Askofu Mkuu Isaac Amani Massawe Jubilei Miaka 50 ya Upadre
Na Sarah Pelaji, Vatican Na Sr. Ernestina Patrick Lasway, SAC., Arusha.
Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jubilei ni kipindi cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Ni wakati muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka anazowakirimia waja wake hata bila mastahili yao. Ni muda wa kuomba msamaha kwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika maisha na utume, tayari kuomba tena neema na baraka ya kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi, tayari kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini kwa watu waliovunjika na kupindeka mioyo! Katika tukio adhimu la kihistoria kwa Kanisa Katoliki nchini Tanzania, maelfu ya waamini, viongozi wa Kanisa, viongozi wa serikali na wageni kutoka sehemu mbalimbali nchini Tanzania walikusanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Theresa, Jimbo Kuu Katoliki Arusha, kushiriki Misa Takatifu ya shukrani ya Jubilee ya miaka 50 ya Upadre wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha Isaac Amani Massawe. Ibada hiyo takatifu iliyofanyika tarehe 20 Julai 2025, iliongozwa kwa namna ya kipekee na kuhudhuriwa na maaskofu kutoka majimbo mbalimbali nchini Tanzania, akiwemo Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Wolfgang Pisa OFM Cap, Makamu wake Askofu Eusebius Nzigilwa, pamoja na viongozi wa juu wa Serikali, familia na waamini kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Katika mahubiri yake ya siku hiyo, Askofu Rogath Kimario wa Jimbo Katoliki Same, ambaye ndiye alikuwa mhubiri rasmi wa sherehe hiyo, alieleza kwa kina maana ya maadhimisho ya Jubilei kama kutimilika kwa neema ya Mungu katika maisha ya wito. Akirejea Injili ya Yohane 6:52-69, Askofu Kimario alibainisha kuwa swali la Yesu kwa wanafunzi wake kama wanataka kuondoka lilikuwa ni jaribio la imani na mwaliko wa kudumu katika sadaka ya Ekaristi Takatifu. Akizungumza kwa uchaji na heshima, Askofu Kimario alisema: “Askofu Amani amekuwa mfano wa kweli wa uaminifu katika wito wake. Ameonesha kiu ya Ekaristi Takatifu, moyo wa uchungaji, hekima ya malezi, na umoja ndani ya kanisa na taifa.” Alisisitiza kuwa maisha ya Askofu Amani yanadhihirisha kaulimbiu yake ya kiaskofu: "Mwondoko: Kujitambua, Kuwajibika na Kushirikiana katika Kristo kwa Matendo."
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC., Wolfgang Pisa OFM Cap, akitoa salamu kwa niaba ya Baraza, alimpongeza Askofu Amani kwa uongozi wake wa mfano katika kipindi cha nusu karne kama Padre, miaka 17 ya Uaskofu, na miaka 7 ya kuwa Askofu Mkuu. “Askofu Amani siyo tu mchungaji bali pia mwalimu na kiongozi. Ameandika barua za kichungaji, amekuwa msikivu kwa waamini, na kiongozi mwenye maono katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge,” alisema Askofu Pisa. Katika hotuba yake ya shukrani, Mhashamu Askofu Mkuu Amani alionesha unyenyekevu wa kiroho kwa kumshukuru Mungu na wale wote waliomsindikiza katika safari yake ya maisha na wito. Akinukuu Zaburi 138:1 alisema, “Nitakushukuru kwa moyo wangu wote, mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.” Alisisitiza kuwa wito wa upadre ni furaha ya kumtumikia Mungu na kuwahudumia watu wake. Askofu mkuu Amani pia aliwahimiza vijana na watoto kujitayarisha vyema kwa miito mbalimbali, hasa wito wa ndoa, alioufananisha na “kitalu cha miito mingine ya maisha ya kitakatifu.” Aliwataka wazazi kuwa walezi bora kwa watoto wao ili kuwasaidia kugundua na kuishi wito wao kwa uaminifu. Alihitimisha kwa kuwasihi waamini kuendelea kuiombea nchi amani, maendeleo na ustawi.
Maisha na Safari ya Kihistoria ya Askofu mkuu Amani: Askofu Mkuu Isaac Amani alizaliwa tarehe 10 Juni 1951 katika Kijiji cha Mloe, Parokia ya Mango, Jimbo Katoliki Moshi. Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Mango, kisha akaendelea na masomo ya seminari ndogo ya Mtakatifu Yakobo Jimbo la Moshi. Baadaye, alisoma falsafa katika Seminari Kuu ya Ntungamo mnamo 1970 – 1972 na Taalimungu katika Seminari Kuu ya Kipalapala iliyopo Jimbo Kuu Katoliki Tabora mnamo 1972 – 1975. Alipata Daraja Takatifu la Upadre tarehe 29 Juni 1975 katika Jimbo Katoliki Moshi. Safari ya kichungaji na uongozi: Baada ya kupadrishwa, alihudumu kama Paroko Msaidizi katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Narumu mwaka 1975 – 1976 na Moshi Kanisa kuu 1976 –1979. Kati ya mwaka 1980 - 1986, alihudumu kama Mwalimu na Makamu Gambera wa Seminari Ndogo ya Mtakatifu Yakobo, Moshi. Aliendelea na masomo ya elimu na ushauri wa kichungaji katika Chuo Kikuu cha Walsh, Ohio, Marekani mwaka 1986 – 1989. Baada ya kurejea, alihudumu kama Padri na Mlezi wa Shirika la Mabruda wa Mkombozi Jimbo Katoliki Moshi mwaka 1990 – 2003 na pia alikuwa Paroko wa Kanisa Kuu la Kristo Mfalme, Jimbo Katoliki la Moshi kuanzia Julai 2003.
Daraja Takatifu la Uaskofu: Tarehe 21 Novemba 2007, aliteuliwa na Papa Benedikto XVI kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Moshi na kuwekwa wakfu tarehe 22 Februari 2008. Baadaye, tarehe 27 Desemba 2017, Papa Francisko alimteua kuwa Askofu mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha na kusimikwa rasmi tarehe 8 Aprili 2018. Maadhimisho ya jubilei ya miaka 50 ya upadre: Maadhimisho haya ya Jubilei ya Miaka 50 ya Upadre wa Askofu mkuu Isaac Amani ni fursa ya kutafakari na kusherehekea maisha ya huduma ya kiroho na uongozi uliotukuka. Ni wakati wa waumini na jamii kwa ujumla kumshukuru Mungu kwa zawadi ya kiongozi huyu na kuendelea kumwombea afya njema na nguvu katika kuendeleza utume wake.