Nigeria:Padre Godfrey Oparaekwe,auawa akijaribu kusuluhisha mzozo wa Familia!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Padre wa Kikatoliki aliuawa nchini Nigeria alipokuwa akijaribu kusuluhisha mzozo wa kifamilia. Padre Godfrey Oparaekwe, Paroko wa Kanisa la Mtakatifu Ambrose huko Ubakala, Umuahia Kusini mwa LGA, katika Mkoa wa Abia (kusini mwa Nigeria), alifariki jioni ya tarehe 17 Juni 2025. Kulingana na kile kilichowasilishwa na Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari na na Jimbo la Umuahia, Padre huyo alikuwa amekwenda nyumbani kwa mwanamume huyo, akiwa na binti wa wanandoa hao na mwanamume mwingine ili kutafuta pikipiki ya msichana huyo. Wenzi hao walikuwa wamepatwa na matatizo kwa muda, hivi kwamba mke na watoto waliiacha nyumba hiyo na kumwacha mwanamume huyo peke yake.
Padre Oparaekwe alikuwa amejaribu kupatanisha lakini alikuwa ametishwa na mwanamume huyo. Jioni ya tarehe 17 Juni 2025 ghafla alimchoma Padre Oparaekwe kwa kisu, na kumjeruhi vibaya, kisha kutishia watu wengine kwa kifaa hicho hicho. Mshambulizi huyo alizirai huku Padre Oparaekwe akipelekwa hospitalini. Hata hivyo, saa chache baada ya kulazwa, Padre huyo alikufa.
Padre Godfrey alizaliwa tarehe 4 Oktoba 1953 huko Ulakwo, Owerri, Nigeria. Alipewa daraja la Upadre mwaka 1983 katika Seminari ya Mtakatifu Joseph huko Ulakwo, Oweni, Nigeria, Jimbo kuu la Umuahia. Mnamo 2000, alipata Shahada ya Uzamili ya Taalimungu kutoka Chuo Kikuu cha Wafransiskani cha Steubenville, Arizona. Kuanzia 2002 hadi 2012, alihudumu katika nyadhifa mbalimbali katika Jimbo la Tucson, Arizona (Marekani) kabla ya kurejea Nigeria.