Siku kuu ya Mtakatifu Karoli Lwanga na wenzake mashahidi
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mtakatifu wa Siku ni mapitio ya kila siku ya Watakatifu, yaliyohifadhiwa katika kumbukumbu ya Kanisa. Historia za walimu wa maisha ya Kikristo wa nyakati zote ambao, kama miale angavu, hutuongoza njia. Ni katika Muktadha huo ambapo Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 3 Juni uwakumbuka Mtakatifu Karoli Lwanga na wenzake wa Uganda. “Nitakushika kwa mkono, ikiwa ni lazima tufe kwa ajili ya Yesu, tutakufa pamoja, tukiwa tumeshikana mikono:”Haya ni maneno ya mwisho yaliyosemwa na Karoli Lwanga na kumwambia kijana Kizito, ambaye alikufa naye akiwa na umri wa miaka 14 tu, kwa sababu ya watesi wao kuichukia imani. Kuuawa kwa imani pamoja wenzake, Wakatoliki na Waanglikani, walioathiriwa na mateso dhidi ya Wakristo yaliyotokea nchini Uganda mwishoni mwa 1800.
Mkutano na “Mababa Weupe”na uongofu kwa Ukristo
Historia yao ilifanyika chini ya utawala wa Mwanga II, mfalme wa Buganda (sasa ni sehemu ya Uganda), kati ya Novemba 1885 na katikati ya 1886. Karoli, hasa, alikuwa wa ukoo wa Ngabi, lakini maneno ya Injili yanayosemwa na kushuhudiwa na Wamisionari wa Afrika, wanaojulikana zaidi kwa jina la “Mababa Weupe” shirika lililoanzishwa na Kardinali Lavigerie, yana mvuto kwake. Kijana Lwanga aliongoka na kuwa Mkristo na mwaka 1885, aliitwa mahakamani kama gavana wa Jumba la Kifalme. Tangu mwanzo kabisa, alikuwa kielelezo kwa wengine, hasa kwa waongofu wapya, ambao imani yao aliiunga mkono na kuitia moyo.
Mwanzo wa mateso
Hapo awali, Mfalme Mwanga - ambaye pia alielimishwa na "Mababa Weupe", lakini mkaidi sana na waasi - alimkaribisha kwa ukarimu. Kisha, akichochewa na waganga wa kienyeji walioona nguvu zao zikiathiriwa na nguvu ya Injili, mtawala huyo alianza mateso ya kweli dhidi ya Wakristo, hasa kwa sababu hawakubaliana na matakwa yake yasiyofaa. Mnamo tarehe 25 Mei 1886, Kalori Lwanga alihukumiwa kifo, pamoja na wengine. Siku inayofuata, mauaji ya kwanza yalianza.
Siku nane "njia ya Msalaba"
Ili kuongeza mateso ya waliohukumiwa, Mfalme aliamua kuwahamisha kutoka jumba la Kifalme ya Munyonyo hadi Namugongo, mahali pa kunyongwa katika mji mkuu Kampala: maili 27 inayotenganisha sehemu hizo mbili, na ambazo ziligeuka kuwa "njia ya msalaba halisi.” Njiani, Karoli na wenzake walifanyiwa vurugu na askari wa mfalme ambao walijaribu, kwa njia yoyote ile, kuwafanya wakanushe imani yao. Katika siku nane za kutembea, wengi walikufa kwa kuchomwa na mikuki, kunyongwa na hata kutundikwa kwenye miti.
Kuchomwa moto akiwa hai kwenye kilima cha Namugongo
Mnamo tarehe 3 Juni, manusura waliobaki walifika wakiwa wamechoka sana kwenye kilima cha Namugongo, ambapo kigingi kiliwangoja. Karoli Lwanga na wenzake, pamoja na baadhi ya waamini wa kianglikana, walichomwa moto wakiwa hai. Walisali hadi mwisho, bila kutamka, wakitoa uthibitisho wa imani yenye kuzaa matunda. Mmoja wao, Bruno Ssrerunkuma, alisema, kabla ya kufa: "Chanzo ambacho kina vyanzo vingi hakitawahi kukauka. Na wakati hatutakuwapo tena, wengine watakuja baada yetu."
Mtakatifu na Paulo VI aliwatangaza kuwa watakatifu mnamo 1964
Mnamo 1920, Papa Benedito XV aliwatangaza kuwa Wenyeheri. Miaka kumi na minne baadaye, mnamo 1934, Papa Pio XI alimtangaza Karoli Lwanga kuwa "Mlinzi wa vijana Wakikristo wa Afrika. Wakati huo ndipo Papa Paulo VI alipotangaza kundi zima kuwa watakatifu tarehe 18 Oktoba 1964, wakati wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatikacan ukiendelea. Na alikuwa Papa Montini, ambaye alikwenda Uganda mnamo mwaka 1969, ambaye aliweka wakfu madhabahu ya juu ya Namugongo, iliyojengwa kwenye kitovu cha kifo chao. Umbo la Kanisa ambalo limesimama hapo leo hii linaibua kibanda (msonge)cha kiutamaduni cha Kiafrika na kuegemea kwenye nguzo 22 zinazowakilisha wafia dini 22 wa Kikatoliki.
Papa Francisko:“Mashahidi wa uekumene wa damu”
Ikumbukwe ilikuwa tarehe 28 Novemba 2015, wakati wa ziara yake ya kumi na moja ya kitume nchini Uganda, Hayati Papa Francisko aliadhimisha Misa katika Madhabahu hiyo hiyo, baada ya kutembelea Kanisa la Kianglikani lililo karibu, ambalo pia limewekwa wafu kwa ajili ya mashahidi wa nchi hiyo. Katika wakati ule Papa akielezea juu ya ushuhuda wao alisema wakati wa mahubiri yake kuwa "Leo, tunakumbuka kwa shukrani dhabihu ya mashahidi wa Uganda, ambao ushuhuda wao wa upendo kwa Kristo na Kanisa lake umefika hadi miisho ya dunia. Tunawakumbuka pia wafia dini wa Kianglikani, ambao kifo chao kwa ajili ya Kristo kinashuhudia uekumene wa damu… Maisha yaliyotiwa alama kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, maisha ambayo hata sasa yanashuhudia nguvu inayobadilisha ya Injili ya Yesu Kristo.”