Sherehe ya Pentekoste: Mwanzo wa Kanisa: Kuyatakatifuza Malimwengu!
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: “Roho wa Bwana ameujaza ulimwengu…” Hek 1:7. Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican leo ni Sherehe ya Pentekoste, ‘Heri ya kuzaliwa Mama Kanisa Mtakatifu…’ ndio, heri sana Mama na Mwalimu wetu na kimbilio la wote wenye kumtafuta Bwana! Sherehe ya Pentekoste ni siku ya hamsini, hitimisho la Pasaka ya Bwana, Roho Mtakatifu anawashukia Mitume na hivyo kushirikishwa kama Nafsi ya Mungu; kutoka katika utimilifu wake Kristo Yesu, Bwana anammimina Roho kwa wingi. Hii ni siku ambayo Fumbo la Utatu Mtakatifu linafunuliwa kwa ukamilifu. Toka siku hiyo, ufalme uliotangazwa na kushuhudiwa na Kristo Yesu uko wazi kwa ajili ya wale wanaomwamini na kumsadiki, katika hali ya unyenyekevu na imani wanashiriki ushirika wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Roho Mtakatifu ni paji la Mungu na kwa nguvu ya Roho Mtakatifu waamini wanaweza kuzaa matunda ya Roho Mtakatifu ambayo: ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Rej. KKK 731-747. Katika dunia yenye giza la vita, hofu, na kukata tamaa, Jubilei ya Matumaini hutualika kuwa watu wa Roho Mtakatifu – wenye tumaini, ujasiri, mshikamano, na utume hai.
Baba Mtakatifu Leo XIV anatualika kuwa Kanisa la Roho Mtakatifu, linalosikiliza historia, linalojenga upatanisho na mshikamano wa tunu za Kiinjili. ‘Roho wa Bwana ameujaza ulimwengu…’ anashuka kwa nguvu na uwezo kwa upepo uvumao na ndimi za moto akileta uhai na kufanya uso wa dunia kuwa mpya… Wapo wanaomtazama huyo kimakosa kama nguvu fulani tu kama ilivyo nishati ya jua au umeme tunayoipewa kutoka kwa Mungu… Kadiri ya Maandiko Matakatifu Roho wa Bwana ni Nafsi hai mwenye fikra, utashi na vionjo ndio sababu tunaaswa tusimuhuzunishe (Efe 4:30)… Ni Zao la kupendana kusiko na kikomo kwa Baba na Mwana, Mungu milele na milele… anakuja kwetu ili kile alichokianzisha Kristo kijipatie mwendelezo hai, kidumu imara katika misukosuko ya nyakati na majira hadi utimilifu wa dahari… anatusaidia kulijua pendo la Mungu lililomiminwa ndani yetu kwa njia yake Yeye tuliyempewa sisi (Rum 5:5) na kwa hakika anakuja auhakikishe ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki na hukumu (Yn 16:8-11).
Roho wa Bwana ameujaza ulimwengu alleluia… kwa ishara yake ya moto (somo I – Mdo 2:1-11) anatakasa na kuchoma uchafu wa roho za waamini akizirudishia usafi wake wa asili, akija kama moto anakuwa ishara ya uwepo wa Mungu kama katika kichaka kile kilichowaka bila kuteketea, kama katika nguzo ya moto jangwani na kama ilivyokuwa siku ile juu ya mlima Sinai (Kut 3:2-5, 13:21-22, 24:17)… kwa ishara ya upepo huvuma ndani ya mioyo ya watu akiwapa pumzi ya uhai na kuwajaza paji la imani (Yn 3:8)… kwa ishara ya maji anatimiza na kuzima kiu ya mioyo katika kumjua Mungu (Yn 7:37-3.) Na kwa ishara ya Njiwa anatangaza zama mpya za baraka na mwanzo wa uumbaji mpya wa ulimwengu vile njiwa alivyomrudia Nuhu kwenye safina na jani bichi la mzeituni mdomoni pake akithibitisha kuwa uhai umerudi duniani (Mwz 8:11). “Pokeeni Roho Mt…” ni Zawadi ya Kristo leo (Yn 20:19-23), kwa njia ya Zawadi hii Sakramenti ya Kitubio inapata kipeo chake na uwezo wa mitume wa kuondolea ama kufungia dhambi unathibitika, Yeye aliye Dawa ya dhambi anawezesha huruma na msamaha wa Mungu kutufikia kwa njia ya toba na maondoleo ya dhambi na kutupatia tena amani ya moyo, ya roho, ya akili… amani ya nafsi nzima.
UFAFANUZI Sherehe ya Pentekoste, Roho Mtakatifu anashuka juu ya itume na kuwawezesha kutangaza Injili kwa lugha mbalimbali. Huu ni uzinduzi rasmi wa Kanisa, lililo hai, lenye utume wa kimataifa. Katika mwanga wa Jubilei, tunaalikwa kuwa Kanisa lililo hai, lisilo na hofu, linalotangaza Injili kwa watu wa kila taifa na lugha. “Pokeeni Roho Mt…” Kristo anatuvuvia Roho wake aangaze usomaji mzuri na tafsiri maridhawa wa Maandiko Matakatifu, afufue mioyo iliyokufa kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya (Tito 3:5), atuumbe upya, atutunze… tunampokea Roho wa Bwana makusudi ajalie akili na hekima, awezeshe unabii, atawale vionjo vyetu, atupe nguvu za kutoa ushuhuda, atuelimishe. Mwaliko kwa wote uwe ni kukumbuka na kushukuru juu ya uwepo wake ndani yetu hasa katika Sakramenti za Ubatizo na Kipaimara… kujiimarisha kama Ngome imara dhidi ya aina zote za vishawishi na majaribu kwa msaada wake… kuomba msaada wa Roho Mt katika kuwaza, kunena na kutenda, katika kuachana na nguvu za ubaya, tabia na maelekeo yasiyofaa na badala yake kujivika upendo, wema na uzuri… kuisikiliza sauti yake anapozungumza nasi kwa njia ya Biblia na nasaha njema za wenzetu… kuomba bila kuchoka asituache, abaki nasi akitunyeshea mvua ya baraka yake na kutushushia mapaji yake saba, matunda ya roho (Gal 5:22-23) na karama zake zote.
Mtakatifu Paulo anaeleza kazi ya Roho katika kuwagawa karama kwa wingi, lakini kwa ajili ya mwili mmoja. Roho Mtakatifu anatuunganisha katika utofauti wetu, kwa huduma ya pamoja. Katika dunia iliyogawanyika, Kanisa linaitwa kuwa ishara ya umoja, kwa neema ya Roho. Kusali kwa Baba katika Roho Mtakatifu kwa njia ya Kristo Bwana wetu... zaidi sana aandamane nasi katika safari yetu ya maisha ili tuishi katika ukamilifu wake wote tukishika wajibu zetu kiaminifu kila mmoja kadiri ya nafasi yake kikanisa na kijamii, maisha ya sadaka na majitoleo, maisha yaliyojaa furaha takatifu. Yesu anawapa Mitume wake Roho Mtakatifu na mamlaka ya kusamehe dhambi. Roho anatolewa kwa ajili ya upya wa maisha, msamaha, na amani. Katika Jubilei hii, tunaitwa kuwa vyombo vya msamaha na uponyaji wa moyo kwa dunia inayoumia. Tunaitwa kumpenda Yesu kama huyo Yesu alivyotupenda sisi kwanza bila kuhesabu gharama, tukimtolea Yeye kila hatua tunayopiga katika maisha na kila pumzi yake tunayovuta anavyosema nasi Mtakatifu Paulo “… basi nasema enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili… tukiishi kwa Roho na tuenende kwa Roho” (Gal 5:16, 25)… na wakati huohuo tukizitumia karama za Roho kuujenga mwili wa fumbo wa Bwana yaani Kanisa na kufaidiana wenyewe kila mmoja na jirani yake (somo II- 1Kor 12:3b-7,12-13)… naam, katika Roho Mtakatifu tuzungumze lugha moja tu, lugha nzuri mdomoni na tamu masikioni, lugha inayoeleweka na watu wa hulka na kariba zote… lugha ya upendo kwa wote, msamaha kwa wote, lugha ya umoja na mshikamano!
Baba Mtakatifu Leo XIV katika maono yake ya kitume amesisitiza Kanisa kuwa ni chombo cha upatanisho na matumaini. Roho Mtakatifu ni moyo wa Kanisa, na kupitia kwake, tunakuwa mashuhuda wa: imani, mapendo na matumaini kwa waliosongwa na hofu. Amehimiza Kanisa liwe la kimisionari, la huruma na la amani. Pentekoste ni: Siku ya kuzaliwa kwa Kanisa Mwanzo wa utume wa dunia nzima, Kilele cha ahadi ya Yesu ya kutototuacha yatima, Katika Jubilei ya Matumaini: Tunaalikwa kuwa Kanisa la Roho Mtakatifu, lenye tumaini, lenye kutangaza Injili kwa ujasiri, na lenye kuponya kwa huruma." Ee Roho Mtakatifu, njoo katika mioyo yetu, familia zetu, makazini kwetu, na popote walipo watu wa Mungu Tuangaze kwa nuru yako, tuunganishe kwa upendo wako, na tutume kwa ujasiri wako ili tuwe mashahidi wa tumaini kwa ulimwengu huu Ewe kidole cha Mungu tuelekeze yatupasayo kutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu. Amina.