杏MAP导航

Tafuta

Tafakari na Neno la Mungu, Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu.: Mungu mmoja katika Nafsi Tatu! Tafakari na Neno la Mungu, Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu.: Mungu mmoja katika Nafsi Tatu! 

Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu: Mungu Mmoja Katika Nafsi Tatu!

Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, msingi wa Mafumbo yote yanayosherehekewa na Kanisa kwa nyakati mbalimbali. Hili ni Fumbo la imani na la maisha ya Kikristo. Ni Fumbo la Mungu ndani yake Mwenyewe. Mwenyezi Mungu katika historia na Mpango wa ukombozi amejifunua kuwa ni Mungu mmoja katika Nafsi Tatu. Mungu Baba Muumbaji; Mungu Mwana Mkombozi na Mungu Roho Mtakatifu ni Mfariji na Mtakatifushaji.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, katika Sherehe ya Utatu Mtakatifu, Fumbo kuu la imani yetu kuwa katika Mungu mmoja kuna Nafsi tatu: Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu, zote zikiwa sawa katika uasili wao. Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, msingi wa Mafumbo yote yanayosherehekewa na Kanisa kwa nyakati mbalimbali. Hili ni Fumbo la imani na la maisha ya Kikristo. Ni Fumbo la Mungu ndani yake Mwenyewe. Mwenyezi Mungu katika historia na Mpango wa ukombozi amejifunua kuwa ni Mungu mmoja katika Nafsi Tatu. Baba Mungu Mwenyezi Mwumba mbingu na nchi, na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Kanisa linasadiki kwa Kristo Yesu, Mwana wa pekee, wa Mungu aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote. Ni Mungu aliyetoka kwa Mungu, Mwanga kwa mwanga. Mungu kweli kwa Mungu kweli. Aliyezaliwa bila kuumbwa, Mwenye umungu mmoja na Baba. Ndiye aliyeshuka kutoka mbinguni kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kanisa linasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana na mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa na Baba na Mwana: Aliyenena kwa vinywa vya Manabii.

Fumbo la Utatu Mtakatifu
Fumbo la Utatu Mtakatifu   (@VATICAN MEDIA)

Utatu Mtakatifu ni moyo na kiini cha imani yetu ya Kikristo. Ni fumbo asili la imani na maisha ya Kikristo. Kwa Utatu Mtakatifu tunafunuliwa upendo, wema, ukuu, mamlaka na huruma ya Mungu. Ni katika Utatu Mtakatifu ndimo tunamopata ufupisho na simulizi la asili yetu tangu kuumbwa hata ukombozi kwa njia ya Yesu Kristo, Nafsi ya pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu ndimo zinamolala sala zetu na matumaini yetu kufikia utimilifu wa upendo kwa kuungana na yule aliye asili ya upendo (KKK 249-256, 290-292). Hili ni adhimisho la fumbo la imani na imani tu yaelewa. Ni katika muktadha huu mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “E Mungu Baba, uliwafumbulia watu fumbo lako la ajabu, hapo ulipompeleka Neno wako na Roho Mtakatifu ulimwenguni. Utujalie kuutambua utukufu wa Utatu Mtakatifu wa milele katika kuungama imani ya kweli na kuabudu Umoja wa Mungu katika enzi ya fahari yake”. Kuufahamu na kuuelewa Utatu Mtakatifu ni kuziangalia na kuzitafakari kazi zake katika maisha yetu kwa kuidhihirsha huruma yake kama wimbo wa mwanzo unavyosema: “Asifiwe Mungu Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; kwa sababu ametufanyizia huruma yake.”

Fumbo la Utatu Mtakatifu Mungu Mmoja Nafsi tatu
Fumbo la Utatu Mtakatifu Mungu Mmoja Nafsi tatu   (@Vatican Media)

Masomo kwa ufupi: Somo la Kwanza ni la Kitabu cha Mithali (Mit. 8:22-31). Sehemu ya somo hili inatukumbusha kipindi Waisraeli wakiwa utumwani Babeli. Nalo linazungumzia juu ya hekima iliyojionesha kama nafsi aliyekuwa pamoja na Mungu kabla ya kumbwa chochote. Hekima hii ni Yesu Kristo Nafsi ya pili ya Mungu. Kumbe, tunaona kuwa katika Agano la Kale ukweli juu ya siri ya Fumbo la Utatu Mtakatifu ilianza kujidhihirisha.  Somo la pili la ni la waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 5:1-5). Somo hili linatufundisha kwamba kwa imani tunashiriki uzima wa Utatu Mtakatifu. Mungu Baba ndiye aliyetufanya tuwe wenye haki na watakatifu kwa njia ya Mwanawe Yesu Kristo. Tena pendo la Baba na Mwana limemiminwa mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Na Injili ni ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 16:12-15). Sehemu hii ya Injili inatufundisha kuwa Yesu alipotumwa na Mungu Baba, alikuwa na mengi ya kuwaambia wanafunzi wake kabla ya kifo chake. Lakini kwa kuwa uwezo wa mwanadamu una mipaka na hivyo wasingeweza kustahimili makuu haya Mungu, aliwaahidi Roho Mtakatifu atakayewakumbusha mafundisho yake na kuwaangazia ili wayafahamu kikamilifu. Kumbe hivi ndivyo Utatu Mtakatifu ulivyojifunua na kujidhihirisha kwetu katika matendo haya makuu ya Mungu.

Fumbo la Utatu Mtakatifu msingi wa mafumbo yote ya Kanisa
Fumbo la Utatu Mtakatifu msingi wa mafumbo yote ya Kanisa   (@Vatican Media)

Utatu Mtakatifu ni Fumbo la Imani. Na kuuelewa muungano na umoja uliopo katika nafsi hizi tatu katika Mungu mmoja kwa akili za kibindamu ni jambo lisilowezekana kwani fumbo hili lapita uwezo wa ufahamu wetu. Ni Mungu pekee ndiye anayetuwezesha kulifahamu kwa njia ya ufunuo wake mwenyewe. Mtakatifu Augustino alipojaribu kwa akili yake kupembua siri hii kuu, Mungu mwenyewe alimuweka wazi kupitia malaika katika mfano wa mtoto mdogo na kumwambia wazi kuwa akili ya mwanadamu ni ndogo kiasi kwamba haiwezi lolote. Ndiyo maana anatufundisha akisema; “Inatupasa kusadiki kwa sababu Mungu ametufunulia. Lakini mafumbo kama haya katika imani yetu ni kama mifupa katika nyama. Kama tusivyoitupilia mbali mifupa pamoja na nyama iliyo juu yake bali tunakwangua nyama yote na kuachana na mifupa, na haya mafumbo hatuwezi kuyakimbia moja kwa moja tutafanya tuwezalo ili kuelewa kinachoweza kueleweka; pale tutakapokwama na kushindwa, hatuna budi kupiga magoti na kusadiki.” Naye Thomaso wa Akwino anashauri kwamba: “ukikutana na lolote ambalo hulielewi ama katika Biblia au katika mafundisho ya Kanisa usiseme mambo haya hayaeleweki au yamekosewa bali useme akili zangu ni ndogo kuelewa ukweli huu.” Fanya juhudi kuelewa utakavyoweza. Yatakayokushinda “Inamisha kichwa mpaka nchi na kusema pamoja na mtakatifu Hipoliti kuwa; “nasadiki kwa kuwa sina uwezo wa kueleza” (Nasadiki kwa kuwa ni upuuzi).

Fumbo la Utatu Mtakatifu: Umungu Msalabani na Ubinadamu Altareni
Fumbo la Utatu Mtakatifu: Umungu Msalabani na Ubinadamu Altareni   (@Vatican Media)

Yeye huyu Mtakatifu Thoma wa Akwino aliyejaliwa uelewa mkubwa na wa hali ya juu wa mambo yamhusuyo Mungu katika wimbo tunaouimba wakati wa kuabudu Ekaristi Takatifu anasema; “Waficha Umungu msalabani, na ubinadamu altareni, mafahamu yangu yadanganya yanapokuona, nami nasadiki bila haya”. Mtume Paulo naye anasema: “Basi, sisi twafundisha, si kwa maneno tuliyofundishwa na hekima ya binadamu, bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua mambo ya kiroho kwa walio na huyo Roho. Mtu wa kidunia hapokei mambo ya Roho wa Mungu. Kwake mtu huyo mambo hayo ni upumbavu mtumpu; yanapita akili yake; maana yanaweza tu kutambuliwa kwa msaada wa Roho. Maandiko yanasema, nani awezaye kuifahamu akili ya Bwana? Lakini sisi tunayo akili ya Kristo (1Kor.2:13-16). Mama Kanisa anafuata maandiko matakatifu ambayo kwayo Mungu mwenyewe anajifunua kwetu. Katika kitabu cha Mwanzo 1:1-2 tunasoma: “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji. Roho wa Mungu akatulia juu ya uso wa Maji.” Hili ni dokezo la udhihirisho wa uwepo wa Roho Mtakatifu tangu mwanzo. Katika kitabu cha Methali 8: 1-36 kinamtaja Hekima (Neno wa Mungu ambaye ni Kristo) akisema; “Kabla Mungu hajaumba dunia na mashamba yake, nilikuwa pamoja naye kama fundi stadi.”. Mwanzo 1:24 “Mungu akasema; Natumfanye mtu kwa sura na mfano wetu.

Roho Mtakatifu ni Mfariji
Roho Mtakatifu ni Mfariji   (@Vatican Media)

Mungu akasema (ni mmoja anayesema), kwa sura na mfano wetu (ni wingi). Hii tayari inatuonyesha kuwa Mungu ni Mmoja katika Nafsi zaidi ya moja ndiyo maana Kumbukumbu la Torati 6:4 liliwakumbusha Waisraeli likisema; “Sikiliza ee Israeli Bwana Mungu wetu Bwana ndiye Mmoja”. Katika Yohane 14: 15-17, Yesu anasema; “Mkinipenda mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine ndiye Roho wa Ukweli.” Pale Filipo alipomwuliza tuoneshe Baba yatutosha, Yesu alijibu kama anavyoandika Mwinjili Yohane 14:8-10 akisema; “Filipo; aliyeniona mimi amemwona Baba, Mimi ni ndani ya Baba na Baba yu ndani yangu.” Jibu hili ni gumu kuelewa kwa akili ya kibinadamu, imani tu yaelewa. Naye Mtume Paulo anapowasalimu wakristo katika Salamu-tangulizi za barua zake haachi kusema “neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba na ushirika wa Roho Mtakatifu viwe nanyi nyote.” Katika Injili ya Mathayo 28:19 Yesu anaagiza “watu wa mataifa yote wabatizwe kwa jina la Utatu Mtakatifu-Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.”

Roho Mtakatifu ni Mfariji na analitakatifuza Kanisa
Roho Mtakatifu ni Mfariji na analitakatifuza Kanisa   (@Vatican Media)

Mtakatifu Augustino anasema; ‘‘Roho Mtakatifu anatoka kwa Baba kama chanzo cha kwanza, na ni paji la milele analolitoa Baba kwa mwana, anatoka katika umoja wa Baba na Mwana.’’ Kupelekwa kwa Roho Mtakatifu ambaye Baba anamtuma kwa jina la Mwana na ambaye Mwana anamtuma toka kwa Baba, kunafunua kwamba yeye pamoja nao ni Mungu huyo huyo mmoja (Yon. 14:15-17) katika nafsi tatu. Ni kwa upendo wa Mungu dunia na vyote vilivyomo, vinavyoonekana na visivyoonekana vilifanyika (Yon.1:2). Ni kwa upendo wa Mungu taifa la Israeli liliandaliwa kwa ajili ya wokovu wa wanadamu. Ni kwa upendo wa Mungu Baba, “Kristo alijinyenyekeza akawa mtii mpaka mauti, naam hata mauti ya msalaba” (Wafilipi. 2:8) na ni kwa upendo wa Mungu Baba, Kanisa liliimarishwa na kuendelea kukua kutokana na ujio wa Roho Mtakatifu aliyetoka kwa Baba na Mwana siku ya Pentekoste (Mdo.1:8; 2:1-13). Na huu ni udhibitisho wa Kibibilia wa ufunuo wa Utatu Mtakatifu kwa sababu aliyetufunulia ni Mungu mwenyewe, nasi hatuna budi kuamini na kusadiki kuwa huu ni ukweli mtupu. Ufunuo huu wa Utatu Mtakatifu unatuonyesha kuwa Baba ni Muumbaji, Mungu Mwana ni Mkombozi na Mungu Roho Mtakatifu ni Mfariji. Lakini katika yote haya hawakuachana. Katika uumbaji, Mungu Mwana alikuwepo na kushiriki: “Hapo mwanzo kulikuwa Neno naye Neno alikuwa kwa Mungu naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo, wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika” (Yoh.1:1). Katika ukombozi Mungu Baba alikuwepo: “Yesu akasema, wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo ninyi nyote mtatawanywa kila mtu kwake, nami nitaachwa peke yangu. Lakini mimi siko peke yangu, maana Baba yangu yu pamoja nami’ (Yn.16:32).

Fumbo la Utatu Mtakatifu Chimbuko la Mafundisho ya Kanisa
Fumbo la Utatu Mtakatifu Chimbuko la Mafundisho ya Kanisa   (@Vatican Media)

Katika maisha yetu ya kila siku tunakiri na kuutangaza Utatu Mtakatifu. Kila mara katika sala zetu tunaanza na kuhitimisha kwa ishara ya msalaba huku tukitamka waziwazi maneno; “Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu.” Katika hii sala rahisi, tunakiri kile tunachokiamini kwa kirefu katika Kanuni ya Imani katika sehemu kuu tatu tukianza kwa kusema: “Nasadiki kwa Mungu Baba Mwenyezi, mwumba wa mbingu na Dunia… Nasadiki kwa Yesu Kristo, Mwana wa pekee wa Mungu, ameshuka toka mbinguni kwa ajili yetu sisi wanadamu na kwa ajili ya wokovu wetu…Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima…” Tunapaswa kufanya hivyo kabla ya kulala na kila tunapoamka, kabla na baada ya kula, kabla na baada ya kazi, na nyakati mbalimbali katika maisha yetu ya kila siku. Ni kwa njia hii tunatangaza waziwazi msingi wa imani yetu. Tunaposherehekea Fumbo la Utatu Mtakatifu tuombee umoja katika familia, Kanisa la nyumbani. Ndiyo maana Katekisimu inatufundisha hivi: “Familia ya Kikristo ni umoja wa watu,ishara na mfano wa umoja wa Baba na Mwana na Roho Mtakatifu” (KKK 2205). Tuombee umoja katika Kanisa kama Yesu alivyotuombea: Nawaombea wawe kitu kimoja kusudi ulimwengu upate kuamini kwamba wewe ulinituma” (Jn 17:21). Basi tuzingatie wosia wa Paulo: “Hatimaye ndugu, kwa herini; mtimilike, mfarijike, nieni mamoja, mkae katika amani; na Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi katika Utatu Mtakatifu. Salimianeni kwa busu takatifu” (2Kor 13:11-14). Tumsifu Yesu Kristo!

Fumbo la Utatu Mtakatifu
13 Juni 2025, 15:58