杏MAP导航

Tafuta

Mwenyezi Mungu, mwingi wa mapendo, mwingi wa huruma na neema hayupo mbali na watu wake. Mwenyezi Mungu, mwingi wa mapendo, mwingi wa huruma na neema hayupo mbali na watu wake.  (AFP or licensors)

Tafakari Dominika 15 Mwaka C wa Kanisa: Amri Kuu ya Upendo: Injili ya Msamaria Mwema

Ujumbe wa Dominika ya Utume wa Bahari tarehe 13 Julai 2025 unanogeshwa na kauli; “Mahujaji wa matumaini, Madaraja ya Kuwakutanisha Nchi Maadui, Manabii wa Amani.” Liturujia ya Neno la Mungu inatualika kuwa na “upendo kwa Mungu aliye karibu nasi, kwa kumpenda jirani” Mwenyezi Mungu, mwingi wa: Neema, huruma na mapendo, yuko karibu na waja wake. Huu ni wito wa kuhakikisha kwamba, Amri ya upendo kwa Mungu na jirani inamwilishwa katika maisha.

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya 15 ya Mwaka C wa Kanisa. Ujumbe wa Dominika ya Utume wa Bahari tarehe 13 Julai 2025 unanogeshwa na kauli; “Mahujaji wa matumaini, Madaraja ya Kuwakutanisha Nchi Maadui, Manabii wa Amani.” Kwa hakika bahari ni kiungo muhimu sana kwa Jumuiya ya Kimataifa, changamoto na mwaliko wa kuwa na mwelekeo mpana zaidi, kwa kudumisha amani badala ya kuendekeza migogoro, mipasuko na vita. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Rej. Gaudium et spes, 1. Huu ni ujumbe mahususi kwa watu wa Mungu, Waraka huu wa Kanisa Katika Ulimwengu Mamboleo, kwa mwaka 2025 unapoadhimisha kumbukizi ya miaka 60 tangu kuchapishwa kwake. Mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao, kamwe wasijisikie pweke, katika mchakato wa kutafuta haki, utu, heshima na furaha ya kweli. Maendeleo fungamani ya binadamu ni mchakato unaowakumbatia na kuwaambata watu wote: kimwili, kiroho na katika mwelekeo wa kijumuiya. Mahali ambapo Injili inatangazwa, inamshuhudia na kumkaribisha Kristo Mfufuka, lazima kunatokea mabadiliko na Ulimwengu hauwezi kubaki kama ulivyo, kwa sababu Yule aliyeshinda dhambi na mauti anasema, “Tazama, nayafanya yote kuwa mapya.” Ufu 21:5.

Dominika ya Utume wa Bahari 2025
Dominika ya Utume wa Bahari 2025

Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatualika kuwa na “upendo kwa Mungu aliye karibu nasi, kwa kumpenda jirani” Mwenyezi Mungu, mwingi wa mapendo, mwingi wa huruma na neema hayupo mbali na watu wake. Neno lake na Sheria zake si ngumu, wala hazipo mbali nasi (Kum 30:10-14). Ameweka amri na sheria zake ndani ya moyo wa kila mmoja mmoja wetu, na wajibu wetu ni kumpenda yeye kama alivyotupenda sisi kwanza. Kumpenda Mungu kweli ni kuzishika na kuziishi Amri na Sheria zake alizoziandika ndani ya mioyo yetu, na kulishika na kuliishi Neno lake katika maisha yetu ya kawaida kabisa ya kila siku, yaani kwa huduma ya upendo, huruma na sadaka kwa Jirani, yaani maskini, wagonjwa, wajane, wazee, yatima, waliokataliwa, waliosahauliwa na jamii, waliotengwa, walio gerezani na wote wanaoteseka kwa namna mbalimbali. Katika Dominika ya leo tumshukuru Mungu ambaye yu daima karibu nasi. Neno lake linaishi ndani ya mioyo yetu, sheria yake ni hai ndani mwetu. Tumwombe Mungu atupe nguvu na Utayari wa kukubali Neno lake liguse kabisa mioyo yetu, na sheria yake iyaongoze daima maisha yetu. Tuweze kumpenda Mungu kweli kwa kuwapenda, kuwajali, kuwahurumia, kuwathamini na kujitoa sadaka kwa ajili ya Jirani zetu. Kwa njia hiyo tutaweza kweli kuurithi Ufalme wa Mbinguni.

Tarehe 13 Julai 2025 ni Dominika ya Utume wa Bahari: mahujaji wa imani
Tarehe 13 Julai 2025 ni Dominika ya Utume wa Bahari: mahujaji wa imani   (ANSA)

Somo la Kwanza: Ni kutoka kitabu cha Kumbukumbu la Torati 30:10-14. Somo la kwanza ni kutoka katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati. Somo hili ni sehemu ya hotuba ya Musa kwa taifa la Israeli wakiwa Moab karibu kabisa na mto Jordan kabla hawajaingia katika Nchi ya Ahadi (Kum 30:10-14). Wanapokaribia kabisa kuingia nchi ya Ahadi, Musa anawakumbusha tena juu ya kulishika Agano na Amri na Sheria ya Mungu, kwamba huo ndio ulikua uzima wao. Kuingia kwao nchi ya ahadi na kuirithi kulitegemea uaminifu wao katika amri na maagizo ya Mungu. Zaidi ya hayo, Musa anawakumbusha na kuwapa moyo kwamba Mungu hayupo mbali nao, bali yu karibu kabisa. Neno lake si gumu wala lisilofikika, wala halipo mbali. Dini za kipagani katika kipindi hiki cha Musa walifundisha kuwa, Mungu hakuweza kufikiwa na kila mtu, bali watu wachache waliokuwa na uwezo wa kuongea na Mungu kwa niaba ya wengine. Lakini Mwenyezi Mungu anadhihirisha kwa Musa kuwa, Neno lake, sheria yake haipo mbali na watu, haipo ng’ambo ya Bahari, si mbinguni hata waseme nani atakayewapandia mbinguni akawaleteee na kuwaambia, wayasikie na waweze kuyafanya. Neno lake na Amri zake si ngumu, maagizo yake si mazito. Mwenyezi Mungu yu katikati ya watu wake, Neno lake na sheria yake ameviandika ndani ya mioyo yetu, vinatusukuma kumpenda yeye kwa moyo wetu wote, kwa roho yetu yote kwa nguvu na kwa akili zetu zote, na kisha kutubidiisha katika kuwapenda Jirani zetu kama tunavyojipenda sisi (Jeremia 31:33, Eze 36:26-27). Hii ndio sheria ya dhahabu ambayo Kristo anaizungumzia katika somo la Injili Takatifu kwa kutoka mfano wa Msamaria Mwema.

Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza Injili ya Msamaria Mwema
Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza Injili ya Msamaria Mwema   (AFP or licensors)

Ndugu zangu katika somo hili la kwanza tuna mambo manne ya kujifunza. Kwanza: Mwenyezi Mungu amefanya Agano nasi, ametupenda kwanza.  Mwenyezi Mungu alifanya Agano na watu wake, akawa Mungu wao nao wakawa watu wake. Sio kwa sababu nyingine yoyote ile kwamba aliwachagua bali ni kwa sababu ya upendo. Nasi sote ametufanya kuwa taifa lake jipya, watu wa kila kabila, lugha, jamaa na taifa, kwa njia ya sadaka ya Kristo sio kwa sababu nyingine yoyote, ni kwa sababu alitupenda. Taifa la Israeli walipaswa kutambua kuwa wao ni wana wa Agano, ni wana wapendwa wa Mungu na hivyo walipaswa kuishi Kadiri ya Agano hilo, wakifurahia, hawakupaswa kuwa na hofu na mashaka juu ya miungu wengine, wala hawakupaswa hata mara moja kuwa na shaka juu ya nguvu, uweza, enzi na utukufu wa Mungu, Mungu wa Israeli. Ndugu mpendwa, mimi na wewe tu wana wapendwa wa Mungu. Sisi tu wana wa Agano. Mungu ametuumba kwa mapendo, akatukomboa kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Tumefanya Agano na Mungu kwa njia ya ubatizo wetu tukishiriki kwa namna ya pekee zawadi hii ya ukombozi wetu, na hivyo tumekuwa Watoto wa Mungu na Watoto wa Mama kanisa. Kisha kubatizwa, hatuna hofu tena, hatuna mashaka kwa kuwa tu na Mungu ndani mwetu. Si magonjwa, si hofu wala mashaka, sio dhiki, sio vita wala misukosuko ya maisha, sio njaa wala kifo, hakuna kitakachoweza kututenga sisi na Mungu aliyetupenda kwa mapendo makubwa namna hiyo.

Tangazeni Injili ya Matumaini kwa waliopondeka na kuvunjika moyo
Tangazeni Injili ya Matumaini kwa waliopondeka na kuvunjika moyo   (AFP or licensors)

Taifa la Israeli walikua na hofu na mashaka nyakati fulani na wakapoteza Imani kwa Mungu aliyewapenda, aliyewafanyia mambo makuu, aliyewatoa Misri akasafiri nao kote kule mpaka sasa akawafikisha karibu kabisa na nyumbani, karibu kabisa na nchi ya ahadi. Musa anawakumbusha na anawasihi wasimwache Mungu, wabaki waaminifu kwa Mungu. Ndugu mpendwa, kamwe usimwache Mungu, usikane Imani kwa sababu ya shida, hofu changamoto, magumu na mateso, huenda Mungu anasema nawe ukiwa karibu kabisa kufika nchi ya Ahadi akikukumbusha tena na tena kuwa yeye ni Mungu. Jipe moyo, simama imara katika Imani na tumaini, tambua mapendo makubwa aliyokupenda nayo Mungu, hata akakuumba na kukukomboa. Mungu atakufungulia njia kama alivyowafungulia wana wa Israeli nao wakaingia katika nchi ya ahadi. Pili: Mungu hayupo mbali nasi, anasema nawe, ameandika Amri yake na Neno lake ndani ya moyo wako. Musa anawakumbusha wana wa Israeli kwamba, Mungu hayupo mbali nao. Mungu yu karibu kabisa nao, anatembea nao. Sheria na maagizo yake hayapo mbali, wala si ng’ambo ya pili ya bahari bali Neno lake li katika mioyo yetu, katika vinywa vyetu. Walifikiri nyakati fulani kuwa Mungu alikuwa mbali nao, na kwamba haikua rahisi wao kukutana na Mungu, kama walivyosikia kutoka kwa dini za kigani. Ila Musa anawahakikishia kuwa, Mungu yu kati yao, Mungu yu karibu nao.

Injili ya huruma na upendo kwa Mungu na jirani
Injili ya huruma na upendo kwa Mungu na jirani   (AFP or licensors)

Ndugu mpendwa, Mwenyezi Mungu yu karibu kabisa nasi. Amejifunua kabisa kwetu kwa njia ya mwanaye wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo. Alitwaa mwili akakaa kati yetu, na bado ameendelea kuwa nasi kwa sasa na kwa daima katika Ekaristi Takatifu. Kristo ni ufunuo wa Mungu asiyeonekana. Aliyemwona Kristo amemwona Baba. Mungu hayupo mbali nasi. Tunaye kila siku katika Neno lake, anasema nasi katika nyakati mbalimbali za maisha yetu, kupita nyakati na mazingira mbalimbali. Neno lake linatupa nguvu, linatuinua, linatubariki, linatukumbusha, linatakasa fikra na mitazamo yetu, linainua matumaini yetu, linaimarisha imani yetu. Kuna nyakati ndugu mpendwa waweza kuwa umekata tamaa kabisa katika safari ya maisha. Neno moja tu kutoka kwa Kristo, katika adhimisho la Misa Takatifu, katika maeneo yetu ya kazi, kutoka kwa marafik, ndugu na jamaa zetu likatupa nguvu ya kusimama na kuanza upya. Huenda wapo kati yetu waliobatilisha mipango ya kujidhuru kwa kuwa walipata nafasi ya kusikia Neno moja tu kutoka kwa Kristo, likawainua na kuwapa nguvu tena ya kusonga mbele na leo hii wanatoa ushuhuda kwamba, ni Mungu alisema nami, ni Mungu alisema na moyo wangu, ni Mungu alisema na familia yangu, ni Mungu alisema na watoto wangu, ni Mungu alisema na kazi yangu, ni Mungu alisema nami nilipokua katika bonde la uvuli wa mauti.

Vita, chuki na uhasama ni kinyume cha Injili ya Msamaria mwema
Vita, chuki na uhasama ni kinyume cha Injili ya Msamaria mwema   (AFP or licensors)

Tatu: Wajibu wetu ni kumpenda Mungu, kuzishika na kuziishi amri zake kwa matendo. Musa anawakumbusha taifa la Israeli kwamba, kama Mungu alivyowapenda namna hiyo, akakubali kukaa kati yao, wao pia walikua na wajibu wa kumpenda Mungu na kuiishi kiaminifu Torati. Torati hii ilipaswa kuwa mwongozo wa maisha yao yote, kwamba walipaswa kumpenda Mungu kwa moyo, kwa roho, kwa nguvu na kwa akili yao yote, kisha kumpenda jirani kama walivyojipenda wenyewe. Hii ndio sheria ya dhahabu ambayo Kristo ataisisitiza tena katika somo la Injili Takatifu. Ndugu mpendwa, Mungu hatudai mambo makubwa ili kuupata uzima wa milele. Anatudai kuzishika amri zake, na kuziishi kweli katika uhalisia wa mahusiano yetu sisi naye na mahusiano yetu sisi kwa sisi. Haitoshi kusema ninazijua sheria, ninazijua amri za Mungu ila siziweki katika matendo. Kurudisha upendo wetu kwa Mungu ni kuwapenda kweli wenzetu. Kuonesha upendo wa kweli kwa wenzetu, upendo ambao huvumilia, hufadhili, upendo usiohusudu, upendo usiotakabari, upendo usiojivuna, upendo ambao hautafuti faida binafsi, upendo usiohesabu mabaya, upendo usiovumilia na kufurahia udhalimu. Upendo unaovumilia yote, unaoamini yote, kutumaini yote na kustahimili yote. Tujiulize kila mmoja wetu, mimi ninapenda namna gani? Je, ninampenda Mungu kiasi gani? Ninapata Muda wa kusema na Mungu wangu, kumshukuru kwa mapendo makubwa aliyonipenda nayo kwanza, kumshukuru kwa neema na baraka mbalimbali anazonijali kila siku?  Ninawapenda kiasi gani wengine? Mara kadhaa twaweza kusema tunampenda Mungu ila hilo lisionekane kabisa katika maisha yetu, tukaendelea kuishi kwa vinyongo, mioyo yetu ikajawa na shauku ya kulipa visasi, chuki, wivu, ugomvi, tukadhaniana vibaya, tukashindwa kuchukuliana kwa upole katika madhaifu yetu nk.

Injili ya Msamaria Mwema: Huruma na upendo; utu, heshima na haki
Injili ya Msamaria Mwema: Huruma na upendo; utu, heshima na haki   (AFP or licensors)

Nne: Matokeo ya kulishika na kuliishi Neno na Sheria ya Mungu Mungu ni mafanikio ya kweli. Katika somo la kwanza, Musa anawakumbusha taifa la Israeli wakiwa bado safarini kuelekea nchi ya ahadi na wakiwa wanakaribia kabisa kuingia nchi ya Ahadi kwamba, walipaswa kuendelea kuwa waaminifu katika Agano, amri na sheria za Mungu. Walipaswa kushika sheria ya Mungu kwa moyo, kwa akili, kwa roho na nguvu, yaani katika uzima wao. Matokeo ya kulishika Neno lake, kushika amri na maagizo yake, kuweka Neno lake kweli ndani ya mioyo yao ilikua ni kuingika katika nchi ya ahadi na kufurahia ahadi za Mungu, katika amani na utulivu. Ndugu mpendwa, matokeo ya kulishika Neno la Mungu, kuliweka moyoni, na kuliishi ni mafaniko yetu ya kweli ya kiroho na ya kimwili. Neno la Mungu linapokaa ndani mwetu, linatusukuma katika kuendea kuamini na kutumaini katika ahadi za Mungu kwetu. Ahadi kubwa ya Kristo kwetu ni uzima wa milele, baada ya maisha haya ya hapa duniani. Kama taifa la Israeli walivyoingia katika nchi ya ahadi, sisi nasi ingawa tunatembea bado katika nyika na jangwa hapa duniani tuna Imani thabiti kwa Krito tumaini letu, tumaini ambali halitatuhadaa. Pia Neno la Mungu ndani mwetu linatukumbusha daima juu ya wajibu wetu kwa wengine.  Matokeo ya kulishika na kuliishi Neno la Mungu ni, huruma, upendo, msamaha, wema, sadaka, utu, unyenyekevu na Fadhili nyingine nyingi. Familia zetu zitakua sehemu salama ambapo upendo wa kweli unakua na kustawi, jamii yetu itakua sehemu salama ambapo kila mmoja anamchukulia mwenzake kuwa ni bora kuliko nafsi yake, hatutakua na vita, hofu, chuki, visasi, hakutakua na manyanyaso, wivu nk. Fungua mioyo yetu Ee Bwana ili tuyatunze maneno ya mwanao (Mdo 16:14). Fungua moyo wangu Ee Bwana ili niyatunze maneno ya mwanao.

Mmshikamano wa upendo kwa wahanga wa vita na machafuko
Mmshikamano wa upendo kwa wahanga wa vita na machafuko

Somo la Injili: Ni Injili kama ilivyoandikwa na Luka 10:25-37. Yesu anatoa mfano wa Msamaria Mwema, akijibu swali la mwanasheria mmoja aliyemjaribu akisema, “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele” Kristo anatufundisha kuwa Jirani yetu ni nani hasa? Je, ni wale wanaotupenda, wale wanaotusaidia, wale walio marafiki zetu, wale wanaotuombea mema, au wale wanaotujali tu? Hapana. Jirani ni yeyote yule anayehitaji msaada wetu hata kama ni adui zetu. Sheria ya Wayahudi ilifundisha kuwapenda Jirani na kuwachukia maadui au wale waliokwaza na kuudhi. Lakini Kristo anafundisha, “Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi” (Mt 5:44-45). Kristo anamjibu Mwanasheria huyu kwa kutoa mfano wa Msamaria mwema. Wasamaria walikua ni akina nani? Wasamaria walikua ni taifa lilozaliwa kutokana mchangayiko wa kabila la Israeli na Waashuru. Makabila 10 ya Israeli mwaka 722BC walichukuliwa mateka na kupelekwa utumwani na hawakuwahi kurudi tena katika nchi yao. Huko utumwani ndipo wakazaliwa wasamaria. Na hawa hawakupatana kabisa na wayahudi kwa kuwa hawakua wayahudi halisi bali mchanganyiko wa wayahudi na waashuru. Kristo anatoa mfano wa Mtu aliyevamiwa na kupigwa na wanyang’anyi, na waliomwacha karibu kufa. Akiwa katika hali hiyo, alipita kuhani, wala hakuguswa na shida yake, na mlawi hali kadhalika. Lakini Msamaria, mtu wa mataifa aliyechukuliwa kuwa adui anamwonea huruma, anashuka anamsaidia. Huyu ndiye Jirani wa kweli na Yesu anatutaka sote kufanya kama huyu. Kuona, kuguswa, na kutenda kwa wakati, hiyo ndio amri kuu kuliko zote. Myahudi huyu hakusaidiwa na wayahudi wenzake bali alisaidiwa na mtu wa mataifa ambaye aliongozwa na kusukumwa na upendo.

Injili ya Msamaria mwema: Bomoeni kuta za utengano na ubaguzi
Injili ya Msamaria mwema: Bomoeni kuta za utengano na ubaguzi   (AFP or licensors)

Katika somo hili la Injili dominika ya leo tuna mafundisho manne ya kujifunza. Kwanza: Uzima wa milele ni matokeo ya mahusiano mema, sio tu sheria. Katika somo la Injili Takatifu, mwanasheria huyu alikuja kwa Yesu akimjaribu kwa kumuuliza swali kwamba, “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Mwanasheria huyu aliifahamu vyema Torati na aliifahamu hakika. Sawa na Wayahudi wengine, alifikiri uzima wa milele upo katika kuzishika tu sheria, na kuzijua. Kristo anatoa fundisho hapa kwamba sheria zote zapaswa kudhihirika katika mahusiano, kati yetu sisi kwa sisi na kati yetu sisi na Mungu, na hapo ndipo tunaweza kuupata uzima wa milele. Ndugu mpendwa, swali la mwanasheria huyu huenda ni maisha yetu ya kawaida ya kila siku, kwamba, ninaishi kweli Neno la Mungu katika Matendo? Je, amri za Mungu zote ambazo nimejifunza tangu utoto wangu zinanisaidia kuboresha mahusiano yangu na Mungu na mahusiano yangu na Jirani zangu? Huenda nimezishika hizo pamoja na mambo mengine mengi yahusuyo dini na Imani yangu lakini bado nimekuwa mkavu rohoni mwangu. Je, Nimekosa huruma, nimekua mgumu kutoa msamaha, nimefunga moyo wangu kuwapokea wengine hata wale walioniumiza nyakati Fulani, walionisema vibaya, walionisingizia mabaya, walionitenga nyakati za shida? Kumbe namna tunavyoziishi amri za Mungu katika kuhusiana sisi kwa sisi na kuhusiana sisi na Mungu ndio njia ya kuupata uzima wa milele.

Utu, heshima na haki msingi za binadamu
Utu, heshima na haki msingi za binadamu   (AFP or licensors)

Pili: Upendo wa kweli unavunja kuta /unabomoa viunzi vya utengano kati yetu. Katika mfano wa Yesu, msamaria mwema alisukumwa na upendo wa kweli, akavuka mipaka ya utaifa, mipaka ya ukabila, mipaka ya sheria na kumsaidia myahudi aliyeangukia kati ya wanyang’anyi. Hakuwaza kuwa, huyu sio msamaria mwenzangu, hakuwaza kuwa, hawa huwa ni maadui zetu bali aliguswa, akasukumwa na upendo na akaona na kutenda wema bila kujali mipaka ya kijamii. Ndugu mpendwa, mfano huu wa Kristo unatupa changamoto sisi sote kujitafakari ni kwa jinsi gani tunapenda. Je ninapenda na kuhurumia kwa kuwa huyu ni ndugu yangu, au ni mtu wa kabila langu, au ni mtu wa nyumbani kwetu, au tunatoka nchi moja, au tulisoma pamoja? Au ninaguswa kusaidia kwa kiwango sawa kwa wote kwa kuwa ninasukumwa na upendo na huruma ndani mwangu. Mara kadhaa mipaka ya kijamii, lugha, kabila, nk vinafufanya kujifungia katika ukuta na kushinda kuwa tayari kufungua mioyo kwa wengine wanaohitaji msaada wetu wa hali na mali, msaada wa Faraja, ushauri, nk. Mwenyezi Mungu atuepushe na yale yote yanayojenga kuta na viunzi kati yetu na atupe nguvu ya kuwa na upendo wa kimungu.

Tangazeni na kushuhudia Injili ya matumaini
Tangazeni na kushuhudia Injili ya matumaini   (AFP or licensors)

Tatu: Dini yetu, Imani yetu bila Upendo na Matendo ya huruma ni bure. Katika mfano wa Yesu, walipita watu wawili kabla ya yule msamaria mwema. Alipita kuhani, akaenda zake, akapita mlawi naye akaenda zake. Hawa wote walikuwa wakitoka Hekaluni Yerusalemu, kusali na kutoa sadaka. Licha ya kwamba walikua wamekwisha maliza kazi yao kule hekaluni, bado hawakuwa tayari kumsaidia huyu mtu aliyehitaji msaada wao. Waliamua kutojihusisha katika kukiishi kile walichokiamini, yaani kuonesha Imani yao katika Matendo. Ndugu mpendwa, mtume Yakobo anatufundisha kuwa Imani bila Matendo imekufa (Yakobo 2:17). Imani yetu yapaswa kuwa hai katika Matendo yetu. Katika maisha yetu ya kawaida ya kiroho, tunapaswa kuwa na uwiano kati kila tunachoamini na kile tunachokiishi. Haifai kitu kama tutashindwa kuonesha katika Matendo kwamba sisi tu Wafuasi kweli wa Kristo, Kristo aliyeona na kuguswa na shida na mahangaiko ya watu, akavunja mipaka ya sheria na torati ya Musa na akatenda kwa upendo. Tunaona mara kadhaa anawaponya watu siku ya sabato, anakula na wenye dhambi, achangamana na wale walioonekana hawastahili katika jamii.  Je, dini yangu, Imani yangu imeyabadili vipo maisha yangu, imebadili vipo mtazamo wangu, imedili vipi mahusiano yangu kati yangu na Mungu na kati yangu na Jirani zangu? Kuwa kwangu katika vyama mbalimbali vya kitume, kuwa kwangu padre, kuwa mtawa, kuwa Mkristo anayeshika na kufuata amri za Mungu, kumenisaidia kuboresha mahusiano mema katika familia yangu, katika jumuiya yangu ya kitawa, katika kazi yangu nk?

Injili ya amani ni chemchemi ya matumaini kwa watoto
Injili ya amani ni chemchemi ya matumaini kwa watoto   (AFP or licensors)

Nne: Unyenyekevu katika kushuka na kushiriki mateso ya wengine. Msamaria Mwema anaakisi upendo na huruma ya Mungu, Mungu anayeguswa na kushuka na kushiriki mahangaiko yetu ya kila siku. Anapomkuta myahudi huyu aliyepigwa na kuumiza na wanyang’anyi, anashuka, anamwonea huruma, anamsaidia. Ndugu mpendwa, Mungu wetu anashuka kila siku, anakuja kwetu sisi ambao nyakati mbalimbali tunapigwa na hali mbalimbali za maisha, tunajeruhiwa katika nyakati mbalimbali za maisha yetu, tunatengwa na kutelekezwa mfano wa huyu myahudi aliyetelekezwa hata na ndugu zake wayahudi. Katika hali hiyo Yesu anashuka kwetu kila siku katika adhimisho la misa Takatifu, anasulubiwa na kufa tena kwa ajili yangu mimi na wewe. Anatuhurumia, anatufunga jeraha zetu, anatusaidia na kuturudishia tena matumaini na uhai. Nasi sote tunapaswa kuwa na roho hiyo hiyo ya kukubali kushuka. Mara kadhaa hatupo tayari kushuka, hatupo tayari kutoa muda wetu, hatupo tayari kutoa karama zetu, hatupo tayari kutoa mali zetu kwa ajili ya kuwainua wale walio chini, wale waliokata tamaa kabisa, yatima, wazee, wajane, waliokata tamaa, waliotengwa na ndugu na jamaa zao. Kukubali kupoteza ili wengine wapate, sio jambo rahisi, kukubali kushuka ili wengine wainuke sio jambo rahisi vile vile. Tunaitaji neema ya Mungu ili tuweze daima kujitoa sadaka ya kweli kwa ajili ya wengine. Hiki ndicho anachomtuma huyu mwanasheri kwenda kukifanya. Sisi sote tunaalikwa pia kwenda kuiishi Misa takatifu ambapo tumekutana na Kristo, mara baada ya kutoka, pale Padre anapotuambia: “Nendeni na Amani.” Tunakwenda kuishi upendo, huruma, msamaha, wema, sadaka, upatanisho na unyenyekevu.

Injili ya Msamaria Mwema: Upendo kwa Mungu na Jirani
Injili ya Msamaria Mwema: Upendo kwa Mungu na Jirani   (AFP or licensors)

Somo la pili: Ni Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai 1:15-20. Mtume Paulo anawaandikia wakristo wa Kolosai anawafundisha kuwa, Kristo ni mfano wa Mungu asiyeonekana. Mungu aliamua kujifunua kwetu kwa njia ya Mwanaye Yesu Kristo, aliyetwaa mwili, akakaa kati yetu, akawa sawa na sisi katika mambo yote isipokuwa dhambi. Kumbe Mungu yupo karibu kabisa na nasi, amejifunua kwetu na ameutufunulia mpango wake wa ukombozi kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Ni ukombozi tulioupata kwa njia ya sadaka ya Kristo, tukafanywa kuwa huru kutoka katika dhambi na mauti. Nasi sote tulio mwili wake, tunapaswa kumtambulisha Kristo kwa wengine kwa njia ya kuiishi amri kuu ya mapendo. Hitimisho: Katika Dominika ya leo tumshukuru Mungu ambaye yu daima karibu nasi. Neno lake linaishi ndani ya mioyo yetu, sheria yake I hai ndani mwetu. Tumwombe Mungu atupe nguvu na Utayari wa kukubali Neno lake liguse kabisa mioyo yetu, na sheria yake iyaongoze daima maisha yetu. Tuweze kumpenda Mungu kweli kwa kuwapenda, kuwajali, kuwahurumia, kuwathamini na kujitoa sadaka kwa ajili ya Jirani zetu. Kwa njia hiyo tutaweza kweli kuurithi Ufalme wa Mbinguni.

Tafakari D 15 Mwaka C
12 Julai 2025, 14:05