杏MAP导航

Tafuta

Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatutafakarisha juu ya, “FURAHA YA INJILI"  sanjari na Ukuu na Utukufu wa Msalaba Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatutafakarisha juu ya, “FURAHA YA INJILI" sanjari na Ukuu na Utukufu wa Msalaba  (Erika Santelices)

Tafakari Dominika 14 ya Mwaka C wa Kanisa: Mashuhuda wa Furaha ya Injili na Matumaini

Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatutafakarisha juu ya, “FURAHA YA INJILI” Katika somo la kwanza, (Isa 66:10-14) Nabii Isaya anatangaza Habari Njema ya furaha na matumaini kwa Taifa la Israeli waliorejea kutoka tumwani kwamba Mungu atawabariki tena, atawapa amani, atarejesha mahusiano mema mema kati yake na taifa lake. Mzaburi katika zaburi ya 66:1-7, 16, 20, anatualika kufurahi, kumpigia Mungu kelele za shangwe! Mashuhuda wa furaha ya Injili.

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya 14 ya mwaka C wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatutafakarisha juu ya, “FURAHA YA INJILI” Katika somo la kwanza, (Isa 66:10-14) Nabii Isaya anatangaza Habari Njema ya furaha na matumaini kwa Taifa la Israeli waliorejea kutoka tumwani kwamba Mungu atawabariki tena, atawapa amani, atarejesha mahusiano mema mema kati yake na taifa lake. Mzaburi katika zaburi ya 66:1-7, 16, 20, anatualika kufurahi, kumpigia Mungu kelele za shangwe kwa sababu ya matendo yake makuu kwa taifa lake. Mwenyezi Mungu anatimiza furaha ya ukombozi wa milele kwa taifa lake kwa njia ya Neno wake, aliyetwaa mwili akakaa kwetu, Bwana wetu Yesu Kristo (Yn 1:12, 14). Katika somo la Injili, Kristo anawatuma wafusi sabini kwenda kuhubiri Habari Njema ya Injili, kuusimika ufalme wa Mungu kati ya watu. Anawapa maelekezo namna walivyopaswa kwenda kuhubiri Habari Njema, nao wanarudi kwa furaha kwa kuwa walifanikiwa katika utume wao.  Mtume Paulo katika somo la pili (Gal 6:14-18) anatualika kuona Fahari juu ya Msalaba wa Kristo ambao kwao sisi tumepata ukombozi wa milele. Sisi sote tuliobatizwa tumepokea Habari Njema ya ukombozi kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Tunatumwa kila mmoja kuwa mashuhuda wa furaha hii ya Injili kwa njia ya maneno na matendo yetu.

Wito na mwaliko wa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya furaha
Wito na mwaliko wa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya furaha   (@Vatican Media)

Somo la Kwanza: Ni kutoka katika Kitabu cha Nabii Isaya 66:10-14. Somo la kwanza ni kutoka katika kitabu cha Nabii Isaya. Mazingira ya somo hili (Sitz im Leben) ni baada ya taifa la Israeli kurejea kutoka utumwani Babeli ambapo walikaa kwa muda wa takribani miaka 70, yaani kuanzia mwaka 605 BC hadi mwka 538 BC. 70 ni namba yenye maana ya kipindi kirefu katika Maandiko Matakatifu, ni muda wa kutosha. Hivyo kwa kukaa utumwani miaka sabini, taifa la Israeli waliteseka kwa muda wa kutosha. Waliporejea katika nchi yao (539/38 BC) wakaanza maisha upya, maisha ambayo hayakuwa rahisi kwa kuwa mji wa Yerusalemu ulikuwa umeharibiwa vibaya na Mfalme Nebukadneza, hekalu lao ambalo lilikua ni ishara ya utakatifu na ukuu wa Mji wa Yerusalemu, ishara ya uwepo wa Mungu kati yao lilivunjwa, walipoteza mali zao, walipoteza ardhi yao, walipoteza ndugu na jamaa zao, walipoteza utamaduni wao, walipoteza amani na matumaini. Kwa ujumla waliishi maisha yenye changamoto nyingi, kiimani, kisiasa, kiuchumi na kijamii. Katika hali hiyo, Nabii Isaya katika sura hii ya mwisho kabisa ya kitabu hiki, sura ya 66, anawapa matumaini taifa la Israeli waliokata tamaa, anawatia moyo kwamba, Mungu anawakumbuka, Mungu hajawasahau na kwamba atawabariki zaidi ya ilivyokuwa Mwanzo. Katika Agano la kale, taratibu tunaona namna Mwenyezi Mungu kupitia taifa lake teule la Israeli anavyoanzisha upya kazi ya ukombozi ambayo ilitimizwa na Bwana wetu Yesu Kristo wakati ukamilifu wa nyakati ulipowadia (Gal 4:4-5).

Tangazeni furaha ya Injili
Tangazeni furaha ya Injili   (@Vatican Media)

Ndugu zangu katika somo hili la kwanza na zaburi tuna mambo manne ya kujifunza. Kwanza: Kwa sababu ya dhambi sisi sote tulikuwa watumwa. Taifa la Israeli kwa muda wa miaka sabini walikuwa utumwani Babeli. Sababu kubwa ya wao kuwa utumwani ni ukosefu wa uaminifu kwa Agano waliloweka na Mungu, kwa amri na maagizo ya Mungu. Mwenyezi Mungu anawafundisha, anawakumbusha kwa kuwapeleka utumwani. Huko waliteseka sana, walitengwa na Hekalu lao, walitengwa na ndugu na jamaa zao, waliondolewa katika nchi yao na kupoteza neema na baraka zote za Mungu. Ni kwa sababu ya dhambi, ni kwa sababu ya ukosefu wa uaminifu. Ndugu mpendwa, dhambi inatutenga sisi na Mungu. Inatuweka mbali na uwepo wa Mungu wetu. Dhambi inajenga ukuta kati yetu sisi kwa sisi, inavunja mahusiano mema kati yetu na Mungu. Ukosefu wa uaminifu katika familia, katika kazi, katika jamii, katika mahusiano ni chanzo cha huzuni na mahangaiko katika familia zetu na katika jamii zetu. Tujiulize kila mmoja wetu ni nini kinanifanya kila mara kuwa mbali na Mungu wangu? Ni kazi yangu? ni vipaji na karama zangu? Ni marafiki zangu? Ni starehe na anasa za ulimwengu huu? Ni uchu wa madaraka, vyeo, sifa na utukufu katika maisha haya ya kupita?  Ni mara ngapi nimekua chanzo cha maumivu kwa wengine, kwa uzembe, kwa kutotimiza wajibu wangu kikamilifu, kwa wivu, kwa visasi, chuki, ubinafsi, kwa vinyongo, tamaa na uchu wa sifa na utukufu binafsi? Hayo yote kwa nyakati mbalimbali yametusababishia vidonda, vilio, uchungu, hofu, kukata tamaa, mashaka na shauku ya kulipiza kisasi kwa wale waliotuumiza, huenda ni mume, au ni mke, au ni ndugu, au ni marafiki zetu. Tumwombe Mungu atukumbushe daima kutafuta kwa bidii kuwa na amani kati yetu sisi kwa sisi na amani ya kweli kati yetu sisi na Mungu Baba yetu.  

Tangazeni na kushuhudia fahari ya Msalaba
Tangazeni na kushuhudia fahari ya Msalaba   (ANSA)

Pili: Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma, hajatusahau. Kwa muda wa miaka 70 taifa la Israeli walikua utumwani huko Babeli. Ni muda mrefu, ni muda wa kutosha. Mwenyezi Mungu kwa muda na wakati wake, akawakumbuka, akawakomboa akawarejesha katika nchi yao. Licha ya kwamba walikua wameshakata tamaa, kutokana na hali ngumu ya maisha waliyoikuta waliporejea katika nchi yao, bado Mungu anawapa moyo. Anatumia picha cha Mama, namna anavyombeba, kumnyonyesha na kumbembeleza mwanaye, ndivyo Mungu atakavyowafariji, kuwalinda na kuwabariki zaidi ya mwanzo,“Mfano wa mtu ambaye Mama yake amfariji, nanyi mtafarijiwa katika Yerusalemu (Isa 66:13)“ Ndugu mpendwa, Mungu wetu ni mwingi wa Upendo, huruma na neema. Kwa kuwa anatupenda, hafurahii mateso, shida na mahangaiko ambayo kila mmoja kwa wakati wake anaweza kuwa anapitia. Kila mmoja wetu anafahamu historia yake, anafahamu nyakati, majira na mapito mbalimbali ambayo amepitia. Huenda ni changamoto za afya, changamoto za kiuchumi, changamoto za masomo, amani katika familia, changamoto katika ajira nk. Mungu anakuahidi baraka zake kwa wakati wake. Taifa la Israeli walirejeshewa wingi wa baraka za Mungu baada ya miaka 70 ya mateso, katika muda wa Mungu, Mungu akajibu sala zao, akawarejeshea baraka zake. Mungu hajakusahau ndugu mpendwa, anaguswa na changamoto zako, anaguswa na imani yako thabiti hata katika nyakati hizi ngumu ambazo tunapitia kila mmoja wetu kwa wakati wake. Anakupa matumaini mapya kwamba, atakubariki tena, atakuinua tena, atakurejeshea wingi wa neema zake. Usikate tamaa, kamwe usimwache Mungu. Mungu anakuona, Mungu anakusikia, Mungu anakuonea huruma, Mungu anakupenda sana. Jipe moyo, atakujibu kwa wakati.

Fahari ya utukufu na ukuu wa Fumbo la Msalaba
Fahari ya utukufu na ukuu wa Fumbo la Msalaba

Tatu: Tubaki imara katika imani kwa Mungu, chanzo cha amani na furaha yetu. Mwenyezi Mungu aliwapeleka watu wake utumwani ili kuwafundisha nyakati zote ambazo walikosa uaminifu kwa amri na maagizo yake. Aliwakumbusha kuwa yeye ni Mungu na kwamba walipaswa kubaki waaminifu kwake. Anapowarejesha katika nchi yao anawaahidi baraka nyingi na kubwa kuliko zile za mwanzoni, anaposema,“Tazama nitamwelekezea amani kama mto, na utukufu wa mataifa kama kijito kifurikacho.“ Ndugu mpendwa, tusijisikie wanyonge na dhaifu pale tunapopita katika changamoto mbalimbali katika maisha. Huenda changamoto hizo ndio njia yetu kuelekea kwenye utimilifu wa baraka za Mungu katika maisha yetu. Huenda ndio muda ambapo tunakaribia kabisa katika furaha ya kweli itokayo katika uaminifu wa Mungu kwetu. Tudumu na tubaki daima katika imani na matumaini. Tuseme pamoja na mtakatifu Paulo kwamba, nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu 8:18). Jipe moyo, sema na Yesu kila siku unapokutana naye, mwambie ni mimi tena nimekuja mbele yako Ee Yesu wangu, ninaomba unikumbuke katika nia zangu, ikumbuke familia yangu, ikumbuke ndoa yangu, kumbuka watoto wangu, kumbuka biashara na kazi yangu, kumbuka masomo yangu, ninakuomba unibariki Ee Yesu wangu. Ninakuombea wingi wa baraka za Mungu, baki katika tumaini, Mungu atatenda.

Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha ya Injili
Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha ya Injili   (@Vatican Media)

Nne: Mungu anapotubariki, tunakua ushuhuda wa ukuu wake kwa wengine. Nabii isaya anawahakikishia wa Israeli kwamba, watakua mashuhuda wa matendo makuu ya Mungu kwa macho yao wenyewe, kisha watakua ushuhuda kwa watu wa mataifa. Mara kadhaa walikua na mashaka kwamba, je, Mungu ametusahau? Mungu atatubariki tena. Na watu mataifa waliwashangaa kwamba mbona Mungu wao mwenye nguvu, Mungu aishiye, anawaacha katika mateso? Nabii anawapa moyo kwamba, watakuwa ushuhuda wa matendo makuu ya Mungu. Ndugu mpendwa, Mungu aliwatumia taifa la Israeli ili kudhihirisha ukuu na utukufu, upendo na uaminifu wake. Aliwatumia hivyo taifa lake ili wawe ushuhuda wa utukufu wa Mungu kwa watu wa maifa yote. Mungu anatutumia nasi pia kupitia nyakati mbalimbali za maisha yetu kama ushuhuda kwa wengine. Huenda ustahimilivu wetu katika imani umekua chanzo cha wengine pia kuendelea kutumaini, chanzo cha kuwatia moyo wale waliokaribia kukata tamaa. Tunaposoma katika Maandiko Matakatifu Kitabu cha Ayubu tunaweza kuona jinsi gani imani ya Ayubu inavyotupa moyo sisi sote katika nyakati mbalimbali tunazopitia. Tuombe neema ya kuwa watulivu wa wastahimilivu pale Mungu anapotutumia sisi kama ushuhuda wa ukuu wake kwa wengine. Tusema pamoja na mzaburi,“Njoni sikieni ninyi nyote mnaomcha Mungu, nami nitayatangaza yote aliyonitendea” (Zab 66:16). Mungu akutimizie haja za moyo wako, nawe ukawe ushuhuda wa ukuu na utukufu wa Mungu.

Wakristo wanatumwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili
Wakristo wanatumwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili   (@Vatican Media)

Somo la Injili: Ni Injili ya Luka 10:1-12, 17-20. Somo la Injili Takatifu kutoka katika Injili ya Luka, Bwana wetu Yesu Kristo anawatuma wafuasi wake 70, wawili wawili wamtangulie kwenda kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe. Yesu yupo tayari njiani kuelekea Yerusalemu. Kristo anawatuma wafuasi wengine sabini, ishara ya kwamba, kazi ya kuhubiri habari Njema siyo ya wale mitume kumi na wawili pekee, bali ni kazi na wajibu wa watu wote. Anawatuma wawili wawili, ishara ya umoja na ushirikiano katika utume lakini pia ili ushuhuda wao uhesabiwe kuwa wa kweli kadiri ya tamaduni za Wayahudi. Kisha anawapa maelekezo na kuwatuma. Habari Njema iliyonenwa na manabii katika Agano la kale inatimizwa kwa utume na maisha ya Kristo hapa ulimwenguni na anatuachia sisi sote wajibu huo wa kutangaza habari Njema ya Injili ya furaha na matumaini. Katika somo hili la Injili dominika ya kumi na nne ya Mwaka C wa Kanisa tuna mafundisho sita ya kujifunza: Kwanza: Kazi ya kutangaza Habari Njema ni kazi ya kila mbatizwa, ni kazi yetu sote. Yesu anawatuma wafuasi wengine sabini. Hii yaturejesha katika Agano la kale katika kitabu cha Hesabu 11:16-17 ambapo Musa aliwachagua wazee sabini akaingia nao katika hema ya kukutania, na Mwenyezi Mungu akashuka akasema nao, na akawashirikisha roho ya unabii iliyokuwa juu ya Musa Nabii mkuu ili wasadiane pamoja na Musa katika kuliongoza taifa la Mungu. Vivyo hivyo, kazi ya kuhubiri Habari Njema Kristo anawashirikisha pia wafuasi wake, anatushirikisha sisi sote. Ndugu mpendwa, sisi sote tuliobatizwa tunaalikwa kuwa mashuhuda wa Injili ya Kristo kwa maneno na kwa matendo yetu. Kwa ubatizo, tumefanywa kuwa wafalme, kazi ya mfalme ni kungoza, tunapaswa kuwa mfano wa kuongoza kundi tulilokabidhiwa na Mungu, iwe ni familia yako, iongoze kwa upendo, kwa sadaka, kwa huruma, kwa wema, linda kundi lako, ili asipotee hata mmoja wapo.

Wanawekwa wakfu kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili
Wanawekwa wakfu kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili   (@Vatican Media)

Tumefanywa kuwa Manabii, kazi ya nabii ni kufundisha, kukemea na kuonya. Kuwa mwalimu wa maadili, mwalimu wa imani kwa maneno na kwa matendo. Tumefanywa kuwa makuhani, kazi ya kuhani ni kujitoa daima sadaka kama vile Kristo alivyojitoa sadaka kwa ajili yetu sisi sote. Hudumia kwa sadaka, kubali kushuka ili wengine wainuke, toa sadaka ya muda, hali, mali, karama, vipaji ili kuleta furaha, amani, matumaini na upendo kwa watu wengine. Tumebatizwa, sisi sote tu kati ya hawa sabini ambao Kristo anawatuma leo hii.  Pili: Kazi ya kutangaza habari Njema ni mpango wa kimungu, tusali na kumshirikisha Mungu. Kristo anavyowatuma hawa sabini na wawili anawaambia, mavuno ni mengi lakini watenda kazi ni wachache, basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake. Kazi ya kutangaza habari Njema sio matokeo ya nguvu na jitihada za kibinadamu bali ni kazi ya Kimungu. Tunashiriki kufanya kazi ambayo ni Kristo mwenyewe anaitenda kupitia sisi. Ndugu mpendwa, ili kuweza kuifanya kazi ya Mungu kwa mafaniko tunahitaji nguvu ya Mungu mwenyewe. Hatuwezi kufanya peke yetu kazi ya Mungu bila kumshirikisha Bwana mwenye mavuno yake. Hii yatukumbusha kuwa tunapaswa kila mara kuunganika na yule aliyetuita, akatutuma kufanya kazi kwa niaba yake. Kila mmoja kama nilivyotangulia kusema kwa wito wetu wa kwanza kama wabatizwa na kisha kila mmoja kwa wito wake ambao Mungu amemwita anaalikwa daima kuunganika na kuwa na mahusiano ya ndani na ya pekee kabisa na Kristo kwa mfano wa mzabibu na matawi yake kama anavyotufundisha Kristo katika Injili ya Yohane 15. Tujitahidi kusali na kushiriki sakramenti mbalimbali za kanisa, ibada ya misa Takatifu, kumwabudu Yesu Ekaristi Takatifu na ibada nyingine mbalimbali ambazo zinatuweka karibu zaidi na Kristo. Nyajibu zetu zinapokuwa ngumu turudi kwa Kristo, tuketi miguuni pake, atupe nguvu, atupe mwelekeo. Ainue kati yetu pia moyo na ari ya kuyashika mafundisho yake ili nasi tuwe watenda kazi hodari katika shamba lake. Mafanikio yetu yanategemea ni jinsi gani tumeunganika na Kristo aliye Bwana wa mavuno. Tatu: Injili ile izae matunda hatuna budi kumtegemea Kristo. Yesu anawaambia mitume wake wasichukue mfuko wala mkoba, wala viatu.  Katika tamaduni za Wayahudi, viatu, chakula cha njiani, fimbo na nguo ya ziada vilikua ni vitu vya muhimu sana katika safari. Licha ya kuwa vya muhimu na vinavyohitajika sana, Kristo anawaambia mitume wake wasichukue ziada. Hii ni ishara ya kwamba walipaswa kutegemea ukarimu wa kimungu, kuweka matumaini na imani yao yote kwa Kristo aliyewaita na kuwatuma. Lakini pia walipaswa kutegemea ukarimu wa watu ambao walikwenda kuwapelekea habari Njema.

Waamini wote ni mashuhuda wa furaha ya Injili na utukufu wa Msalaba
Waamini wote ni mashuhuda wa furaha ya Injili na utukufu wa Msalaba   (@Vatican Media)

Ndugu mpendwa, kazi ya kuhubiri Injili sio kazi yetu, ni kazi ya Mungu na yeye anajua jinsi tutakavyoifanya na kuikamilisha. Katika utume wetu kila mmoja kwa nafasi yake, tunapaswa kuweka imani na matumaini yetu yote kwa Kristo. Tunapoitwa na Kristo kuitenda kazi yake, tunapaswa kuachana na mambo yote ambayo yanaweza kutufanya tusimtumikie Kristo vile inavyotupasa. Tunaweza kuwaza kumtumikia Mungu na wakati huo huo tukayapa kipaumbele sana mambo ya ulimwengu huu, kazi zetu, majukumu yetu, biashara zetu, mali, fedha, vyeo, heshima nk. Tunapomwachia Mungu yote na kumfuasa kwa imani kubwa ni dhahiri kwamba hata mambo yetu menngine yote yatafanikiwa, biashara zetu zitafanikiwa, familia zetu zitakuwa na amani, nyumba zetu zitakua na upendo, masomo yetu yatafanikiwa, kazi zetu zitafanikiwa kwa kuwa tumempa Mungu nafasi ya kwanza. Mwachie Yesu kazi zako, mwachie majukumu yako, mwachie familia yako, mwachie utume wako, mwachie ndoa yako, mwambie Bwana wewe wajua yote, wajua ya kuwa nakupenda. Ninayakabidhi yote mikononi mwako, nitendee unavyotaka. Nne: Kutangaza furaha ya Injili ni jambo la dharura. Yesu anawaonya mitume wake kwamba wasimwamkie mtu njiani. Hii ina maana kuwa, kazi ya kuhubiri Injili ni kazi ya dharura, na hawakupaswa kupoteza muda njiani kwa mambo yasiyo ya muhimu. Ndugu mpendwa, kazi ya kuhubiri Injili, kazi ya ukombozi kwa ajili yetu na kwa ajili ya wengine ni jambo la dharura. Tumeshabatizwa, hatuna cha kusubiri zaidi ya kuishi kweli ushuhuda wa imani yetu. Wapo ndugu, jamaa na marafiki zetu ambao kwa namna moja au nyingine bado hawajapata ujumbe wa Neno la Mungu, au pengine wamerudi nyuma kwa sababu mbalimbali. Huenda wamekata tamaa ya maisha kwa sababu ya changamoto na magumu wanayopitia. Tuwe wa kwanza kutafutana sisi kwa sisi nyakati ambazo tunakwenda mbali na Mungu. Familia zetu zilizosambaratika ni wajibu wetu wa kufanya kila jitihada ili kuleta tena mapatano. Ni ugomvi na chuki kati yetu, tusisubiri kesho, wakati ndio sasa, saa ya wokovu ndio sasa. Tufanye jitihada kutumia vyema zawadi ya muda na maisha ya hapa duniani kuwa sehemu ya kuwainua wengine kwa njia ya ushuhuda wa maisha yetu, kuwa chanzo cha wokovu na matumain mapya kwa wengine sisi tulio mahujaji wa matumaini hapa duniani.

Utukufu wa Fumbo la Msalaba
Utukufu wa Fumbo la Msalaba   (@Vatican Media)

Tano: Kristo Yesu anatupa nguvu ya kushinda yote yanayoweza kuzuia ufanisi wa utume wetu. Kristo anawapa mitume wake nguvu ya kumshinda shetani na vikwazo vyote vinavyoweza kuzuia ufanisi wa kazi ya kuusimika ufalme wake kati ya watu. Anawapa mitume nguvu ya kuponya magonjwa, anawapa nguvu ya kukanya nyoka na ng’e na nguvu zote za yule mwovu shetani na yale yote yanayoweza kuwadhuru. Ndugu mpendwa, Kristo anapotutuma kuifanya kazi yake kila mmoja kadiri ya wito wake, anatupa na nguvu za kushinda katika magumu na mitego mbalimbali ya yule mwovu shetani. Nguvu hii tunaipata katika Neno lake, neno linalotuimarisha imani na matumaini yetu kwamba daima tupo naye, tunatembea naye, anatulinda, anatuongoza, anatuonesha njia ya kwenda, anatufundisha lipo la kusema na kutenda. Tunapokea nguvu yake pia katika Sakramenti mbalimbali za kanisa. Zinatupa nguvu na uhai rohoni, Kristo aliye chanzo cha na nguvu yetu anakaa ndani mwetu na hivyo hatuna hofu na wala yule mwovu shetani hawezi kutuangusha. Daima tusimwache Mungu, tusiwe mbali na Mungu kwa kuwa wakati tutakapomwacha ndipo shetani atapata nafasi ya kutuangusha. Tunayo nguvu ya Mungu ndani mwetu, tuwaponye watu kwa maneno maneno yetu ya kutia moyo, faraja na matumaini. Tuponye mahusiano yetu kwa kuwa tayari kujinyenyekesha, kuombana msamaha pale tunapokosana, msamaha unaponya, msamaha unatibu.

Mwenyezi Mungu anawakumbuka waja wake
Mwenyezi Mungu anawakumbuka waja wake   (@VATICAN MEDIA)

Sita: Kazi ya kuhubiri Injili si rahisi, tutakutana na changamoto, tusife moyo. Kristo anapowatuma wanafunzi wake anatambua wazi kuwa watakutana na upinzani. Wapo watakao pokea Habari Njema, lakini wapo pia ambao hawataipokea Habari Njema. alikwishawaambia kuwa ninawatuma kama kondoo kati ya mbwa mwitu, kuonesha kuwa kazi ya kuhubiri haitakuwa rahisi. Watahubiri lakini pia kwa nyakati fulani hata maisha yao yatakuwa hatarini katika kusimami mafundisho yao. Licha ya hayo, mwisho wanatoa ushuda wa furaha ya Injili, ni kwa jina la Kristo waliyaweza yote. Ndugu mpendwa, kazi ya kumhubiri Kristo haijawahi kuwa rahisi. Inakumbwa kwa nyakati zote na upinzani. Kuyafundisha mafundisho ya Kristo kwahitaji sadaka na utayari hata wa kuhatarisha maisha. Tunaishi katika ulimwengu ulio na changamoto mbalimbali ambazo twapaswa kuzitolea majibu. Unyanyasaji, vita, kutokuwajibika, ukandamizaji wa haki, mmomonyoko wa maadili na mambo mengine mengi. Haya yote yatupasa sisi kama wafuasi wa Kristo kuyasimamia bila kuogopa. Twapaswa kumwomba Kristo pia ili neema yake ifanye kazi ndani ya watu na dunia yetu iweze kuwa mahali salama ambapo ufalme wa Mungu unakua, unastawi na matokeo yake yanaonekana wazi. Somo la pili: Ni Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia 6:14-18. Katika somo la pili, mtume Paulo anawaandikiwa Wagalatia ambao walisumbuliwa na watu waliokuja kufundisha mafundisho ya uwongo baada ya Mtume Paulo kuhubiri na kuondoka. Aliwakasirika Wagalatia ambao kwa haraka walishasahau na kuyaacha mafundisho ya kweli kutoka kwa Paulo, juu ya thamani ya sadaka ya Kristo juu ya kazi na matendo ya sheria. Kutahiriwa wala kutotahiriwa si kitu bali kuipokea Injili ya Kristo, Injil ya furaha na matumaini kwa watu wote, wayahudi hali kadhalika na watu wa mataifa. Na kwa njia hiyo tunashirikishwa mateso na kifo cha Kristo. Sisi sote kwa njia ya ubatizo tunapokea neema hii kubwa ya ukombozi, nasi tunapaswa kuona fahari juu ya thamani hii ya ukombozi wetu. Hitimisho: Ndugu mpendwa, Mungu anatupenda kwa mapendo makuu. Kuna nyakati kila mmoja wetu anapitia katika changamoto mbalimbali. Katika yote tutambue kuwa Mungu yupo nasi daima, anatupenda, anatukumbuka, anatuahidi mwanzo mpya, siku mpya za furaha na amani, na utulivu. Tumwombe atuongezee daima imani na saburi katika kungojea ahadi zake kwetu, yeye ni mwaminifu, atatenda kwa wakati wake.

Tafakari D 14 ya Mwaka C

 

 

 

05 Julai 2025, 16:07