杏MAP导航

Tafuta

Maaskofu Katoliki Tanzania wamewataka watanzania kukita maisha yao katika kutangaza na kushuhudia: ukweli, haki na amani. Maaskofu Katoliki Tanzania wamewataka watanzania kukita maisha yao katika kutangaza na kushuhudia: ukweli, haki na amani.  

Watanzania Kiteni Maisha Yenu Katika: Ukweli, Haki na Amani

Katika maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste kwa Mwaka 2025, baadhi ya Maaskofu Katoliki Tanzania wamekazia umuhimu wa Watanzania kupenda kutawaliwa na fadhila za kimungu yaani: za haki, amani, ukweli na maridhiano ili kuendelea kulijenga taifa kulingana tunu walizoacha waasisi wa taifa la Tanzania. Hali ya haki, amani na maridhiano ni tete nchini Tanzania, kumbe kuna haja ya watanzania kujiuliza ni mambo yepi ambayo yamepelekea hadi kufikia hapo!

Na Sarah Pelaji, - Vatican.

Sherehe ya Pentekoste: Hii ni Siku Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume, utimilifu wa ahadi ya Kristo Yesu, mwanzo wa maisha mapya. Hii ni Siku ambayo Kanisa lilizaliwa, Mitume wakapata ari na ujasiri wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Kwa Sherehe ya Pentekoste, waamini wanaitwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya maisha yao; ili kuyatakatifuza malimengu. Ni mwisho wa Kipindi cha Pasaka! Katika maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste ujumbe wa: ukweli haki, amani umeendelea kutawala katika siku hiyo ambapo baadhi ya Maaskofu Katoliki Tanzania wamekazia umuhimu wa Watanzania kupenda kutawaliwa na fadhila za kimungu yaani: za haki, amani, ukweli na maridhiano ili kuendelea kulijenga taifa kulingana tunu walizoacha waasisi wa taifa la Tanzania. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi OFM Cap., wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam wakati wa mahubiri yake katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu Jimbo kuu la Dar es Salaam alitoa katekesi juu ya Pentekoste kwa kusema kwamba, “Roho Mtakatifu ni zawadi tuliyozawadiwa na Bwana Yesu Kristo. Ndiye uhai, chimbuko na nguvu ya Kanisa.  Alieleza kuwa Mitume wa Yesu walijifungia ndani wakiwaogopa Wayahudi kwa sababu Wayahudi walimtenda vibaya Yesu Kristo kwa namna ambayo haikuzingatia haki. Yesu aliyeteswa, aliyekufa na aliyefufuka hakutendewa haki. Changamoto na mwaliko kwa watanzania kujikita katika kutenda haki. Katika mazingira hayo ya woga Bwana Yesu aliwaahidia wafuasi wake kwamba atawapelekea mfariji, mtetezi, mwalimu, na mwanga ambaye atawatia nguvu na kuwapa uthubutu wa kusimamia ukweli, haki na yote ambayo yanampendeza Mungu. Siku ya Pentekoste ahadi ya Kristo Yesu ilitimia. Mitume wakiwa katika ubaridi wa woga wakajikuta wanashukiwa na Roho Mtakatifu.

Sherehe ya Pentekoste: Roho Mtakatifu anawashukia Mitume, Mwanzo wa Kanisa
Sherehe ya Pentekoste: Roho Mtakatifu anawashukia Mitume, Mwanzo wa Kanisa

Pamoja na mambo mengine amesisitiza waamini na wote wenye mapenzi mema kuishi matendo makuu ya Mungu na jambo la kwanza likiwa ni tendo la ukweli kwa sababu Mungu mwenyewe ni ukweli hivyo kila mmoja aishi, kutetea, kusimamia na kuuishi ukweli. Tendo jingine la Mungu ni haki ambayo ni zawadi ambayo Mungu anawakirimia wanadamu kwa mwenendo wa maisha yao. Hivyo lazima kila mwanadamu awe tayari kumpa kila mtu mastahili yake. “Usimpunje, usimwonee, usimdhulumu wala kumyang’anya mtu haki yake. Unapofanya kinyume unaenda kinyume na utashi wa Mungu, kinyume na misingi ya haki na kinyume na misingi ya Roho Mtakatifu. Aidha ameeleza kuwa, kazi ya Mungu ni amani akisisitiza kuwa, amani siyo ukosefu wa vita na siyo utulivu holela bali ni uwepo wa mahusiano yaliyotengemaa katika nyanja zote. Ili iwepo amani ya kweli iliyotengamaa lazima iwemo kwenye mahusiano katika ya mtu na nafsi yake. Pia lazima yawepo mahusiano yaliyotengamaa katika ya mtu na mtu na mtu na mazingira yake. Pia kunao ulazima wa kutengeneza mahusiano bayana na ya juu kabisa kati ya mwanadamu na Mungu wake ili aishi katika hali ya neema. “Kama raia wa Tanzania, nchi ambayo tunajitapa kama kisiwa cha amani tupende kushughulikia mambo yetu kwa msingi wa ukweli, haki na amani na unaompendeza Mungu ili tuendelee kudai kuwa sisi ni kisiwa cha amani. Katika yale yanayoendelea katika zama hizi katika nchi yetu ninashauri tusithubutu kujiita kuwa ni kisiwa cha amani, tusithubutu kujitanabaisha kama kisiwa cha amani. Tumwombe Mungu atubadilishe, atugeuze, atuongoe na atufanye kweli watu wanaoakisi amani yake. Tumwombe Roho Makatifu atuimarishe.

Askofu Stephano Lameck Musomba, OSA: Haki, Ukweli na Amani
Askofu Stephano Lameck Musomba, OSA: Haki, Ukweli na Amani   (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Askofu Musomba asema: Hatuwezi kuwa na amani bila haki na ukweli: Naye Askofu Stephano Lameck Musomba OSA wa Jimbo Katoliki Bagamoyo katika maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste alihamashisha amani Tanzania akitaka maridhiano ya kitaifa, ili Kanisa liweze kufanya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili katika watu waliojawa na amani. Amedokeza juu ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Mwezi Oktoba mwaka huu 2025 akisema, watanzania wachague viongozi wanaoweza kusimamia ukweli katika mambo yanayofaa.  Viongozi walio na wajibu wa kusema ndiyo pale panapostahili kusema ndiyo na hapana pale panapostahili kusema hapana. “Unachagua mbunge anayeenda kukuwakilisha bungeni kwa kusema ndiyo kwa kushabikia kila kitu, hapana, tunahitaji viongozi wakweli… Yaani ndiyo katika kila kitu kwenye ulimwengu huu inatupeleka wapi? Huko ni kutesa watu. Wakati mwingine katika harakati za siasa zetu hapa Tanzania unasikia viongozi wa dini wanashutumiwa kuwa wamechanganya siasa na dini. Hivi tunawezaje kufaulu kuhubiria mtu anayekufa kwa njaa, watu wanaonyanyaswa, wanaopigwa makofi na kuhuzunika halafu mimi kiongozi wa dini nakuja na mahubiri ya kawaida ya Mungu anawapenda endeleeni hivyo hivyo, hiyo ni Injili ipi ninayoihubiri,” alihoji Askofu Musomba. “Mafundisho jamii ya Mama Kanisa yanaweka bayana kwamba hatuwezi kuhubiri Injili pale ambapo haki haitendeki, tuhubiri Habari Njema pale ambapo haki inatendeka maana tutaulizwa na Mungu wewe hukukemea hapa, hukuwa na sauti ya kinabii, watu wanateseka na wewe umekaa kimya.”

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi Tanzania si tena Kisiwa cha amani
Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi Tanzania si tena Kisiwa cha amani

Ujumbe wa Mungu unamjia mwanadamu katika mazingira yake ya kijamii, kisiasa na kidini. Huwezi kumtenganisha mwanadamu kwamba leo yupo kwenye siasa kesho yupo kwenye dini kwani Wanafalsafa walisema mwanadamu ni mwanasiasa na mwajamii kwa asili yake. Hata kwenye familia kuna siasa. Ukisoma mitandao ya kijamii baadhi wanapendekeza kwamba kiongozi wa dini anapaswa kuwaelimisha waamini maana ya Pentekosite tu, nasi tunamfundisha asili na maana ya Pentekoste katika mazingira yake ya sasa kwamba: Roho Mtakatifu aliwashukia Mitume akawapa nguvu ya kutangaza na kuenenza imani, wakaondolewa woga hivyo Kanisa likazaliwa na Injili ikasambaa duniani kote katika misingi ya kuuishi ukweli wa Mungu. “Kama wakristo, Pentekoste inatupa ujasiri wa kusema ukweli, kuishi amani ambayo ni zawadi ya Kristo Yesu aliyotupa wakati wa Pasaka,” ameeleza. Aidha amesisitiza kuwa katika dunia hii ili kuishi vizuri unaowatangazia amani lazima haki itendeke ili pawe na amani. Kama hatuheshimiani tukae chini tujitathmini kwanini tumefika hmu. Ukienda kwenye mitandao ya kijamii inatia huruma kuona namna vijana wadogo wanavyotukana lakini lazima tukae chini tuambizane kwanini tumefika hapo.

Hali ya haki, amani na maridhiano Tanzania kwa sasa ni tete sana
Hali ya haki, amani na maridhiano Tanzania kwa sasa ni tete sana

Askofu mkuu Nkwande ataka mazungumzo ya kitaifa: Askofu mkuu Renatus Nkwande wa Jimbo Kuu Katoliki Mwanza katika misa ya maziko ya Mzee Silvin Ibengwe Mongella ambaye ni mume wa Mama Getrude Mongella aliyefariki dunia tarehe 31 mwaka huu 2025  na kuzikwa  tarehe 7 Juni 2025 jijini Mwanza, aliwaambia waamini pamoja na viongozi wa serikali walioshiriki maziko hayo kuwa, wafanye tathmini katika yote yanayotokea nchini Tanzania na kuratibu namna ya kufanya muafaka wa majadiliano ya kitaifa ili kila mmoja atoe mawazo yake na hatimaye waweze kufikia mwafaka wa pamoja. “Lazima tukiri kuwa taharuki ipo tena tupo katika mahangaiko. Vijana wanasema mengi kwenye mitandao, wakati mwingine wanatukana, kila mmoja anasema la kwake. Hii si ishara nzuri kama taifa. Ninatambua kutokana na mila zetu kuna staha ya kuzungumza na mtu ambaye ni mkubwa kwako lakini ukiona vijana wanatukana mtu mzima anayeweza kuwazaa bila woga lazima tushtuke tufanye mazungumzano ili kusikiliza sauti za wote kwani hatuwezi kupata suluhisho kwa kuzomeana au kubezana. Tusiwazie watu kusema bali tusikilizane na kujitathmini ni kitu gani kimetufikisha hapa. Lazima viongozi wawe mstari wa kwanza kujiuliza kwanini watu wanashambuliana huku wengine wakiishi kwa woga hata wachungaji kutembea na walinzi maana pengine amenusa shida. Viongozi ambao wamepewa dhamana ya kulinda watanzania, watafute jukwaa la kuwakutanisha    watanzania ili waweze kuzungumza kwa huru na kutoa hoja na maoni yao. Utaratibu unaondelea ambapo watanzanaia kila mmoja akizungumza yake hapo kila mmoja atataka lake lipite si utaratibu mzuri. Kuendelea   haiwezekanila sivyo litakuwa ni taifa la ajabu. Historia na mnyororo wa amani ili isiharibikie kwenu kwani historia itadai amani ya Tanzania iliharibika wakati gani na nani alikuwepo madarakani.  Mnalo jukumu la kutafuta suluhisho tusipotoa fursa hii kila mmoja atazungumza lake. Tusizuie watu kusema, bali tujiulize ni kitu gani kimetufikisha hapa,” amesema.

Pentekoste Amani
11 Juni 2025, 14:58