Sherehe ya Pentekoste: Roho Mtakatifu; Kanisa, Ushuhuda Na Kipindi Pasaka
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi: Wapendwa taifa la Mungu, siku ya Hamsini baada ya Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Pentekoste. Liturjia ya Neno la Mungu katika sherehe hii inatutafakarisha juu ya, “Zawadi ya Roho Mtakatifu, kuzaliwa kwa Kanisa na ushuhuda wa Mitume” Katika sherehe hii ya Pentekoste tunaadhimisha mambo yafuatayo. Kwanza, ni siku Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume wakiwa wamekusanyika pamoja. Ishara kuu za uwepo wa Roho Mtakafu ni Upepo wa nguvu, ndimi za moto na kunena kwa lugha mbalimbali matendo makuu ya Mungu (Mdo 2:1-4). Ni utimilifu wa Ahadi ya Kristo Yesu kwa Mitume wake, kwamba, hatawaacha yatima, atawatumia msaidizi yaani Roho Mtakatifu (Yn 14:26; 16:7). Pentekoste ni utimilifu wa ahadi hiyo na ni Mwanzo wa maisha mapya ya kiroho kwa waamini wa kanisa la Mwanzo. Pili, ni siku lilipozaliwa rasmi Kanisa, ambapo baada ya kumpokea Roho Mtakatifu, Mitume walianza kuhubiri Injili hadharani bila hofu. Watu wengi walibatizwa siku hiyo, takribani watu 3,000 (Mdo 2:41) na jumuiya ya kwanza ya wakristo ikaundwa, ndilo kanisa la Mwanzo. Tatu, kwa kuadhimisha Sherehe ya Pentekoste tunahitimsha rasmi kipindi cha Pasaka, Roho Mtakatifu anaendelea kuliongoza Kanisa nasi sote katika kumshuhudia Kristo Mfufuka katika maisha yetu ya kila siku. Katika Sherehe hii ya Pentekoste, tumshukuru Kristo ambaye kwa njia ya Roho Mtakatifu sisi sote tumezaliwa upya, tumeimarishwa na kutiwa nguvu ili tuwe mashuhuda Hodari wa Injili ya Kristo kwa watu wote. Tunaposherehekea siku lilipozaliwa rasmi kanisa, tuliombee Kanisa, ili liendelee kuwa chombo cha huruma ya Mungu isiyo na mipaka, na kwa njia hiyo sisi sote tuupate uzima wa milele.
Maana na chimbuko la Sherehe ya Pentekoste. Sherehe ya Pentekoste ni moja kati ya sherehe kubwa tatu na za muhimu dini ya Wayahudi yaani (Pasaka, sherehe ya Vibanda na Pentekoste). Sherehe hii ya Pentekoste iliadhimishwa siku ya Hamsini baada ya sherehe ya Pasaka. Ilijulikana kama sherehe ya majuma (Feast of the weeks au Shavuot), siku ya kusherehekea mavuno ya kwanza hasa mavuno ya ngano, ikiwa ni mavuno yao ya kwanza baada ya kuingia katika Nchi ya Ahadi. (Kut 34:22, Mambo ya Walawi 23:15-21). Ni siku pia waliposherehekea kupokelewa kwa Sheria ya Musa katika mlima Sinai. Hivyo watu wote katika sherehe hizo tatu tajwa walipaswa kwenda Yerusalemu kila mwaka kuziadhimisha katika Hekalu. Mitume wa Kristo Yesu siku hii ya 50 baada ya Sherehe ya Pasaka, ikiwa pia ni sikukuu ya wayahudi ya kusherehekea mavuno ya kwanza kama ilivyokuwa desturi yao, Roho Mtakatifu anashuka juu yao walipokuwa wakisali pamoja huko Yerusalemu. Kama ilivyokuwa adhimisho la mavuno ya kwanza kwa Pentekoste ya Wayahudi, Roho Mtakatifu vivyo hivyo kwetu Wakrsto ni tunda la kwanza la Kristo kwa Mitume wake, baada ya mateso, kifo, ufufuko na kupaa kwake Mbinguni. Mitume wakiisha kumpokea Roho Mtakatifu, wanakumbushwa yote waliyofundishwa na Kristo na wanapata nguvu ya kuanza kuhubiri na kumshuhudia Kristo Mfufuka, na hapo Kanisa linazaliwa rasmi. Nao watu wote waliofika Yerusalemu kutoka pande mbalimbali wanakuwa mashuhuda wa jambo hilo, wakiwashuhudia Mitume wakinena hata kwa lugha zao. Hii ni ishara ya Kristo anayetuleta tena sote pamoja, tuliokuwa mbali kwa sababu ya dhambi. Pentekoste kwa Wayahudi ilikua pia ni siku ambapo walisherekea kutolewa kwa sheria ya Musa kule mlimani Sinai. Kwetu sisi Wakristo, kama vile Torati ilivyotolewa kwenye mlima Sinai, sasa Roho Mtakatifu anashushwa, akichora sheria mpya ndani ya mioyo ya waamini wote (Yer 31:33; Eze 36:26-27). Nasi tunakuwa mashuhuda kweli wa Imani yetu kwa Kristo.
Somo la Injili: Ni Injili ya Yohane 20:19-23. Somo la Injili Takatifu (Yn 20:19-23) yatueleza tokeo la Yesu baada ya ufufuko kwa wanafunzi wake ambao walikua wamejifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi. Wakiwa katika hali hiyo, Yesu alisimama katikati yao, na neno lake la kwanza kwao ni, “Amani iwe kwenu” na kisha anawaonesha mikono yake na miguu yake ya kwamba ni yeye. Wanafunzi wanafurahi wanapomwona Bwana. Akiisha kuwaondolea hofu, anawatuma Mitume wake kwenda kufanya kazi ilele ile ambayo yeye alitumwa na Baba kuja kuifanya akiwaambia, “Kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawatuma ninyi.” Ili Mitume waweze kutekeleza wajibu huu mkubwa wa kuwa mashuhuda wa Injili, walihitaji nguvu ya Mungu ndani mwao, ndiyo ahadi ya Roho Mtakatifu ambayo Kristo alishanena juu yake wakati akiwa bado angali pamoja nao. Anawavuvia Roho Mtakatifu. Anatimiza ahadi yake kwamba, sitowaacha yatima. Roho Mtakatifu aliwasaida Mitume kutimiza agizo la Kristo Yesu la kwenda kuhubiri Injili kwa watu wa Mataifa yote. Pili walipata mamlaka ya kuwaondolea watu dhambi zao na kuwapatanisha watu na Mungu. Ni kwa njia ya Roho Mtakatifu sisi sote tunapata msamaha wa dhambi. Tunaposamehewa dhambi tunakuwa kuwa vyombo vya huruma ya Mungu, kwa kupenda na kusameheana sisi kwa sisi na ni Roho Mtakatifu anayetusaidia katika kupenda na kusamehe. Sakramenti ya upatanisho inatuondolea hofu na mashaka, inaturudishia amani na furaha ya kweli mioyoni mwetu na na inatibu tena mahusiano mema kati yetu sisi kwa sisi na kati yetu sisi na Mungu wetu.
Katika somo hili la Injili dominika ya Sherehe ya Pentekoste tuna mafundisho matano ya kujifunza. Kwanza: Roho Mtakatifu anatuondolea hofu na mashaka, anatupa Amani. Mitume wa Yesu mara baada ya Yesu kukamatwa, kuteswa na kufa Msalabani, wengi walikimbia na walijawa na hofu na mashaka wakajifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi. Kristo mfufuka alipowatokea aliwaambia, “Amani iwe kwenu” Alitambua ya kuwa walikua na hofu na mashaka, na hivyo anawapa habari njema ya furaha kwamba, amefufuka kwa hivyo hawakupaswa kuwa na hofu tena. Nao wanafurahi walipomwona Bwana. Huenda tuna Ndugu mpendwa, katika maisha yetu ya kila siku kuna nyakati tunakuwa na hofu hofu juu ya maisha, juu ya familia zetu, juu ya kazi zetu za kila siku, juu ya malezi ya watoto wetu, juu ya mustakabali wa maisha yetu, hofu ya maradhi, hofu ya kifo, hofu ya majukumu mbalimbali yanayotukabili ambayo tunaona pengine ni mzigo mkubwa kuubeba na mlima kubwa sana kuukwea. Ni katika hali hiyo Kristo anakuja kwangu na kwako, ukiwa umejifungia katika hali hiyo ya hofu na mashaka, Neno lake kwako ni, “Amani iwe kwako” Ni mimi usiogope. Ni maneno ya kutia moyo kwamba, Yesu hawezi kuaniacha kamwe, Roho Mtakatifu aliye ndani mwetu anatusaidia kutambua kuwa Kristo yupo daima nasi, anatembea nasi katika safari yetu ya maisha. Anajidhihirisha kwetu sasa na daima, katika hali mbalimbali ambazo kila mmoja wetu anaweza kuwa anaipitia kwa wakati wake. Roho Mtakatifu akusadie kusikia sauti ya Kristo anayesema na moyo wako, amani iwe kwako. Nawe ufurahi ukutanapo na Kristo.
Pili: Roho Mtakatifu anaigeuza huzuni yetu kuwa furaha. Kristo alipowatokea Mitume, aliwaonesha mikono yake na ubavu wake. Hii ni ishara ya wazi kwamba utambulisho wake baada ya ufufuko ni matokeo ya mateso na kifo. Kisha Mitume wanafurahi wanapomwona Bwana. Ndugu mpendwa, Yesu anatimiza ahadi yake kwa Mitume ambao walijawa na huzuni kubwa baada ya mateso na kifo cha Bwana wao kwamba, “Huzuni yenu itageuka kuwa furaha” (Yn 16:20). Aliwaambia maneno haya alipokuwa akikaribia kuingia katika mateso, na kifo chake katika karamu ya mwisho. Kumbe kabla ya kumpokea Roho Mtakatifu, Kristo anawaponya kutoka katika huzuni na hofu zao. Anawakumbusha kuwa utukufu huja baada ya mateso na kifo, hivyo hawapaswi kuogopa. Ndivyo anavyotupa moyo Kristo anapotokea katikati yetu. Anatuponya kutoka katika hofu na huzuni zetu, anatuondolea mashaka yetu. Anatupa nguvu ya kutambua kuwa, kwa njia ya roho Mtakatifu hatupaswi kuogopa mateso na kifo kwani ndiyo njia yetu ya kuupata utukufu pamoja na Kristo mfufuka. Roho Mtakatifu aliye ndani mwetu atuondolee hofu na mashaka yote, tuwe imara katika Imani, matumaini na mapendo ya kweli kwa Kristo, nasi tutaipata furaha ya kweli.
Tatu: Roho Mtakatifu anatupa nguvu ya kuwa mashuhuda wa Imani yetu. Kristo alipojidhihirisha kwa wanafunzi wake na kisha kuwaondolea hofu na mashaka, aliwatuma kwenda kuhubiri habari njema, kutoa ushuhuda wa maisha. Anawaambia, “Kama vile Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapelekea ninyi” Ni kwa njia ya Roho Mtakatifu waliweza kutekeleza agizo hili la Kristo. Sisi sote tuliobatizwa tunatumwa na Kristo kwa namna ile ile alivyowatuma Mitume wake. Tunatumwa kuwa mashuhuda wa Imani yetu kiaminifu ulimwenguni. Kusimamia ukweli mafundisho na Imani yetu, kuiishi kweli Imani yetu bila kuogopa mateso, kusema ukweli na kutenda haki, kukemea maovu, katika familia zetu, jumuiya zetu, katika kanisa na katika Taifa letu. Kristo alifanya kazi aliyotumwa na Baba kwa Uaminifu na anawataka Mitume wake kufanya hivyo hivyo. Kila mmoja amwombe Roho Mtakatifu amsaidie kutimiza kazi aliyotumwa na Kristo kuifanya kila mtu kwa nafasi yake. Kila mmoja atekeleze kwa uaminifu wito wake bila kuchoka, kwa kuwa tumekwisha imarishwa na Kristo kwa njia ya Roho Mtakatifu.
Nne: Roho Mtakatifu ni uhai, pumzi ya Mungu ndani mwetu. Kristo anawavuvia mitume wake, akiwaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu, wowote mtakaowaondolea dhambi wameondolewa na wowote mtakaowafungia dhambi wamefungiwa” Kitendo cha kuvuvia ni ishara ya uumbaji, tukirejea katika kitabu cha Mwanzo 2:7, Mwenyezi Mungu alipomwumba mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai (Ruach/pneuma), na mtu akawa nafsi hai. Kumbe Yesu anawavuvia Mitume wake, anawapa nguvu ya kusamehe watu dhambi kwa njia ya Kanisa, ambao tunakuwa wapya kila tunaposamehewa dhambi zetu. Ndugu mpendwa, Kristo aliwapa mitume uwezo wa kuwaondolewa watu dhambi zao. Ni sakramenti ya kitubio, inayotupatanisha sisi na Mungu wetu, kielelezo cha huruma yake isiyo na mipaka kwa wanadamu. Anawavuvia, ishara ya uumbaji mpya ndani mwao. Ndio matokeo ya Sakramenti ya kitubio ndani ya mioyo yetu. Tunatakaswa na kundolewa dhambi, tunakuwa safi kabisa roho mwetu, tunaumbwa tena upya. Kristo Yesu anadhihirisha huruma kubwa ya Mungu wetu katika ondoleo la dhambi kwa njia ya sakramenti hii ya upatanisho, inayoponya mahusiano mema kati yetu sisi kwa sisi na kati yetu sisi na Mungu. Tano: Roho Mtakatifu anatusaidia kupenda na kusamehe. Ni kwa njia ya Roho Mtakatifu sisi sote tunapata ondoleo la dhambi. Wajibu wetu hauishii hapo bali unatudai na sisi sote kusameheana sisi kwa sisi. Roho Mtakatifu afungue mioyo yetu, tuwe tayari kusamehe na kuwapokea wale waliotukosea. Kristo anatupokea kila siku na kila mara tunapotubu na kwa njia ya Roho Mtakatifu anatutakasa na kutufanya wapya kabisa. Tujisikie hitaji hili la kuwasamehe wote waliotukosea na kuwa tayari kusukumwa na Roho Mtakatifu kufanya upatanisho wa kweli katika maisha maisha yetu.
Somo la 1: Ni kitabu cha Matendo ya Mitume Mdo 2:1-11. Somo la kwanza kutoka katika kitabu cha Matendo ya Mitume laeleza tukio la kushuka kwa Roho Mtakatifu juu ya Mitume wa Yesu siku ya Pentekoste. Kristo anatimiza ahadi yake kwa Mitume wake, ahadi ya kuwapelekea msaidizi, Roho Mtakatifu, atakayewafundisha na kuwakumbusha yote walioyofundishwa na kuyaona kutoka kwa Kristo. Ishara ya uwepo wa Roho Mtakatifu ni Upepo wa nguvu, ndimi za moto na kunena kwa lugha. Upepo wa nguvu ni ishara ya Roho wa Mungu (Ruach kwa lugha ya Kiebrania au “Pneuma” kwa lugha ya Kigiriki), pumzi au roho. Ni nguvu ya Roho Mtakatifu, itiayo uhai, iletayo uzima, inayobadilisha, yenye mamlaka ya kufanya upya. Kama vile Mungu alivyompulizia Adamu pumzi ya uhai (Mwanzo 2:7) ndivyo Mungu anavyopuliza pumzi yake ya uhai ndani ya kanisa ili liwe hai na imara katika kuishuhudia Injili. Ndimi za moto, ni ishara ya utakatifu na uwepo wa Mungu (Kutoka sura ya 3, Musa na kichaka kinachowaka moto). Ndimi za moto ni ishara ya mtendaji mpya wa ndani, Roho Mtakatifu akiwasha mioyo ya waamini kwa mapaji yake saba ili yawaimarishe katika kuishuhudia Imani yao kwa Kristo. Ndimi nyingi za moto ni ishara ya karama mbalimbali ambazo zote zatoka kwa Roho yule yule mmoja. Kunena kwa lugha, ni ishara ya wazi kuwa, ujumbe wa Injili sio kwa Wayahudi pekee bali na kwa watu wa mataifa yote. Roho Mtakatifu analeta tena umoja kati ya watu wa mataifa yote, anaondoa mkanganyiko uliotokea katika mnara wa Babeli (Mwanzo 11) ambapo lugha ziliwagawanya watu. Katika Pentekoste, lugha zinawakusanya tena watu, zinaleta umoja katika Kristo. Karama zote za za roho Mtakatifu lengo lake ni kujenga na kuimarisha umoja katika jumuiya ya waamini, yaani Kanisa.
Katika somo hili la kwanza dominika ya leo tuna mafundisho manne ya kujifunza. Kwanza: Roho Mtakatifu anafanya uumbaji mpya ndani mwetu. Upepo mkali ulikuja ghalfa kutoka mbinguni ilikuwa ni ishara ya wazi ya Roho Mtakatifu. Ni ishara ya pumzi ya Mungu (Ruach) inayotia uzima, inayoleta mabadiliko ya ndani, yenye mamlaka ya kufanya upya. Ndugu wapendwa, kwa njia ya ubatizo, sisi tunazaliwa upya kwa njia ya Roho Mtakatifu. Tunakuwa hivyo watoto wa Mungu, tunakufa na kufufuka pamoja na Kristo, tunavua utua wa kale na kuvaa utu mpya. Tunapokea utimilifu wa mapaji yake katika sakramenti ya kipaimara. Hatupaswi kurudi tena katika utu wetu wa kale, hatupaswi kurudi tena katika maisha ya dhambi. Ni roho huyo ndiye anayetia uzima wa kimungu ndani mwetu. Pili: Roho Mtakatifu anatutakasa. Ishara ya pili ya uwepo wa roho Mtakatifu ilikua ni ndimi za moto zilizowashukia mitume. Moto ni ishara ya utakaso. Roho Mtakatifu anatutakasa, kutoka katika dhambi na uovu wetu katika sakramenti ya kitubio. Yesu alipowatokea mitume aliwapa uwezo wa kuwatakasa watu dhambi zao. Kumbe ni roho Mtakatifu ambaye kila mara tunapoanguka katika dhambi na udhaifu anatutakasa, anatusafisha ili tuweze kustahili kujongea tena mbele ya Mungu aliye Mtakatifu sana. Tatu: Roho Mtakatifu anawasha moto ndani mwetu. Ndimi za moto ni ishara ya Roho Mtakatifu anayewasha moto ndani mwetu. Nyakati fulani tunakuwa dhaifu, tunakata tamaa, tunapoteza matumaini, tunakuwa waregevu kiroho, ni Roho Mtakatifu anayewasha tena moto wake ndani mwetu nasi tunakuwa hai tena, wenye ari na nguvu katika kuendelea kuishuhuidia imani yetu. Licha ya magumu ambayo kila mmoja wetu anapitia, roho Mtakatifu ni mfariji wetu mwema, anaamsha matumaini ndani mwetu, nasi kwa ujasiri tunaweza kusema, kesho Mungu ataniinua, Mungu atanibariki, Mungu ananisikia na atanijibu sala na maombi yangu.
Nne: Roho Mtakatifu analeta umoja kati yetu. Ndimi za moto zilizogawanyika ziliwashukia wote waliokuwamo ndani ya nyumba. Walipokea karama mbalimbali na zote chanzo chake ni kimoja, ni Roho Mtakatifu. Waliweza kunena kwa lugha mbalimbali, licha ya utofauti huo, waliweza kuhubiri na kusema matendo makuu ya Mungu na kila mmoja akaelewa kwa lugha yake. Ndugu wapendwa, katika sherehe hii ya Pentekoste, tusali na kuomba umoja katika familia zetu, katika taifa letu na kwa ulimwengu mzima. Zipo familia nyingi zilizovunjika kwa sababu ya kukosekana kwa amani, haki, usawa, ukweli, uwajibikaji nk. Yapo mataifa ambayo yameingia katika vita na migogoro mikubwa ya wenyewe kwa wenyewe kwa sababu ya uchu wa madaraka, ukosefu wa haki na ustawi kwa watu wote, ukosefu wa amani, na tunu za kiutu. Roho Mtakatifu akatulete sote pamoja, aunganishe tena familia ziliovunjika, alete amani katika nchi zenye vita na migogoro ya kisiasa, atukusanye na kutuleta sote pamoja chini ya mchungaji mmoja yaani Bwana wetu Yesu Kristo.
Somo la Pili: Ni Waraka wa Kwanza wa Mtume Paulo 1 Kor 12:3b-7, 12-13. Katika somo hili la pili, Mtume Paulo anafundisha kuwa, Roho Mtakatifu ni msingi wa karama zote na huduma mbalimbali katika kanisa. Aliwaandikia waraka huu Kanisa la Korintho ambalo lilikuwa limegawanyika kwa sababu ya mashindano, majivuno, kiburi na maoni mbalimbali juu ya karama za roho Mtakatifu. Wengine walijiona bora kwa sababu walikuwa na karama fulani (kama kunena kwa lugha) na kuwadharau wengine waliokuwa na karama zisizoonekana kama huduma na msaada. Mtume Paulo anasisitiza kuwa karama zote zinatoka kwa roho yule yule, na zote ni kwa ajili ya faida ya wote, kuletea umoja, kujenga jumuiya na wala sio manufaa binafsi. Ndugu zangu katika somo hili la pili tuna mambo matatu ya kujifunza. Kwanza: Roho Mtakatifu ni chanzo cha karama zote. Mtume Paulo anawafundisha Wakorintho kwamba karama zote chanzo chake ni roho Mtakatifu. Hakuna mtu anapaswa kujivuna kwa kuwa hatuna karama yoyote inayotoka kwetu bali ni Roho Mtakatifu ndiye mgawaji wa karama zote. Ndugu mpendwa, Pentekoste inatukumbusha juu ya ukarimu wa kimungu, anayegawa karama na vipaji mbalimbali kadiri apendavyo. Wengine wamepewa vingi kuliko wenzao, wengine wamepewa vichache. Hatupaswi kujivuna na kujiona kwamba sisi ni wa pekee sana kuliko wengine, tukawadharau na kuwanyanyasa wengine ambao pengine hawana karama na vipaji kama vile Mungu alivyonijalia mimi na wewe. Tunapaswa kumshukuru Mungu na kuvipokea vyote kwa unyenyekevu mkubwa tukijua kuwa ni Mungu ametupatia bure.
Pili: Karama zote za Roho Mtakatifu zapaswa kutuunganisha na kujenga jumuiya moja. Mtume Paulo anaelezea karama za roho Mtakatifu kwa mfano wa mwili wenye viungo vingi, yaani kanisa moja ambalo kichwa chake ni Kristo nasi sote tu hivyo viungo vya mwili wa Kristo. Karama zote ambazo tunazo ndugu wapendwa ni kwa ajili ya kuleta umoja na mshikamano kwetu sisi sote tulio ndani ya Kanisa. Roho Mtakatifu ni chanzo cha umoja, na hivyo karama yoyote yenye lengo la kuleta utengano hiyo sio karama ya Roho Mtakatifu. Je, ninatumia karama za Roho Mtakatifu katika kuleta umoja na mshikamano katika ufuasi wangu kwa Kristo? Tatu: Karama zote za Roho Mtakatifu ni kwa ajili ya huduma kwa wengine. Mtume Paulo anawafundisha wakorintho nasi sote pia kwamba karama zote za Roho Mtakatifu lengo lake ni huduma kwa wengine. Katika Kanisa la Korintho, karama za kiroho zilianza kutumika vibaya, waliokua nazo wakazitumia kwa ajili ya kujipatia sifa na utufukufu badala ya kulenga katika kuhudumia wengine katika jumuiya. Tumwombe roho Mtakatifu atusaidie tukumbuke kuwa tumepewa karama hizi bure, nasi tunapaswa kuzitoa bure kwa wengine bila majivuno, tukilenga katika kuhudumia na kuwastawisha wengine ili wakue na kuimarika kiroho Hitimisho: Katika Sherehe hii ya Pentekoste, tumshukuru Kristo ambaye kwa njia ya Roho Mtakatifu sisi sote tumezaliwa upya, tumeimarishwa na kutiwa nguvu ili tuwe mashuhuda Hodari wa Injili ya Kristo kwa watu wote. Tunaposherehekea siku lilipozaliwa rasmi kanisa, tuliombee Kanisa, ili liendelee kuwa chombo cha huruma ya Mungu isiyo na mipaka, na kwa njia hiyo sisi sote tuupate uzima wa milele.