杏MAP导航

Tafuta

Injili ya Msamaria Mwema ni muhtasari wa historia nzima ya ukombozi na ni kiini cha Injili kwani Mungu ni upendo. Injili ya Msamaria Mwema ni muhtasari wa historia nzima ya ukombozi na ni kiini cha Injili kwani Mungu ni upendo.   (ANSA)

Tafakari Dominika 15 ya Mwaka C wa Kanisa: Injili ya Msamaria Mwema!

Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho Yesu alijifanya sawa na binadamu katika mambo yote akawa sawa na mwanadamu isipokuwa Yeye hakutenda dhambi. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, Yesu amekuwa ni jirani zaidi kwa mwanadamu, kiasi cha kuyamimina maisha yake kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Kwa njia hii, amemwonjesha mwanadamu huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka, changamoto ya waamini kupendana lakini zaidi adui!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 15 ya mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe mahususi katika masomo ya dominika hii umejikita katika kuimwilishwa amri kuu ya mapendo katika matendo ya huruma, ili kutimiza sheria na torati yote. Nasi tukifanya hivyo tutastahilishwa kuuona uso wa Mungu kama wimbo wa mwanzo unavyosema; “Bali mimi nikutazame uso wako katika haki, niamkapo nishibishwe kwa sura yako” (Zab. 17:15). Injili ya Msamaria Mwema ni muhtasari wa historia nzima ya ukombozi na ni kiini cha Injili kwani Mungu ni upendo. Hivi ndivyo Yesu anavyowawajibisha wafuasi wake, kuhakikisha kuwa wanamwilisha katika maisha yao amri kuu ya upendo kwa Mungu na jirani, kiini na muhtsari wa Injili. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho Yesu alijifanya sawa na binadamu katika mambo yote akawa sawa na mwanadamu isipokuwa Yeye hakutenda dhambi. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, Yesu amekuwa ni jirani zaidi kwa mwanadamu, kiasi cha kuyamimina maisha yake kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Kwa njia hii, amemwonjesha mwanadamu huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka, changamoto ya waamini kupendana lakini zaidi, kuwapenda hata adui zao, kwani huu ndio upya wa amri ya upendo inayofumbatwa katika matendo, kweli na sheria adili. Mama Kanisa Dominika tarehe 13 Julai 2025 anaadhimisha Dominika ya Utume wa Bahari, fursa kwa Familia ya Mungu sehemu mbalimbali za dunia, kumshukuru Mungu kwa huduma na mchango mkubwa, unaotolewa na mabaharia pamoja na wavuvi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Dominika ya Utume wa Bahari Kwa mwaka 2025
Dominika ya Utume wa Bahari Kwa mwaka 2025   (AFP or licensors)

Ni siku maalum ya kutambua na kuthamini sadaka ya watu hawa ambao wakati mwingine: haki, utu na heshima yao vinahatarishwa kutokana na changamoto mbalimbali, wanazokumbana nazo wakati wa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa jamii. Hii ni siku maalum ambayo Kanisa linatambua mchango mkubwa unaotolewa na Mabaharia pamoja na wavuvi katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi katika nyanja mbalimbali za maisha. Ni katika muktadha huu Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu, wawaonyesha mwanga wa ukweli wako wale wanaodanganyika, ili waweze kurudia njia ya haki. Uwawezeshe wote wanaoshika imani ya kikristo, wayakatae mambo yanayopingana na jina hilo, na kuyafanya yale yanayopatana nalo.” Somo la kwanza ni la kitabu cha kumbukumbu la Torati (Kumb 30:10-14). Ujumbe mkuu katika somo hili ni huu; Kumpenda Mungu ni kushika amri zake. Amri hizi si nzito wala hazipo mbali nasi, zimesimikwa ndani ya mtima wa moyo wa kila mtu. Kumbe si vigumu kuzishika Amri na sheria za Mungu maana hazitoki nje ya mtu, haziko mbali hata tuseme nani ataenda kutuletea, zi karibu, tena zinatiririka kutoka ndani ya moyo wa mtu na wala si ngumu kuzifuata. Amri hizi zinatuelekeza katika kumpenda Mungu na jirani. Na kama tukizishika, hakika wokovu u-pamoja nasi, kwa maana Mungu anakuwa daima karibu nasi, kila tumuitapo atasikia sauti za dua zetu na kutuokoa na kila uovo na ubaya wote.

Tangazeni na kushuhudia Injili ya matumaini kwa waliokata tamaa
Tangazeni na kushuhudia Injili ya matumaini kwa waliokata tamaa   (AFP or licensors)

Ni katika muktadha huu Zaburi ya wimbo wa katikati inasema hivi; “Nami maombi yangu nakuomba Wewe Bwana, wakati ukupendezao; Ee Mungu, kwa wingi wa fadhili zako unijibu. Katika kweli ya wokovu wako, Ee Bwana unijibu, maana fadhili zako ni njema, kwa kadiri ya rehema zako unielekee. Nami niliye maskini na mtu wa huzuni, Ee Mungu, wokovu wako utaniinua. Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo, nami nitamtukuza kwa shukrani. Walioonewa watakapoona watafurahi; Enyi mumtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe. Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji, wala hawadharau wafunga wake. Maana Mungu ataiokoa Sayuni, na kuijenga miji ya Yuda, Wazao wa watumishi wake watairithi, nao walipendao jina lake watakaa humo (Zab. 68:13, 16, 29-30, 32-33, 35-36). Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa wakolosai (Kol. 1:15-20). Ujumbe mahususi katika somo hili ni huu; Kristo Yesu alikuwepo tangu milele yote, na katika Yeye vitu vyote vimeumbwa. Tena Mungu anataka viumbe vyote vipate utimilifu na upatanisho katika Yeye peke yake. Lakini kwa nini Paulo aliandika ujumbe huu? Historia inasimulia kuwa Kolosai ulikuwa mji uliostawi sana, na idadi kubwa ya Wakristo walikuwa ni wongofu wapagani, watu wa mataifa mengine wasio waisraeli, waliohubiriwa na Epaphras.

Mshikamano wa upendo na wale waliovunjika na kupenda moyo
Mshikamano wa upendo na wale waliovunjika na kupenda moyo   (AFP or licensors)

Waamini hawa waliishi kwa hofu imani yao ya kikristo, wakiogopa kuwa kuiacha mizimu waliyoiabudu kabla ya kuongokea ukristo, inaweza kukasirika na hivyo kuwadhuru. Lakini pia kufuatia mafundisho potofu ya walimu wa uongo na wazushi, yaliwafanya kutilia mashaka kama imani kwa Kristo, ilitosha kuwaokoa. Hiyo wakawa na imani nusu nusu, nyingine kwa Kristo na nyingine kwa miungu mingine. Epapharas alimtumia Mtume Paulo, habari za walimu wa uongo waliojitokeza na mafundisho yao kwa Wakristo wa Kolosai. Ndipo akawaandikia barua hii akiwafundisha kuwa; Kristo yuko juu ya vitu vyote na roho zote. Kila mtu na kila kitu kiko chini ya utawala wake, kwa sababu katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana. Yeye ndiye anayeviwezesha kuwepo. Bila yeye ulimwengu wote hauwezi kuwapo. Na kila alichoumba Mungu, ni chema sana. Roho chafu na ovu ni matokea ya uasi dhidi ya Mungu. Na Yesu alijimwilisha, akawa mwanadamu, ili atupatanishe na Mungu Baba kwa mateso, kifo na ufufuko wake. Kupatanishwa kwetu na Mungu ni kazi ya Kristo mwenyewe. Baada ya kufa, alifufuka kutoka wafu. Hivyo ameshinda nguvu zote za kuzimu. Yeye ni mwanzo na mwisho wa maisha yetu. Yeye ni alpha na omega. Hivyo tukiwa tumeungana naye hatupaswi kuogopa chochote.

Wakimbizi wakitafuta fursa za kupenya ili kupata maisha mazuri
Wakimbizi wakitafuta fursa za kupenya ili kupata maisha mazuri   (ANSA)

Injili ni kama ilivyoandikwa na Luka (Lk. 10:25-37). Katika sehemu hii ya Injili Kristo Yesu anatufundisha kuwa kumpenda na kumsaidia mtu yeyote mwenye shida hata kama ni adui yetu, tunatimiza amri kuu ya mapendo. Yesu anatoa fundisho hili baada ya kuulizwa swali na mwana-sheria: “Mwalimu, nifanye nini, ili nipate kuurithi uzima wa milele? (Lk 10:25). Katika Injili ya Marko na Mathayo tunasoma hivi: “Mwalimu katika Torati ni Amri ipi iliyo kuu?” (Mk 12:28, Mt 22:35). Lakini Yesu hatoi jibu la moja kwa moja kwa swali la huyu mwana-sheria, bali anamwuliza: “Imeandikwa nini katika Torati? Wasomaje? (Lk 10:26). Naye akinukuu Maandiko Matakatifu, alijibu: “Mpende Bwana Mungu wako, kwa Moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako” (Kumb 6:5, Wal 19:18). Yesu alimwambia; Umejibu vyema; fanya hivi nawe utaishi. Kisha akauliza swali lingine: “Na Jirani yangu ni nani? (Lk 10:29). Kwa maneno mengine, ni yupi ninayepaswa kumpenda na yupi ninapaswa kumchukia? Hii ni kwa sababu kwa Wayahudi wa wakati ule, jirani yao alikwa ni Myahudi tu na siyo watu wa mataifa mengine. Hivyo upendo kwa jirani uliwahusu Wayahudi tu. Jibu la Yesu ni simulizi maarufu la Msamaria mwema, lenye ujumbe kuwa kila mtu alimeumbwa kwa Sura na Mfano wa Mungu. Kumbe kila binadamu ni jirani yetu, anastahili kupendwa, kuheshimiwa, na kusaidiwa anapokuwa katika shida. Hivyo basi Msamaria akisukumwa na upendo kwa Mungu na jirani, alitimiza sheria kwa utimilifu wake na akapata dhawabu machoni pa Mungu, tofauti na Kuhani na Lawi ambao walishika sheria ya kutojitia unajisi, wakashindwa kutimiza amri ya mapendo kwa Mungu na jirani (rej. Wal. 21:1-4).

Tangazeni Injili ya huruma, upendo na matumaini
Tangazeni Injili ya huruma, upendo na matumaini   (AFP or licensors)

Yesu kumtolea Msamaria mfano wa mtu mwema, ilikuwa ni kuvunja mzizi wa fitina na chuki kati ya Wayahudi na Wasamaria iliyodumu kwa mda mrefu, na kuonyesha kuwa upendo unapita sheria na uadui wote, na kipimo chake ni matendo ya huruma. Itakumbukwa kuwa wasamaria ni uzao mchanganyiko wa Wayahudi na Wapagani, watu wa mataifa mengine, wakati wa uhamisho wa Babeli. Hivyo Wayahudi halisi waliwaona ni wasaliti, hata kutumia jina Msamaria kama tusi. Myahudi kumtukana Myahudi mwenzake ilitosha tu kumwambia wewe ni “Msamaria”. Tunasoma hivi; “Je, sisi hatusemi vema ya kwamba, wewe u- “Msamaria,” nawe una pepo?” (Yn. 8:48). Ni katika hali hii wasamaria hawakuruhusiwa kuabudu katika Hekalu la Yerusalemu, ndiyo sababu walijenga Hekalu lao katika mlima Gerizimu nao walikubali “Vitabu 5 tu vya Musa – Torati kama vitabu halali katika Biblia na vingine vyote walivikataa. Ni katika muktadha huu mitume walishangaa kumkuta Yesu akiongea na mwanamke msamaria katika kisima cha Yakobo (Yn 4:1-19). Na alipokuwa anaelekea Yerusalemu, ujumbe wake ulipokataliwa katika vijiji vya Wasamaria, Yohani na Yakobo walimwambia: “Bwana wataka tuagize, moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize? (Lk 9:51-56). Yesu aliwakemea na kuwaambia kuwa “sikuja kuwaita wenye haki bali wenye dhambi” (Mt 19:13).

Jengeni madaraja ya kuwakutanisha watu na wala si kuta za kuwatenganisha
Jengeni madaraja ya kuwakutanisha watu na wala si kuta za kuwatenganisha   (AFP or licensors)

Kwa moyo wa upendo tunaalikwa kutenda matendo ya huruma, saba ya kimwili – kuwalisha wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu, kuwavika nguo walio uchi, kuwatembelea wafungwa, kuwakaribisha wageni, kuwatembelea wagonjwa – na saba ya kiroho – kuwazika wafu, kuwafundisha wajinga, kuwaonya wakosefu, kuwashauri walio mashakani, kuwafariji wenye huzuni, kuvumilia kwa saburi maovu tutendewayo, na kuwasamehe waliotukosea, na kuwaombea wazima na wafu. Katika maisha yetu tunakutana na watu waliovamiwa na wanyang’anyi, wakajeruhiwa kimwili, kiroho, kihisia, kisaikolojia au kimahusiano. Hawa wanahitaji faraja na huruma yetu. Katika mazingira tunakoishi wapo maskini, wajane, yatima, watoto wanaoitwa wa mitaani, wagonjwa, wafungwa wa roho na mwili, nao wamejeruhiwa kwa namna moja au nyingine. Tujivike moyo wa msamaria mwema, tuwaendee na kuwahudumia. Huu ni utume wa kila mbatizwa ili tuwe watakatifu kama Mungu Baba yetu wa mbinguni. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi: “Ee Bwana, tazama dhabihu za Kanisa lako liombalo. Nasi waamini wako utujalie tuzile tupate kuzidishiwa utakatifu”. Na katika sala baada ya kumunio anapohitimisha maadhimisho ya dominika hii anasali hivi; “Ee Bwana, baada ya kuzipokea fadhili zako, tunakuomba utuzidishie mapato ya wokovu wetu, kila tunapopoke fumbo hili”. Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari D 15 Mwaka C
11 Julai 2025, 09:15