Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Ishara Upendo na Ukarimu wa Kimungu
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Sherehe ya Mwili na Damu Takatifu sana ya Bwana wetu Yesu Kristo, Sherehe ijulikanayo kama “Sollemnitas Sanctissimi Corporis et Sanguinis Christi.“ Liturujia ya Neno la Mungu katika Sherehe hii inatutafakarisha kuwa, “Ekaristi Takatifu ni Ishara ya Upendo na Ukarimu wa Kimungu.” Sherehe hii huadhimishwa Alhamisi baada ya Sherehe ya utatu Mtakatifu, lakini kwa sababu za kichungaji, katika majimbo mbalimbali huadhimishwa Dominika baada ya Sherehe ya Utatu Mtakatifu. Mama Kanisa ameamua hivyo ili kuwapa Watoto wake nafasi ya kufurahia, kumsifu, kumwabudu na kumpa Mungu heshima ya pekee katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, kwa maandamano yanayofanyika baada ya Misa Takatifu ili kuliishi, kulitafakari, kulishuhudia na kuonesha umuhimu na uhitaji wa Fumbo hili Takatifu katika Maisha yetu ya kiroho. Waamini waoneshe moyo wa upendo kwa kushikamana na Kristo Yesu katika safari ya maisha yao, kwa kujiandaa kikamilifu, ili kuweza kumpokea Kristo Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai! Ekaristi Takatifu inawakirimia waamini chakula cha uzima wa milele na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, ili hatimaye, kuweza kushiriki katika maisha, uzima na utukufu wa Baba wa milele! Ekaristi Takatifu inajenga Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Mwili na Damu yake Azizi inayotolewa kwa ajili ya kurutubisha maisha ya walimwengu. Kwa kumpokea Yesu kwa imani, mwamini anakuwa sawa na Yesu na hivyo kufanyika kuwa mwana katika Mwana.
Kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Kristo Yesu anaandamana na wafuasi wake kama ilivyokuwa kwa wale Wafuasi wa Emau! Anasafiri na waja wake katika historia ili kuwakirimia imani, matumaini na mapendo; kwa kuwafariji wakati wa majaribu na magumu ya maisha; na hatimaye, kuwaunga mkono katika mchakato wa mapambano ya kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; ni chemchemi ya utakatifu wa maisha ya waamini, kumbe, linapaswa lisadikiwe kwa dhati, liadhimishwe kwa ibada na uchaji na limwilishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Katika Sherehe hii ya Ekaristi Takatifu, tunamshukuru Mungu ambaye kwa mapendo makubwa alimtoa kwetu mwanaye wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo, akatwaa mwili na kukaa kati yetu, akashiriki ubinadamu wetu ili atushirikishe Umungu wake, na bado amebaki nasi kwa daima katika maumbo ya mkate na divai. Tuombe neema ya kudumu katika ushirika na Kristo, kwa kumpokea daima kwa imani na katika hali ya neema katika Ekaristi Takatifu ili tuweze kunufaika na matunda yatokanayo na kule kupokea kwetu Fumbo hili Takatifu.
Chimbuko la Sherehe ya Mwili na Damu Takatifu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Sherehe ya Mwili na Damu Azizi ya Bwana wetu Yesu Kristo ilianzishwa rasmi katika Kanisa kutokana na uwepo na kusambaa kwa ibada mbalimbali kwa heshima ya Ekaristi Takatifu, uwepo halisi wa Mungu katika maumbo ya mkate na divai mapema katika karne ya 13AD. Kwa kusaidiwa na wanateolojia mbalimbali na viongozi wa Kanisa kwa wakati huo, Sherehe hii iliadhimishwa kwa mara ya kwanza kabisa mwaka 1246 katika Jimbo la Liége huko Ubelgiji ikijulikana kama “Corpus Christi”, yaani Sherehe ya Mwili wa Kristo. Mwaka 1264 Baba Mtakatifu Urbano IV aliidhinisha Sherehe hii iadhimishwe katika Kanisa kote ulimwenguni. Alimwomba Mtakatifu Thoma wa Aquino kuandika nyimbo na machapisho mbalimbali ya kiliturjia kwa ajili ya sherehe hii kama vile “Pange Lingua, Tantum Ergo na Adore te.” Mwaka 1263, uliotokea muujiza wa Ekaristi Takatifu huko Bolsena Italia ambapo Hostia Takatifu ilivuja damu wakati wa Ibada ya Misa Takatifu wakati ambapo Padre aliyeadhimisha alikua na mashaka juu ya uwepo halisi wa Kristo katika maumbo ya mkate na divai. Muujiza huu ulipeleka kukua na kusambaa kwa haraka kwa ibada kwa Ekaristi Takatifu, na kwa namna ya pekee Sherehe hii ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Baadaye Mababa wa Mtaguso wa Trento (1545-1563) walifundisha kuwa, “Tunapaswa kumpa heshima Bwana wetu Yesu katika Ekaristi Takatifu hadharani ili wale wanaotazama Imani ya Wakristo Wakatoliki waweze kuvutwa na Yesu Ekaristi Takatifu, na kuweza kuamini katika Umungu wa Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai na mzima katika Fumbo Takatifu sana la Ekaristi Takatifu” Hii ilitokana na kuwepo kwa mafundisho mbalimbali ya uzushi juu ya Ekaristi Takatifu juu ya uwepo halisi wa Kristo (Real Präsenz) katika maumbo ya Mkate na divai, kuabudu Ekaristi Takatifu nje ya Ibada ya Misa Takatifu na maandamano ya Ekaristi Takatifu. Katika majiundo ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican: 1962-1965, Sherehe hii iliunganishwa na Sherehe ya Damu Azizi ya Yesu ambayo huadhimishwa tarehe 1 Julai, ili kusisitiza taalimungu ya Ekaristi Takatifu, yaani Mwili na Damu Azizi ya Bwana wetu Yesu Kristo. Na hivyo jina lilibadilika kutoka Corpus Christi yaani Sherehe ya Mwili wa Kristo na kuitwa “Sollemnitas Sanctissimi Corporis et Sanguinis Christi”, yaani Sherehe ya Mwili na Damu Azizi ya Bwana wetu Yesu Kristo na ndivyo inavyojulikana hata sasa.
Msingi katika Maandiko Matakatifu. Imani yetu katika uwepo halisi na kweli wa Kristo katika maumbo ya mkate na divai upo katika maandiko Matakatifu ambapo ni Kristo mwenyewe alitoka mwili wake kama Chakula na Damu yake kama kinywaji kwa ajili yetu na akawapa Mitume wake mamlaka ya kuadhimisha Fumbo hilo Takatifu kwa ukumbusho wake mpaka atakaporudi tena (Mt 26:26-29; Mk 14:22-25; Lk 22:14-20; 1 Kor 11:23-26 na Injili ya Yohane sura ya 6). Ndilo Adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu tunaloadhimisha kila siku, ukumbusho wa sadaka ya Kristo pale msalabani. Nini kinatokea katika mageuzo wakati wa ibada ya misa Takatifu? Katika ibada ya Misa Takatifu, mkate hugeuzwa kuwa mwili wa Kristo na Divai kuwa Damu ya Kristo, mabadiliko yajulikanayo kama “Transubstantiation.” Ndugu wapendwa, mababa wa Mtaguso wa Trento wanasema hivi, “Kwa sababu Kristo Mkombozi wetu ndiye alisema mwenyewe kwamba huu ndio mwili wangu, akautoa mwenyewe kwa namna ya mkate na damu kwa namna ya divai. Hivyo kwa kutakatifuza mkate na divai hutokea mabadiliko ya kiini chote cha mkate kuwa katika kiini cha mwili wa Kristo Bwana wetu na kiini chote cha divai kuwa katika kiini cha damu yake.” Uwepo huu halisi na kweli katika maumbo haya ya mkate na divai huanza katika mageuzo na hudumu muda wote maumbo haya yanapokuwapo. Hivyo, Kristo yupo mzima na mkamilifu katika kila mojawapo ya maumbo ya mkate na divai na ni mzima na mkamilifu katika kila sehemu yao. Kwa jinsi hii, kuimega Ekaristi Takatifu hakumgawanyi Kristo hata kidogo. Uwepo wa Yesu unabaki kwenye kila kipande kidogo kilichovunjika hata katika kila tone la damu yake, uwepo wa Yesu umo kamili kabisa kama katika Ekaristi Takatifu nzima (KKK 1376-1377).
Somo la 1. Ni kitabu cha Mwanzo 14:18-20. Katika somo la kwanza tumesikia habari juu ya Melkizedeki kuhani mkuu na Ibrahimu. Huenda tukawa tunajiuliza maswali mengi kuwa huyu Melkizedeki ni nani hasa na kwa nini anatajwa katika Maandiko Matakatifu? Katika maandiko Matakatifu, Melkizedeki anatajwa kuwa alikua ni Mfalme wa Salemu (shalom/peace) na kuhani mkuu wa Mungu aliye juu sana (El Elyon). Anatajwa katika waraka kwa Waebrania sura ya 7:1-3 kuwa asiye na Baba wala Mama, hana wazazi, hana Mwanzo wala mwisho wa uhai wake, bali amefananishwa na Mwana wa Mungu, huyo adumu kuhani milele. Maana ya jina Melkizedeki ni “Mfalme wa Amani, Mfalme wa haki” Somo hili latueleza jinsi Melkizedeki Mfalme huyu wa Salemu alivyomkaribisha Ibrahimu ambaye alikua ametoka kupigana vita na wafalme ambao walimteka ndugu yake Lutu. Melkizedeki alileta mkate na divai na kumbariki Ibrahimu. Melkizedeki Mfalme wa haki, Mfalme wa Amani, na sadaka anayotoa ya Mkate na divai vyazungumza juu ya Kuhani Mkuu Bwana wetu Yesu Kristo katika Agano jipya. Kristo ni Mfalme wa amani, ni Mfalme wa haki, aliyejitoa yeye mwenyewe kama sadaka kwa Baba wa milele kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu, kwa ajili ya kutufanya wenye haki mbele za Mungu na kutuletea amani. Katika Ekaristi Takatifu, nasi tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya ukombozi tulioupata kwa sadaka ya mwili na Damu ya Kristo Msalabani. Yeye ni Kuhani, ni sadaka na Altare na hivyo ni mkuu kuliko wafalme na makuhani wa Agano la kale. Anasimama kama kuhani mkuu anayetufaa kati yetu sisi Mungu.
Somo la Pili: Ni kutoka katika Waraka wa Kwanza wa Mtume Paulo 1 Kor 11:23-26. Mtume Paulo katika sura hii ya kumi na moja kuanzia aya ya 17-33 azungumzia juu ya Adhimisho la Karamu ya Bwana, akionya hasa ushiriki usiostahili katika karamu ya hii Takatifu na Matumizi mabaya ya karamu ya Bwana. Kimsingi Ekaristi Takatifu ilikua ni Adhimisho la mlo, karamu ya pamoja ambapo aliyekuwa mkuu wa nyumba aliandaa karamu na kuwaalika watu kushiriki pamoja kama Kristo Yesu alivyoamuru ifanywe kwa ukumbusho wake. Mtume Paulo anasikia habari kuwa wapo waliowatenga maskini katika karamu ya Bwana na kuandaa kwanza karamu kwa ajili yao, watu waliokuwa matajiri na wenye hadhi katika jamii ya wakorintho, wakala, wakanywa na kushiba. Wakabadili maana ya Ekaristi kama karamu ya Bwana, kama ushirika, kama ukumbusho wa mateso na kifo cha Kristo, na kuiadhimisha vile isivyostahili na wakafanya kama Adhimisho la kula na kunywa na kusaza. Mtume Paulo katika somo hili anaanza kwa kueleza kiini na maana ya Ekaristi Takatifu, kama alivyopokea fundisho hilo kutoka kwa Kristo mwenyewe, fundisho ambalo Injili zote tatu zalielezea kwa kina. Sadaka hii ni ukumbusho wa mateso na kifo cha Kristo. Kisha atasisitiza katika aya zifuatazo juu ya kushirikia vile inavyostahili karamu ya Bwana ili kupata neema zitokanazo na kule kushiriki kwetu Ekaristi Takatifu.
Somo la Injili: Ni Injili kama ilivyoandikwa na Luka 9:11-17. Katika somo la Injili Takatifu, tunasikia mwujiza wa Kristo kuongeza mikate mitano na Samaki wawili na kuwalisha watu 5,000. Kristo aliwakaribisha watu, akawafundisha kwa Neno lake habari za ufalme wa Mungu, na kuwaponya wale wenye haja ya kuponywa. Kristo anahusika na mahitaji ya kiroho na kimwili ya kondoo wake. Akiisha kuwalisha kwa Neno, Mitume wanamwomba awaage makutano, hawaamini kama Kristo aweza kufanya jambo kubwa kuliko vile walivyoweza kuwaza kwa akili na uelewa wao. Lakini Kristo anawaambia, “wapeni ninyi chakula” Anataka Mitume washirikishe watu hata kwa kile kidogo walichokuwa nacho. Kristo anawaamuru kuwaketisha watu na anafanya muujiza wa kuzidisha mikate na Samaki na watu wanakula na kushiba. Muujiza huu unafanyika nyikani, waturudisha nyuma katika Agano la Kale namna Mungu kwa ukarimu alivyowalisha watu wake kwa mkate utokao mbinguni, katika safari yao jangwani kuelekea katika nchi ya ahadi. Kristo Yesu, anatulisha sisi kwa mwili wake na damu yake, tuwapo jangwani kuelekea katika nchi yetu ya Ahadi Mbinguni. Wakiisha kula wanakusanya mabaki vikapu kumi na viwili, idadi ya makabila kumi na mawili ya Israeli. Kumbe wakiisha kula na kushibishwa na Kristo, kila mtume wa Kristo anapewa kikapu chake, yaani wito wa kwenda kumpeleka Kristo kwa watu wote, kwa makabila yote. Ndio utume wa Kanisa na utume wetu sote tunaopokea Neno la Kristo na kushibishwa kwa Ekaristi Takatifu.
Tunapoadhimisha Sherehe ya Mwili na Damu Azizi ya Bwana wetu Yesu Kristo tuna mambo yafuatayo ya kujifunza: Kwanza: Uwepo halisi wa Kristo katika Ekaristi Takatifu (Real Presence of the Lord in the Eucharist). Ekaristi Takatifu sio tu alama, ni uwepo halisi na kweli wa Yesu katika maumbo ya Mkate na divai, Kristo mwenywe aliposema, Huu ndio mwili wangu…hii ndiyo Damu yangu (Lk 22:19-20). Kanisa latufundisha kuwa, kwa kutakatifuza mkate na divai hutokea mabadiliko ya kiini chote cha mkate kuwa katika kiini cha mwili wa Kristo Bwana wetu na kiini chote cha divai kuwa katika kiini cha damu yake”. Uwepo huu halisi na kweli katika maumbo haya ya mkate na divai huanza katika mageuzo na hudumu muda wote maumbo haya yanapokuwapo. Ndugu mpendwa, kila mara tunaposhiriki Ekaristi Takatifu tufahamu ya kuwa tunakutana na Kristo mwenyewe. Ni Kristo ambaye anatuonea huruma, anayetupokea kama tulivyosikia katika somo la Injili Takatifu, Kristo anayeguswa na matatizo yetu, anayeguswa na mahitaji yetu. Anatulisha kwa Neno lake na kwa Ekaristi Takatifu kila mara tunapokutana naye, anatuponya na kutupa nguvu rohoni ya kusonga mbele katika safari yetu ya maisha kuelekea kwake. Kristo Mfalme wa amani yupo kila siku kati yetu, tumkabidhi familia zetu aziongoze ili ziwe vitalu vya amani, haki na upendo, tumkabidhi taifa letu ili liwe kisiwa cha amani, haki na upendo wa kweli, tumkabidhi kazi zetu zote ili aziongoze. Tumkabidhi Kristo hali zetu, kukata tamaa kwetu kwa sababu mbalimbali, mashaka na hofu zetu, furaha na huzuni zetu ili ayatawale kabisa maisha yetu. Lakini pia tunapokutana na Kristo kila siku tumshukuru kwa kutupenda upeo, tumwabudu, tumsifu na kumtukuza mwokozi wetu ambaye ameamua kubaki nasi katika Maumbo ya mkate na divai. Yupo nasi kila siku katika sakramenti Takatifu ya Altare. Pili: Ekaristi Takatifu ni ukumbusho wa sadaka ya Kristo (Anamnesis). Adhimisho la Ekaristi Takatifu sio sadaka mpya, bali ni adhimisho lile lile la sadaka ya Kristo aliyejitoa kwa mapendo makuu pale msalabani Mwili wake na Damu yake kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Kile alichoadhimisha Kristo katika karamu ya mwisho siku ya alhamisi kuu na na kuhitimishwa pale msalabani siku ya ijumaa kuu, kinarudiwa tena sasa na wakati huu katika kila adhimisho la Ibada ya misa Takatifu, ikiwa na matazamio ya karamu ya mbinguni. Mtume Paulo anatufundish katika somo la pili kuwa kila tulapo mkate na kukinywea kikombe tunatangaza mauti ya Bwana hata ajapo.
Ndugu wapendwa, kila mara tunaposhiriki Adhimisho la Ekaristi Takatifu tunakumbuka juu ya mapendo yasiyo na mipaka ya Mungu kwetu hata akamtoa mwanaye wa pekee kwa ajili yetu. Ni Kristo ambaye katika kila adhimisho la Misa Takatifu anajitoa kwa Baba wa milele. Tunaposhiriki Ekarsiti Takatifu tukumbuke wajibu wetu wa kujitoa sadaka kwa ajili ya utumishi wa upendo (diakonia) kwa wengine. Tujiulize kila mmoja, kushiriki kwangu Ekaristi Takatifu kumeathiri vipi mapendo yangu kwa Mungu na kwa wengine? Nimekua na mapendo ya kweli na ya dhati kwa familia yangu, kwa nyajibu zangu mbalimbali, kwa majirani zangu, kwa mwenzangu wa ndoa, kwa mtawa mwenzangu, kwa wafanyakazi wenzangu nk? Nimetenga muda wangu kukaa na Yesu kumshukuru kwa mapendo hayo makuu na baraka zake nyingi katika maisha yangu? Yesu anatupenda na anatupa nafasi ya kuendelea kuonesha na kudhihirisha mapendo yetu kwake. Anatutazama kwa jicho la upendo. Tatu: Ekaristi Takatifu ni Ushirika (Koinonia/Communion). Kristo anatuambia, “Aulaye mwili wangu na kuinywa Damu yangu hukaa ndani yangu nami hukaa ndani yake (Yn 6:56). Sherehe hii ya Mwili na Damu Azizi ya Bwana wetu Yesu Kristo yatukumbusha kuwa tunapopokea Ekaristi Takatifu tunaingia katika ushirika na Kristo, anakaa ndani mwetu nasi tunakaa ndani mwake. Ndugu mpendwa, Ekaristi Takatifu yatupa nafasi ya kuingia katika ushirika na Mungu. Katika ibada ya misa Takatifu, Padre anapochanganya maji na divai wakati akiandaa vipaji, anasali na kusema, “Kwa fumbo la maji haya na divai hii tujaliwe kushiriki Umungu wa Kristo, yeye aliyekubali kushiriki ubinadamu wetu” Kumbe Mungu aliye mtakatifu amekubali kuingia katika historia yetu ya dhambi ili aigeuze kuwa historia ya wokovu wa milele. Tunapoingia katika ushirika na Mungu tunaalikwa kuingia katika ushirika kati yetu sisi kwa sisi. Tunaalikwa kupokeana katika mazuri na madhaifu yetu, tunaalikwa kuchukuliana kwa upendo na upole, tunaalikwa kusameheana pale tunapokosana bila masharti. Kila mara tunapoharibu ushirika huu mtakatifu kwa sababu ya dhambi tunaalikwa kuendea sakaramenti ya Kitubio ili daima tuwe wamoja na Kristo na matunda ya uwepo wake ndani mwetu yaonekane katika kusema na kutenda kwetu.
Nne: Ekaristi ni Sadaka ya Shukrani (Eucharistein). Ekaristi maana yake ni shukrani kwa Mungu. Melkizedeki alimtolea Mungu mkate na divai, shukrani kwa matendo makuu na ushindi aliomtendea Ibrahimu. Katika ibada ya Misa Takatifu, nasi tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya ukombozi tuliyoipata kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Tunamshukuru Mungu kwa mapendo yake yasiyo na mipaka, tunamshukuru kwa ukarimu wa kimungu. Ndugu mpendwa, Sherehe hii ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo yatukumbusha kuwa watu wa Shukrani kwa Mungu, kwa neema na baraka, kwa afya njema, kwa nguvu za kufanya kazi, kwa zawadi ya watoto, kwa zawadi ya familia, kwa zawadi ya utulivu na amani ya moyo, kwa ustahimilivu hata katika nyakati ngumu ambapo Mungu alikushika mkono akakuinua. Mkate ni zao la ngano iliyosagwa na divai ni zao la mzabibu uliopondwa pondwa. Kumbe nasi tunaalikwa kujitoa maisha yetu, kukubali kujimega na kujitoa sadaka kwa wengine, kwa hali, kwa mali, kwa karama, kwa vipaji nk. Tuwe sehemu ya kuleta furaha na nafuu katika maisha ya watu wengine, tuwe baraka katika maisha ya wengine. Kuwa tayari kuumia kwa ajili ya familia yako, kwa ajili ya shirika lako, kwa ajili ya jumuiya yako, kwa ajili ya wananchi wako, kuwa tayari kuhisi maumivu, shida na vilio vya wengine kuwa sababu ya kuleta tena furaha, amani, tabasamu na utulivu kwa wengine.
Tano: Ekaristi Takatifu na Utume (Eucharist and Mission). Katika somo la Injili Takatifu, Kristo anawakaribisha watu, anawafundisha na kuwaponya, utume ambao atawatuma mitume wake kwenda kuufanya. Akiisha kuwafundisha anaamuru mitume akiwaambia, “wapeni ninyi chakula” ishara kuwa ni wajibu wao kuguswa kwa nafasi ya kwanza katika mahitaji ya watu na kujibu kilio chao. Kisha Kristo anafanya muujiza huu wa kuzidisha mikate mitano na samaki wawili. Watu walipokwisha kula na kusaza, mitume walikusanya vikapu kumi na viwili. Ni idadi ya makabila kumi na mawili ya Israeli. Kumbe kwa kukusanya vikapu kumi na viwili, ni kusema kuwa kila mtume alipewa kikapu chake ili kwenda kuwashibisha na wengine. Kuona, kuguswa na kutenda ni sehemu muhimu katika utume wetu. Sisi sote tukiisha kupokea Ekaristi Takatifu, tunatumwa kwenda kuiishi Ekaristi katika maisha yetu. Tunatumwa kuwa wajumbe wa upendo, sadaka, ukarimu, wema, upole, msamaha katika maisha yetu ya ila siku. Tunaalikwa kumtumainia Mungu na kufanyia kazi hata kile kidogo ambacho Mungu ametupatia kila mmoja wetu. Tusiache kufanya kitu kwa kulalamika kuwa, “ni kidogo sana na hakitoshi kitu” bali tuinue macho yetu mbinguni, tumshukuru Mungu na kumwomba avibariki, na avizidishe kwa wakati wake. Kama ni kipaji Mungu amekupa, mshukuru na kifanyie kazi, ni kazi Mungu amekupa, mshukuru na ifanyie kazi, ni afya njema Mungu amekupa, mshukuru na uifanyie kazi, ni amani ya moyo Mungu amekupa mshukuru na uifanyie kazi kuzidisha zaidi na zaidi kwa ajili yako na kwa ajili ya wengine. Kuwa balozi wa baraka za Mungu, zitumie kuwainua wengine na Mungu atakubariki zaidi na zaidi.
Sita: Kupokea Ekaristi Takatifu kwa Heshima na katika Mastahili. Mtume Paulo katika somo la pili, anatoa fundisho juu ya nini maana ya Ekaristi Takatifu baada ya jumuiya ya Wakristo wa Korintho kutumia vibaya adhimisho la Karamu ya Bwana. Mtume Paulo anatuonya nasi sote ya kuwa tunapopokea Ekaristi Takatifu pasipo mastahili tunajipatia hatia ya mwili na damu ya Kristo (1 Kor 11:27). Yesu aliye mtakatifu sana anatuhitaji nasi kujitakatifuza ili tuweze kustahili kuwa makao yake ndani mwetu. Sherehe hii ya Mwili na Damu Takatifu sana ya Bwana wetu Yesu Kristo itukumbushe wajibu wetu wa kujongea sakramenti ya kitubio kila mara kabla ya kupokea Ekaristi Takatifu ili tustahili kupokea neema na baraka zote zitokanazo na Adhimisho la Ekaristi Takatifu. Ili Kristo akae ndani mwetu tunapaswa kuandaa mazingira mazuri, kwa kujitakasa na kuweka mioyo yetu yalipo makazi ya Mungu katika hali ya utakatifu kabla ya kushiriki Ekaristi Takatifu. Siku hii itukumbushe wajibu wetu wa kupokea kwa heshima Ekaristi Takatifu. Yesu yupo mzima na hai katika kila kipande hata kidogo kabisa cha Hostia Takatifu. Tunakumbushwa kila tunapopokea Ekaristi takatifu kuhakikisha hakibaki hata kipande kidogo mkononi. Kwa kuwa tukiacha chembe hata hizo ndogo ndogo ziakaanguka ni sawa na kutupa Ekaristi nzima. Hivyo tuwe makini kila tupokeapo Ekaristi Takatifu. Saba: Kuabudu Ekaristi Takatifu. Sherehe hii ya mwili na damu Takatifu sana ya Bwana wetu Yesu Kristo yatukumbusha wajibu wetu wa kuabudu Ekaristi Takatifu, Yesu aliye nasi kwa daima katika Tabernaklo takatifu. Kila siku tupate nafasi ya kukaa mbele ya Yesu hata kwa dakika chache, tuzungumze na Yesu, tumshirikishe mambo yetu, tumshukuru, kumtukuza na kumwomba atufundishe, ayaongoze maisha yetu sisi tulio nyikani hapa duniani, tupo safarini jangwani kulekea katika nchi yetu ya ahadi. Tumwombe atushibishe roho zetu ili tuwe na nguvu na afya ya kuendelea mbele katika safari yetu ya maisha, sisi mahujaji wa matumaini. Hitimisho: Katika Sherehe hii ya Ekaristi Takatifu, tunamshukuru Mungu ambaye kwa mapendo makubwa alimtoa kwetu mwanaye wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo, akatwaa mwili na kukaa kati yetu, akashiriki ubinadamu wetu ili atushirikishe Umungu wake, na bado amebaki nasi kwa daima katika maumbo ya mkate na divai. Tuombe neema ya kudumu katika ushirika na Kristo, kwa kumpokea daima kwa imani na katika hali ya neema katika Ekaristi Takatifu ili tuweze kunufaika na matunda yatokanayo na kule kupokea kwetu Fumbo hili Takatifu.