Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo: Mahujaji wa Imani na Matumaini
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya Neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican leo ni Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume. Mitume hawa walikuwa ni mashuhuda wa maisha, msamaha na mashahidi wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Ni Mitume waliojisadaka kutangaza, kushuhudia na kuishi utume wao, hija ambayo imewafikisha hadi Roma, na hapa wakayamimina maisha, kielelezo makini cha ushuhuda kwa Kristo Yesu, maisha na msamaha! Mitume Petro na Paulo walikuwa ni mashuhuda wa maisha ambayo yalisimikwa katika maisha ya kiroho kwani walikuwa ni wachamungu! Ni watu ambao walionesha udhaifu mkubwa wa kibinadamu, kiasi hata cha Mtakatifu Petro kumkana Kristo Yesu mara tatu wakati ambapo Mtume Paulo alilidhulumu Kanisa la Kristo. Lakini wote hawa wakaoneshwa na kuonjeshwa upendo wa Kristo hasa pale Yesu alipomuuliza Mtume Petro mara tatu, ikiwa kama alikuwa anampenda, Petro akasononeka sana. Mtume Paulo akaulizwa kwanini alikuwa analidhulumu Kanisa lake? Wote wawili waliitwa kwa majina yao, hali ambayo iliwaletea toba na wongofu wa ndani. Hawa ni wadhambi wawili waliotubu na kumwongokea Mungu; ni watu ambao walitambua kwamba ni: wadhambi na Yesu akachukua fursa hii kuwafanyia miujiza, kielelezo cha huruma na upendo wake, kwa wale wote wanaothubutu kumfungulia hazina ya nyoyo zao, kwa kujiweka mbele ya Kristo, ili aweze kuwatumia kama vyombo na mashuhuda wake.
Ni watu walioonesha moyo wa unyenyekevu hadi dakika ya mwisho wa maisha yao, kiasi hata cha Mtume Petro kusulubiwa miguu juu, kichwa chini! jina Paulo maana yake ni “mtu mdogo”, kielelezo cha unyenyekevu uliomfanya hata watu kusahau jina lake la asili, Saulo, aliyekuwa Mfalme wa kwanza wa Israeli. Mitume hawa wakatambua kwamba, utakatifu wa maisha unafumbwa katika unyenyekevu, kwa kutambua na kukiri udhaifu na umaskini wao, kiasi cha kujiaminisha kwa Kristo Yesu, aliyewatendea miujiza kwa kuwanyanyua juu, kwa njia ya Msamaha unaoganga na kuponya! Mitume Petro na Paulo ni mashuhuda wa msamaha wa Kristo Yesu, uliowajalia toba na wongofu wa ndani, wakabahatika kuwa watu wapya, wenye furaha na amani ya ndani. Wakasahau ya kale na kuanza kuyaambata maisha mapya yaliokuwa yameboreshwa kwa huruma na upendo wa Kristo uliokuwa na nguvu kubwa kupita hata mapungufu na makosa yao ya kibinadamu. Huruma ya Mungu inawajalia waamini kuwa na maisha mapya, changamoto na mwaliko kwa waamini kukimbilia Sakramenti ya Upatanisho katika maisha yao! Mitume Petro na Paulo walikuwa ni mashuhuda wa Kristo Mfufuka; mashuhuda wa msamaha unaoganga na kuponya na hatimaye, wakawa ni mashuhuda wa Masiha, Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai.
UFAFANUZI: MTUME PETRO alizaliwa katika kijiji cha Betsaida (Yoh 1:44).Baba yake aliitwa Yohane au Yona (Yoh 1:42,21:15-17).Ndugu yake mwingine alikuwa Andrea,mtu wa ukimya.Kama Wayahudi wengine Petro alipata elimu ya msingi,alifunga ndoa (Mk 1:30).Baadaye alihamia Kafarnaum.Hakuwa fukara mno wala tajiri;bali alikuwa mtu wa wastani .Kazi yake alikuwa mvuvi,akisaidiwa na Yakobo na Yohane wana wa Zebedayo (Lk 5:9-10.) Simon na ndugu yake Andrea na Yohane mwana wa Zebedayo walikuwa wa kwanza kuitwa na Kristo”walikuwa miongoni mwa wale waliomsikia Yohane na kumfuata Yesu”(Yoh 1:40) Walikutana na Bwana kwenye Yordane alikofundisha Yohane mbatizaji.Yesu alimpa jina jipya aliposema,”Simon bin Yona utaitwa Petro”(Yoh 1:42).Toka wakati ule Petro alimfuata Yesu mara nyingi katika safari zake.Lakini baadaye alikwenda tena nyumbani na kufanya kazi ya kuvua samaki.Mwaka mmoja baada ya kukutana kwao mara ya kwanza,Yesu alitembea kando ya ziwa genesareti,karibu na Kafarnaum;”Alimwona Simon na nduguye Andrea wakitupa wavu baharini kwa maana walikuwa wavuvi.Yesu akawaambia njooni mnifuate,nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu,wakaacha nyavu zao wakamfuata”(Mk 1:16-18) Basi Petro aliacha nyumba yake,familia yake na kazi yake.Kwa kifupi aliacha yote apate kumfuata Kristo toka saa ile. Sifa zake: Mtakatifu Petro alikuwa kigeugeu. Alipokea neno kwa furaha,alikuwa mwepesi wa kusema na kufanya mambo kabla ya kufikiri.Alifikiri baada ya kuwa tayari amesema.Alikuwa kidomodomo, mropokaji, anatamka kitu kibaya katika muda mbaya! Alizidi katika kufurahi na kuhuzunika.Yesu alipotaja mara ya kwanza mateso yatakayompata,Petro alimkatiza maneno akasema,”Hasha bwana hayo hayatakupata”(Mt 16:22).Mkombozi alipogeuka sura mlimani Tabor, Petro alitaka kusema vilevile neno,maana aliona ni vigumu kunyamaza.Lakini maneno yake hayakuwa na busara sana.Alisema “Bwana ni vizuri sisi kuwapo hapa na tujenge vibanda vitatu tuweze kushinda hapa zaidi”(Mk 9:4), Petro alikuwa mtu wa unyenyekevu.Alipokamata samaki wengi mno kwa amri ya Yesu akamwngukia,akasema”Bwana ondoka kwangu kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi”(Lk 5:8.)
Hatimaye, aliwekwa kuwa kiongozi wa Mitume. Kristu akamchagua awe mchungaji mkuu wa kundi lake lote yaani Kanisa akisema,”Wewe ndiwe Petro na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu na nguvu za kuzimu hazitaweza kulishinda”.Petro alijua cheo chake yaani kuwa mwamba wa Kanisa,kuwa mshika ufunguo wa kanisa hivyo kuwa na mamlaka juu yake,kufunga na kufungua.Katika semi za watu wa wakati ule maneno ya Yesu yalifahamika kwa mitume,kufunga na kufungua kulikuwa sawa na kutoa amri na ni nani atakayetengwa nao.Hivyo ni Petro aliyepewa uwezo huu kwa agizo la Mungu.”Lolote utakalofunga duniani litafungwa vilevile mbinguni,na lolote utakalofungua duniani litafunguliwa vilevile mbinguni” Kazi hii inaendelezwa na Baba Mtakatifu LEO XIV akiwa na Papa wa 267 tangu Petro, aliye wakili wa Kristo na Khalifa wa Mtume Petro. (Rejea injili ya leo) Hatimaye wakati wa utawala wa Kaisari Nero wakristu walidhulumiwa naye alikamtwa na kufungwa gerezani kwaajili ya dini yake ya kikristo,kati ya mwaka 64 au 65 alihukumiwa kufa kwa ajili hiyo.Kristo mwenyewe alikuwa amemwagulia Petro,kuwa atauawa,”ulipokuwa kijana ulijifunga mwenyewe na kwenda utakapo;lakini utakapo kuwa mzee,utanyoosha mikono yako na mwingine atakufunga na kukupeleka usikotaka”(Yoh 21:18)-ndiko msalabani.Mapokeo yatueleza kwamba alisulubiwa kichwa chini miguu juu kwa sasbabu aliona hastahili kusulubiwa sawa na Bwana wake.
Mtume Paulo alizaliwa Tarso huko Kilikia,”Mimi ni Myahudi mzaliwa wa Tarso katika Kilikia.Mimi ni raia wa mji maarufu” (Mdo 21:39) Wazazi wake walikuwa wayahudi,yeye alizaliwa katika nchi za nje.Kutokana na sababu mbalibali kama vile vurugu za vita au kukimbia umaskini,wayahudi wengi waliiacha nchi yao na kujijengea makazi nchi za nje.Kwasababu tusizozijua wazazi wa Paulo waliishi katika nchi za Kigiriki katika mji wa Tarso mkoa wa Kilikia.Paulo anajigamba kuwa ni raia wa mji maarufu,yeye ni “mtoto wa mjini”.Kutokana na mji huo kuwa sehemu nzuri kijiografia,upo kando ya bahari ya mediterania ilipo bandari kubwa,barabara nzuri na hivyo kuwa kituo cha biashara na mahali pa mkutano wa mataifa mengi na palikuwa na chuo kikuu maarufu sana kilichoshika nafasi ya tatu katika ulimwengu wa wakati ule. Mwito wa Paulo: Mtakatifu Paulo alipata barua kutoka kwa makuhani wa Yerusalemu zilizompa idhini ya kuwashika na kuwaadhibu wafuasi wa Yesu. Akiwa na barua hizo Paulo alielekea Damasko.Njiani alipigwa mwanga mkali hata akaanguka chini.Alisikia sauti iliyomwuliza kwanini alilidhulumu Kanisa.Paulo aliuliza sauti hiyo ilikuwa ya nani akajibiwa kuwa ilikuwa ya Yesu.Kisha Paulo alielekezwa aende mjini ambako alikutana na Anania aliyefungua macho ya Paulo na kumbatiza.Mapokeo huliita tukio hilo “kuongoka kwa Paulo”.Leo wataalam hufikiri kuwa ni sahihi zaidi kuliita tukio hilo,mwito wa Paulo.Kwa nafasi hiyo Paulo hakumwacha Mungu mmoja na kumfuata Mungu mwingine,wala hakubadilika kutoka mtu wa maadili mabaya kuwa mtu aliyeshikilia maadili mema.
Yeye mwenyewe anapoeleza juu ya tukio hili maelezo yake yanafanana na yale yanayosimulia juu ya kuitwa kwa nabii Yeremia(1:5) na nabii Isaya (6).Kitabu cha Matendo ya Mitume kinatilia mkazo mambo ya ajabu ajabu yaliyoonekana au kusikika,Paulo mwenyewe katika barua zake hasemi lolote juu ya hayo bali anatilia mkazo mambo 2;kuwa alioneshwa Yesu mwana wa Mungu na alitumwa na Yesu akahubiri habari njema kwa watu wa mataifa mengine.Anasema,”Lakini Mungu kwa neema yake alikuwa ameniteua hata kabla sijazaliwa,akaniita nimtumikie.Mara tu alipoamua kunifunulia mwanaye kusudi niihubiri Habari Njema kwa watu wa mataifa mengine,bila kutafuta maoni ya binadamu,bila kwenda kwanza Yerusalemu kwa wale waliopata kuwa Mitume kabla. Sifa zake: Paulo anasifika na kufahamika sana kuwa ni mtume wa mataifa.Katika Injili neno hili mtume linatumika kwaajili ya watu 12 walioteuliwa na Yesu wakae naye,awatume kuhubiri na wawe na mamlaka ya kufukuza pepo,(Mk 3:14-15)Katika kipindi cha Agano Jipya neno hilo lilichukua maana pana zaidi,Mathia alichaguliwa na mitume kumi na mmoja achukue nafasi ya mtume Yuda.Sifa ya mtume huyo mpya ni kwamba alifuatana na Yesu tangu Yohane alipokuwa anabatiza mpaka siku ile alipokuwa anapaa mbinguni (Mdo 1:21-22) Barnaba pamoja na Paulo wanaitwa mitume (Mdo 14:14-15).Kwa hoja gani basi Paulo hujieleza kuwa mtume?Paulo anayo sifa muhimu ya mtume,alimwona Kristo mfufuka(1Kor 9:1,15)uteuzi wake haukufanywa kwa kura au kwa maoni ya binadamu bali kwa uwezo wa Yesu Kristu mwenyewe(Gal 1:2)Mwana wa Mungu alimtokea na kumkabidhi jukumu la kuhubiri habari njema kwa watu wa mataifa mengine (Gal 1:16)Alikuwa mtu mwenye nguvu,aliyeelimika na kuwa mwenye ufasaha wa lugha na hoja,mwenye kujituma,,mvumilivu na mwenye imani ya kweli.Baadaye akawa mmisionari mkuu kwani alisafiri katika nchi za ng’ambo na kuunda makanisa mengi wakati wa safari zake.
Katika maisha yetu nyakati zetu: Mitume Petro na Paulo ndiyo nguzo kuu katika Kanisa aliloanzisha Yesu.Historia ya maisha yao,sifa zao tulizo ziona,hazikuwa za pekee sana, lakini walifanya mambo ya pekee ambayo leo mimi na wewe tunayafaidi na kujipatia hazina ya imani na fadhila katika kumtafuta na kumtumikia Mungu ili tuweze kupata taji ya utukufu usiofifia.Kwahiyo ndugu zangu sikukuu hii ya leo ichochee imani yetu,ituondolee unyonge wa kujiona kama hatuwezi kumtangaza Kristo.Kwa Sakramenti ya ubatizo tumekuwa mitume wa Yesu tuifanye kwa uvumilivu,saburi na dhamiri safi kazi hiyo.Kuanzia katika familia zetu.Kila mmoja pale alipo amtangaze Kristo na kuimarisha imani kwa ndugu zake.Lakini kufanya yote hayo tutegemee kupata magumu,upinzaji,mateso kutoka kwa ndugu na jamaa zetu.Tuyapokee hayo yote kama changamoto inayotudai kumtegemea Mungu na kumpendeza yeye.Tujitoe bila kujihurumia katika kumtumikia Mungu na wenzetu. Tutambue kuwa mateso huyapa maisha yetu ladha ya kuteswa pamoja na Kristu na hivyo kupata maana halisi ya maisha ya kumfuata na kuandamana daima na Kristo aliyeteseka hata kufa msalabani ili kutukomboa sisi.Watakatifu petro na paulo watuongoze kutambua vema fumbo la mateso ambalo wao walishiriki kwaajili ya Bwana wao. Wewe Bwana uliyeweka Kanisa lako juu ya msingi wa Mitume, tujalie sisi sote – na hasa mapadre wapya – kuwa taa ya matumaini katika dunia ya giza. Tupatie roho ya Petro na moyo wa Paulo. Amina.