杏MAP导航

Tafuta

Wakristo wanaitwa na kutumwa kuwani vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili Wakristo wanaitwa na kutumwa kuwani vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili  (@Vatican Media)

Tafakari Dominika 14 ya Mwaka C wa Kanisa: Vyombo na Mashuhuda wa Furaha ya Injili

Wakristo ndio wadau wa mchakato wa uinjilishaji wanaoitwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka, bila ya kutumbukia kwenye kishawishi kwamba, kazi ya uinjilishaji inaweza kutekelezwa na watu wengine. Kuhubiri upya kunaweza kuwapa waamini, pamoja na wale waliolegea na wasioiishi imani yao, furaha mpya katika imani na uaminifu katika kazi ya uinjilishaji. Wakristo wanapojitahidi kurudi katika chanzo na kuupata tena ule upya wa asili wa Injili, mwelekeo mpya.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya Neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican leo Dominika ya 14 Mwaka C, Mama Kanisa anatualika kutafakari kuhusu furaha ya Injili. Katika Ulimwengu mamboleo, Wakristo ndio wadau wa mchakato wa uinjilishaji wanaoitwa na kutumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka, bila ya kutumbukia kwenye kishawishi kwamba, kazi ya uinjilishaji inaweza kutekelezwa na watu wengine. Kuhubiri upya kunaweza kuwapa waamini, pamoja na wale waliolegea na wasioiishi imani yao, furaha mpya katika imani na uaminifu katika kazi ya uinjilishaji. Wakristo wanapojitahidi kurudi katika chanzo na kuupata tena ule upya wa asili wa Injili, mwelekeo mpya huonekana, njia mpya za ubunifu hufunguka na uinjilishaji unapyaishwa. Daima wema hutaka kusambaa. Kila mara ukweli halisi na wa uhakika unapotambulika, kwa asili yake unatafuta namna ya kukua ndani mwa waamini na mtu yeyote aliyewahi kupata ukombozi wa ndani huwa mwepesi zaidi kutambua mahitaji ya wengine. Rej. Evangelii gaudium No, 9 & 11. Wazo la kufurahi linajitokeza katika somo I (Isa 66:10-14) ambapo wana wa Israeli, wakiwa wamerudi tu kutoka utumwa wa Babeli, walikuwa wamekata tamaa sababu ya athari iliyotokana na adha ya utumwa, walikuwa karibu kupoteza imani yote, matumaini yamekwisha, kila kitu ni giza na maisha hayakuwa na maana tena sababu Yerusalemu, mji wao wa amani na fahari yao kuu, naam, Mlima Sayuni ulikuwa mahame na Hekalu lao halikutazamika.. katika mazingira hayo MUNGU anamtuma Nabii Isaya anayetamka maneno mazuri ajabu, “furahini pamoja na Yerusalemu…” Maneno haya yaliwapa moyo wana wa Israeli wakapata nguvu na kuanza kuujenga tena mji huo na kupata tumaini la ukombozi kutoka kwa Masiha atakayekuja. Sisi pia, leo na siku zote, tunaalikwa kufurahi pamoja na Yerusalemu iliyo mioyo mikunjufu na roho nyenyekevu… tuwe ni watu wenye furaha!

Wakristo wanaitwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili
Wakristo wanaitwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili   (@Vatican Media)

Masomo haya yanatufundisha kuwa, Mungu ni chanzo cha faraja ya kweli (Isaya), Msalaba wa Kristo ni alama ya ushindi wa upendo na tumaini jipya (Wagalatia),Wito wa Kikristo ni kuwa mashahidi wa amani na matumaini ulimwenguni (Injili Yesu anawapeleka wafuasi wake kama wajumbe wa matumaini, wakibeba ujumbe wa amani, wakiponya, na kutangaza kuwa Ufalme wa Mungu umefika karibu. Je Mkristo, baada ya kuhubiriwa Habari Njema tangu utoto, nyakati tofauti, kutoka wahubiri na Makanisa mbalimbali mijini na vijijini (urbi et orbi), ya Parokia na Vigangoni, Jumuiyani na katika Taasisi, katika vipindi mbalimbali vya raha na karaha, umekuwa ni mtu mwenye furaha? Huenda una huzuni kubwa kiasi cha kufa, huna matumaini, huna amani sababu nyumba yako imekosa upendo, sakramenti ya Ndoa inakuja halafu kama inakataa hivi, malengo hayajatimia, watoto wanasumbua, jirani hawakupendi, ni mtu wa kusengenywa... Labda umekosa furaha sababu vita ni kubwa kati yako na mwanandoa wako, ulimwengu na malimwengu vimekushika, hakuna anayekusikiliza wala kukutilia maanani, pengine huoni haki ikitendeka, hofu ipo pande zote nk.

Kristo Yesu ndiye chanzo na kilele cha uinjilishaji wote
Kristo Yesu ndiye chanzo na kilele cha uinjilishaji wote   (Vatican Media)

UFAFANUZI: Katika Maadhimisho ya mwaka huu wa Jubilei, Kanisa linatangaza kwa sauti kuu: “Mungu hayuko mbali nasi – yuko karibu nasi katika historia yetu, katika huzuni na furaha, na anatutuma tuwe mashuhuda wa tumaini lake.” Dominika hii inatuonesha sura halisi ya "wajumbe wa matumaini" Watu wa sala, si wa hofuWatangazaji wa amani, si wa mashaka, Wenye moyo wa huruma na uponyaji, si wa hukumu. Katika Jumuiya zetu, familia na ulimwengu uliojeruhiwa, tunaitwa kueneza tumaini lenye miguu: linalotembea, linalozungumza, linaloponya. Katika hali hii Injili inabeba uzito wowote na kukupa tumaini lenye heri na kukufanya ufurahi? Hapa tunaweza kujipatia sababu ya kuwa na mashaka kwamba ahadi za kiinjili za amani na furaha zinaweza kutimizwa. Nabii Isaya anapotuambia tufurahi basi na tufurahi kweli kama watu wenye matumaini. Furaha ya Kikristo inadai tabia safi na nidhamu binafsi “mwanangu, kama moyo wako una hekima moyo wangu utafurahi, naam viuno vyangu vitafurahi midomo yako inenapo maneno mema” (Mith 23:15-16). Lakini, tutapataje furaha katika mazingira yetu magumu? Furaha haipo katika wingi wa mali au katika kuwa na akaunti nono, haipo katika kumiliki majumba au kutokuwa na changamoto...Yesu anawatuma wale sabini na wawili kwa utume wa amani, uponyaji, na kutangaza Ufalme wa Mungu. Tazama wafuasi 70 wa Kristo katika Injili ya leo (Lk 10:1-12) wanamrudia wakiwa wamefurahi baada ya kutimiza alichowatuma. Kwa utii wao kwa Kristo hata pepo waliwatii naye Yesu anawaambia wazidi kufurahi kwa sababu alimwona shetani akianguka kama umeme, anawasisitiza wafurahi zaidi sababu majina yao yameandikwa mbinguni.

Tangazeni na kushuhudia kwamba, Ufalme wa Mungu umekaribia
Tangazeni na kushuhudia kwamba, Ufalme wa Mungu umekaribia   (Vatican Media)

Katika mwaka huu wa Jubilei, Kanisa linatangaza kwa sauti kuu: “Mungu si mbali nasi – yuko nasi katika historia yetu, katika huzuni na furaha, na anatutuma tuwe mashahidi wa tumaini lake.” Dominika hii inatuonesha sura halisi ya "wajumbe wa matumaini" Watu wa sala, si wa hofu, Watangazaji wa amani, si wa mashaka, Wenye moyo wa huruma na uponyaji, si wa hukumu, Katika Jumuiya zetu, familia na ulimwengu uliojeruhiwa, tunaitwa kueneza tumaini lenye miguu: linalotembea, linalozungumza, linaloponya. Kumbe siri ya kuwa na furaha ni kuwa watii kwa mwito ambao Kristo anatuitia yaani kwenda kote ambako kadiri ya Injili ya leo anakusudia kwenda mwenyewe.. Anatutuma wawiliwawili nasi kweli twende wawiliwawili sababu kazi ya uinjilishaji sio jambo la mtu mmoja, tukiwa wawili neno letu litathibitika, ushahidi unajipatia nguvu na mmoja akianguka mwenzake atamnyanyua, ikiwa ni hivi basi usiri na ubinafsi usitajwe kwetu… Maisha ya pamoja ni muhimu na mazuri, kwa njia ya kushirikiana kwa umoja na majitoleo kamili Ufalme wa Mungu utashamiri duniani. Tunakwenda kama kondoo kati ya mbwa mwitu, ndio ishara ya vurugu na kukataliwa, hata hivyo tunapaswa kuhubiri amani na upatanisho, tusiruhusu ndani mwetu hasira na ukatili wa mbwa mwitu bali tuuvae unyenyekevu na utulivu wa mwanakondoo. Tusihamehame nyumba hii na ile ila tuwe na msimamo, tusiweke mazingira magumu ila tule na kunywa vya kwao kwani mtenda kazi anastahili posho yake… basi na tulitegemeze Kanisa letu kwa zaka, kwa sadaka na kwa huduma.

Hata katika changamoto za maisha, iweni mashuhuda wa furaha ya Injili
Hata katika changamoto za maisha, iweni mashuhuda wa furaha ya Injili   (AFP or licensors)

Papa Leo XIV amekuwa mstari wa mbele kusisitiza kuwa “Katika dunia ya leo iliyojaa migawanyiko, hofu na vita vya ndani na nje, tunahitaji mitume wa matumaini.”Katika ujumbe wake wa kichungaji kwa Dominika hii, anatoa mwelekeo wa kitume, Kila Mkristo ni balozi wa matumaini: si kwa maneno tu, bali kwa maisha ya huruma na utumishi. Kanisa la leo ni Kanisa la kutoka: likituma wanaume na wanawake walio tayari kuwasha taa ya matumaini.Wito wa uinjilishaji si wa wataalamu pekee, bali wa kila mmoja wetu aliyeonja faraja ya Mungu. “Furahini pamoja na Yerusalemu…” tutaipata furaha ya kweli ikiwa kwa imani yetu tutaunganika sana na Kristo wa Msalaba (somo II Gal 6:14-18), kwamba imetupasa kuona fahari katika Msalaba wa Bwana na kuwa viumbe wapya… Furaha ya Yesu haindolewi na hali ya maisha, ni hali ya amani na nguvu inayomwezesha mwamini afurahi hata katika hali ya huzuni. Basi tukatae dhambi sababu dhambi ina tabia ya kuondoa furaha na kuleta mashaka, hata tukifaulu kutenda dhambi bila kupatwa na chochote dhamiri zetu huumia, huzuni hutawala, mashaka hujaa na furaha kudorola… kumbuka, furaha uipatayo baada ya kukamilisha dhambi si furaha safi nayo huongeza uzito wa dhambi yako (sinful joy). Basi na tufurahi katika Kristo, Ni Yeye pekee, anasema leo Nabii Isaya, ndiye atakayetuelekezea amani kama mto, nasi tutapata kunyonya, tutabebwa na juu ya magoti tutabembelezwa mfano wa mtu ambaye mama yake amfariji, nasi tutaona na mioyo yetu itafurahi, na mifupa yetu itasitawi kama majani mabichi (Isa 66:12). Kristo anatuita, kama alivyowaita wale 72, kuwa mashahidi wa Amani inayotuliza mioyo, Upendo unaoponya majeraha, Tumaini lisilokoma – hata katikati ya giza, Katika mwaka huu wa Jubilei ya Matumaini. Bwana Yesu, umetutuma kwa jina lako – tusaidie kuwa vyombo vya amani, mashahidi wa matumaini, na wajenzi wa Ufalme wako. Katika kila neno na tendo letu, tukujulishe kwa dunia inayokuhitaji. Amina.

Liturujia D 14 Mwaka C
05 Julai 2025, 15:15