杏MAP导航

Tafuta

Sherehe ya Pentekoste ni siku ya waamini walei kutangaza na kushuhudia Injili inayosimikwa katika ushuhuda wa maisha yao adili na matakatifu. Sherehe ya Pentekoste ni siku ya waamini walei kutangaza na kushuhudia Injili inayosimikwa katika ushuhuda wa maisha yao adili na matakatifu.   (Vatican Media)

Sherehe ya Pentekoste: Kuzaliwa Kwa Kanisa, Mwanzo wa Maisha na Ushuhuda wa Waamini

Sherehe ya Pentekoste ya kwanza, Ujio wa Roho Mtakatifu aliyeliwezesha Kanisa kuwa ni: moja, takatifu, katoliki na la mitume kuzaliwa. Hii ni siku ya walei kutangaza na kushuhudia Injili inayosimikwa katika ushuhuda wa maisha yao adili na matakatifu. Huu ni mwaliko wa kugundua kwa mshangao zawadi ya Injili waliyoipokea katika lugha zao wenyewe. Kugundua ile zawadi ya kuinjilishwa na kwa kupokea zawadi ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, katika Sherehe ya Pentekoste, siku ya hamsini baada ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kanisa limezaliwa kutoka katika nguvu ya Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Mwanga wa Kristo Mfufuka katika Jumuiya ya kwanza ya wafuasi wa Kristo Yesu umevunjilia mbali ubinafsi na woga dhidi ya wafuasi wengine. Mwanga huu ukawahamasisha kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari hadi miisho ya dunia! Huko, wakatangaza na kushuhudia upendo wa Mungu uliomwilishwa katika umoja na ushirikiano; ushuhuda na udugu! Hii ni changamoto kwa Wakristo kuendelea kuishi katika umoja unaofumbatwa katika utofauti wao kama ulivyoshuhudiwa na Kristo Yesu. Pentekoste ni siku ya udhihirisho wa hadhara wa Yesu (KKK 767, 1076), siku ya utimilifu wa ufunuo wa Utatu Mtakatifu (KKK 732), siku ya mmimino wa Roho Mtakatifu (KKK 696, 731, 1287, 2623). Kumbe katika sherehe hii tunasherehekea utimilifu wa fumbo la ukombozi wetu kwa Roho Mtakatifu kuwashukia mitume. Yeye huyu Roho Mtakatifu ndiye ishara ya umoja wetu na Mungu kama wimbo wa mwanzo unavyoimba; “Roho ya Bwana imeujaza ulimwengu, nayo inayoviunganisha viumbe vyote, kujua maana ya kila sauti, aleluya” (Hek.1:7). Kazi yake ni kutuunganisha sisi na Mungu na sisi kwa sisi ili tuishi kwa pendo lake Mungu lililomiminwa katika mioyo yetu, kupitia huyu Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi. Aleluya! (Rum.5:5).

Sherehe ya Pentekoste, Mwanzo wa Kanisa, Maisha na Utume wake
Sherehe ya Pentekoste, Mwanzo wa Kanisa, Maisha na Utume wake

Hii ni siku ya kukumbuka kuzaliwa kwa Kanisa na mwanzo wa utume wake. Ni katika tumaini hili Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu, wewe unalitakasa Kanisa lako lote lililo kati ya makabila na mataifa yote kwa fumbo la sikukuu ya leo. Eneza mapaji ya Roho Mtakatifu po pote duniani; na zile karama ulizozitoa tangu mwanzo wa kuhubiri Injili, hata sasa uzieneze kwa juhudi ya waamini wako.” Ikumbukwe kuwa Sherehe hii inahitimisha kipindi cha Pasaka. Katekisimu inatufundisha hivi; “Siku ya Pentekoste, mwishoni mwa juma saba za Pasaka, Pasaka ya Kristo inatimilika kwa kummimina Roho Mtakatifu, ambaye amedhihirishwa, ametolewa na kushirikishwa kama nafsi ya Mungu: kutoka utimilifu wake Kristo, Bwana anammimina Roho kwa wingi” (KKK 731). Hivyo Mshumaa wa Pasaka unazimwa na kutunzwa kwa heshima karibu na kisima cha Ubatizo kama kipo au sehemu nyingine na unawashwa wakati wa ubatizo, ili mishumaa ya wabatizwa iwashwe kutokea mshumaa huu, na katika mazishi unawekwa kando ya jeneza, ishara ya kifo cha mkristo ni Pasaka halisi. Na kuanzia Jumatatu baada ya Pentekoste, tunaacha kusali sala ya Malkia wa mbingu, na tunaanza kusali sala ya Malaika wa Bwana na tunaendelea na kipindi cha kawaida cha dominika za mwaka C na sherehe zingine.

Sherehe ya Pentekoste: Roho Mtakatifu aliwashukia Mitume
Sherehe ya Pentekoste: Roho Mtakatifu aliwashukia Mitume   (Vatican Media)

Somo la kwanza ni kutoka katika la Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 2:1-11). Somo hili linasimulia jinsi tukio la ujio wa Roho Mtakatifu lilivyotukia siku ya Pentekoste kuwa; kulitokea upepo wa nguvu na ndimi za moto, alama ya Roho Mtakatifu, viliwashukia mitume, na kwa nguvu zake walipata ujasiri wa kuhubiri Injili. Pia umoja na uelewano uliopotea sababu ya dhambi uliletwa tena kati ya mataifa kwa watu wote kusikia mitume wakisema kwa lugha zao matendo makuu ya Mungu. Ni katika muktadha huu utangulizi wa sherehe hii unasema hivi; “Hapo mwanzo wa Kanisa huyo Roho Mtakatifu aliyafundisha mataifa yote kumjua Mungu, akawaunganisha watu wa lugha mbalimbali katika kuungama imani moja.” Mzaburi alivyoyatafakari matendo haya makuu ya Mungu aliimba zaburi hii ya wimbo wa katikati akisema; “Ee nafsi yangu umhimidi Bwana, Wewe, Bwana, Mungu wangu, umejifanya mkuu sana; Ee Bwana, jinsi yalivyo mengi matendo yako! Dunia imejaa mali zako. Waiondoa pumzi yao, wanakufa, na kuyarudia mavumbi yao, waipeleka roho yako, wanaumbwa, nawe waufanya upya uso wa nchi. Utukufu wa Bwana na udumu milele; Bwana na ayafurahie matendo yake. Kutafakari kwangu na kuwe kutamu kwake; Mimi nitamfurahia Bwana (Zab. 104:1, 24, 29-31,34).

Pentekoste ni mwaliko wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi
Pentekoste ni mwaliko wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi   (@Vatican Media)

Somo la pili ni la waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorinto (1Kor.12:3b-7,12-13). Katika sehemu hii ya waraka wake, Mtume Paulo anatueleza kuwa Roho Mtakatifu ni msingi wa karama na huduma mbalimbali katika Kanisa (KKK 1830-1832). Naye ndiye anayezifanya karama hizo zilete faida na umoja katika jumuiya nzima kama viungo mbalimbali vya mwili vinavyosaidiana kwa faida ya mwili mmoja. Fundisho hili la mtume Paulo ndilo msingi wa sala baada ya komunio anayosali mama Kanisa akisema; “Ee Mungu, umelijalia Kanisa lako mapaji yako ya mbinguni. Uilinde neema hiyo uliyotujalia, ili mapaji ya Roho Mtakatifu tuliyoyapokea yasitawi daima, nacho chakula cha roho kituongezee ukombozi wa milele. Kumbe vipaji tulivyo navyo, kila mmoja wetu ni zawadi ya Mungu kwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu, nasi tunapaswa kuvitumia kwa kufaidiana sisi kwa sisi.

Pentekoste; Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia Injili
Pentekoste; Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia Injili   (@Vatican Media)

Injili ni ilivyoandikwa na Yohane (Yn.20:19-23). Sehemu hii ya Injili inatufundisha kuwa Roho Mtakatifu aliyefanya kazi ya kuwaunganisha Mitume na Yesu mfufuka, sasa anatuunganisha sisi na Mungu kwa kutuondolea dhambi zetu tunapotubu na kuomba msamaha kwa moyo wa majuto. Pato la kazi hii ya Roho Mtakatifu ni amani kati ya Mungu na sisi. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba Roho Mtakatifu atufumbulie zaidi siri ya sadaka hii, kama alivyotuahidia Mwanao. Atujulishe pia ukweli wote kwa rehema yake.” Kumbe, tunaona kuwa tunaposherehekea ujio wa Mungu Roho Mtakatifu, nafsi ya tatu ya Utatu Mtakatifu, asiye na mwanzo wala mwisho, tunapata nguvu za kuishuhudia imani yetu maana yeye ndiye mfariji, mtakatifuzaji, kiongozi na mwalimu wetu. Ndiye anayewajalia watu anaowashukia vipaji nyake; hekima, akili, shauri, nguvu, elimu, ibada na uchaji kwa Mungu na karama zake; unabii, uponyaji, ualimu na kunena kwa lugha, kila mmoja kadiri atakavyo yeye kusudi tuvitumie kwa kufaana. Hivyo basi, yatupasa kutambua kuwa karama hizi ni zawadi kutoka kwa Mungu zinazotufikia kwa njia ya Roho Mtakatifu. Nasi hatuna budi kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Roho Mtakatifu kwa kuzitumia vyema karama anazotujalia kwa manufaa ya wote, kwa maana tusipozitumia vyema tutadaiwa siku ya mwisho. Tutambue kuwa vipaji hivi ni zawadi kwa ajili ya kuhudumiana, kujengana na kufaidiana sisi kwa sisi tukiongozwa na upendo wetu kwa Kristo Yesu, Bwana na Mwokozi wetu.

Roho Mtakatifu ni chemchemi ya furaha ya familia
Roho Mtakatifu ni chemchemi ya furaha ya familia

Tujihadhari na dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu (KKK 1864), kwa kwani Yesu anasema; “kwa sababu hiyo nawaambieni, watu watasamehewa dhambi na kufuru zao zote, lakini hawatasamehewa dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu” (Mt.12:31). Basi tukubali kuongozwa na Roho Mtakatifu, na kujitahidi kuiishi amri kuu ya mapendo katika kila hatua ya maisha yetu. Kwa maana upendo daima huvumilia, ni mpole, hauna wivu, haujidai, haujivuni, una adabu, tena hautafuti faida yake binafsi, haufurahii maovu, bali ukweli (1Kor.4-6). Tumruhusu Roho Mtakatifu akae ndani ya mioyo yetu, ndani ya nafsi zetu, ndani ya familia zetu na jumuiya zetu atufundishe kuishi kwa upendo, atufanye tuwe safi, aondoe tabia zinazoendana na hila za shetani. Awashe ndani mwetu moto wa mapendo, atupe Roho ya hekima na elimu, atufundishe kusali vizuri, atushushie kipaji cha ukweli na mapendo ya kweli. Aondoe vilema vyote vinavyoweza kutuvuruga na kutuletea maafa, atutie nguvu ya kuweza kufahamu madhaifu yetu, ili sote tuungane na kuwa mwili mmoja katika Kristo na tuione sura ya Mungu katika wenzetu kwa kuwapenda kama Kristo Yesu alivyoagiza. Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari Pentekoste
05 Juni 2025, 16:22