalipo pia tuwakumbuke na wengine, tusisali kwa ajili yetu tu, sala ina nguvu, tusali na kuombea wengine katika mahitaji yao ya kimwili na kiroho.

Tumieni fursa mbalimbali kutafuta na kuambata utakatifu wa maisha
Tumieni fursa mbalimbali kutafuta na kuambata utakatifu wa maisha

Pili: Jina lako litakaswe. Jina la Mungu ni Takatifu sana, hakuna aliye Mtakatifu kama Mungu wetu (1 Sam 2:2). Tunaposali sala ya Bwana tunatambua Utakatifu wa Mungu wetu na hitaji letu sisi la kujitahidi kuwa watakatifu. Jina lake lapaswa kutukuzwa juu ya vitu vyote, hakuna aliye sawa na Mungu. Hatupaswi kuwa na miungu mingine, hatupaswi kuabudu vitu vingine bali tunapaswa kumwabudu na kumtukuza Mungu peke yake, kwa kuwa ndiye Mungu wa kweli, Mungu wa milele, na jina lake latukuka juu ya dunia yote. Ndugu mpendwa sala ya Bwana yatukumbusha wajibu wetu wa kuutafuta Utakatifu kwa kuwa Mungu wetu ni mtakatifu. Kwa njia ya Mama kanisa Mtakaifu tunapata nafasi ya kutakaswa ili tuweze kujongea mbele ya Mungu wetu aliye Mtakatifu. Kwa njia ya Neno la Mungu na sakramenti za kanisa, tunatakasa fikra zetu, tunatakaza mitazamo yetu kuhusu Mungu, tunakatakasa mioyo yetu ili tuweze kumpokea katika hali ya Utakatifu na uwepo wake ulete mabadiliko ndani mwetu. Tatu: Ufalme wako uje. Ufalme wa Mungu ni utawala wa Mungu kati yetu, utawala wa haki, amani, wema, huruma, upendo nk. Tunaposali sala ya Bwana tunaomba ili ufalme wake uje nasi tuupokee. Kristo amekwisha usimika ufalme wa Mungu kati yetu, ufalme wa haki, amani, wema, sadaka, usawa, huruma, upendo nk. Nasi ndio vyombo vya kuueneza ufalme huo. Tusali na kuomba ili kila mmoja wetu awe tayari kuupokea ufalme wa Mungu ndani ya mioyo yetu na ufalme huo ukue na kuzaa matunda katika maisha yetu ya kila siku. Tuwe watu wa haki, amani, usawa, tuishi upendo wa kweli, tujitoe sadaka, tuwe wapatanishi, wasamehevu nk. Hio ndio namna ya kuiishi sala ya Bwana kwa Matendo. Na baada ya maisha haya tuweze kuuingia mbinguni katika ule mji mtakatifu, Yerusalemu mpya (Ufunuo 21:1-4.) Nne: Mapenzi yako yatimizwe, duniani kama huko mbinguni. Mwenyezi Mungu anatawala kutoka mbinguni, kwa haki na huruma (Isa 30:18). Mapenzi yake ni kwamba tumpende na kumtukuza, na tupendane sisi kama yeye alivyotupenda kwanza. Tunajifunza hili kutoka katika amri kuu ya Mapendo aliyotufundisha Bwana wetu Yesu Kristo (Mt. 22:37-40). Tunaposali sala hii tunajibakabidhi kabisa katika mapenzi ya Mungu na kumwomba Mungu atupe daima nguvu katika kuyapokea na kuyatenda yale tu yaliyo mapenzi yake. Katika furaha, katika huzuni, katika hofu na katika mashaka yetu, tuombe daima tuyapokee yote kwa kuwa ni si mapenzi yetu bali mapenzi ya Mungu yatimizwe. Tano: Utupe leo mkate wetu wa kila siku. Mkate wetu wa kila siku ni yale mahitaji yetu ya kila siku katika maisha yetu. Ombi hili lamaanisha utegemezi wetu kwa Mungu anayejua mahitaji yetu yote ya mwili ya Roho. Mkate wetu wa kila siku kwanza kabisa ni Neno la Mungu ambalo ni chakula cha Roho zetu kwa kuwa mtu hataishi kwa mkate tu bali kwa kila Neno litokalo katika kinywa cha Bwana. Tunaomba kwanza nguvu za kiroho ili tuweze kuimarika katika kutafuta mahitaji yetu mengine mbalimbali ya kimwili. Tunapata nguvu ya kiroho katika sakramenti ya Ekaristi Takatifu, inatupa nguvu ya kuendelea mbele katika safari yetu kama mahujaji hapa duniani.

Sala ni mawasiliano kati ya mwamini na Muumba wake
Sala ni mawasiliano kati ya mwamini na Muumba wake   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Sita: Utusamehe dhambi zetu kwa kuwa sisi nasi tunamsamehe kila tumwiwaye. Ombi hili latukumbusha wajibu wetu wa kuomba huruma ya Mungu kwa ajili ya msamaha wa dhambi zetu. Sisi pia tunapotarajia kupokea huruma na msamaha toka kwa Mungu nasi pia tuwe tayari kuwasamehe wale wanaotukosea. Kristo alituhurumia akatusaheme bila masharti nasi pia tunapaswa kusamehe bila masharti, mara nyingi iwezekanavyo ili nasi tuweze kusamehewa na kuhurumiwa na Mungu. Katika sala yako mwombe Mungu akupe neema ya kusamehe. Saba: Na usituache majaribuni. Majaribu yanatupelekea kuanguka katika dhambi. Mwenyezi Mungu hatutii katika majaribu bali ni sisi kwa akili na utashi wetu wenyewe tunaamua na kuchagua kutenda kinyume na amri na mapenzi ya Mungu. Lakini Mungu wetu ni mwanifu kwa kuwa hatatuacha tujaribiwe kupita uwezo wetu (1 Kor 10:13). Tunamwomba Mungu atuongoze katika njia zetu, atawale Mawazo na matendo yetu ili daima tuwaze na kutenda yale yanayompendeza yeye tu. Nane: Lakini utuopoe na yule mwovu. Ombi hili latukumbusha kuwa mara kadhaa shetani mwovu anatushawishi na kututoa katika njia njema ya kuzishika na kuzifuata amri za Mungu. Tunaposali tumwombe Mungu atupe nguvu za kutambua hila na mitego ya yule mwovu na kukwepa vishawishi vyote vinavyoweza kutuangusha katika dhambi.

Nguvu ya sala kwa ajili ya wengine
Nguvu ya sala kwa ajili ya wengine   (Vatican Media)

Pili: Anawafundisha udumifu na ustahimilivu katika kuomba kwa kuwa Mungu anatusikia. Katika sehemu ya pili ya Injili Yesu anawafundisha Mitume wake juu ya ustahimlifu na udumifu katika kuomba.  Anatoa mfano wa mtu aliyemwendea Jirani yake usiku wa manane akimwomba amkopeshe mikate mitatu kwa kuwa alifikiwa na mgeni na hakua na chochote cha kumpatia. Licha ya kuwa alikataliwa ombi lake, yeye hakusita kuendelea kuomba na kusisitiza, na hatimaye rafiki yake akaamka na kumpatia Kadiri ya alichotaka. Ndivyo tunavyopaswa kwa Mungu wetu. Hatusali leo hii na kupata muda ule ule kila tulichoomba kutoka kwa Mungu. Mungu anafahamu ni muda na wakati gani atatujibu sala yetu bali sisi hatupaswi kuchoka kuendelea kusali na kuomba. Huenda umesali kwa ajili ya amani ya familia yako, usichoke, umeomba kwa ajili ya Watoto wako, usichoke, umeombea kwa ajili ya ajira, kwa ajili ya mitihani unayopitia katika maisha, usichoke. Mungu anafahamu mahitaji yetu yote hata kabla hatujamwomba. Kwa kuwa kama sisi tunafahamu kuwapa Watoto wetu yale yaliyo mema, si zaidi baba yetu aliye mbinguni? Jipe moyo, Mungu anakupenda na atakujibu kwa wakati wake.Somo la Pili: Ni Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai 2:12-14. Mtume Paulo katika somo la pili (Kol 2:12-14) anatufundisha nguvu ya sadaka ya Kristo Yesu, ambaye ni mwombezi na mpatanishi wetu kwa Mungu, kwamba hapo Mwanzo tulikua tumekufa lakini kwa njia ya sadaka yake sisi sote tumefufuliwa na tu hai tena. Kristo anatuombea sisi kwa Baba, ndiye kuhani mkuu anayetufaa sana, anayechukuana nasi katika udhaifu wetu. Hitimisho: Katika Dominika ya leo tumshukuru Mungu, Baba yetu mwingi wa huruma na mapendo, anayetusikia sala zetu kila tunapomwomba kwa moyo mnyofu na unyenyekevu, kwa Imani thabiti bila kuchoka. Tuombe neema ya kutambua umuhimu na nguvu ya sala na kudumu katika muungano na Mungu Baba yetu, Mungu anayefahamu mahitaji yetu yote hata kabla hatujamwomba. Tuombe neema ya kumshukuru Mungu kila wakati na kukumbuka kuwaombea pia wengine katika sala zetu.

Tafakari D 17
25 Julai 2025, 18:05