杏MAP导航

Tafuta

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu Kiini cha Imani na Mafumbo ya Kanisa. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu Kiini cha Imani na Mafumbo ya Kanisa.  (@Vatican Media)

Sherehe ya Utatu Mtakatifu: Kiini cha Imani Na Mafumbo ya Kanisa

Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu ni msingi wa Mafumbo yote yanayosherehekewa na Kanisa. Hili ni Fumbo la imani na la maisha ya Kikristo. Ni Fumbo la Mungu ndani yake Mwenyewe. Mwenyezi Mungu katika historia na Mpango wa ukombozi amejifunua kuwa ni Mungu mmoja katika Nafsi Tatu. Baba Mungu Mwenyezi Mwumba mbingu; Kristo Yesu, Mwana wa pekee, wa Mungu aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote.; Roho Mtakatifu ni Bwana mleta uzima na mfariji.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: “Umoja wetu - u - katika Utatu Mtakatifu Mungu Mmoja chanzo na tumaini letu.” Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya Neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican leo, Katika Dominika hii Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Sherehe hii hutupatia kwa muhtasari maana ya Fumbo hili tunaloliadhimisha. Imani yetu katika Mungu mmoja si umoja wa nafsi bali ni Mungu mmoja katika nafsi tatu, yaani, Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Neema ya Bwana wetu Kristo Yesu, na pendo la Mungu na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote! Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, msingi wa Mafumbo yote yanayosherehekewa na Kanisa kwa nyakati mbalimbali. Hili ni Fumbo la imani na la maisha ya Kikristo. Ni Fumbo la Mungu ndani yake Mwenyewe. Mwenyezi Mungu katika historia na Mpango wa ukombozi amejifunua kuwa ni Mungu mmoja katika Nafsi Tatu. Baba Mungu Mwenyezi Mwumba mbingu na nchi, na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Kanisa linasadiki kwa Kristo Yesu, Mwana wa pekee, wa Mungu aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote. Ni Mungu aliyetoka kwa Mungu, Mwanga kwa mwanga. Mungu kweli kwa Mungu kweli. Aliyezaliwa bila kuumbwa, Mwenye umungu mmoja na Baba. Ndiye aliyeshuka kutoka mbinguni kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kanisa linasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana na mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa na Baba na Mwana: Aliyenena kwa vinywa vya Manabii.

Fumbo  la Utatu Mtakatifu ni kiini cha imani na mafumbo ya Kanisa
Fumbo la Utatu Mtakatifu ni kiini cha imani na mafumbo ya Kanisa   (@Vatican Media)

Hili ni fumbo la msingi la imani na la maisha ya kikristo, ni Fumbo la Mungu ndani yake mwenyewe na ni chanzo cha mafumbo mengine yote ya imani. Utatu Mtakatifu ni fumbo la kimungu na kwa sababu linagusa moja kwa moja undani wa Mungu mwenyewe undani ambao mwanadamu kwa uwezo wake hawezi kuuingia kuupambanua. Kumbe licha ya kuwa sherehe ya kuadhimisha kiri ya imani yetu juu ya Mungu mmoja katika nafsi tatu, ni sherehe inayotualika kuielekeza akili, mioyo na utashi wetu kumuelekea Mungu ambaye hujifunua kwetu kila siku ya maisha yetu. Huu ni wito wa kuishi maisha yetu kwa mfano wa upendo wa Utatu – umoja katika utofauti, mshikamano katika hali ya kipekee, na utoaji wa nafsi kwa ajili ya mwingine. Naye Roho Mtakatifu ni upendo wao, upendo usioelezeka, upendo wa ajabu na wa kina hivi kwamba nao ni Nafsi kamili... kwa uweza wake huyo Roho Mtakatifu, Baba ameumba vyote kwa njia ya Neno wa milele aliye Hekima ya Mungu ya tangu milele kadiri ya somo I (Mit 8:22-31), Kristo Bwana wetu. Kwa hakika Mungu wetu aliye mmoja, mkuu, muweza, mtakatifu na wa milele ni BABA… Yesu Kristo amemtaja kama Baba katika Injili ya leo (Yn 16:12-15.)

Baba ni Muumbaji, Mwana ni Mkombozi na Roho Mtakatifu ni Mfariji
Baba ni Muumbaji, Mwana ni Mkombozi na Roho Mtakatifu ni Mfariji   (@VATICAN MEDIA)

Na nukuu nyingi za Biblia, ni Muumba, Bwana wa historia na nyakati… Mungu wetu ni MWANA, akiambatana nasi safarini katika Nafsi ya Yesu Kristo, yupo kati yetu kama “Mfufuka”, Mshindi wa dhambi na mauti, Immanuel, Mfalme… na halafu tunapata kumfahamu Mungu na kuyajua mapenzi yake kwa njia ya Mungu aliye ROHO akijidhihirisha kama nguvu ya uhai na uumbaji mpya… asante sana “ufunuo” Mtakatifu uliowezesha kumjua na kumuelezea Mungu walau kwa kiasi hiki kidogo… Mtakatifu Anselmo katika “monolojia“  yake anasema hakuna maneno yanayostahili kueleza fumbo hili lililo kiini cha imani ya Kikristo kwa vile linagusa asili ya Mungu mwenyewe na hakuna aliyemuona Mungu wakati wowote isipokuwa Mwana pekee (Yn 1:18), maneno kama “nafsi, dutu, umoja, utatu nk…” yapo kibinadamu zaidi na hufafanua kwa uzuri vitu visivyo Mungu… tunasadiki Mungu mmoja aliye Baba, Mwana na Roho Mt na mengine yahusuyo asili yake yanabaki kuwa fumbo lisilofahamika wala kusogeleka, basi tubakie katika kusali na kutimiza mapenzi yake hadi nyakati zitakapotimia nasi kufunuliwa na kumuona kama alivyo (1Kor 13:12, 1Yoh 3:2).

Fumbo la Utatu Mtakatifu: Umoja na Ushirika
Fumbo la Utatu Mtakatifu: Umoja na Ushirika   (@Vatican Media)

UFAFANUZI: Katika Injili, Yesu anawaambia wanafunzi wake kwamba Roho atakuja kuwaongoza katika ukweli wote. Hii ni alama ya Utatu unavyofanya kazi pamoja: Baba hutuma Mwana, naye Mwana anamtuma Roho – wote wakitenda kazi kwa upendo na umoja kamili. Kutoka kina na marefu na mapana ya upendo wake, tumejaliwa kuwa washiriki wa fumbo la Utatu Mt kwa njia ya maisha na utume wa Mama Kanisa hasa kupitia adhimisho la Sakramenti Kuu ya Altare, sakramenti nyinginezo na huduma nyinginezo. Ekaristi Tak ni ufunuo dhahiri wa Mungu katika Utatu wake mtukufu, Mungu Baba anavitakatifuza vipaji vya mkate na divai katika Roho Mt ili viwe ‘mwili na damu’ ya Bwana wetu Yesu Kristo, tunaposhiriki vema fumbo la Altare tunafanyika washiriki wa mafumbo matakatifu kwa wokovu wa wote, nzuri sana! Katika muktadha wa Jubilei ya Matumaini 2025, ni mwaliko wa kuwa watu wa matumaini katika dunia yenye migawanyiko, hofu, na uchungu. Katika muktadha huu: Baba – ni chanzo cha uhai na matumaini Mwana – ni mwanga wa upendo ulio hai kwa wanadamu Roho Mtakatifu – ni nguvu ya upyaisho na mshikamano, Kupitia Utatu, tunaalikwa kuwa watu wa umoja, mshikamano, na upya wa maisha, tukileta tumaini kwa dunia inayovunjika.

Fumbo la Utatu Mtakatifu Chimbuko la Mafundisho ya Kanisa
Fumbo la Utatu Mtakatifu Chimbuko la Mafundisho ya Kanisa   (@Vatican Media)

Tunapomtafakari Mwenyezi Mungu katika Utatu Mtakatifu, mosi tujifunze kubaki tumeungana katika umoja wa imani vile somo II (Rum 5:1-5) linavyotufundisha leo, imani kwa Mungu Baba aliyetufanya wenye haki kwa njia ya Mwanaye Yesu Kristo katika pendo la Mungu lililomiminwa mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu tuliyempewa sisi. Halafu tujifunze utendaji wa pamoja. Tazama Mungu Baba anapanga, Mungu Mwana anatenda alichopanga na kuamua Baba huku Roho Mtakatifu akiwezesha na kukifunua alichokipanga Baba na kutendwa na Mwana… Baba alituchagua, Mwana akatukomboa naye Roho akatutia muhuri (Efe 1:2-13)... ikiwa nafsi za Mungu zinatenda kwa umoja hivi, zikiambatana hatua kwa hatua katika historia nzima tangu uumbaji, umwilisho, ubatizo wa Kristo, kung’ara sura kileleni Tabor, ufufuko wa Bwana, Ekaristi Tak, agizo la Mitume kuhubiri na kubatiza kwa Jina la Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu maadhimisho ya Kanisa. Sisi tunaoamini yatupasa kuakisi neno hili kubwa, tunaporuhusu migogoro, migawanyiko, ugomvi na malumbano labda katika familia, mahali pa kazi, katika jumuiya na popote tunapokuwapo hatumdhihirishi Mungu tunayemkiri, tutafute njia nzuri za kuondoa migawanyiko na wakati huohuo kukubaliana, kuheshimiana na kupokeana katika tofauti tulizonazo.

Utatu Mtakatifu ni Fumbo la Mungu mwenyewe
Utatu Mtakatifu ni Fumbo la Mungu mwenyewe   (@Vatican Media)

Tatu, kutoka mahusiano ya “Nafsi za Mwenyezi Mungu” basi ubinafsi usitajwe kwetu, tena tusitende lolote kwa nia ya kujinufaisha binafsi bali yote tufanyayo yalenge manufaa ya taifa la Mungu, tusimnyanyapae yeyote, tusimuweke jirani miguuni tukimtazama kutoka juu bali tushuke katika usawa wa kimo bila kujali hali yake, huyo ni ndugu, kaka na dada yako katika Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Nne, upendo wa Baba na Mwana ndiye Roho Mtakatifu huo unatufunika na kutuunganisha sote… tujifunze kupenda kwa moyo, kwa maneno machache na utendaji mwingi, upendo uhusishe pia kuona na kushukuru mazuri ya wenzetu. Mkazo wa Kitume wa Papa Leo XIV, Papa Leo XIV katika ujumbe wake wa Kitume kwa Jubilei amesisitiza kuwa: “Utatu Mtakatifu si fumbo la mbali bali ni maisha tunayoitwa kuyaiga: kuwa watu wa huruma, wa matumaini, na wa ushirika wa kweli.” Ametilia mkazo umuhimu wa Kanisa kuwa shirika la utatu, yaani, Kama Baba – likilea na kulinda, Kama Mwana – likitoa huduma ya upendo na msamaha Kama Roho – likijenga umoja na kuwasha upya ari ya imani Basi na tujinyenyekeshe na kumuabudu vema Mungu katika Utatu Mtakatifu tusali “Kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mt” na kumtukuza kwa “Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu kama mwanzo na sasa na siku zote na milele, amina” uwepo wetu mbele yale umtukuze kwa sifa ipasayo.

Fumbo la Utatu Mtakatifu ni chemchemi ya matumaini ya waamini.
Fumbo la Utatu Mtakatifu ni chemchemi ya matumaini ya waamini.   (@Vatican Media)

 

Askofu mwenye midomo ya dhahabu Mtakatifu Yohane Krisostom anasema: “Ukiwa mbele ya madhabahu Kristo alipo hupaswi kufikiri kuwa u katikati ya watu wanaokuzunguka ila uamini kwa dhati kabisa kwamba makundi ya malaika na malaika wakuu wamesimama kando yako muda huo wakitetemeka kwa heshima kuu mbele ya Bwana wa mbingu na ulimwengu, kwa hiyo uwapo Kanisani ukae kwa kutulia, keti katika ukimya, uchaji na ibada” Utatu Mtakatifu hutufundisha kuwa ukamilifu wa maisha ya Kikristo unapatikana kwa kuishi upendo unaotoka kwa Mungu, unaoshirikishwa katika Mwana, na unaowaka kwa njia ya Roho Mtakatifu. Katika mwaka wa Jubilei: Tuwe watu wa Utatu – tuliojaa matumaini, tulio tayari kuishi kwa ajili ya wengine, na tuliounganika katika Roho mmoja. “Ee Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, tufundishe kuishi kwa upendo wako. Tuunganishe kama familia yako, tuongoze katika ukweli, na tujalie tumaini jipya kwa kila mtu tunayekutana naye.  Mtume Paulo anasema. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, na upendo wa Mungu Baba na ushirika wa Roho Mt viwe nanyi nyote. Amina.

Liturujia Utatu Mtakatifu

 

14 Juni 2025, 09:06