Malawi:watoto 1400 kushiriki Kongamano la I kitaifa kama wamisionari wa matumaini!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Watoto na barubaru 1,400, wenye umri kati ya miaka 8 na 14, wakisindikizwa na viongozi 200, kutoka Majimbo yote nane nchini wanatarajiwa mjini Lilongwe kuanzia 31 Julai 2025 na kuwa wahusika wakuu wa Kongamano la 1 la Kitaifa la Utoto, lililohamasishwa na Baraza la Maaskofu la Malawi, lililoandaliwa na Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa (PMS), na kuungwa mkono na Sekretarieti ya Kimataifa ya Shirika la Kipapa la Utoto wa Kimissionari. Kauli mbiu ya mpango huo uliopangwa kufanyika kuanzia Julai 31 hadi Agosti 4 katika Parokia ya Don Bosco mjini Lilongwe, ni “Watoto ni Wamisionari wa Matumaini,” kufuatia ujumbe wa Siku ya Kimisionari Duniani kwa mwaka 2025.
Kukuza mbegu ya kimisionari kwa vizazi vijavyo
Kongamano linalenga kukuza mbegu ya roho ya kimisionari katika vizazi vijavyo, ili watoto na vijana waweze kuwa "wainjilisti" kati ya wenzao. Kauli mbiu ya Kongamano ni "Watoto waombee watoto na wasaidie watoto wengine." Vipindi vya siku hizi vitabadilishana shughuli mbalimbali: michezo, tamasha za kwaya, chemsha bongo za Biblia, ukumbi wa michezo, ngoma za kitamaduni, maonyesho ya vipaji, na mikutano kuhusu mada za maendeleo ya kiroho na kibinadamu, mafundisho ya Kikatoliki, sakramenti, liturujia, ustawi wa akili, ulinzi wa watoto, biashara haramu ya binadamu na ajira ya watoto, watoto na teknolojia, na hatimaye mabadiliko ya hali ya hewa.
"Katika Kanisa Katoliki la Malawi, hasa katika Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu wa kimisionari, tumejawa na furaha na shauku kwa ajili ya tukio hili kubwa na linalosubiriwa kwa hamu, la kwanza katika historia yetu," alieleza mkurugenzi wa PMS nchini Malawi, Padre Ephraim Peter Madeya, ambaye pia alisimamia awamu nzima ya maandalizi ya Kongamano hilo, linalofanyika na katika ngazi za kitaifa kupitia kamati za jimbo.
Wageni wa ndani na nje ya nchi
Vikao vya Kongamano vitaongozwa na wageni wa ndani na nje ya nchi, akiwemo Sista Inês Paulo Albino A.S.C., Katibu Mkuu wa Shirika la Kipapa la Wamisionari la Utoto Mtakatifu na Dalia Braithwaite, Mratibu wa Elimu ya Kimisionari kwa Jimbo Kuu la Boston nchini Marekani. Padre Kizito Nhundu, Mkurugenzi wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, naye atawasili kutoka Zimbabwe akiwa na takriban wajumbe kumi na watano.