Rais TEC:Afya ya Katibu Mkuu TEC,Padre Charles Kitima yaimarika,ameanza utume!
Na Sarah Pelaji – Vatican.
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC), Askofu Wolfgang Pisa OFM Cap, ametoa habari njema kwa waamini wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania na wote wenye mapenzi mema kuwa afya ya Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC), Padre Charles Kitima imeimarika na sasa ameanza kazi rasmi za kiofisi kama Katibu Mkuu. Akizungumza na Radio Vatican , tarehe 3 Juni 2025, wakati Mama Kanisa anawakumbuka Mtakatifu Karoli Lwanga na wenzake Mashahidi, Askofu Pisa amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumlinda na kumjalia afya njema tangu aliposhambuliwa na watu wasiojulikana, usiku wa tarehe 30 Aprili 2025 akiwa kwenye makazi yake yaliyopo Ofisi za Baraza la Maaskofu(TEC), Kurasini, Dar Es salaam nchini Tanzania. Baada ya tukio hilo baya, Padri Kitima amekuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Aghacan iliyoko jijini Dar es Salaam kwa takribani mwezi mmoja hivi.
“Tumshukuru Mungu kwa upendo aliouonesha katika kipindi hiki kigumu. Namshukuru pia Padri Kitima kwa ujasiri wake wa kumtumikia Mungu. Amekuwa na ujasiri na uzalendo wa kufanya kazi hata katika hali ngumu,” alisema Rais wa TEC.
Mashahidi wa Uganda
“Leo Kanisa linaadhimisha siku kuu ya Mashahidi wa Uganda ambapo kati yao 22 walikuwa ni wakatoliki na 23 walikuwa ni waanglikani. Baada ya mateso yale yote ya mashahidi wa Uganda, vijana wengi waliokuwa wapagani walimuongokea Mungu wakaomba kubatizwa. Hilo liliamsha ari na moyo wa utume katika Kanisa.” Alisisitiza Askofu wa Lindi. “Hivyo baada ya shambulizi lile nampa moyo Padri Kitima kuendelea kuimarika kiroho, utume wake kama Padre na kiongozi katika Kanisa na jamii, asitetereke kamwe kumshuhudia Kristo katika nyakati zetu ngumu tunazopitia,” amlisema Askofu Pisa.
Wito kwa waamini wa Kanisa Katoliki Tanzania
Wito wake Askofu kwa waamini wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania ni kuendelea kuishi wito wao wa ukristo wa kumuweka Mungu kwanza kabla ya kitu chochote. Pia kuwa wazalendo wa imani yao na kuwa na upendo kwa jirani. Amri Kuu inawafundisha waamini kumpenda Mungu kwa moyo wote na kumpenda jirani.
“Ninawaasa kila mmoja kumpenda jirani kama nafsi zao, kuwa mlinzi wa ndugu yako, ukiona jirani yako hayuko salama nawe pia si salama. Ubinafsi unaoingia katika taifa letu asiwepo mtu anayejiona kuwa hahusiki bali sote tunahusika. Tuwe wazalendo wa kuishi kwa amani, tulijenge Kanisa na taifa letu kwani ni vitu viwili ambavyo haviwezi kutengana. Tuimarishe umoja, amani, mashikamano na uwajibikaji,” amesema Askofu Pisa.
Padre Kitima ameadhimisha Misa ya kumshukuru Mungu
Tarehe 3 Juni 2025, Padre Kitima ameadhimisha ibada ya Misa Takatifu ya kumshukuru Mungu kwa ulinzi na kumrejeshea afya yake. Ni misa iliyofanyika katika Kanisa la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili lililopo TEC Kurasini jijini Dar es Salaam ikihudhuriwa na wafanyakazi wa sekretariet ya TEC wakiwemo mapadri, watawa na waamini walei. Katika Homilia Takatifu Padre Kitima amemshukuru Mungu kwa ulinzi, kumtunza na kumrejeshea afya yake baada ya shambulizi lililokusudiwa kukatisha maisha yake. Aidha amewashukuru watu wote wenye mapenzi mema waliomuombea, kumjulia hali na kumhudumia katika kipindi chote alipokuwa mgonjwa.
“Tumshukuru Mungu kwa wema wake, pia tunawashukuru watu wote walioguswa na tukio lile. Tuombe ili Kanisa lizidi kuwa imara siku zote bila kutetereka. Tukumbuke kuwa Kanisa Katoliki ni taasisi inayotegemewa na watu wengi, ni sauti ya wasio na sauti ni msindikizaji wa wanyonge. Tuliombee Kanisa letu lizidi kuwa mwanga na matumaini ya Watanzania.”
Kadhalika Padre Kitima aliwataka wanasekretarieti ya kuyapokea mambo yote yaliyotokea kwa jicho na moyo wa imani akisisitiza kuwa katika mambo yote ambayo Kanisa linayasimamia kwaajili ya wanyonge Mungu atayasikiliza. “Mungu hatakaa kimya atajibu sala zetu. Tuwe imara katika kazi zetu tukikumbuka kuwa hata mitume wa Yesu walipata misukosuko. Tusirudi nyuma tubaki katika imani thabiti,”alisema.