Tafakari Dominika 16 ya Mwaka C wa Kanisa: Ukarimu ni Mlango wa Neema na Baraka
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 16 ya Mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatuasa tuwe wakarimu kwa wahitaji ikiwa ni pamoja na kuwapokea na kuwahudumia wageni ili tuweze kupata neema na baraka kutoka kwa Mungu zitusaidie katika maisha yetu. Ni katika muktadha huu zaburi ya wimbo wa mwanzo inasema; “Tazama, Mungu ndiye anayenisaidia; Bwana ndiye anayenitegemeza nafsi yangu. Kwa ukunjufu wa moyo nitakutolea dhabihu; Ee Bwana, nitalishukuru jina lako, maana ni jema (Zab. 54:4, 6). Na ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Bwana, uwarehemu watumishi wako, uwazidishie kwa wema baraka za neema yako. Hivyo waendelee kuzishika daima amri zako kwa moyo wa matumaini, imani na mapendo.” Somo la kwanza ni la kitabu cha Mwanzo (Mwa 18:1-10a). Somo hili linatusimulia jinsi Ibrahimu Baba wa imani alivyoonyesha fadhila ya ukarimu kwa kuwapokea wageni na kuwahudumia. Kwa tendo hili aliwapokea wajumbe wa Mungu, akaahidiwa kupata mtoto, licha ya uzee wao, yeye na mkewe Sara, maana kwa Mungu hakuna lisilowezekana, na ahadi hii ilitimia kwa kuzaliwa Isaka. Kumbe huduma kwa wengine, zinakuwa ni chanzo cha neema na baraka machoni pa Mungu kwa maana ukarimu unaotoka ndani ya moyo uliojaa upendo, haki na wema, unaakisi neema na baraka zitokazo kwa Mungu.
Ni katika muktadha huu zaburi ya wimbo wa katikati inatoa wasifu wa mtu atakayeingia katika ufalme wa Mungu; “Bwana, ni nani atakayefanya maskani yake katika kilima chako kitakatifu? Ni yeye aendaye kwa ukamilifu, na kutenda haki; Asemaye kweli kwa moyo wake, asiyesingizia kwa ulimi wake. Yeye ambaye hakumtenda mwenziwe mabaya, wala hakumseng’enya jirani yake. Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa, bali huwaheshimu wamchao Bwana. Yeye ambaye hakutoa fedha yake apate kula riba, hakutwaa rushwa amwangamize mtu asiye na hatia. Mtu atendaye mambo hayo hataondoshwa milele” (Zab. 15).Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai (Kol. 1:24-28). Ujumbe mkuu katika somo hili ni huu; kwa kuwa Kristo aliteswa kwa hiari yake akawakomboa watu wote, akaujenga na kuusimika ufalme wa Mungu duniani. Basi nao wanaoendeleza kazi yake, hawataepuka dhiki na mateso katika kuwahudumia wengine. Hata yeye mtume Paulo aliyatoa maisha yake, akavumilia taabu, mateso na mahangaiko ili upendo wa Mungu kwa njia ya Yesu Kristo uweze kudhihirishwa katika yeye. Anasema hivi; “Sasa nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu; tena nayatimiliza katika mwili wangu yale yaliyopungua ya mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake, yaani, Kanisa. Hii ndiyo siri iliyofichwa kwa wamchao Mungu, yaani Watakatifu wake. Siri hii iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, na sasa imefunuliwa kwa watakatifu wake. Ni kwa siri hii, nimefanywa mhudumu wake, sawa sawa na uwakili wa Mungu, niliyopewa kwa faida ya watu, nikilitimiza neno la Mungu” (Kol.1:24-25). Haya yote Mtume Paulo aliyaweza kwa upendo wa Kristo. Nasi tukifanya hivyo tutastahilishwa kuushiriki uzima wa milele pamoja na Kristo Bwana wetu huko mbinguni.
Injili ni ilivyoandikwa na Luka (Lk. 10:38-42). Sehemu hii ya Injili inahusu simulizi la Maria na Martha kumkaribisha Yesu nyumbani kwao. Hawa, pamoja na kaka yao Lazaro, walikuwa ni marafiki wapendwa wa Yesu Kristo. Ujumbe mkuu tunaoupata ni kuwa huduma na utumishi kwa wengine vijikite katika kumuendeleza mtu mzima – kimwili, kiroho na kiakili, vyote vikiongozwa na moyo wa ukarimu na upendo wa kimungu, kwa maana moyo utoao kwa ukarimu hupokea zaidi. Maandiko Matakatifu yanasema hivi; “Mwenye jicho la ukarimu atabarikiwa na Mungu, maana huwapa maskini chakula chake” (Mithali 22:9). Mzaburi anasisitiza; “Heri amkumbukaye mnyonge, maana Bwana atamwokoa siku ya taabu” (Zab. 41:1). Naye Mtume Paulo anasema hivi; “Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu” (2Kor 9:6-7). Ndiyo kusema ukarimu hugeuka kuwa neema na baraka, hazina yetu tunayojiwekea “mbinguni ambako nondo na kutu hawawezi kuharibu, wala wezi hawaingii wakaiba. Maana pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako” (Mt. 6:19-21). Hivyo basi kujikusanyaji na kujiwekea hazina mbinguni kunafanyika kwa kujikusanyia mali za duniani, na kuzitumia kwa kuwahudumia wengine, wasioweza kujikusanyia, kwa moyo wa ukarimu na upendo, na ni katika kuwasaidia wengine, muujiza hufanyika, vitu hugeuka kuwa neema, na neema hizo huwekwa mbinguni kwenye hazina yako, ambapo ndipo utakuwa moyo wako. Kwa hiyo kadri ulivyo na neema hizo kwa wingi mbinguni, wakati utakapokuwa umekwenda kuzimiliki, nawe utaweza kuwagawia wanaokuomba msaada wa neema hizo, nazo haziishi, kama ule unga wa mjane wa Sarepta aliyemsaidia Nabii Elia wakati wa njaa. Kwa tendo hilo la ukarimu, unga wake haukupungua, wala mafuta katika chupa hayakuisha (1Fal. 17:16). Neema hizo za mbinguni, ndizo zinaweza kufanya miujiza hapa duniani wakati tuombapo sala zake, yeye akiwa mbinguni.
Ndiyo maana, Kanisa linapofanya mchakato wa kumtangaza mtu kuwa Mtakatifu, linaomba muujiza kwa maombezi yake kwa nguvu za neema alizonazo mtumishi wa Mungu mwenye kufanyiwa mchakato huo. Ombi la mtu aliyejaa neema husikilizwa haraka mbele ya kiti cha Mungu, halikataliwi, majibu yanatokea mara moja. Kwa hiyo kadri mtu alivyo na neema kwa wingi katika hazina yake, ni kadri hiyo hiyo anavyoweza kutusaidia kwa msaada wa sala zake. Kama neema ni kidogo hataweza kutupatia, maana hataweza kutoa zaidi ya alichonacho. Ndiyo maana kwa wengine miujiza inatokea haraka kwa sababu wanazo neema kwa wingi, na kwa wengine miujiza inachelewa au hata kukosekana kabisa; kwa sababu hazina ya neema waliyojiwekea mbinguni ni kidogo. Basi tujitahidi kuwa na moyo wa ukarimu ili tujiwekee hazina mbinguni. Lakini ukarimu wetu lazima uongozwe na upendo, na sio kwa woga kwamba, nisipofanya matendo ya huruma sitaenda mbinguni, au kwamba nitatupwa katika moto wa milele. Mtakatifu Basili anasema; “Kama tukiacha kutenda dhambi kwa sababu ya woga, tuko katika hatari ya kuwa watumwa; kama tukishikilia ushawishi wa mishahara tutafanana na mamluki au askari wa kukodiwa. Lakini kama tukitii kwa ajili ya uzuri wenyewe na kwa sababu ya upendo kwake, tuko katika nafasi ya wana na watoto wa Mungu.” Upendo unapaswa utawale katika kutenda matendo ya huruma, maana ajuaye ni Mwenyezi Mungu, Yeye anayapima matendo yote kwa kipimo sahihi (1Sam. 2:3). Tusifanye matendo ya huruma ili watu watuone na kutusifu, maana tukifanya hivyo hatutapata thawabu machoni pa Mungu (Mt. 6:5), yaani uzima wa milele mbinguni. Kwa maana tumekwisha kuipata thawabu yake hapa duniani, yaani, sifa na mashangilio ya watu wanayotupatia. Lakini tukifanya matendo ya ukarimu kwa upendo wa Kristo (2Kor. 5:14), Mungu Baba aonaye sirini atatujazi (Mt. 6:6). Ni katika tumaini hili Mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Mungu, ulihalalisha kafara mbalimbali za zamani katika sadaka hii moja iliyo kamili. Uipokee sadaka hii tunayokutolea sisi watumishi amini. Uibariki kama ulivyoibariki ile sadaka ya Abeli, ili kitu alichokutolea kila mmoja wetu kwa kuuheshimu utukufu wako, kitufae sote kwa wokovu”. Na katika sala baada ya komunyo anapohitimisha maadhimisho ya dominika hii anasali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba uwe na sisi taifa lako. Na kama ulivyotujalia mafumbo haya ya mbinguni, utuondoe katika maisha ya zamani na kutuweka katika maisha mapya.” Na hili ndilo tumaini letu, kuingia katika maisha mapya, maisha ya uzima wa milele mbingu. Tumsifu Yesu Kristo.