杏MAP导航

Tafuta

Yesu alisema "Mtu yeyote akitaka kunifuata ajitikwe Msalaba wake anifuate.Hivyo vijana wanapaswa kubeba misalaba ya maisha yao." Yesu alisema "Mtu yeyote akitaka kunifuata ajitikwe Msalaba wake anifuate.Hivyo vijana wanapaswa kubeba misalaba ya maisha yao." 

Padre Kamugisha,Katekesi kwa vijana:Hakuna mafanikio yasiyo na Msalaba!

Vijana lazima kuwa waangalifu kwani Imani mambo leo inaukataa Msalaba,inamkataa Kristo bila msalaba.Waamini wanataka Msalaba usio na Yesu.Wapo wengi katika Ulimwengu huu wana mateso lakini hawana Yesu.Wanamtaka Yesu asiye na mateso.Vijana ni mahujaji wa matumaini wasikate tamaa,kama Jubilei ya 2025 inavyosisitiza.Alisema hayo Padre Kamugisha wa Jimbo Katoliki la Bukoba Tanzania,wakati wa Kongamano la Kitaifa la TYCS lililofanyika Jimbo la Shinyanga,kuanzia 7 hadi 12 Juni 2025.

Na Sarah Pelaji – Vatican.

Padre Faustine Kamugisha wa Jimbo Katoliki la Bukoba – Tanzania, alishiriki Kongamano la Kitaifa la Vijana Wanafunzi Wakatoliki wa Shule za Sekondari Tanzania(TYCS), lililofanyika katika Shule ya Don Bosco iliyopo huko Didia, Jimbo Katoliki la Shinyanga, kuanzia tarehe 7 mpaka 12  Juni 2025 ambapo zaidi ya vijana 1, 200 kutoka majimbo 33 ya Kanisa Katoliki nchini walishiriki. Kongamano hilo liliongozwa na kauli mbiu: "Ewe kijana  Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako,"  kutoka kifungu cha (Mhubiri 21:12,1.) Padre Kamugisha katika tafakari yake aliwasihi vijana kuzingatia masuala matatu ya kuishi imani Katoliki katika ulimwengu wa sasa.  Mosi ikiwa ni mafanikio kwamba  anayeamini katika  mafanikio ya kidunia (fedha magari mashamba) atapata lakini lazima  asali na kufanya kazi kwa bidii  kama ilivyo falsafa ya Wabenediktini ya Ora et labora yaani sala na kazi.” Alirejea Mafundisho ya Papa Leo XIII katika Waraka wake wa  Rerum Novarum uliochapishwa kunako tarehe 15 Mei 1891 unaojikita katika mafundisho ya Kanisa juu ya jamii na siasa. Padre Kamugisha alisema “Neno kazi na neno mafanikio linalotangulia ni kazi. Kumbe kazi inatangulia mafanikio hivyo Ili ufanikiwe lazima ufanye kazi. Asiyefanya kazi na asile(Rej. Thes 3:10), kwamba kazi na sala vyote vinaendana huku akihimiza zaidi kuwa kazi isizuiye sala na sala isizuiye kazi,” alisisitiza Padri Kamugisha.

Kongamano la TYCS 7-12 Juni 2025
Kongamano la TYCS 7-12 Juni 2025   (Tanzania Episcopal conference (TEC).)

Kijana shiriki majibu ya sala

Pili Padre Kamugisaha aliwasisitiza kushiriki majibu ya sala kwamba  “Imani pasipo matendo imekufa”(Mt. 7:7), “ombeni nanyi nanyi mtapewa, tafuteni mtapata, bisheni hodi mtafunguliwa,”  kwa hyo “Omba lakini tafuta, omba lakini fanya kitu.  Lazima kupoteza muda wa kutafuta ili upate kitu” akitumia msemo  kwamba asiyepoteza kitu haokoti. “Lazima kupoteza muda kusoma ili ufaulu mitihani, ukitupa mahindi kwenye shamba utapata mazao. Ni lazima upoteze muda katika kazi. Jambo la tatu ni vijana kukataa mafanikio bila mateso ambapo kwa lugha nyepesi ya Kanisa “ni hakuna Jumapili ya Pasaka bila Ijumaa Kuu (Lk 24;26).  Yesu alipata  mateso ili aingie katika Utukufu kama  vile  Papa  Francisko alivyofundisha kuwa  Pasaka bila Ijumaa Kuu si Injili. Kila umilele unapitia mateso na baada ya dhiki faraja,” Alisistiza.

Kongamano la TYCS 7-12 Juni 2025
Kongamano la TYCS 7-12 Juni 2025   (Tanzania Episcopal conference (TEC).)

“Hatuongelei miujiza bila kazi na hapa vijana lazima kuwa waangalifu kwani Imani mambo leo inaukataa Msalaba, inamtakaa Kristo bila msalaba. Waamini wanataka msalaba usio na Yesu. Wapo wengi katika ulimwengu huu wana mateso lakini hawana Yesu. Wanamtaka Yesu asiye na mateso, asiye na shida, ambaye hakuteswa.. Kristo mwenyewe alisema: “Mtu yeyote akitaka kunifuata ajitikwe Msalaba wake anifuate. Hivyo vijana wanapaswa kubeba misalaba ya maisha yao katika mazingira yao ili wafanikiwe. Ukiubeba vyema Msalaba utakubeba. Hatupaswi kuogopa Msalaba,” alisistiza

Vijana ni mahujaji wa matumiani wasikate tamaa

Padre Kamugisha pia aliwasilisha mada ya ‘Vijana Mahujaji wa Matumaini” huku akiwakumbusha kaulimbiu ya Jubilei Kuu isemayo: Jubilei kuu 2025 Mahujaji wa Matumaini.”  Kwamba vijana katika harakati za maisha yao wanakumbwa na changamoto mbalimbali za maisha yakiwemo masomo, ujana wao nk. Lakini sikuzote wakumbuke wapo hapa duniani kama mahujaji wa matumaini ambao hawapaswi kukata tamaa. Aliwafariji kwa msemoa wa ‘Mambo hayajaisha mpaka Mungu aseme yameisha. Maisha ni kama mechi ya mpira ambayo haijaisha mpaka Mungu aliye refarii apulize kipenga cha mwisho.” Alirejea ujumbe wa Papa  Fransisko alipokuwa akitangaza Jubilei Kuu 2025 aliyetaka  tuwaige Simeoni na Anna  Mahujaji wa matumaini waliojua kuupokea ujio wa Mungu kwa furaha na kuamsha matumaini mioyoni mwao.

Kongamano la TYCS 7-12 Juni 2025
Kongamano la TYCS 7-12 Juni 2025   (Tanzania Episcopal conference (TEC).)

Padre huyo kwa vijana alisisitiza kuwa Mahujaji wa matumaini ni wajenzi wa amani. kwa kuendelea alisema “Katika  ujumbe wake wa siku ya miito duniani, Papa Fransisko alisisitiza kuwa  “safari yetu ya maisha siyo ya kutangatanga tu bali ni hija yenye lengo  linalochochewa na matumaini na imani.” Akamnukuu alisema ‘Tuinuke kama mahujaji  wa matumaini kwa sababu sala hufungua mlango wa matumaini. Matumaini daima yapo lakini kwa sala yangu naufungua mlango wake.” Aidha, Papa Francisko alipokuwa anazungumza na vijana wasioona aliwatia moyo kuishi kama mahujaji wenye mwelekeo akisema kuwa, hija ni safari ya mtu mwenye lengo na kwa mwaka wa Jubilei ni mlango Mtakatifu unaotuwezesha kuingia kwenye Maisha mapya. Usisimame kamwe, usikome kamwe songa mbele.

Kongamano la TYCS 7-15 Juni 2025
Kongamano la TYCS 7-15 Juni 2025   (Tanzania Episcopal conference (TEC).)

Kijana hakuna kusimama songa mbele

“Katika safari ya Wana wa Israeli kuelekea Kaanani walianza kumlalamika Mungu baada ya kupata changamoto lakini Mungu akamwambia Musa waendelee mbele,   nami nakuambia kijana endelea mbele. Usipoweza kupaa kimbia, usipoweza kukimbia tembea, usipoweza kutembea tambaa ilimradi unakwenda mbele usisimame endelea mbele. Dawa ya uchovu ni kuanza safari kama  mhujaji wa matumaini,” alisisitiza. Papa Fransisko aliwasihi waamini ulimwenguni wasiwe watalii wa Maisha bali waishi kwa kusudi na uvumilivu. Matumaini hushinda uchovu wote, kama kuna lengo zuri basi kuna haja ya kuendelea kutembea kwa sababu zawadi ya mwisho ni ya ajabu isiyoelezeka. Tunaitafuta mbingu, hata katika Maisha yenye changamoto mbeleni, kwani itapendeza! Maisha yenye lengo yanasaidia sana (purpose drives life). Jubilei hii itubadilishe kuwa mahujaji wa matumaini. Lipo tumaini katika kila kitu.”

Kongamano la TYCS 7-12 Juni 2025
Kongamano la TYCS 7-12 Juni 2025   (Tanzania Episcopal conference (TEC).)

Padre Kamugusha alihitimisha kwa kuwatia moyo vijana kuacha kukata tamaa kwani lipo tumaini. “Mhujaji siyo mtu wa bahati nasibu bali mwenye lengo na matumaini.  Mungu ana lengo kubwa kwa kila aliyemuumba.” Alitumia Mwalimu wa Kanisa kwamba, “Mtakatifu Theresia wa Avila alisema tunaposhindwa mara nyingi ni kwasababu tulikata tamaa hatua moja kabla ya ushindi. Unapokata tamaa unakuwa umebakiza hatua moja umalize. Mwenye kuvumilia hata mwisho huyo ndiye atakayeokoka (rej. Mt 24:13) Mvumilivu hula mbivu.

Kongamano la TYCS 7-12 Juni 2025
Kongamano la TYCS 7-12 Juni 2025   (Tanzania Episcopal conference (TEC).)
Tafakari ya Padre Kamugisha kwa Kongamano la TYC
14 Juni 2025, 10:24