Tafakari Dominika 16 ya Mwaka C wa Kanisa: Ukarimu na Mungu Apewe Kipaumbele cha Kwanza
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya 16 ya mwaka C wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatutafakarisha kuwa, “Ukarimu ni chanzo cha baraka, tumpe Mungu nafasi ya kwanza” Mwenyezi Mungu ni Mungu anayehusiana nasi, hayupo mbali bali yupo daima karibu nasi. Anakuja kwetu katika hali ya kawaida, anajidhihirisha kwetu katika nyakati mbalimbali, katika mazingira, na watu wa kawaida kabisa. Wajibu wetu wa kwanza ni kumpokea, kwa upendo, utii, unyenyekevu na ukarimu, katika Neno lake, katika Sakramenti na katika nafsi za wenzetu. Pili ni kumsikiliza na kukaa miguuni pake, kujifunza kutoka kwake yale tunayopaswa kuwaza, kusema na kutenda kwa ajili ya Mungu na kwa ajili ya wengine. Matokeo ya hayo, Mwenyezi Mungu atatimiza kwetu Agano na ahadi zake, atatenda makubwa maishani mwetu kama alivyotenda kwa Ibrahimu na Sara na kama alivyotenda kwa Marta na Maria na Lazaro, ambao walimpa Mungu nafasi, walimkaribisha Mungu nyumbani mwao. Tuombe neema ya kufungua milango, kwanza kabisa mioyo yetu. Tuwapokee wote wanaohitaji msaada wetu wa hali na mali, wageni, wagonjwa, wazee, yatima, wajane, watoto wa mitaani, wafungwa, maskini, waregevu nk, ndivyo Mungu anavyokuja nyumbani kwangu na kwako. Mwisho, tujinyenyekeshe daima kwa Kristo na tujifunze daima kutoka kwake ili tuweze mwisho wa maisha yetu kustahililishwa kuingia katika hema yake, baada ya maisha haya ya kupita ya hapa duniani.
Somo la Kwanza: Ni kitabu cha Mwanzo 18:1-10. Somo la kwanza ni kutoka katika kitabu cha Mwanzo, Mwenyezi Mungu alimtokea Ibrahimu kwa njia ya watu watatu wageni karibu na Mialoni ya mamre alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake. Ilikua ni desturi katika jamii ya Wayahudi kuwapokea, kuwakirimu na kuwatendea fadhila wageni (hachnasat orchim, Rej. Mwa 18, Kut 22:12, Kum 10:19). Wageni katika jamii za wafugaji katika kipindi hicho walichukuliwa kuwa ni watu walioleta habari Njema kutoka kwa Mungu au miungu (kwa kuwa si wote waliokua na imani kwa Mungu wa Israeli). Hivyo, Ibrahimu anawapokea na kuwatendea wema na ukarimu mkubwa watu hawa watatu waliofika nyumbani kwake. Kwa kupitia ukarimu huo, Mwenyezi Mungu anathibitisha tena ahadi alizonena na Ibrahimu wakati alipomwita na kufanyua naye Agano kwa mara ya kwanza katika (Mwa 12). Anamwahidi kuwa, mkewe Sara atapata mwana, licha ya ahadi hiyo kibinadamu kuonekana kuwa ni ngumu kutimilika. Kumbe tunapomkaribisha kumpokea na kumsikiliza Mungu katika upendo na ukarimu, anatenda na kutimiza kwetu mambo makubwa hata yale ambayo sisi kwa akili na uwezo wetu wa kibinadamu tunaweza kuona hayawezekaniki.
Ndugu zangu katika somo hili la kwanza tuna mambo mawili ya kujifunza. Kwanza: Mungu anakuja kwetu katika hali na mazingira ya kawaida kabisa, tumkaribishe. (Divine Presence in Ordinary encounters). Katika somo hili la kwanza, Mwenyezi Mungu anamtokea Ibrahimu katika hali na mazingira ya kawaida kabisa. Anamtokea kwa njia ya watu watatu wageni waliomfikia Ibrahimu akiwa karibu na mialoni ya Mamre. Mwenyezi Mungu hamtokei Ibrahimu katika kichaka cha moto, wala katika radi, wala katika tetemeko la ardhi, wala katika upepo, wala katika miale ya moto. Anamtokea kwa kupitia wageni watatu. Wageni watatu wamwelezea Mungu aliye katika nafsi tatu, Mungu aliye katika jumuiya, Mungu anayehusiana daima nasi. Mungu anasema nasi kwa njia hiyo hiyo katika matukio mbalimbali ya maisha yetu. Anasema nasi; Kwanza: Katika Neno lake: Ndugu mpendwa, Mwenyezi Mungu wetu hayupo mbali nasi. Anakuja kati yetu katika hali ya kawaida kabisa. Amesema nasi kwa njia ya Mwanaye Yesu Kristo, Neno wake, aliyetwaa mwili na akakaa kati yetu. Kristo anabisha hodi ndani ya moyo wangu kila siku, katika Neno lake. Anatuambia kuwa, “Mtu akinipenda atalishika Neno langu, na Baba yangu atampenda nasi tutakuja kwake” (Yn 14:23). Kristo katika Neno lake, anatamka kwetu neema na baraka alizoandaa kwa ajili yetu, anatamka kwetu utimilifu wa Ahadi za Mungu alizonena nasi, atatufariji wakati wa shida na mahangaiko yetu mbalimbali katika maisha yetu ya ufuasi. Neno lake linatuinua pale tunapokata tamaa, pale tunapopoteza matumaini na kuanguka chini kabisa, Neno lake linatuponya majeraha yetu, Neno lake linatuonya na kutukumbusha kutimiza wajibu wetu kwa Mungu, kwa Kanisa, kwa jamii, kwa familia, katika utume wetu, kwa kuhudumia kwa haki, upendo, amani, wema, ukweli na uwajibikaji nk.
Pili: Katika Sakramenti mbalimbali za kanisa. Kristo anasema nasi katika Sakramenti zake. Yupo kati yetu katika Ekaristi Takatifu, Mwili wake na Damu yake Azizi, Roho na Umungu wake, katika kila adhimisho la ibada ya misa takatifu. Anatupa nafasi ya kumpokea ili akae nasi, aingie na kukaa ndani ya mioyo yetu, aguse hali zetu mbalimbali tunazopitia, atuondolee hofu zetu, mashaka yetu, huzuni, kukata tamaa kwetu, masikitiko yetu, na udhaifu wetu mbambalimbali, atuponye, aponye majeraha yaliyo ndani ya mioyo yetu. Mara kadhaa tunakuwa na makovu ya majeraha ya matukio mbalimbali yaliyotokea katika maisha yetu, huenda ni katika familia, katika kazi, katika mahusiano, katika famili nk. Kristo anakutembelea, anakuja kukuponya, anakuja kukugusa na kuyaponya majeraha yako ya zamani na ya sasa. Fungua moyo wako, mpokee Yesu na umwombe akuguse na kukuponya katika nia zako mbalimbali kila mara unapopata nafasi ya kumpokea. Jenga urafiki na Yesu, na Yesu rafiki mwema atafanya makazi ndani ya moyo wako. Tatu: Katika kusanyiko la sala: Mungu anazungumza nasi katika kusanyiko la sala. Tuaposali tumamwalika Mungu kati yetu. Kristo anatufundisha kuwa, “Kwa kuwa waliopo wawili au watatu kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao” (Mt. 18:20). Ndugu mpendwa, sala inatuleta karibu kabisa na Kristo, sala inajenga urafiki kati yetu na Mungu, anakuja kwetu na kufanya makao kwetu. Tusipojenga urafiki ya Mungu kwa njia ya sala ni wazi kabisa tutakua mbali naye na hatimaye tutakua mbali na wenzetu. Mkaribishe Yesu nyumbani mwako, mkaribishe katika ndoa yako, mkaribishe katika kazi zako za kila siku, mkaribishe katika masomo yako, mkaribishe katika biashara zako, mkaribishe katika hali zako zote. Tukiwa karibu naye naye atakua karibu nasi.
Nne: Katika nafsi za wengine: Mwenyezi Mungu anakuja kwetu katika nafsi ya watu wengine, wagonjwa, wazee, wajane, yatima, maskini, wasiojiweza, wafungwa, wakimbizi nk. Tuna kila sababu ya kuwapokea na kuwasadia wale wote wanaoteseka kwa namna mbalimbali kwa kuwa kwa kufanya hivyo tunampokea Kristo mwenyewe. Kristo anatufundisha kuwa lolote mnalomtendea mmoja wapo wa watumishi wangu walio wadogo, mmenitendea mimi, kwa maana nalikua na njaa, nalikua na kiu, nalikua kifungoni, nalikua uchi, nalikua mgeni nk. Tunaposhindwa kuona na kuguswa na shida za wengine hatuwakatai na kuwaumiza tu hao bali tunatenda hivyo, na kumuumiza hivyo Kristo ambaye anajitambulisha kwetu daima katika nafsi za watu hao. Ndugu mpendwa tuombe neema ya kumtambua Kristo anaposema nasi kupitia nafsi za wengine. Nyosha mkono wako, tenda kwa ukarimu, pokea, hudumia bila kujali malipo na sadaka, kwani thawabu yake ni kubwa mbinguni.
Tano: Katika nafsi ya Padre: Kristo yupo kati yetu katika nafsi ya kuhani, ambaye anatolea sadaka katika nafsi ya Kristo (persona Christi) katika adhimisho la ibada ya Misa Takatifu, yaani adhimisho la Ekaristi Takatifu. Pia ni kwa njia ya Padre, tunapata nafasi ya kushiriki sakramenti nyingine mbalimbali za kanisa, ubatizo, mpako wa wagonjwa, ndoa, pamoja na huduma nyingine mbalimbali kwa ajili ya ustawi wa roho zetu. Ni kwa njia ya Padre, Kristo anabaki daima katikati yetu katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu katika Tabernaklo. Kristo ametupatia yote tunayohitaji ili tuwe karibu naye, ili tujenge urafiki naye, ili akae kwetu nasi tukae ndani mwake na tuupate uzima wa milele. Pili: Matokeo ya ukarimu ni utimilifu wa baraka za Mungu. Ibrahimu aliwatendea kwa wema watu wa Mungu, kwa kuwakaribisha na kuwahudumia kwa upendo na fadhila. Watu hawa mwisho wanatangaza mpango aliokuwa nao Mungu tangu mwanzo kwa Ibrahimu kwamba, mkewe Sara atapata mtoto. Ni mpango ambao Mungu alishanena na Ibrahimu wakati alipomwita na akarudia tena alipofanya naye Agano (Mwa 12:2-3, 15:5,17:4-5). Alichonena na Ibrahimu sasa anakwenda kukitimiza. Ndugu mpendwa, sisi nasi tunapokubali kumpokea Mungu anapokuja kwetu kwa njia mbalimbali, tunapokea neema na baraka zake, tunapokea ujumbe wa baraka na matumaini, tunapokea uzima na uhai, tunapokea mwanzo wa maisha mapya. Ibrahimu anatangaziwa habari Njema, habari ya furaha kwamba sasa Mungu anakwenda kutimiza yote aliyonena naye. Kibinadamu ilikua ni ngumu sana kuelewa na kuamini kwamba Sara angeweza kuapata mtoto kwa wakati ule lakini baraka za Mungu zinavunja mipaka ya asili. Ndugu mpendwa, Mungu anapokuja kwako anabadili historia yako. Anabadili aibu yako kuwa heshima, vile alivyobadili aibu ya Sara kuwa heshima. Anabadili huzuni yetu kuwa furaha na kicheko, anabadili udhaifu wetu kuwa nguvu na ushindi, anabadili hofu zetu kuwa ujasiri. Yesu ninakuomba ufungue macho na akili yangu, ili nikutambue unaposema na moyo wangu, unapokuja na kutafuta makazi kwangu katika hali, nyakati, watu na mazingira mbalimbali katika maisha yangu. Usiache baraka za Mungu zikapita kwa kukosa ukarimu na utayari wa kumpokea.
Wimbo wa katikati: Ni kutoka katika zaburi ya 15. Itakumbukwa kwamba, Zaburi ya 15 ni moja kati ya Zaburi zinazojulikana kama zaburi ya kuingia Hekaluni Yerusalemu (Entrance liturgy). Zaburi hizi ziliimbwa wakati watu walipofanya hija kuja Hekaluni Yerusalemu kwa ajili ya sikukuu kubwa katika dini ya Wayahudi. Katika hija hiyo watu walipanda kueleka mlima Sayuni lilipokuwa limejengwa hekalu la Yerusalemu. Walipofika katika lango la hekalu ndipo zaburi hizi ziliimbwa. Mzaburi anauliza swali, Bwana ni nani atakayekaa katika hema yako? Ni nani atakayefanya maskani katika kilima chako kitakatifu? Hapa anataja sifa za mtu anayestahili kuupanda mlima wa Bwana na kuingia katika hema ya Bwana, yaani katika uwepo wa Mungu wetu. Kwanza: Ni yeye aendaye kwa ukamilifu: kwenda kwa ukamilifu ni kuishi kwa kuzifuata kwa uaminifu mkubwa amri na maagizo ya Mungu. Kuliishi Neno la Mungu na kuziishi amri zake katika matendo. Kama ilivyokuwa kwa wayahudi walipokuwa katika hija kueleka kupanda mlimani kwa Bwana, na kuingia katika hekalu lake, sisi pia hapa duniani tupo safari, tupo katika hija kama mahujaji wa matumaini tunaoelekea mlimani Sion, katika mlima wa Bwana, katika Hekalu la Mungu wetu. Ndugu mpendwa, kila mmoja ajiulize kwa nafasi yake, katika hija yake, je nimeishi kwa ukamilifu kiasi gani amri za Mungu? Je nimekua mtu wa kuzishika amri za Mungu lakini hazina uhusiano wowote na maisha yangu ya kila siku? Mimi ni Mkristo, nimebatizwa lakini bado sina upendo, sina huruma, sina ukarimu, sijitoi sadaka nk. Nikiishi kweli kwa ukamilifu nitapata nafasi ya kuingia katika hema ya Bwana, kupanda mlimani mwake yaani kuurithi uzima wa milele. Pili: Kutenda haki na kusema ukweli: Mzaburi anatupa sifa ya pili kwamba anayestahili kupanda mlima wa Bwana na kuingia patakatifuni pake ni yule anayetanda haki na kusema ukweli.
Ndugu mpendwa katika safari yetu kama mahujaji wa matumaini, tunaalikwa kuwa mabalozi wa haki na ukweli. Ukweli daima unatuweka huru, na haki ndio tunda la amani ya kweli. Kila mmoja ajiulize, je nimekua imara kiasi gani katika kusimamia haki na ukweli? Je nimekandamiza haki na na kufukia ukweli ili nifanikishe nia na malengo yangu binafsi? Katika famili zetu, katika kazi zetu, katika mahusiano yetu, katika jamii yetu, katika nchi yetu nk, nimekua mkweli kiasi gani? Nimetenda haki kiasi gani? Tumwombe Mungu atupe nguvu daima ya kusema ukweli na kusimamia haki. Tatu: Kutosingizia kwa ulimi wetu, wala kuwatendea wengine mabaya: Mahujaji wa matumaini tunaalikwa kutumia vyema vivnywa vyetu, kwa kutosingizia mtu kwa ndimi zetu wala kuwatendea wengine mabaya. Kutumia ndimi zetu katika kusema na kutangaza mema na mazuri ya wengine. Ndugu mpendwa, kila mmoja ajiulize ninatumiaje ulimi wangu? Je ninautumia katika kusema na kutangaza mema na mazuri ya wengine au nimetumia ulimi wangu katika kuwauwa wengine kwa maneno mabaya, kwa kuwasingizia uwongo, kwa kuwazushia na kuwasingizia mabaya? Tutumie vinywa vyetu katika kumsifu na kumtukuza Mungu aliyetupenda na kuamua kuakaa nasi, tutumie vinywa vyetu kuwapokea wengine na kuwafariji kwa maneno ya faraja yenye kutia moyo, tutumia vinywa vyetu kuwatetea wale wasio na watetezi, tutumia vinywa vyetu kutangaza wema, ukuu na uweza wa Mungu wetu. Nne: Yeye asiyetoa rushwa ili kuwaangamiza wasio na hatia. Mzaburi anatufundisha kuwa yeye ambaye hakutoa fedha yake ili apate kula riba, asiyetoa rushwa ili kuwaangamiza wasio na hatia, huyo ataingia katika hema ya Mungu. Ndugu mpendwa, rushwa imekua chanzo kikubwa sana cha ukosefu wa haki, au ukandamizwaji wa haki hasa kwa wale walio wadogo, maskini na wanyonge. Kristo alishatufundishwa kwamba kuwa kutenda hivyo tunapoteza nafasi ya kukaribishwa na Kristo, wale waliobarikiwa na Baba yake kuurithi uzima wa milele. Nasi tulio mahujaji wa matumaini tunapaswa kujiepusha na vitendo vyovote vya rushwa na uporwaji wa haki za wengine. Tujiepushe kutafuta faida kupitia dhuluma na unyanyasaji kwani kwa kufanya hivyo tunapoteza neema na baraka za Mungu katika maisha yetu. Tuombe neema ya kuwa imara katika kutenda tu yale yampendezayo Mungu.
Somo la Injili: Ni Injili kama ilivyoandikwa na Luka 10:38-42: Somo la Injili Takatifu kutoka Injili ya Luka, Martha dada ya Lazaro na Maria anamkaribisha Yesu nyumbani na anamhudumia kwa ukarimu mkubwa. Martha, Maria na Lazaro walikua ni marafiki wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kristo akiwa safarini kuelekea Yerusalemu, alipofika Bethania alikaribishwa na Martha nyumbani kwao. Hili lilikua ni tendo kubwa na la ukarimu mkubwa kwa wageni katika tamaduni za Wayahudi. Maria, dada yake na Martha anakaa miguuni pa Yesu, Rabi, Mwalimu, anamsikiliza na Marta yeye anajishughulisha na shughuli mbalimbali kwa ajili ya Yesu, mgeni aliyewatembelea. Katika Injili hii Yesu anamkaripia Martha ambaye alilalamika kukosa msaada kutoka kwa Maria, si kwa sababu alishughulika kwa ajili yake kama mgeni, bali ni kwa sababu alijushughulisha na mambo yaliyohusu mwili tu badala ya kutenga muda pia kukaa miguuni pa Yesu na kusikiliza habari za wokovu wa roho. Kumbe nasi tunaalikwa kuweka mambo yote katika mzani. Kuwa martha anayekaa miguuni pa Yesu, na Maria anayehudumia, yaani kumsikiliza Yesu kwanza kisha kwenda kutenda. Hatupaswi kusikia neno la Mungu tu bila kwenda kuhudumia (diakonia) kwa upendo, sadaka, na ukarimu na huruma, wala hatupaswi kujihusisha tu na huduma bila kuwa na muda wa kukaa miguuni pa Yesu.
Katika somo hili la Injili dominika ya Kumi na sita ya Mwaka C wa Kanisa tuna mafundisho manne ya kujifunza: Kwanza: Tujenge urafiki na Yesu, atatutembela, atakaa kwetu. Bwana wetu Yesu Kristo katika maisha na utume wake, alifika mara kadhaa nyumbani kwa akina Martha, Maria na Lazaro. Walijenga urafiki na Yesu na hata kaka yao Lazaro alipofariki, Yesu alikwenda na alimfufua. Ni kwa njia ya upendo na ukarimu, familia hii walimkaribisha Yesu na kujenga urafiki naye. Kristo anawakumbuka wakati wa shida na changamoto zao. Ndugu mpendwa, Kristo anakuja kwetu kila siku, kwa namna mbaimbali na kwa njia nyingi. Anasema nasi katika nyakati mbalimbali, anabisha hodi ili tumfungulie mlango na akae ndani mwetu nasi ndani yake, apate makazi ndani ya mioyo yetu. Tumpe muda wetu, tumpe mioyo yetu, kwa njia ya sala na sakramenti mbalimbali, kwa njia ya neno lake, anakuwa daima karibu nasi. Tujenge urafiki naye kwa kuwapokea wale wote wanaohitaji msaada wetu wa hali na mali, maskini, wanyonge, yatima, wajane, waliotengwa na jamii, walio magerezani, wagonjwa mahospitalini na majumbani. Yesu akiwa rafiki Yetu tunakuwa na ujasiri wa kumkumbusha kila mara yale yote ambayo tunahitaji katika maisha yetu. Ninakua na ujasiri na nguvu ya kumwambia, Yesu, tazama familia yangu, ninakuomba uwakumbuke watoto wangu, ninakuomba ukumbuke afya yangu, huenda ni magonjwa ya muda mrefu au ni kushindwa katika kutimiza mafaniko yetu, mkumbushe Kristo rafiki mwema, aliyekupenda akaja kwako, akafanya makao kwako.
Pili: Kipaumbele chetu kiwe kwanza kulisikia Neno la Mungu. Martha alimkaribisha Bwana wetu Yesu Kristo lakini hakupata nafasi ya kukaa miguuni pa Yesu na kusikiliza Neno lake. Alijishughulisha na shughuli nyingi kwa ajili ya Kristo Mgeni wao hata akaanza kulalamika kwamba Maria alimwacha kutumika peke yake. Kristo anamuonya kwa upole. Katika tamaduni za kiyahudi, kitendo cha kuita mara mbili, “Martha, Martha” kinatafsirika kama namna ya upole na urafiki ya kuelekeza au kuonya. Kristo anamwonya Martha sio kwa kuwa alifanya vibaya kumhudumia bali ni kwa sababu Martha alijishughulisha na shughuli nyingi na hakutoa kipaumbele kwa neno la Kristo. Ndugu mpendwa, huenda nasi tumekuwa na shughuli nyingi na kusahau kutoa muda kwa ajili ya kukaa miguuni pa Yesu, kumsikiliza, ili aweze kutufundisha yale yatupasayo kutenda. Je, kipaumbele/Priority zangu ni zipi? Pengine nimekosa muda kwa ajili ya kushiriki ibada ya Misa Takakatifu kwa sababu ya kazi zangu na biashara zangu za kila siku, nimekosa muda kukaa na Yesu katika Ekaristi Takatifu walau saa moja, kumshirikisha Yesu maisha yangu, mafanikio yangu, changamoto zangu, huzuni zangu, na kushindwa kwangu kwa sababu ya kujishughulisha na mambo mengi ya kidunia na ya kimwili. Yesu anatupenda sana, anatuita mara mbili kama alivyomwita Martha. Anatuita kwa upendo na upole ili aseme nasi, ili atupe neno la Faraja, Neno la uzima wa milele, neno la matumaini mapya, Neno la kutia moyo. Huenda umejishughulisha na mambo mengi peke yako, kwa nguvu zako, akili na maarifa yako, huenda ni malezi ya Watoto na familia yako, huenda ni biashara zako za kila siku, au kazi yako, au wito wako, Yesu anakuita kwa upole uje umsikilize. Leta yote miguuni pake, kaa kimya, msikie anasema nini nawe. Mshirikishe changamoto zako zote, mwachie Yesu ambaye ametupenda kwanza. Naye atakwambia umechagua fungu lililo jema ambalo halitaondolewa kwako. Hujachelewa, anza na Mungu siku zote na siku yako itajazwa na kila neema na baraka za mbinguni.
Tatu: Neno la Mungu tulisikialo tuwapo miguuni pake tuliishi. Maria alikaa miguuni pa Yesu akimsikilza. Katika tamaduni za Wayahudi, mwanafunzi ili athibitishwe kuwa alielewa vyema maandiko matakatifu alipaswa kukaa miguuni mwa Rabi kwa muda wa kutosha ili aweze kujifunza na kuyaelewa yote. Maria anajifunza kutoka kwa Yesu. Ndugu mpendwa, tukishalisikia Neno la Mungu, likatupa nguvu, likatufungua akili na mioyo yetu, likatufariji, likatuinua, likatukumbusha wajibu wetu kwa Mungu na kwa wenzetu, tunapaswa kuliweka katika Matendo. Haitoshi tu kukaa miguuni pa Yesu na kumsikiliza na isionekane katika maisha yetu ya kawaida ya kila siku, namna tunavyowawazia wengine, namna tunavyowatendea wengine, namna tunavyowapokea, kuwahurumia na kuwahudumia wengine, namna tunavyotimiza na kutekeleza wajibu wetu kwa wengine nk. Tuombe neema ya Mungu ili kweli kukaa kwetu na Kristo, imani yetu, matumaini na mapendo yetu kwake yatusukume katika huduma ya ukarimu na upendo wa kweli kwa ndugu zetu. Nne: Yesu Mkarimu anatoa nafasi kwa wote kumsikiliza. Katika tamaduni za wayahudi, wanawake hawakua na haki ya kuketi miguuni pa Yesu kama Maria alivyofanya. Ilikua ni jambo la kushangaza Kadiri ya mila na desturi zao. Kristo Mwalimu, rafiki mwema na mkarimu ameleta mtazamo mpya kwa jamii ile ambayo mwinjili Luka anawaandikia. Luka aliandika Injili yake kwa watu wa mataifa, watu waliokuwa hawana thamani, na huko Kristo anawainua wale wote waliokuwa wanaonekana kuwa hawana thamani, wanawake, maskini, wagonjwa, Watoto, nk. Ndugu mpendwa, Yesu Mkarimu ametupokea sote kama tulivyo. Kwa sadaka yake msalabani alimnunulia Mungu watu wa kila kabila, lugha, jamaa na taifa. Sisi sote tumepata nafasi ya kukaa miguuni pa Yesu. Kila siku anatuandalia karamu, mwili wake na Damu yake, akitukumbusha tena na tena kwamba anatupenda. Kristo anakukumbusha ndugu mpendwa kwamba wewe ni wa thamani kubwa sana machoni pake, una nafasi ya pekee kanisa miguuni pake, umsikilize, akufundishe, akuinue, akubariki.
Somo la pili: Ni Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai 1:24-28: Mtume Paulo katika somo la pili, anawaandikia Wakolosai akifurahi kwa kuwa anashirikia mateso pamoja na Kristo. Mtume Paulo aliandika waraka huu kwa Wakolosai akiwa gerezani kule Roma na baada ya muda aliuwawa kifo dini. Alifurahia mateso aliyokua akipitia kwa ajili ya wengine, na anasema anayatimiza katika mwili wake yale yaliyopungua katika mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake yaani Kanisa. Mtume Paulo hivyo alikua tayari kuiishi Injili kwa ajili ya wengine kama vile Kristo alivyoubali kuteseka na kufa kwa ajili yetu sisi, kielelezo cha upendo na ukarimu usio na mipaka. Sisi nasi tuombe neema ya kulishika kiaminifu na kuliishi Neno la Mungu, kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine, kuwapokea wengine katika mazuri na madhaifu yao, kama vile Kristo alivyotupenda na kutupokea sisi sote. Hitimisho: Tuombe neema ya kufungua milango, kwanza kabisa mioyo yetu. Tuwapokee wote wanaohitaji msaada wetu wa hali na mali, wageni, wagonjwa, wazee, yatima, wajane, watoto wa mitaani, wafungwa, maskini, waregevu nk, ndivyo Mungu anavyokuja nyumbani kwangu na kwako. Mwisho, tujinyenyekeze daima kwa Kristo na tujifunze daima kutoka kwake ili tuweze mwisho wa maisha yetu kustahililishwa kuingia katika hema yake, baada ya maisha haya ya kupita ya hapa duniani.