杏MAP导航

Tafuta

Sala ya Baba Yetu ni Muhtasari wa Injili yote. Hii ni Sala ya Bwana "Oratio Dominica." Sala ya Baba Yetu ni Muhtasari wa Injili yote. Hii ni Sala ya Bwana "Oratio Dominica."  (@Vatican Media)

Tafakari Dominika 17 ya Mwaka C wa Kanisa: Nguvu na Umuhimu wa Sala

Mwamini anapaswa kujifunza namna ya kusali vyema, akidumu katika sala, kama inavyojidhihirisha katika Liturujia ya Neno la Mungu, kwa Dominika ya 17 ya Mwaka C wa Kanisa. Sala inaweza kupata chimbuko lake kutoka katika Maandiko Matakatifu, Liturujia ya Kanisa na fadhila za Kimungu. Familia ya Kikristo ni mahali pa kwanza kwa ajili ya malezi ya sala. Ikiwa juu ya msingi wa Sakramenti ya Ndoa, Familia ni Kanisa dogo la nyumbani mahali pa kujifunza sala na tafakari.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 17 ya Mwaka C wa Kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe mahususi wa masomo ya dominika hii umejikita katika nguvu ya sala ya mwenye haki inayotoka ndani ya moyo wake, isiyo na hila wala mawaa, na umuhimu wa kusali bila kuchoka tukimwomba Mungu Baba yetu, kwa upendo wake atujalie mahitaji yetu ya kila siku. Mwamini anapaswa kujifunza namna ya kusali vyema, akidumu katika sala, kama inavyojidhihirisha katika Liturujia ya Neno la Mungu, kwa Dominika ya 17 ya Mwaka C wa Kanisa. Sala inaweza kupata chimbuko lake kutoka katika Maandiko Matakatifu, Liturujia ya Kanisa na fadhila za Kimungu. Familia ya Kikristo ni mahali pa kwanza kwa ajili ya malezi ya sala. Ikiwa juu ya msingi wa Sakramenti ya Ndoa, Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, ambamo watoto wa Mungu wanajifunza kusali katika Kanisa na kudumu katika sala. Huu ni ushuhuda wa wa kwanza wa kumbukumbu hai ya Kanisa inavyoamshwa na utulivu wa Roho Mtakatifu. Ikumbukwe kwamba, sala ni zawadi ya neema na jibu la uamuzi kwa upande wa mwamini. Sala daima inadai juhudu za makusudi. Kusali si lelemama wala maji kwa glasi kuna vikwazo na vishawishi vyake, vinavyopelekea hata wakati mwingine mwamini akashindwa kusali vyema. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, mwamini hafungulii mlango wa uzembe katika maisha yake ya sala na kwamba, sala na maisha ya kikristo ni chanda na pete. Sala ya Baba Yetu ni muhtasari wa Injili yote, ni Sala ya Bwana, "Oratio Dominica". Kutokana na mwelekeo huu, Yesu anakuwa kweli ni mwalimu na kielelezo cha sala kinachosimikwa katika majadiliano kati ya mwamini na Muumba wake.

Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa
Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa   (ANSA)

Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna wazazi wake Bikira Maria, inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Julai. Hii ndiyo familia ambamo Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa amechota fadhila mbalimbali zilizomwezesha kupata upendeleo wa pekee mbele ya Mwenyezi Mungu, kiasi cha kukingiwa dhambi ya asili na hatimaye, kupalizwa mbinguni mwili na roho, kama tunda la kwanza la kazi ya ukombozi. Kumbe, Ibada na heshima kwa watakatifu Joakim na Anna ni mwendelezo wa Ibada kwa Bikira Maria na hatimaye, Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Mama Kanisa daima anapenda kuwambusha watu watakatifu na wateule wa Mungu kwamba, Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Wazazi wake Bikira Maria, wanaonesha umuhimu wa familia kama shule ya upendo, imani na utakatifu wa maisha. Kumbukumbu hii ni muhimu sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu kwani ni fursa ya kuwashukuru na kuwabariki wazee kutokana na mchango wao katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia.

Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kuombea utunzaji bora nyumba ya wote
Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kuombea utunzaji bora nyumba ya wote   (@Vatican Media)

Ni katika muktadha huu wimbo wa mwanzo unaofungua maadhimisho ya dominika hii unasema; “Mungu yu katika kao lake takatifu. Mungu huwakalisha wapweke nyumbani. Yeye huwapa watu wake nguvu na uwezo” (Zab. 68:5-6). Na Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali kwa matumaini haya akisema; “Ee Mungu, wewe ndiwe mlinzi wa wenye kukutumaini; pasipo wewe hakuna lililo thabiti, hakuna lililo takatifu. Utuzidishie huruma yako; utusimamie, utuongoze. Na sasa tutumie vema mambo ya dunia, hali tumeambata na ya milele”. Somo la kwanza ni la kitabu cha Mwanzo (Mw. 18: 20-32). Ujumbe wake unahusu nguvu ya sala ya mtu mwenye haki. Ibrahimu baba wa imani, mtu mwenye haki, anasali na kuomboleza kwa sababu ya dhambi za watu wa Sodoma na Gomora ili Mungu asiwaangamize wenye haki waliopo katika miji hii pamoja na wenye dhambi. Masimulizi ya maandiko matakatifu yanasema kuwa miji hii iliangamizwa kwa sababu hakupatikana mtu mwenye haki ndani mwake. Mababa wa Kanisa wameliona tukio hili kama utabiri wa kukombolewa watu wote na “mwenye haki mmoja, Yesu Kristo” (1Yn. 2:1), kutoka hasira inayokuja (1Tm. 1:10), inayosababishwa na dhambi za watu. Maandiko matakatifu yanatufundisha kuwa, dhambi humtenga mtu na Mungu na kupoteza urafiki wake naye, anakuwa mbali naye na kupoteza uhusiano mwema naye. Hivyo katika hali ya dhambi, sala na maombi yake yanakosa kibali machoni pa Mungu. Nabii Isaya anasema; “Dhambi zenu ndizo zinazowatenga na Mungu, dhambi zenu zimemfanya Mungu ajifiche mbali nanyi hata asiweze kuwasikieni” (Isa. 59:2). Dhambi humtenga mtu na wengine na huathiri mahusiano yake na wengine. Aidha, tunapowadhuru wengine kwa mwenendo wetu mbaya tunamgusa pia Mungu, kwani kila mtu ameumbwa kwa sura na mfano wake. Zaidi sana, dhambi humtenga mtu na nafsi yake mwenyewe, na kumfanya kupoteza hadhi ya kuwa mtoto wa Mungu, na kuwa mwana mpotevu (Lk. 15). Maisha mazuri, furaha na amani vinapotea kwa mwenye dhambi. Taabu, mateso na mahangaiko vinamuandama, hata magonjwa na maumivu ya kimwili yanatokea, kama dalili tu za uozo uliomo ndani mwake, mtu anakuwa mkorofi, mgomvi, msingiziaji. Mwisho wa yote huingia kifo cha mwili na cha roho maana mshahara wa dhambi ni mauti (Rm. 6:23; Lk. 15:32).

Tafuteni mahali faragha ili kuweza kusali vyema.
Tafuteni mahali faragha ili kuweza kusali vyema.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kama Ibrahamu baba wa imani, mtu mwenye haki alivyosali kuiombea miji ya Sodoma Gomora isiangamizwe kwa dhambi zake, vivyo hivyo nasi tunapaswa kusali na kujiombea sisi wenyewe kwa dhambi zetu na za wengine ili tusiangamizwe nazo. Lakini ili sala zetu zisikilizwe yatupasa kujipatanisha kwanza na Mungu, kutubu dhambi zetu, kujipatanisha na wenzetu, kutoa msamaha kwa waliotukosea, kufanya malipizi, na kujisamehe sisi wenyewe. Tukifanya hivyo, tutakapomlilia Mungu, atasikia kilio chetu na kutuokoa. Ni katika muktadha huu Zaburi ya wimbo wa katikati inasema hivi; “Siku ile niliyokuita uliniitikia, ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu. Nitakushukuru kwa moyo wangu wote, mbele ya miungu nitakuimbia zaburi. Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu. Nitalishukuru jina lako, kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako, kwa maana umekuza ahadi yako, kuliko jina lako lote. Siku ile niliyokuita uliniitikia, ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu. Ingawa Bwana yuko juu, amwona myenyekevu, naye amjua mwenye kujivuna tokea mbali. Nijapo kwenda kati ya shida utanihuisha. Utanyoosha mkono wako juu ya hasira ya adui zangu. Na mkono wako wa kuume utaniokoa. Bwana atanitimiliza mambo yangu; Ee Bwana, fadhili zako ni za milele; usiziache kazi za mikono yako” (Zab. 137 ; 1-3, 6-9).

Papa Francisko alipenda kusali na watu wa Mungu katika maisha na utume wake
Papa Francisko alipenda kusali na watu wa Mungu katika maisha na utume wake

Somo la Pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai (Kol 2: 12-14). Na ujumbe wake ni huu; kwa ubatizo, mkristo anakuwa sehemu ya mwili wa Kristo yaani Kanisa. Kama vile tohara, katika Agano la Kale, ilivyokuwa alama ya kuwa mshiriki wa taifa teule, vivi hivi ubatizo hutufanya washiriki wa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, ambaye ameifuta hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui wetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomelea msalabani. Ukombozi huu ni wa thamani sana kwa maana tumekombolewa “si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu… bali kwa damu ya thamani ya mwana-kondoo asiye na hila, asiye na waa, yaani, Damu ya Kristo” (1Pet 1:18-19).  Hivyo yatupasa tuwe kielelezo chake, katika maisha yetu ya kila siku kwa maneno na matendo mema, hata katika mateso. Injili ni kama ilivyoandikwa na Luka (Lk 11:1-13). Ujumbe mahususi wa sehemu hii ya Injili ni umuhimu wa sala na namna tunavyopaswa kusali. Yesu Kristo, ni mwalimu na kielelezo cha mtu wa sala. Injili zinashuhudia jinsi alivyojikita katika sala kabla ya kufanya jambo lolote muhimu. Daima alienda mahali pa faragha hasa milimani nyakati za usiku ili kusali – kabla ya kubatizwa na Yohani mtoni Yordani, alisali (Lk 3:21), kabla ya kuwachagua mitume 12, alikesha akisali (Lk 6:12), alisali kumwombea Petro, ili akiisha kukomaa katika Imani awaimarishe na wenzake (Lk 22:32), aligeuka sura akiwa katika kusali (Lk 9:27-28), alisali Wagiriki walipoomba kumuona (Yn 12:27-28), kabla ya kumfufua Lazaro, alisali (Yn 11:41-42), wakati wa karamu ya mwisho, alisali sala kuu ya kikuhani (Yn 17), kabla ya mateso na kifo cha msalaba, alikwea mlimani kusali (Mt 26:39-42), na akiwa msalabani kabla ya kifo chake, alisali akiwaombea watesi na wauaji wake (Mt 27:46). Mitume walipomuona alivyokuwa mtu wa sala, walitoa ombi kwake awafundishe na wao kuwali. Kisha Yesu akawafundisha sala ya Baba Yetu. Katika sala hii, Yesu anatufunulia kuwa Mungu ni Baba yetu, anatupenda na kutujali. Hivyo kila tunalomwomba kwa imani na matumaini anatujalia. Katika sala hii, tunaposali tujue kuwa kila tunaloliomba, Mungu Baba alishatupatia kwa njia ya Mwanaye mpendwa Bwana wetu Yesu Kristo – Yeye amelitukuza jina la Mungu Baba, ameufikisha ufalme wake duniani kama ulivyo mbinguni, ametujalia Ekaristi Takatifu, mkate wetu, chakula chetu cha kiroho, ametupatanisha na Mungu Baba kwa kutusamehe dhambi zetu, na kutukinga na mwovu shetani. Hivyo tunaposali, hatuna budi kufungua mikono na mioyo yetu kupokea kile tunachokiomba.

Sala ya Baba Yetu ni muhtasari wa Injili
Sala ya Baba Yetu ni muhtasari wa Injili   (ED Wien)

Tukumbuke kuwa sala ni tendo la imani la kuongea na Mungu. Katika mazungumzo haya kuna pande mbili. Binadamu anapoongea, Mungu anasikiliza, na Mungu anapoongea, mwanadamu anapaswa kusikiliza. Kumbe katika sala tukiongea tu bila kumsikiliza Mungu, tunashindwa kupokea tunachoomba. Mtume Yakobo anasema; “Mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya na mnaomba ili mpate kutosheleza tamaa zenu” (Yk. 4:3). Maandiko matakatifu yanasimulia kuwa Waisraeli walipokuwa jangwani, kila asubuhi, Mwenyezi Mungu aliwapatia Manna. Na aliwapa maagizo kuwa wanapaswa kuokota kinacho watosha tu kwa siku na sio zaidi. Lakini baadhi yao walijilimbikizia kuliko kile walichohitaji kwa siku. Ilitokea kuwa kile cha ziada walichojikusanyia na kujilimbikizia kilioza (Kut 16:19-21). Hali hii iliwafanya watambue kwamba wanapaswa kuweka matumaini yao kwa Mungu naye atawajalia kila wanapohitaji na wasiwe na ubinafsi wa kujilimbikizia na wawe wasikivu, wamsikilize Mungu anapoongea nao na kuwapa maelekezo. Nasi daima tunaposali, tusali kwa unyenyekevu, tumruhusu Mungu atimize mpango wake katika maisha yetu, tusimpangie chochote. Tujibidishe kusali, kuombea kila jambo katika shughuli zetu za nyumbani na sehemu zetu za kazi, asubuhi, jioni, kabla na baada ya kulala. Tushiriki sala za Jumuiya kwa maana Yesu alisema; “wakusanyikapo wawili au watatu kwa jina langu mimi nipo kati kati yao, na lolote watakalomwomba Baba kwa jina langu atawapatia” ikiwa ni pamoja na kuurithi uzima wa milele. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali; “Ee Bwana, tunakuomba upokee vitu hivi ulivyotukirimia ambavyo tunakutolea. Nayo mafumbo haya matakatifu yatutakase hapa duniani kwa nguvu ya neema yako, na kutufikisha kwenye furaha za milele”. Na katika sala baada ya Komunio anapohitimisha maadhamisho haya anasali hivi; “Ee Bwana, tumepokea sakramenti takatifu iliyo ukumbusho wa siku zote wa mateso ya Mwanao. Tunakuomba sakramenti hii aliyotujalia Mwanao kwa mapendo makuu, ituletee wokovu.” Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari D 17
23 Julai 2025, 17:14