Tafakari Dominika 16 ya Mwaka C wa Kanisa: Sala na Kazi: Ora et Labora!
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya Neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican. Ora et Labora: Kipaumbele cha pekee kwa tafakari ya Neno la Mungu, chemchemi ya maisha ya kiroho na kiungo makini cha maisha ya kijumuiya, changamoto na mwaliko wa kuhakikisha kwamba, Neno la Mungu linamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya wakristo. Tafakari ipewe msukumo wa pekee kwa Mkristo mmoja mmoja na jumuiya ya waamini katika ujumla wake, ili kutambua na kumwilisha mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Wakristo wawe makini kusoma alama za nyakati ili kung’amua mapema mambo yanayoweza kuwapeleka mbali na mapenzi ya Mungu. Tafakari ya Neno la Mungu haina budi kumwilishwa katika matendo, kwa kujisadaka kwa ajili ya wengine katika upendo. Hapa kazi inapaswa kutambuliwa kuwa ni mchango katika kazi ya uumbaji, huduma makini kwa binadamu; upendo na mshikamano na maskini, kwa kuwa na uwiano mzuri wa ushirikiano katika masuala haya yanayotekelezwa kila siku ya maisha. Waamini watambue na kuthamini maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano duniani na mchango wake katika uundaji wa mawazo na mahusiano na mshikamano wa watu duniani. Leo ni Dominika ya 16, Masomo ya leo yanatupeleka kwenye hali tatu zinazotufundisha matumaini: Wito wa ukarimu kwa mgeni (Mwanzo 18:1-10a, Abrahamu), Uvumilivu na huduma ya mateso kwa Kanisa (Wakolosai 1:24-28, Paulo), injili Utulivu wa kiroho wa Maria mbele ya Yesu (Luka). Katika nyakati za kisasa zenye msongamano wa shughuli, mashaka ya kiuchumi, vita vya kimfumo, na mivutano ya jamii, masomo haya yanatufundisha namna ya kudumu katika tumaini la Kikristo. Mama utajisikiaje na kufanya nini mume wako akifurahia kiamsha kinywa halafu aende Kanisani kusali kisha abakie huko hadi muda wa chakula cha jioni wewe ukihangaikia kazi zote? Abrahamu anapokea wageni watatu chini ya mti. Kwa ukarimu wake, anapata baraka ya mtoto, hata akiwa mzee. Matumaini hujengwa katika ukarimu. Mwenyezi Mungu anatembea katika nyuso za wageni na wahitaji. Katika Jubilei ya Matumaini: Hayati Papa Francisko anatufundisha kwamba milango ya moyo wa Kikristo haipaswi kufungwa. Katika dunia ya leo yenye ubinafsi mkubwa, ukarimu wa Abrahamu ni mwanga wa tumaini. “Jirani ni mgeni unayemfungulia moyo kwa jina la upendo.” Ukarimu ni mojawapo ya fadhila njema, hali ya kutoa vitu/mali kwa kukaribisha au kusaidia wanaohitaji bila malipo. Maandiko matakatifu yana mifano 2 ya watu wakarimu.
Abraham katika Somo la Kwanza: (Mwz 18:1-10a) na Ayubu aliyejenga nyumba yenye milango 4, 1 kila upande ili maskini wasipate shida kuingia.. sisi kwenye nyumba na kumbi zetu mlango ni 1 na kamati nzito ya ulinzi. Abraham pasi kujua, kwa tendo lake la ukarimu kwa wageni, anakutana na Mungu na mapato ya ukarimu wake anajaliwa mtoto. Nasi kwa ukarimu wetu tutajaliwa ‘mtoto’ yaani yale tunayohitaji zaidi maishani mwetu. Ukarimu unajitokeza pia katika Injili (Lk 10:38-42), wengi tunatumia simulizi hii kuhamasisha maisha ya sala na ukaa pweke.. Dominika iliyopita Yesu alimsifu Msamaria aliyejitoa kumsaidia yule “mtu mmoja” katika dhiki, leo anamsifu mwanamke asiyeinua japo kope kusaidia kazi, tueleweje? twende taratibu. Ni mazingira ya nyumbani, Kristo ni mgeni wa dada wawili, wadogo zake Lazarus. Martha mara moja anaingia kazini, kama mwenyeji mwema anatambua glasi ya divai (kikombe cha chai), kipande cha mkate na cha nyama ya kuokwa kwa mgeni huleta raha moyoni, amani rohoni, utulivu akilini na baraka za mbingu, tendo hili la ukarimu linaonesha tabia njema ya utu na kujali likiongeza ndugu, marafiki na jamaa wengi zaidi... Maria, mdogo mtu, anachukua njia tofauti na dada yake, badala ya kushika kazi jikoni anajisahau kabisa miguuni pa Yesu akimsikiliza kwa makini, na hiki ndicho chanzo cha ugomvi wa dada hawa. BWANA anamtetea Maria akisema “amechagua fungu lililo jema Zaidi.” Mtume Paulo anasema: “Ninafurahia mateso yangu kwa ajili yenu.” Yuko tayari kustahimili kwa ajili ya kusudi la Kristo ndani ya Kanisa. Tumaini lina chimbuko hata katika maumivu. Mateso ya Kikristo huleta uzima na ujenzi wa Kanisa. Ni wazi kuwa hatuwezi kuwa watu wa tumaini bila kuwa tayari kubeba misalaba ya kila siku kwa upendo. Huruma inachipua pale tunapomimina maisha yetu kwa ajili ya wengine.
UFAFANUZI: Yesu anatembelea nyumba ya Martha na Maria. Martha anahangaika na shughuli, lakini Maria anaketi miguuni mwa Yesu. Tumaini la kweli linahitaji usikivu kwa Neno la Mungu. Katika haraka na shughuli, tunaitwa tuwe watu wa utulivu wa kiroho. “Maria amechagua sehemu iliyo bora, ambayo haitanyang'anywa.” Hayati Papa Francisko alisisitiza juu ya utulivu wa kiroho katika dunia yenye kelele nyingi. Tunahitaji nafasi ya kusikiliza-si tu kufanya. Kutoka simulizi hii tujifunze mambo kadha wa kadha... Mosi ‘aliketi miguuni pa Yesu na kusikiliza maneno yake’... kuketi miguuni pa “Mwalimu” ilikuwa ishara ya ufuasi, inaonesha alikuwa mfuasi rasmi wa Kristo aliyefuatilia kwa umakini wote mafundisho ya mwalimu wake. Hata Mt. Paulo anajisifia hilo anaposema ‘Mimi ni mtu wa kiyahudi… nililelewa katika mji huu, MIGUUNI PA GAMALIELI, nikafundishwa sheria za baba zetu kwa usahihi, nikawa mtu wa jitihada kwa Mungu nyinyi nyote mlivyo leo hivi’ (Mdo 22:3)... Maria hakuwa anasikiliza hadithi za uongo na kweli ila alisikiliza neno kutoka kwa Neno wa Mungu... Mimi na wewe tuna mazoea ya kuketi wapi? kwenye miguu ya nani? tunasikiliza nini? na kuongea nini? wapi? lini? namna gani? siku inapoisha huwa tumeongea yepi zaidi, mema au mabaya? tuketi miguuni pa Kristo, tusikilize na kutenda anachotuagiza. Ni kwa nini Kristo anamkaripia Martha mchapakazi na mkarimu na kumsifu Maria ambaye machoni pa wengi ni dada mvivu? Ikiwa suala ni kuwakemea watendaji wazuri na kuwasifu wavivu na waongeaji tu halafu itatuwia vigumu kuelewa Kristo anataka kutufundisha nini.
Martha amejibiwa vile sio kwa ukarimu wake ila “kwa kusumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi” na hasa kuzama katika kazi bila kwanza kusikiliza neno la Mungu. Maria naye anasifiwa si sababu ya uvivu au kukosa ukarimu hapana ila sababu anasikiliza kwanza neno la Mungu, halafu mengine yangefuatia baadaye. Na huu ukawe utaratibu wetu sote, sala na neno la Mungu kwanza na halafu kazi. Bikira Maria alisikiliza neno la Mungu ‘Mimi ni mtumishi wa Bwana’ (Lk 1:38) na halafu ‘vizazi vyote vitamsifu ni mwenye heri’ (1:48b) si kinyume chake. Jambo jingine zuri ni hili, Martha analalamika kwa Yesu ‘huoni vibaya’ na anamalizana na Yesu, hamgusi Maria ambaye ndiye muhusika. Anatambua Yesu ni nani na mamlaka yake, na kwamba kwa Yesu tu ndio kuna majibu, anapojibiwa alivyojibiwa anapokea na kuridhika... Jirani akikukwaza huwa unamwambia nani? Yesu? ah wapi... tunajifunga viuno, na hata kunywa pombe na kulewa kidogo kuondoa aibu na kujipa ujasiri ndipo tunapowainukia wanaotuudhi. Martha anatufundisha tunapokerwa au kufikwa na majanga halafu tumwambie Kristo naye atatuambia ni fungu lipi lililo bora zaidi. Katika mwaka huu wa Jubilei ya Matumaini, Kanisa linatuomba na kutualika Tujenge maisha ya ukarimu kuwasaidia maskini wa hali zote kiroho, kijamii, kiuchumi, kiutu mzingira nk, ziara kwa wagonjwa, kuwakaribisha waliotengwa. Tuvumilie kwa ajili ya wengine – Kuwa mfano wa uvumilivu nyumbani, kazini, kanisani. Tuishi utulivu wa kiroho – Sali kila siku, soma Neno la Mungu, tulia na kutafakari.
Kwa Martha na Abraham tunajifunza ukarimu, na kwa Maria fadhila ya ukarimu na matendo ya huruma vijengwe katika moyo wa sala na uchaji. Tunawahitaji akina Martha wa kutuhudumia, na hata matendo ya huduma na huruma yamepewa jina lake ‘umaritana’. Huduma ya kimwili kwa njia ya ukarimu ni muhimu kwa jamii ambayo katika ulimwengu wa sasa upendo umepungua, ubinafsi umeongezeka na kujali kumeyeyuka, tuwe akina Martha, tushughulike kwa kutumikia ipasavyo kila mmoja alipo, katika nyanja zote za maisha. Huenda wajibu huu unatutesa lakini tunaambiwa na Mt. Paulo katika somo II (Kol 1:24-28) tufurahie mateso yetu kwa ajili ya wenzetu, tutimilize katika miili yetu yanayopungua katika mateso ya Kristo kwa ajili ya Kanisa na wanakanisa, tumfundishe kila mtu katika hekima yote, tupate kumleta kila mtu mtimilifu katika Kristo, huo ndio umaritana yaani huduma kwa jamii. Halafu tunawahitaji pia akina Maria, watu wanaotuombea katika sala zao mchana na usiku. Maombi yao mema yanahitajika sana ili kuwapa nguvu akina Martha. Basi tuagane kwa kusema tusali na kutafakari Neno la Mungu kama Maria ili tupate nguvu ya kuwatumikia na kuwasaidia wenzetu kama Martha, Kristo Yesu aongoze yote, tumsikilize kwanza halafu tumuhudumie. Masomo ya leo yanaonesha kwamba: Matumaini huanza pale tunapowakaribisha wageni. Yanadumu pale tunapobeba msalaba kwa upendo. Yanakua pale tunapochagua kuketi miguuni mwa Yesu. Kwa hiyo, ndugu wapendwa, tujenge matumaini ya kweli, si kwa maneno tu, bali kwa matendo ya ukarimu, ushuhuda na utulivu wa kiroho, ndiyo roho ya Jubilee ya 2025.“Maria alichagua fungu bora.” Leo, na sisi tuchague tumaini la kubakiu na Kristo na wenzetu ili kufikia ukamirifu. Amina.