Tafakari Dominika 14 Mwaka C wa Kanisa: Kutangaza Injili na Fahari ya Msalaba!
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 14 ya Mwaka C wa Kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe wa masomo ya dominika hii umejikita katika wajibu wa kila mbatizwa, kuihuburi Injili na kuona fahari juu ya Msalaba wa Yesu Kristo ambao kwao tumekombolewa. Wimbo wa mwanzo unaofungua maadhimisho ya dominika hii unasema hivi; “Tumezitafakari fadhili zako, ee Mungu, katikati ya hekalu lako takatifu. Kama lilivyo jina lako, ee Mungu, ndivyo na sifa yako hata miisho ya dunia. Mkono wako wa kuume umejaa haki” (Zab. 48:9-10). Na mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi akituombea; “Ee Mungu, kwa njia ya unyenyekevu wake Mwanao, umeuinua ulimwengu uliokuwa umeanguka. Uwajalie waamini wako furaha takatifu; uwapatie furaha za milele hao uliowaondoa katika utumwa wa dhambi.” Somo la kwanza ni la kitabu cha nabii Isaya (Isa 66:10-14). Katika somo hili Nabii Isaya anawapa matumaini waisraeli waliokataa tamaa, wakiwa utumwani Babaeli akiwaambia kuwa Mungu ataletea amani, heri na utukufu, kwao na kwa watu wa mataifa yote wanaomtumainia Yeye. Matumaini na faraja hii yamejidhihirisha kwa mataifa yote kwa njia ya Yesu Kristo ambaye kwa mateso, kifo na ufufuko wake ametukomboa kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Ushindi huu ni kwa watu wote, wa nyakati zote, wanaofungua mioyo yao na kumpokea.
Kumbe wajibu umebaki kwetu, kufungua mioyo, kumpokea Kristo, kuishi vyema maisha yetu ya kikristo kwa kuzishika ahadi zetu za ubatizo, kumkataa shetani na mambo yake yote na fahari zake zote, na kumkiri Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, ili tuweze kuishi kwa amani hapa duniani na kwa Yeye, baada ya maisha ya hapa duniani tukashirikishwe uzima wa milele mbinguni pamoja naye na malaika na watakatifu wote. Ni katika muktadha huu, wimbo wa katikati unatualika kufurahi ukisema; “Mpigie Mungu kelele za shangwe nchi yote, imbeni utukufu wa jina lake. Tukuzeni sifa zake, mwambieni Mungu, matendo yako yanatisha kama nini! Nchi yote itakusujudia na kukuimbia, naam, italiimbia jina lako Takatifu. Njoni yatazameni matendo ya Mungu, hutisha kwa mambo awatendayo wanadamu. Aligeuza bahari ikawa nchi kavu, katika mto walivuka kwa miguu. Huko ndiko tulikomfurahia, atawala kwa uweza wake milele. Njoni, sikieni, ninyi nyote mnaomcha Mungu, nami nitayatangaza aliyonitendea roho yangu. Na ahimidiwe Mungu asiyeyakataa maombi yangu, wala kuniondolea fadhili zake” (Zab. 66: 1-7,16,20).
Somo la Pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia (Gal 6:14-18). Katika somo hili Mtume Paulo anatuasa tuone fahari juu ya Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo ambao kwao tumekombolewa. Mazingira ya ujumbe huu ni kupungua na kufifia kwa imani, uwepo wa ugomvi na mpasuko kati ya waamini, uliosababishwa na mafundisho ya uongo, ikiwa ni pamoja na ulazima wa wapagani, watu wa Mataifa, yaani watu wasio wayahudi kushika sheria za Musa ili wapate kupokelewa, kubatizwa na kuwa wakaristo. Mtume Paulo anapinga mafundisho haya kwa kuonyesha umuhimu wa Imani juu ya Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, kwa ajili ya wokovu wa kila mwandamu. Kushika sheria tu bila kuwa na Imani kwa Kristo, hakuwezi kumwokoa mtu. Hivyo, “kutahiriwa au kutokutahiriwa si kitu, bali kule kuwa kiumbe kipya! Kwa maana tunahesabiwa haki mbele za Mungu, kwa njia ya imani, na tunakuwa watoto wa Mungu kwa imani kwa njia ya Kristo aliyetuweka huru.” Itakumbukwa kuwa nyakati za Mtume Paulo kulikuwa na biashara ya watumwa, ambapo watumwa walipigwa chapa ya bwana wao kwa kutumia chuma cha moto. Ikiwa mtumwa alitoroka alijulikana ni wa nani, na kurudhishwa kwa bwana wake. Akitumia lugha hii ya kupigwa chapa, mtume Paulo anasema kuwa sisi nasi tumepigwa chapa ya ishara ya Msalaba wa Kristo ambao kwao tumekombolewa nao. Basi tusiuonee aibu, bali uwe kwetu ni fahari, kwa kuwa ni ishara ya ushindi, utukufu na uhuru wa kweli. Hivyo kwa upendo wa Kristo tukubali kuyapokea mateso na mahangaiko ya kimaisha, ambayo kwayo yanakuwa ishara ya Msalaba katika maisha yetu. Mtume Paulo anahitimisha akisema kuwa wote watakaoenenda katika kanuni hii, amani na rehema za Mungu, na neema ya Bwana wetu Yesu Kristo zitakuwa pamoja nao, na kuishi kwa furaha na amani hapa duniani na mbinguni katika uzima wa milele.
Injili ni ilivyoandikwa na Luka (Lk 10:1-12, 17-20). Sehemu hii ya Injili inahusu Yesu kuchagua na kuwatuma wafuasi wengine 70 wawili wawili nje na mitume 12, ili wamtangulie kwenda katika kila mji aliokusudia kwenda. Namba hii 70 inasimama mahali pa koo 70 za wana watatu wa Nuhu ambao ni Shemu, Hamu na Yafethi, baada ya gharika kuu (Mwanzo 10). Mababa wa Kanisa wameona katika namba hii koo zote duniani na uwakilishi wa kila mbatizwa na wajibu wake wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo popote pale alipo katika maisha yake kama inavyotufundisha Katekismu ya Kanisa Katoliki kuwa; Kila mbatizwa anashiriki ukuhani wa Kristo, utume wake wa kinabii na kifalme, ni sehemu ya uzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, na milki ya Mungu, hivyo ana wajibu wa kutangaza fadhili zake yeye aliyemuita atoke gizani na kumuingia katika nuru yake ya ajabu. Kwa kuwa kwa ubatizo kila mkristo anashiriki ukuhani wa jumla wa Kristo (KKK 1268). Basi kila mbatizwa ana wajibu wa kukiri mbele za watu imani ambayo ameipokea kwa Mungu, kwa njia ya Kanisa na kushiriki utendaji wa kitume na wa kimisionari wa taifa la Mungu (KKK 1270).
Katika kuutimiza wajibu huu, Kristo anatoa masharti ya kufuata akisema; “Msimwamkie mtu njiani…Msichukue mkoba wa fedha, wala viatu”, kwa maana kwamba tusiweke matumaini yetu katika watu au vitu bali kwa Mungu kwa njia yake Kristo. Kisha akasisitiza; katika kuenenda kwenu, nyumba yoyote mtakayoingia hii iwe ni salamu yenu: “Amani iwemo nyumbani humu; na akiwemo mwana wa amani, amani yenu itamkalia, la hayumo amani yenu itawarudia”. Kumbe kila Mkristo anapaswa kuwa mleta amani na mpatanishi kwa wote. Na hatuwezi kuwa waleta amani ikiwa amani haimo ndani yetu. Tuombe kwanza amani na upendo wa Kristo vitawale katika mioyo ndipo tutakapoweza kuisambaza na kwa wengine tunaokutana nao. Yesu anasisitiza kuwa; “mji wowote mtakaoingia, nao hawakuwakaribisha, tokeni humo nanyi mkipita katika njia zake semeni, hata mavumbi ya mji wenu yaliyogandama na miguu yetu, tunayakung’uta juu yenu. Lakini jueni hili; “Ufalme wa Mungu umekaribia”. Katika kuitangaza Injili tutakumbana na magumu, mahangaiko na mteso mengi. Hatupaswi kuogopa maana Kristo ametupa nguvu ya kuyavumilia na ya kwamba furaha yetu kubwa zaidi ni kuuridhi ufalme wa mbinguni; “Msifurahi kwa vile pepo wamewatii, bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.” Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi: “Ee Bwana, sadaka tunayotoa kwa heshima ya jina lako itutakase, na ituwezeshe siku kwa siku kutenda yafaayo kuleta uzima wa mbinguni”. Na katika sala baada ya komunyo anahitimisha maadhimisho ya dominika hii akisali hivi; “Ee Bwana, sisi tuliojaliwa thawabu zako nyingi sana, tunakuomba utujalie fadhili zako za wokovu; tena tusichoke kamwe kukusifu.”