Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu: Chemchemi ya Imani na Matumaini
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi: Wapendwa taifa la Mungu, Dominika baada ya Sherehe ya Pentekoste, Mama Kanisa anaadhimisha, “Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu” Katekisimu ya Kanisa Katoliki namba 234, 253 na 256 yatufundisha kuwa, Mungu ni mmoja anayeishi katika nafsi tatu, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Wote ni Mungu kweli na bado tuna Mungu mmoja. Mungu Baba ni Muumba (Creator), Mungu Mwana ni Mkombozi (Redeemer) na Mungu Roho Mtakatifu ni mfariji (Councelor/Sanctifier). Katika Sherehe ya Utatu Mtakatifu tunaadhimisha nini? Ukweli huu wa fumbo hili la Imani yetu hautajwi wazi wazi katika maandiko matakatifu, hata neno Utatu Mtakatifu halipo katika maandiko matakatifu. Lakini Mungu amejifunua kwetu katika nafsi tatu katika historia yote ya mwanadamu, kuanzia uumbaji mpaka safari ya nzima ya ukombozi. Mafumbo yote ya ukombozi wetu ni kazi ya utatu Mtakatifu. Sherehe hii inatukumbusha kuwa Mungu anaishi katika umoja na anatualika sisi sote kuwa na umoja na ushirika naye, na kuwa na umoja na ushirika kati yetu sisi kwa sisi. Tunamshangilia Mungu aliyejifunua kwetu katika nafsi tatu, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Tunasherehekea, “FUMBO NA KIINI CHA IMANI YETU. “Maadhimisho yote katika mafumbo ya ukombozi wetu kuanzia umwilisho, kuzaliwa Bwana, Tokeo la Bwana, Ubatizo wa Bwana, Utume wa wazi wa Bwana wetu Yesu Kristo, Mateso, kifo, na Ufufuko wake, kupaa kwake mbinguni na Pentekoste, zaonesha uwepo wa umoja huu Mtakatifu usiogawanyika. Maadhimisho yote katika kanisa, kuanzia Adhimisho la ibada ya Misa Takatifu, maadhimisho ya Sakramenti zote, sala mbalimbali tunazosali, yanaadhimishwa katika utatu Mtakatifu.
Tunabatizwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, tunaondolewa dhambi katika Utatu Mtakatifu, tunapokea utimilifu wa mapaji ya nafsi ya Tatu ya Utatu Mtakatifu kwa Sakramenti ya Kipaimara, na Sakramenti nyingine zote zinaadhimishwa kwa jina la Utatu Mtakatifu. Kila mara tunapofanya ishara ya msalaba tunajikumbusha juu ya ukweli huu wa imani yetu. Tunahitimisha sala zetu kwa kuutukuza utatu mtakatifu tunaposema, atukuzwe Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu…Kumbe Mungu ameamua kutushirikisha maisha yake, kwa kutuumba, kwa kutukomboa hata tulipoanguka katika dhambi, kwa kuja kati yetu na kukaa nasi kwa mapendo makubwa, kwa kutuhurumia kutukomboa. Ni wajibu wetu kila mara kuishi katika ushirika na Mungu ambaye anaishi daima katika umoja. Tunaalikwa kuachana na mambo yote yanayoweza kuuvunja umoja wetu na Mungu, na umoja kati yetu sisi kwa sisi. Chimbuko la fundisho la Utatu Mtakatifu katika Kanisa. Ufafanuzi wa kale kabisa wa mafundisho ya imani yetu juu ya utatu Mtakatifu yanapatikana katika kanuni ya imani ya mitume (Apostles Creed), iliyotumika kama mafundisho msingi kwa ajili ya wakatekumeni na kama Ungamo la Ubatizo (Baptisimal confession) katika karne ya kwanza. Baadaye, kanuni ya imani ya Nicea (Nicene Creed) iliyotokana na Mtaguso wa Nicea mwaka 325 AD yaeleza fumbo hili kwa wazi zaidi.
Baadaye kanuni hii iliingizwa rasmi katika liturujia ya Kanisa la Magharibi katika Mtaguso wa Toledo mwaka 589 AD. Mababa wa Kanisa katika mitaguso hii watufundisha kwamba, Mwenyezi Mungu amefunua kwetu kazi tatu, ambazo zahusishwa na nafsi yatu za Mungu. Mungu Baba ndiye Muumbaji, Mungu Mwana ni Mkombozi na Mungu Roho Mtakatifu ni Mfariji. Maarifa yetu kuhusu Mungu yawezeshwa na Mungu mwenyewe aliyeamua kujifunua kwetu katika nafsi tatu katika historia yote ya maisha ya mwanadamu. Kama Baba, Mwenyezi Mungu ameumba vitu vyote na akamwumba mtu kwa mfano na sura yake mwenyewe. Kama Mwana pekee wa Mungu aliyetwaa mwili akakaa kati yetu, Mungu amejifunua kwetu kama yeye anayesikia kilio cha watu wake, anayejali, anayetulinda, anayejua kila unywele ulio katika vichwa vyetu, anayetupenda kwa mapendo makuu hata akaamua kutwaa hali yetu na kuwa mmoja wetu, akateseka na kufa kwa sababu ya dhambi zetu ili sisi tuwe hai daima ndani yake. Kama Roho Mtakatifu, Mungu ameamua kubaki kati yetu, hajatuacha peke yetu, hajatuacha yatima, anatuongoza, anatukinga, anatutakasa, anatusaida katika udhaifu wetu, anatufundisha, anatukumbusha na kututia nguvu ya kuiishi imani yetu ili tuwe wamoja daima na Mungu Muumba wetu.
Utatu Mtakatifu katika Agano la Kale (Triune God in the Old Testament). Mafundisho ya Imani juu ya Utatu Mtakatifu hayapo wazi sana katika Agano la Kale. Licha ya hivyo, wataalamu mbalimbali wa taalimungu wanatueleza kuwa, katika Agano la kale yapo matukio yanayotueleza uwepo wa utatu Mtakatifu. Kwa akili zetu hatuwezi kueleza fumbo hili kwa kuwa kwa akili zetu hatuwezi kumwelewa na kumwelezea Mungu katika ukamilifu wake kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Agustino alipojaribu kuelezea kuhusu utatu Mtakatifu. Lakini maandiko Matakatifu yatusaidia kuelewa Utatu Mtakatifu katika utendaji, namna nafsi zote tatu zinavyoonekana katika historia ya ukombozi wa Mwanadamu. Katika Agano la Kale katika sehemu mbalimbali twaelezwa namna utatu Mtakatifu unavyoodhihirika kama ifuatavyo. Kwanza: Lugha ya wingi kwa Mungu (Plural language for God) Mwanzo 1:26. Matumizi ya lugha ya wingi katika baadhi ya aya katika Agano la kale yanatueleza kuwa Mungu kwa asili ni Mungu anayehusiana, si Mungu anayeishi peke yake. Katika kitabu cha Mwanzo 1:26, Mungu anasema, “Na tumwumbe Mtu kwa sura na mfano wetu” Aya hii yatuonesha kwa hakika kuwa kazi ya uumbaji ilikua ni kazi ya utatu Mtakatifu. Mwenyezi Mungu hakuumba peke yake, Mwana alikuwepo tangu Mwanzo hali kadhalika na Roho Mtakatifu. Wazo hili laonekana pia katika kitabu cha Mwanzo 11:7, katika simulizi la Mnara wa Babeli. Mwenyezi Mungu anaposema, “Haya, na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao” Matumizi haya ya lugha ya wingi yatupa picha kwamba Mungu anaishi katika jumuiya, anaishi katika umoja, nao ndio utatu Mtakatifu. Pili: Uwepo wa Roho wa Bwana, (Ruach Elohim/Pneuma/The Spirit of God) Mwanzo 1:2. Uwepo wa Roho wa Bwana watupa picha ya kuwa kazi ya uumbaji ni kazi ya utatu Mtakatifu. Katika kitabu cha Mwanzo 1:2 tunaambiwa, “Na Roho ya Bwana ilikua juu ya uso wa maji.” Roho wa Mungu (Ruach Elohim) ni pumzi ya Mungu, ni roho itiayo uhai na uzima, inayobadilisha na yenye mamlaka ya kufanya upya. Ni uwepo wa Mungu anayetenda kazi kwa nguvu na uweza (God’s active presence and power). Ndiye aliyewashukia Mitume siku ya Pentekoste, akawaimarisha Mitume na akapuliza pumzi yake ya uhai ndani ya kanisa ili liwe hai na imara katika kuishuhudia Injili.
Tatu: Neno wa Mungu (The Word of God/ Logos) Zab 33:6. Mzaburi katika zaburi hii ya 33:6 anatuambia, “Kwa Neno la Bwana, Mbingu zilifanyika.” Hii yatuonesha kuwa Neno wa Bwana amekuwapo tangu milele yote na kwa njia yake mbingu zilifanyika. Neno huyu (Divine Logos) ndiye Bwana wetu Yesu Kristo ambaye alitwaa mwili akakaa kwetu, kama anavyoeleza Mwinjili Yohane katika utangulizi wa Injili ya nne (Yn 1:14). Ndiye Mungu aliyetwaa hali yetu ya kibinadamu ili atuumbe upya baada ya anguko la wazazi wetu wa kwanza na kupoteza neema ya utakaso yaani uzima wa kimungu ndani mwetu. Kazi ya ukombozi hivyo ni kazi ya utatu Mtakatifu. Mungu Baba aliyeupenda hivyo ulimwengu alimtuma mwanaye wa pekee ambaye kwa njia ya Roo Mtakatifu akatimiza kazi ya baba ya kuuletea ulimwengu ukombozi wa milele. Nne: Malaika wa Bwana (The Angel of the Lord) Mwanzo 16:7-13, Kut 3:2-6. Katika sehemu mbalimbali katika Agano la Kale, Malaika wa Bwana anaongea kwa nafsi ya kwanza kama Mungu, lakini sio kwa niaba ya Mungu. Kitabu cha kutoka sura hii ya 3, katika aya ya 2, malaika anamtokea Musa katika kichaka cha moto. Lakini katika aya ya 6, anasema huyu anayetambulishwa katika aya ya pili kama Malaika anasema: “Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo...” Hali kadhalika katika kitabu cha mwanzo 16:7-13, Malaika wa Bwana anatoa ahadi kwa Hajiri Mjakazi wa Ibrahimu, ahadi ambazo ni Mungu pekee aweza kutoa anaposema: “Hakika nitakuzidishia uzao wako, wala hautahesabika kwa utakavyokuwa mwingi” (Mwanzo 6:10). Katika aya zote hizi tajwa, tunaona malaika wa Bwana, akiwa ametumwa na Mungu na kwa wakati huo huo yeye ni Mungu. Wataalamu wa maandiko Matakatifu waona katika aya hizi Mungu ambaye anaishi katika nafsi tofauti na hivyo kueleza juu ya Utatu Mtakatifu. Mtakatifu Justini Shahidi, Ireneus na Tertulian watueleza kuwa, malaika wa Bwana anayezungumzwa katika Agano la Kale ndiye Kristo kabla ya umwilisho. Waeleza kuwa ni namna Mungu hatua kwa hatua alivyoanza kujifunua kwetu ((Progressive Revelation) kabla hajajifunua kwetu moja kwa moja (definitevely) kwa njia ya Mwanaye Yesu Kristo. Tano: Hekima kama Nafsi pamoja na Mungu (Personified Wisdom) Mit 8. Katika Kitabu cha Mithali, hekima yajionesha kama nafsi aliyekuwa pamoja na Mungu kabla ya kuumbwa ulimwengu. Mababa wa Kanisa wanaeleza hekima hii kuwa ndiye Bwana wetu Yesu Kristo, tukirejea katika 1 Kor 1:23-24, Mtume Paulo anaposema: “Bali sisi tunamhubiri Kristo aliyesulibiwa, kwa Wayahudi ni kikwazo na kwa Wayunani ni upuuzi. Bali kwao waitwao Wayahudi kwa Wayunani, Kristo ni nguvu ya Mungu na Hekima ya Mungu."
Utatu Mtakatifu katika Agano Jipya (Triune God in the New Testament.) Fumbo la Utatu Mtakatifu, kama ilivyokuwa katika Agano la kale, halielezwi wazi wazi pia hata katika Agano jipya. Hakuna maelezo ya moja kutoka katika maandiko matakatifu yanayoeleza juu ya fumbo hili Takatifu. Licha ya hayo, katika Agano Jipya, tunaona jinsi Mungu ambaye hatua kwa hatua alianza kufunua fumbo hili kuanzia uumbaji sasa twaona namna kazi ya ukombozi wa mwanadamu ilivyo tunda la umoja huu Mtakatifu. Kwanza: Utatu Mtakatifu katika fumbo la Umwilisho (Trinity in Announciation and Incarnation). Katika fumbo la umwilisho tunamshangilia Neno wa Mungu aliyetwaa mwili akakaa kati yetu. Ni neno aliyekuwa kwa Baba tangu milele yote kama tunavyokiri katika kanuni ya Imani yetu. Malaika Gabrieli anavyompasha Habari Maria anawambia, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako na nguvu zake aliye juu zitakufunika kama kivuli, na hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu Mwana wa Mungu” Lk 2:35. Kumbe Mungu Baba, “Yeye aliye juu” anaanzisha mpango huu wa ukombozi, wa kumleta kwetu Neno wake wa milele kwa njia ya Roho Mtakatifu. Nafsi zote zinaonekana katika fumbo hili takatifu la Umwilisho. Pili: Utatu Mtakatifu katika Ubatizo wa Yesu (Baptism of Jesus). Katika ubatizo wa Yesu, Fumbo la Utatu Mtakafu ladhihirika. Mtoni Yordani, sauti ya Baba ilisikika kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni mwanangu mpendwa wangu, ninayependezwa naye (Mt 3:17) Sauti ya Mungu Baba inasikika kutoka mbinguni, Mungu mwana anabatizwa mtoni Yordani kabla ya kuanza rasmi utume wake wa wazi, na hapo Roho Mtakatifu anashuka kwa mfano wa hua na kukaa juu yake, ishara kwamba utume wake utaongozwa na Roho Mtakatifu. Tatu: Utume wa Bwana wetu Yesu Kristo (Public Ministry). Kristo anapoanza utume wake wa wazi, akiwa katika sinagogi huko Nazareti anasoma kutoka katika chuo cha Nabii Isaya, “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuhubiri maskini Habari Njema” (Lk 4:16). Yesu, Mwana wa Mungu anahubiri Habari Njema na kuponya, akitiwa nguvu na Roho Mtakatifu. Anafanya kazi aliyotumwa na Baba kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu. Kristo anatuambia katika Injili ya Yohane 8:29, “Yeye aliyenipeleka yu pamoja nami, hakuniacha peke yangu, kwa sababu nafanya siku zote yale yampendezayo. Kumbe kazi ya ukombozi ni kazi ya utatu Mtakatifu. Nne: Mateso na Kifo cha Kristo (Passion and death). Kristo kwa njia ya Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, sadaka iliyokubaliwa na Mungu Baba, tunasoma katika waraka kwa waebrania 9:14). Mungu Baba kwa upendo mkubwa anamtoa Mwanaye wa pekee Yesu Kristo kama sadaka ya upatanisho kati yake na sisi. Akiwa Getsemane katika mateso, Yesu anasali, akimwomba Baba, ishara ya ukaribu na muunganiko wake wa pekee na Mungu Baba yake. Mwinjili Yohane anatuamba kuwa, pale msalabani Yesu alitoa roho (Yoh 19:30), ishara kwamba, Kristo kwa kifo chake anatoa Roho Mtakatifu kwa ulimwengu. Hivyo hapa twaona ushiriki wa nafsi zote tatu za Mungu katika mateso na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo.
Tano: Ufufuko wa Kristo (Resurrection of Jesus). Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo ni ushindi dhidi ya kifo, dhambi na mauti. Ufufuko wa Kristo hautuoneshi tu ya kuwa Kristo ni mzima, yu hai, bali unatuonesha jinsi Baba, Mwana na Roho Mtakatifu walivyoshiriki pamoja katika kuleta uumbaji mpya (new Creation), ukombozi na uzima wa milele, tunda la ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo kutoka wafu. Ijapokuwa fundisho la Utatu Mtakatifu halitajwi wazi hapa, ufufuko wa Kristo watuonesha namna nafsi zote tatu zilivyoshiriki kwa namna ya pekee kabisa na katika uhusiano wa ajabu katika ufufuko wa Kristo. Sita: Pentekoste. Bwana wetu Yesu Kristo alipokuwa bado pamoja na wanafunzi wake, aliwaahidi kwamba hatowaacha yatima. Atamtuma kwao Roho Mtakatifu, zawadi ya Baba. Kristo Mwana wa Mungu akiisha kukamilisha kazi ya ukombozi aliyotumwa na Baba hapa duniani alipaa mbinguni (Mdo 2:33) Kisha Mungu Baba anatimiza ahadi ya zawadi aliyoisemea Yesu kwa Mitume wake, na Roho Mtakatifu anatumwa, anayewafundisha na kuwakumbusha yote ambayo Kristo alikwisha kuwafundisha alipokuwa bado pamoja nao. Wakiisha kupokea Roho Mtakatifu, waliimarishwa nao wakaenda kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu. Saba: Katika Utume wa Mitume wa Kristo na utume wa kanisa. Kristo anawaachia mitume wake utume kabla ya kupaa kwake kurudia kwa Baba. Yesu anawapa utume, kwamba walipaswa kwenda kuwafanya watu wa mataifa yote kuwa wanafunzi wa Kristo, wakiwabatiza kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu (Mt 28:18). Kazi ya mitume ilikuwa kuusimikia ufalme wa Mungu kwa watu wa mataifa yote. Hii ni kazi ya utatu Mtakatifu. Ndiyo kazi na utume wa Kanisa hata sasa, kuhubiri Habari Njema na kusimika Ufalme wa Mungu kati ya watu. Tunapoadhimisha Sherehe ya Utatu Mtakatifu tuna mambo yafuatayo ya kujifunza. Kwanza: Tunatafakari uhusiano wetu na Mungu Baba yetu anayetupenda. Somo la kwanza kutoka katika kitabu cha Mithali chaeleza juu ya Hekima, ambaye amekuwako kwa baba tangu milele yote. Hekima yajionesha kama nafsi aliyekuwa na Mungu kabla ya kuwako chochote. Hekima ameungana kabisa na Baba tangu milele yote. Hekima huyu ndiye Bwana wetu Yesu Kristo aliyetoka kwa Baba tangu milele yote kama tunavyokiri katika kanuni ya imani yetu. Ndugu mpendwa, sherehe hii yatutafakarisha sisi sote juu ya mahusiano yetu binafsi na Mungu Baba yetu, ambaye anaishi katika umoja na Mwana na Roho Mtakatifu. Kila mmoja apate nafasi ya kujitathmini, mimi nipo karibu kiasi gani na Mungu aliyenipenda hivi hata akaniumba na kunikomboa? Mtakatifu Agustino anatufundisha kuwa Mungu aliyetuumba sisi pasipo sisi kutaka hawezi kutukomboa sisi pasipo sisi kutaka.
Sherehe hii inakuja mara baada ya sherehe ya pentekoste, mara baada ya kuhitimisha kipindi cha Pasaka. Tunakumbushwa bado juu ya thamani ya ukombozi wetu tuliyoipata kwa mastahili ya sadaka ya Kristo kwa fumbo la pasaka, twapaswa kweli kuithamani, kwa kujenga na kudumisha mahusiano mema kati yetu yetu sisi Mungu, kwa njia ya sala na kupokea Sakramenti mbalimbali za Kanisa. Pili: Utatu Mtakatifu ni Fumbo la Upendo, nasi tunaalikwa kudumisha furaha na upendo. Somo la kwanza laendelea kutufundisha kuwa maisha ndani ya utatu Mtakatifu ni maisha yenye mahusiano ya upendo na furaha, hekima anaposema: “Nikawa furaha yake kila siku; nikifurahi daima mbele zake, nikiifurahia dunia inayokaliwa na watu, na furaha yangu ilikuwa pamoja na wanadamu” Mit 8:31. Maisha yetu ndugu wapendwa yapaswa kuakisi maisha ya Utatu Mtakatifu. Tunapaswa kuishi kwa upendo wa kweli, katika mahusiano yanayolenga katika kuleta furaha na upendo kwa wengine. Katika familia zetu, kila mmoja amwombe Mungu amjalie awe balozi wa amani na upendo kwa wengine, katika ndoa na mahuisano yetu kila mmoja awe chanzo cha furaha na upendo kwa wengine. Daima kutokuwa sababu ya maumivu na machozi kwa wengine, kutokuwa sababu ya kuleta vidonda na masikitiko katika mioyo ya wengine. Ni pendo hili ambalo limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu kwa njia ya Roho Mtakatifu kama anavyotufundisha mtume Paulo katika somo la pili Rum 5:1-5.
Tatu: Katika umoja tunaweza kuleta pamoja maendeleo na mafanikio ya kweli. Hekima katika somo hili la kwanza anatueleza ushiriki wake katika uumbaji. Ni ushiriki katika upendo na umoja. Kumbe uumbaji wetu ni matokeo ya utatu Mtakatifu. Tunajifunza kuwa, lolote tunalofanya umoja na ushirika, katika majitolea sadaka ya kweli, tunaweza kufanikiwa. Katika shughuli zetu za kila siku, tujiulize mchango wangu katika maendeleo ya kazi yangu ni upi? Mchango wangu katika maendeleo ya familia yangu, jamii yangu, taifa langu ni upi? Huenda nimekua nafanya kidogo na kutegemea makubwa, au nafanya kwa kutafuta faida zangu binafsi na kusahau kuwa twapaswa kufanya kwa ajili ya faida na maslahi ya watu wote. Kazi ya uumbaji na ukombozi wetu itukumbushe wajibu wetu wa kushiriki pamoja na Mungu katika kuleta maendelo yetu, kwa juhudi, kwa maarifa, kwa sadaka na imani kubwa kwa Mungu ambaye tunafanya daima pamoja naye. Nne: Ni kwa njia ya imani tunashiriki uzima wa Utatu Mtakatifu. Mtume Paulo katika somo la pili anatufundisha kuwa, Mungu Baba yetu ndiye aliyetufanya sisi kuwa wenye haki yaani watakatifu kwa njia ya Mwanaye Yesu Kristo. Anarudisha tena amani kati yetu sisi na Mungu na upatanisho wa kweli. Hakuna tena uadui kati yetu sisi na Mungu ila wana wapendwa wa Baba. Ndugu mpendwa, Sherehe ya Utatu Mtakatifu itukumbushe wajibu wetu wa kuyatamani maisha matakatifu, kwa kutafua kwa bidii kuwa na amani na watu wote. Ili tuweze kushiriki uzima wa Utatu Mtakatifu hatuna budi kujitenga na dhambi. Kwa njia ya ubatizo tumefanyika viumbe wapya, tumevua utu wa kale na kuuvaa utu mpya. Hivyo hatupaswi kurudi tena dhambini bali daima kuuchuchumilia utakatifu. Tunapaswa kuvunja kila aina ya vizingiti kati yetu, kuondoa kila uadui, chuki na vinyongo kati yetu kwa kuwa tumekwishafanywa watakatifu kwa sadaka ya upatanisho ya Bwana wetu Yesu Kristo. Tano: Utatu Mtakatifu katika ukuaji wetu wa kila siku. Mtume Paulo anatueleza namna Utatu Mtakatifu unavyotusaidia kukua kiroho kupitia nyakati mbalimbali tunazokutana nazo hasa mateso. Hatufurahi tu katika tumaini bali hata katika nyakati za mateso na dhiki kwa kuwa, dhiki kazi yake ni kuleta saburi, na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini na tumaini kamwe halitahayarishi, tumaini halitudangani kwa kuwa pendo la Mungu limekwisha kumimina katika mioyo yetu.
Ndugu mpendwa sana, Mungu Baba ndiye chanzo cha tumaini hili la utukufu hata katika nyakati za shida, Mungu Mwana anatupa amani, Mungu Roho Mtakatifu anamimina pendo lake ndani ya nyoyo yetu. Tunapopita katika changamoto mbalimbali katika safari yetu sisi kama mahujaji wa matumaini tuwe na ujasiri kwamba, tumaini halitatuhadaa, kwa kuwa tunaye Mungu katika safari yetu ya maisha. Mungu anayetushika mkono, anayetupa nguvu, anayetufariji nasi tunapata ujasiri wa kusonga mbele. Tumaini halitakuhadaa ndugu mpendwa. Sita: Utatu Mtakatifu unatusaidia kuyafahamu kikamilifu mafundisho ya Kristo. Bwana wetu Yesu Kristo akiwa katika karamu ya mwisho aliwaambia mitume wake kuwa bado anayo mengi ya kuwafundisha lakini wasingeweza kuyastahimili kwa wakati ule. Somo hili la Injili Takatifu Yn 16:12-15 latupa picha ya kuwa sisi kwa akili na uwezo wetu hatuwezi kumwelewa Mungu, wala hatuwezi kuyaelewa na kuyashika kikamilifu mafundisho yake. Lakini kwa njia ya Roho Mtakatifu tutataweza kuyaelewa na kuyaishi yale yote ambayo Kristo ametufundisha. Tunapoendelea na kipindi cha kawaida katika mwaka wa kanisa, tumwombe Roho Mtakatifu tuliyempokea aendelee kufanya kazi ndani mwetu, atufundishe, atuongoze na kutukumbusha yale yatupasayo kutenda ili tuupate uzima wa milele. Hitimisho: Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, na upendo wa Mungu Baba, na ushirika wa Roho Mtakatifu viwe nanyi nyote.