Dominika ya 15 ya Mwaka C wa Kanisa: Injili ya Msamaria Mwema: Kilele cha Amri Kuu ya Upendo
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican leo Dominika ya 15 ya Mwaka C wa Kanisa. Ujumbe wa Dominika ya Utume wa Bahari tarehe 13 Julai 2025 unanogeshwa na kauli; “Mahujaji wa matumaini, Madaraja ya Kuwakutanisha Nchi Maadui, Manabii wa Amani.” Kwa hakika bahari ni kiungo muhimu sana kwa Jumuiya ya Kimataifa, changamoto na mwaliko wa kuwa na mwelekeo mpana zaidi, kwa kudumisha amani badala ya kuendekeza migogoro, mipasuko na vita. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Rej. Gaudium et spes, 1. Huu ni ujumbe mahususi kwa watu wa Mungu, Waraka huu wa Kanisa Katika Ulimwengu Mamboleo, kwa mwaka 2025 unapoadhimisha kumbukizi ya miaka 60 tangu kuchapishwa kwake. Mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao, kamwe wasijisikie pweke, katika mchakato wa kutafuta haki, utu, heshima na furaha ya kweli. Maendeleo fungamani ya binadamu ni mchakato unaowakumbatia na kuwaambata watu wote: kimwili, kiroho na katika mwelekeo wa kijumuiya. Mahali ambapo Injili inatangazwa, inamshuhudia na kumkaribisha Kristo Mfufuka, lazima kunatokea mabadiliko na Ulimwengu hauwezi kubaki kama ulivyo, kwa sababu Yule aliyeshinda dhambi na mauti anasema, “Tazama, nayafanya yote kuwa mapya.” Ufu 21:5.
Kwa mfano wa Msamaria mwema Kristo anatufundisha namna ya kuyaishi mausia ya somo I (Kum 30:10-14), kwamba Neno la Mungu halipo mbali bali li karibu nasi, katika kinywa chetu na moyo wetu tupate kulifanya... Msamaria mwema ni kilele cha Amri Kuu ya mapendo. Mfano huu unanogeshwa na wahusika wanne... wa kwanza ni majeruhi, muhanga wa ujambazi, huyu bwana anaonekana kuwa na tabia ngumu na ya peke yake, kwanza hajulikani ni mtu wa namna gani, Yesu anamwita tu ‘mtu mmoja’, hatujui jinsia yake, kazi yake, umri wake, kabila lake, alitoka Yerusalemu kufanya nini, anaenda Yeriko kwa nani, kwa shughuli gani nk tunachojua alikuwa “mtu” na hilo linatosha. Anashuka kutoka Yerusalemu ulio “Mlima Sayuni” na fahari ya Israel, mji wa amani, mji wa Daudi, mlimani pa BWANA anashuka kwenda Yeriko, mji uliolaaniwa (Yosh 6:26). Yeriko ulikuwa kilomita 27 kutoka Yerusalemu, njia ya mteremko mkali wa mita zaidi ya 2000, kokoto na magenge, majambazi(wanyang’anyi) walitumia njia ile kupora mali na fedha za watu wanaotoka kufanya biashara Yerusalemu kwa kuvizia kwenye miamba, iliitwa njia ya damu, watu walipita kwa makundi tena nyakati za mchana. Huyu “mtu mmoja” anapita peke yake na yanamkuta yaliyomkuta. Vibaka na panya road havijaanza leo tukemee, kwa kuhimiza maadili, Kutenda haki, ili kuwe na amani hasa kutengeneza fursa kwa vijana ili wapate kazi halali na zenye utu.Wa pili alikuwa kuhani, hakutaka kunajisika kwa kugusa maiti, kwake ilikuwa ‘usafi kwanza’ akapita kando kuwahi zamu yake hekaluni... wa tatu ni mlawi, huyu anaonekana kuijua mitego ya majambazi, ni kama mrembo anayesimamisha gari usiku kuomba msaada ili waliofichama kando wakuvamie na kukupora, kwa mlawi ni ‘usalama kwanza’ akapita zake. Kuhani na Mlawi wanashika amri kwa nadharia bila matendo, na huo ni umasikini mkubwa.
Mhusika wa nne alikuwa Msamaria, adui ya wayahudi na mtu duni mbele yao lakini ndiye shujaa wa mfano wa leo... Nimependa maneno ya Yesu anavyoelezea tendo la kujali la Msamaria kuhusu majeruhi yule.. kwanza alimwona (wengi hatuwaoni wenzetu katika dhiki zao), kisha akamhurumia, akamkaribia, akamfunga jeraha zake, baada ya kuzitia mafuta na divai, dawa bora aliyokuwa nayo kwa wakati ule, akampandisha juu ya mwanapunda wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza, akamkabidhi mwenye nyumba ya wageni, amtunza na kulipa gharama... nzuri mno! Kingine, anaonekana ni mtu mwaminifu wa kuaminika hata na mwenye nyumba ya wageni kwamba gharama zitakazozidi atazilipa baadaye, upendo wa Mungu umeujaza moyo wake… hii ni zaidi ya shule kwangu na kwako!
UFAFANUZI: Katika Injili – Luka 10:25?37 Mwalimu wa sheria anamwuliza Yesu, “Nini nifanye ili kupata uzima wa milele?” Yesu anamrejeshea maneno ya Sheria: upendo kwa Mungu na jirani. Kisha anaelezea hadithi ya Samaria aliyeonyesha huruma kwa mwathirika aliyependekezwa — akamponya, akampeleka kwenye nyumba ya wageni, na kukipa gharama—na kumwambia mwana sheria atoke na yeye afanye vivyo hivyo. Katika Injili ya leo, tunaona mtu aliyejeruhiwa kando ya barabara—ameachwa na wale waliotarajiwa kumsaidia, lakini Samaria (asiyeheshimiwa kidini) ndiye anayesimama na kumhudumia. Yesu anatuambia: “Nenda ukafanye vivyo hivyo.” (Lk 10:37) Upendo hautokani na Sheria peke yake, bali huzingatia huruma, kama mbegu inayopandwa na kisha kumea na kustawi.Kutoka mfano wa Msamaria mwema tujifunze yafuatayo… Mosi, wanyang’anyi wapo... tubaki Yerusalemu tusishuke kwenda Yeriko, maana yake tuchuchumie mambo mazuri, tupiganie mazingira bora na yenye usalama, tusitembee peke yetu bali tuongozane na Mungu na wenzetu kwa njia ya sala na maombi kila wakati. Kwenda Yeriko kwa njia ya hatari ni kuishi maisha yasiyo na Mungu, mahusiano yasiyo na afya, udhanifu mbaya, kutothaminiana, kutojaliana... wengi tunatembea, tunadhani tunakwenda wapi? tunapanda kwenda Yerusalem mji wa baraka au tunashuka Yeriko kulikolaaniwa? tupo ambao mwendo wetu unatuelekeza juu na wengine tunaelekea chini kwenye maangamizi... Hadithi ya Samaria inaleta ujumbe wa halisi: jirani ni yule ambaye anasimama karibu, analeta faraja, anatoa gharama, na anafungua moyo wake-si tusitegemee watu wanaofanana nasi, au wenye unasaba nasi hata tusio wajua wanatuhusu kwa utu wao. Ni aina ya utume ambao lazima tuonyeshe kila siku-kutangaza huruma ya Mungu kwa jirani kwa maishsa ya kawaida ya kusaidiana kibinadamu.
Pili, tusipobaki Yerusalemu kwa hakika tutaangukia mikononi mwa wanyang’anyi, hawa kazi yao sio ndogo, Kristo amesema hawa jamaa agenda zao huwa tatu, “mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu” (Yn 10:10a)... Wanyang’anyi ni akina nani? mara si haba ni watu wa karibu, huenda tunawasaidia na kuwaamini, watu tunaowapenda “na mtu atamwambia je, jeraha hizi ulizonazo kati ya mikono yako ni nini? naye atajibu, ni jeraha nilizotiwa katika nyumba ya rafiki zangu” (Zek 13:6).. Yuda mwana wa Simoni Iskariote hakuwa mtu wa mbali, aliketi mezani pa Kristo na akamsaliti vilevile. Hawa wanyang’anyi tunaoangukia mikononi mwao wakituacha karibu kufa wanaweza kuwa wazazi, kaka na dada, marafiki, wenzetu katika kazi na huduma, watu tunaowapenda... uwapo taabuni ni kama hawakuoni, ni kama hawakujui, ukifanikiwa wanakuja na kusema ‘sisi ni ndugu zako’, uwe macho sababu wanaweza hata kukujeruhi wakiwa na midomo yenye tabasamu... Pamoja na ndugu wa karibu wanyang’anyi wanaweza kuwa watu wenye chuki nasi, wanatupiga za uso, mchana wa jua kali, wanaweza hata kuwageuza ndugu na rafiki zetu kuwa adui (Zab 56:2.)
Halafu yupo mnyang’anyi mbaya kuliko wote... wewe mwenyewe! ndio, unaweza kabisa kuwa mnyang’anyi wa nafsi yako mwenyewe! Unaweza kumkwepa mkorofi au kupambana na anayekuchukia lakini adui aliyemo ndani mwako humuoni na hivi hagunduliki mapema na athari zake ni mbaya kuliko ya adui wa nje “...maana dhambi zangu zimenifunikiza, kama mzigo mzito zimenielemea mno, jeraha zangu zinanuka sababu ya upumbavu wangu, nimepindika na kuinama sana, mchana kutwa nimekwenda nikihuzunika” (Zab 38:4-6)... hivi tunapojaribu kupambana na wanyang’anyi nje yetu tujipe muda kumgundua mnyang’anyi aliye ndani yetu, hizo ni tabia, hulka na matendo ya mazoea yasiyofaa. “... akaangukia kati ya wanyang’anyi”... hao walianza kwa kumvua nguo, ishara ya kuaibishana na dharau, tunaweza kununua nguo nyingine lakini ndio ushaaibika tayari, ni ngumu kujenga jina zuri lakini kuliharibu ni sekunde tu na kulijenga upya jina lililochafuliwa ni karibu haiwezekani... Halafu wakamtia jeraha, wengi tumejeruhika jeraha zisizopona ndani ya mtima wetu, tumeachwa karibu kufa. Huenda tunawalaumu ndugu zetu kwa wanayotenda lakini si ajabu wanafanya hayo kwa vile wametiwa jeraha. Kidonda cha nje ni rahisi kukitibia lakini cha moyoni ni mtihani. Mbaya zaidi tukiachwa bila msaada kama kuhani na mlawi walivyofanya.. tunakataliwa, tunatiliwa mashaka, hatueleweki na wenzetu, tunatengwa na kubaguliwa.
Mtu aliyejeruhiwa ni mfano wa walioachwa nyuma: maskini, wakimbizi, waliopoteza kazi, vijana waliokata tamaa. Bwana Yesu anatudai mapinduzi... kwamba ni lazima tumsaidie jirani hata kama amejitakia mwenyewe kama mtu yule aliyesafiri njia hatari ya Yeriko peke yake, halafu mtu yeyote bila kujali tunamjua au la ni ndugu yetu, na mwisho tuiweke amri kuu ya mapendo katika utendaji, tusiishie tu kusema ‘pole sana’ bali tunyooshe mkono wa kusaidia. Huruma inapata maana yake ikiwekwa katika matendo. usimwache pale, simama, mshike mkono.Kanisa linaitwa kuwa “huruma inayoonekana,” si jumba la sheria kali. Baba Mtakatifu anakazia kuwa lazima kutoka nje, hata kama wewe si mkamilifu-kama Msamaria mwewma. Yesu anakemea tusiwe “ kama kuhani au Mlawi,” bali kuwa kama yule mtu aliyechukua hatua.Jubilei ya matumaini inatusukuma kusema: “Leo mimi nitakuwa mtu wa matumaini kwa mwingine hata kama simfaha ila kwa sababu ameumwa kwa sura na mfano wa Mungu.” Tujitahidi kutokuwa wanyang’anyi kwa wenzetu, tusije ili kuiba na kuchinja na kuharibu... katika hili tutakuwa wafuasi wa kweli wa Kristo ambaye kadiri ya somo II (Kol 1:15-20) ni “mfano kamili wa Mungu asiyeonekana... Kichwa cha mwili wake yaani Kanisa… mzaliwa wa kwanza katika wafu… katika yeye kuna utimilifu wote…” Tunaalikwa kuwa waleta matumaini, si kwa maneno tu, bali kwa vitendo vya huruma vinavyotufanya kuwa mabalozi wa Jubilee hii. Huu si mwaka wa sherehe tu, bali wa matendo ya matumaini yanayoonekana. Ni mwaka wa “kubadili fikra kutoka kukata tamaa kwenda matumaini.” Kwa lugha nyingine: kutoka hofu hadi matumaini hai.