杏MAP导航

Tafuta

Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni ni wito na mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni mashuhuda na watangazaji wa Injili ya matumaini katika ulimwengu mamboleo. Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni ni wito na mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni mashuhuda na watangazaji wa Injili ya matumaini katika ulimwengu mamboleo.  (@VATICAN MEDIA)

Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Mashuhuda wa Injili ya Matumaini

Lakini kutoweka kwake na kutomwona tena haina maana kuwa amejitenga nasi na kutuacha Yatima. La hasha! Yesu yupo pamoja nasi katika Neno lake na katika Sakramenti akifanya kazi kwa njia ya Roho Mtakatifu. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatufundisha hivi: “Kupaa kwa Kristo ni alama Dhahiri ya kuingia ubinadamu wa Yesu ndani ya makao ya mbingu ya Mungu, ambako toka huko atarudi, lakini ubinadamu huu kwa sasa unamficha mbele ya macho ya watu. KKK 665.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu katika sherehe ya kupaa mbinguni kwa Bwana wetu Yesu Kristo, mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa. Tukio hili ni ukamilifu wa umasiha wake, ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Sherehe hii inaadhimishwa kila mwaka siku ya arobaini baada ya dominika ya ufufuko. Lakini kwa sababu za kichungaji, inahamishiwa dominika ya karibu zaidi na siku ya 40. Ikumbukwe kuwa siku 40 kibibilia maana yake ni kipindi cha kutosha ambacho Kristo mfufuka aliwatokea wanafunzi wake akiwapa katekesi kusuhu fumbo la ukombozi, yaani mateso, kifo na ufufuko wake. Baada ya kipindi hicho alitoweka rasmi katika upeo wa macho yao wasimuone tena. Lakini kutoweka kwake na kutomwona tena kwa macho ya kibinadamu haina maana kuwa amejitenga nasi na kutuacha Yatima. La hasha! Yesu yupo pamoja nasi katika Neno lake na katika Sakramenti akifanya kazi kwa njia ya Roho Mtakatifu. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatufundisha hivi: “Kupaa kwa Kristo ni alama Dhahiri ya kuingia ubinadamu wa Yesu ndani ya makao ya mbingu ya Mungu, ambako toka huko atarudi, lakini ubinadamu huu kwa sasa unamficha mbele ya macho ya watu (KKK 665). Kupaa kwake Yesu Kristo mbinguni ni tumaini kwetu kuwa tukiyazingatia mafundisho yake, nasi baada ya kifo tutafika huko aliko. Katekisimu inaweka wazi fundisho hili.

Sherehe ya Kupapa Bwana Mbinguni: Injili ya Matumaini.
Sherehe ya Kupapa Bwana Mbinguni: Injili ya Matumaini.

Tunasoma hivi; “Yeye peke yake aliyetoka kwa Baba, ameweza kurudi kwa Baba. Hivyo Yeye peke yake ameweza kumfungulia mtu njia hii ili tukae kukiamini kwamba sisi tulio viungo vyake ametutanguliaa huko aliko Yeye aliye kichwa chetu na shila letu (KKK 661). Ndiyo maana mama Kanisa katika sala ya mwanzo anatuombea kwa matumaini hayo akisali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi, utufanye tuwe na furaha takatifu na shukrani; kwa maana kupaa kwake Kristo Mwanao ni mfano wetu; na huko alikotangulia yeye kichwa chetu, ndiko tunako tumaini kufika sisi tulio mwili wake”. Nasi tunaamini kuwa Yesu anakuja kumchukua kila mmoja kwa wakati wake siku ya kifo chake. Ndiyo maana malaika aliwaambia mitume maneno haya ya wimbo wa mwanzo akisema; “Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Atakuja vivyo hivyo mlivyomwona akienda zake mbinguni, aleluya” (Mdo.1:11).

Waanmini wanaitwa na kutumwa kuwa ni Mashuhuda wa Injili ya Matumaini
Waanmini wanaitwa na kutumwa kuwa ni Mashuhuda wa Injili ya Matumaini   (@Vatican Media)

Somo la kwanza ni la kitabu cha matendo ya Mitume (Mdo. 1:1-11). Somo hili ni wosia wa Bwana wetu Yesu Kristo kwa Mitume kabla ya kupaa kwake mbinguni. Katika wosia huu Yesu anawaambia waihubiri Habari Njema duniani kote na anawaahidi zawadi ya Roho Mtakatifu atakaye wakumbusha yote aliyowafundisha na kuwaongoza siku zote katika kuitangaza habari njema ya wokovu. Baada ya maagizo haya Yesu “alichukuliwa juu na wingu likampokea wasimwone tena katika upeo wa macho yao, lakini akawa pamoja nao kwa njia ya Roho Mtakatifu akiwaimarisha katika kutangaza habari njema ya wokovu. Nasi kwa njia ya ubatizo na kipaimara tumempokea Roho Mtakatifu, hivyo hatuna budi kuwa mashahidi wa Imani yetu kwa Kristo katika maisha yetu ya kila siku kwa furaha tukiziimba sifa za Mungu kama zaburi ya wimbo wa katikati inavyotualika; “Enyi watu wote, pigeni makofi, mpigieni Mungu kelele za shangwe, kwa kuwa Bwana aliye juu, mwenye kuogofya, ndiye mfalme mkuu juu ya dunia yote. Mungu amepaa kwa kelele za shangwe, Bwana kwa sauti ya baragumu. Mwimbieni Mungu, naam, imbeni; mwimbieni mfalme wetu, naam, imbeni. Maana Mungu ndiye mfalme wa dunia yote. Imbeni kwa akili, Mungu awamiliki mataifa, Mungu ameketi katika kiti chake kitakatifu” (Zab. 47:1-2, 5-6, 7-8).

Mashuhuda wa Injili ya Matumaini
Mashuhuda wa Injili ya Matumaini   (@Vatican Media)

Somo la pili ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso (Ef. 1:17-23). Somo hili ni sala ya kitume inayotuombea hekima na ufahamu wa mambo makuu ya Mungu uliofunuliwa katika Kristo Yesu. Tunasoma hivi; “Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwisho wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya Kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.” Kristo ndiye kichwa cha Kanisa na ulimwengu. Yeye yuko juu ya vitu vyote na nguvu zote. Nasi hatupaswi kuwa na wasiwasi wowote, maana tukiwa upande wake hakuna atakayeshinda nasi, akatushinda.

Familia ni msingi bora wa malezi na makuzi ya Kikristo
Familia ni msingi bora wa malezi na makuzi ya Kikristo   (@Vatican Media)

Injili ni ilivyoandikwa na Luka (Lk. 24:46-53). Sehemu hii ya Injili inatueleza kuwa, Yesu kabla ya kupaa mbinguni aliwakumbusha wanafunzi wake kuwa mateso, kifo, ufufuko na uenezaji wa Injili yake duniani kote, vilitabiriwa na manabii toka zamani katika Agano la Kale. Haya yote ni kwa ajili ya toba na ondoleo la dhambi kwa kila anayemwamini. Na nguvu ya Roho Mtakatifu itawawezesha kuieneza Injili kwa furaha duniani kote. Baada ya kuwakumbusha habari hizi na kuwaahidi zawadi ya Roho Mtakatifu, aliwaongoza mpaka Bethania, akawabariki, na kisha kuwabariki akachukuliwa juu mbinguni wasimwone tena kwa macho ya kibinadamu. Huko mbinguni aliko Yeye ni mkuu na mmiliki wa vitu vyote. Yuko juu ya vitu vyote, amevikwa taji ya ushindi na utukufu. Kumbe basi, Sherehe hii ya Kupaa Bwana Mbinguni inatukumbusha kuwa maisha ya hapa duniani ni ya muda tu. Maisha ya umilele yako mbinguni Kristo aliko na ni hamu yetu kufika huko. Ni katika tumaini hili Mama Kanisa kwenye sala zote katika liturujia ya sherehe hii anatuombea akielekeza hamu yetu mbinguni. Katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi, utufanye tuwe na furaha takatifu na shukrani; kwa maana kupaa kwake Kristo Mwanao ni mfano wetu; na huko alikotangulia yeye kichwa chetu, ndiko tunakotumaini kufika sisi tulio mwili wake.”

Mahujaji wa matumaini na wainjilishaji wa upendo
Mahujaji wa matumaini na wainjilishaji wa upendo   (@Vatican Media)

Katika sala ya kuombea dhabihu anasali; “Ee Bwana tunaleta sasa kwa unyenyekevu sadaka yetu kwa heshima ya kupaa kwake Mwanao. Tunakuomba utujalie kila tunapoyapokea mafumbo haya matakatifu, tuzidi kuyajongea ya mbinguni. Na katika sala baada ya komunio inayohitimisha maadhimisho haya anasali hivi; “Ee Mungu mwenyezi, wewe watujalia sisi tulio hapa duniani kushughulika na mambo ya mbinguni. Tunakuomba uuelekeze moyo wetu wa ibada huko aliko Bwana wetu, Mungu-mtu”. Hili ndilo tumaini la kila mwandamu aliye chini ya jua. Sasa ili tuweze kufika Mbinguni aliko Kristo, yatupasa tufuate agizo lake; “Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu (Mt. 28: 19). Hili ni jukumu la kila mbatizwa. Kumbe kuihubiri Injili kwa maneno na matendo yetu, kusali, kulisoma, kulitafakari na kuliishi neno la Mungu, kupokea sakramenti kwa kustahili na kutenda matendo mema, ndiyo masurufu yetu ya njiani kuelekea mbinguni. Tuombe neema ya kuyafanya haya ili siku ya mwisho wa maisha yetu hapa duninia ikiwadia, atakapokuja kutuita dada yetu kifo – kama alivyokuwa anamuita Mtakatifu Fransisko wa Asizi, tupate kustahilishwa kuingia katika uzima wa milele mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo

02 Juni 2025, 13:12