杏MAP导航

Tafuta

Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA ilipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Maaskofu Katoliki Tanzania Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA ilipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Maaskofu Katoliki Tanzania 

Mpango Mkakati wa WAWATA Kwa Kanisa la Tanzania: 2023-2026

WAWATA ilipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Maaskofu Katoliki Tanzania, ili kusikiliza vipaumbele vya Kanisa Katoliki katika kipindi cha miaka kumi ijayo, ili viwasaidie WAWATA kuandaa Mpango Mkakati wa Miaka Kumi wa WAWATA. WAWATA imeainisha vipaumbele vyake, utekelezaji wa miradi mbalimbali pamoja na changamoto katika Ulimwengu mamboleo mintarafu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; umuhimu wa kuwekeza zaidi kwa Makatekista.

Na Mama Evaline Malisa Ntenga, Dar es Salaam, Tanzania.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., kuanzia tarehe 16-19 Juni 2025 limefanya kikao chake cha 109, kwenye Makao yake makuu, Kurasini, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA ilipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Maaskofu Katoliki Tanzania, ili kusikiliza vipaumbele vya Kanisa Katoliki nchini Tanzania katika kipindi cha miaka kumi ijayo, ili viwasaidie WAWATA kuandaa Mpango Mkakati wa Miaka Kumi wa WAWATA. WAWATA imeainisha vipaumbele vyake, utekelezaji wa miradi mbalimbali pamoja na changamoto katika Ulimwengu mamboleo mintarafu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; umuhimu wa kuwekeza zaidi kwa Makatekista pamoja na Kanisa kuendelea kutoa elimu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari. Maaskofu Katoliki Tanzania wamewapongeza WAWATA kwa mchango wao mkubwa wa hali na mali katika maisha na utume wa Makanisa mahalia na wamewaomba wasaidie pia kufufua vyama na mashirika mengine, ili yaweze kuchangia kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Maaskofu wametoa mwaliko kwa WAWATA kujisadaka kwa ajili ya kutoa elimu ya dini mashuleni.

Mama Evaline Ntenga Malisa Ntenga, Rais Wanawake kanda ya Afrika.
Mama Evaline Ntenga Malisa Ntenga, Rais Wanawake kanda ya Afrika.

Utangulizi: Kwa Upendo wa Kristo, Tutumikie na Kuwajibika! Tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai na zawadi ya utumishi katika kanisa kupitia uongozi wa WAWATA. Tunawashukuru wachungaji wetu kwa kutupatia nafasi ya kukutana nanyi. Kwa namna ya pekee, tunatoa shukrani kwa Kanisa kupitia Baraza la Maaskofu kwa kuturuhusu sisi wanawake wakatoliki kuishi wito wetu kama walei ndani ya Kanisa kwa uhuru na heshima. Tunatambua kuwa utume wa walei si fadhila, bali ni wajibu wa kiroho unaozaliwa kutoka kwenye ubatizo na kipaimara. Hili lilielezwa kwa kina katika Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, hasa katika hati ya “Lumen Gentium na Apostolicam Actuositatem,” kuwa waamini walei wanaitwa kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa kama washiriki hai wa Mwili wa Kristo. Tunawashukuru kwa kutufungulia milango ya kushiriki kikamilifu katika utume na maisha ya Kanisa mahalia na taifa. Lengo hasa la kukutana na ninyi wachungaji wetu ni kupata fursa ya kusikia kutoka kwenu, ni nini vipaumbele vya kanisa kwa miaka 10 ijayo ili vitusaidie kuandaa mpango mkakati wa miaka kumi wa WAWATA. Baadhi ya vipaumbele vya WAWATA kwa kipindi cha 2023-2026 ni kama vilivyoainishwa hapa chini. Pamoja na vipaumbele hivi, zipo changamoto ambazo tunapenda kuwashirikisha wachungaji wetu kwa kutambua WAWATA peke yetu hatuwezi kuzitatua. Vipaumbele vya WAWATA kwa Kipindi cha Miaka Mitatu (2023–2026).

Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA: Mpango kazi 2023-2026
Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA: Mpango kazi 2023-2026

Mpango mkakati wa WAWATA 2023–2026 umejengwa juu ya kauli mbiu ya Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani (World Union of Catholic Women Organisations - WUCWO) inayosema: "Wanawake Wakatoliki, Wajenzi Stadi wa Mafungamano ya Udugu wa Kibinadamu kwa Amani ya Ulimwengu." Vipaumbele ni pamoja na: Malezi ya Familia: Kwa kuzingatia waraka wa Papa Francisko Amoris Laetitia. Kauli mbiu ya Sikukuu ya Somo wetu Mama Bikira Maria Msaada wa Wakristo kwa mwaka huu ni Familia: Saidia, Ambatana na kutia moyo: Family: Support/Accompany/Encourage. Utunzaji wa Mazingira/Uumbaji: Kupitia elimu na matendo ya kitume, tunaendeleza kampeni ya ulinzi wa mazingira kwa misingi ya Laudato Si na kuwahusisha watoto, vijana na familia. Kwa sasa tunaendelea na Kampeni ya Kupanda Matumaini (Planting Hope) inayomtaka kila mwanamke mkatoliki kupanda miti miwili kila mwaka na kuitunza.Kuendeleza Mradi wa “World Women Observatory” wenye lengo la kupiga vita aina zote za: nyanyaso, biashara haramu ya binadamu na viungo vyake sanjari na mifumo yote ya utumwa mamboleo hasa kwa makundi yaliyopo hatarini zaidi. Kwa sasa kazi kubwa ni kukuza mtandao, kutoa elimu na kufanya kazi na asasi za kiraia na mashirika ya kitawa ili kuweza kuwafikia watu wengi zaidi. Lengo ni kupaza sauti, kuwawezesha kubadili hali zao. Uongozi wa Kiroho na Kijamii: Kuwezesha wanawake na vijana kupitia safari ya Kanisa la Kisinodi: kusikilizana, kumsikiliza Roho Mtakatifu, kutafakari na kushiriki majukumu ya kiroho, kijumuiya na kijamii. Uraia na Ushiriki wa Demokrasia: Kutoa elimu ya uraia na uongozi kwa kuwajengea uwezo wanawake Kushiriki katika medani za kisiasa. Maendeleo Endelevu ya Kiuchumi: Ili kuwezesha WAWATA kujiendesha, tuliazimia kufanya mambo mawili: Kufufua kitega uchumi cha Ilala; Kufungua Microfinance – ili kuwapatia WAWATA mikopo kama mitaji ya kuanzisha miradi majimboni.

WAWATA Saidieni kufundisha elimu ya dini mashuleni
WAWATA Saidieni kufundisha elimu ya dini mashuleni

Utekelezaji: Kitenga Uchumi cha Ilala: Tumeteua timu ya wataalamu ndani ya WAWATA kufanya tathmini ya kiwanja cha Ilala na jengo lililopo ili kushauri namna ya kufufua kitega uchumi hicho. Kufungua Microfinance ya WAWATA. Baada ya kufanya tathimini ya kina na kwa kuzingatia malengo ya muda mrefu, badala ya kufungua Microfinance, WAWATA imewekeza sehemu ya fedha kwenye HATI FUNGANI za Benki kuu ya Tanzania, BOT., zenye thamani ya shilingi milioni mia tano (shs 500,000,000.00) kwa riba ya asilimia kumi na tano na senti sabini na tano (15.75%) sawa na shilingi milioni sabini na nane laki saba na hamsini (shs 78,750,000.00) kila mwaka. Baada ya miaka ishirini na tano (25) fedha hii itakuwa imezalisha shilingi bilioni moja, milioni mia tisa sitini na nane, laki saba na hamsini (shs 1,968,750,000.00. Fedha hii itatumika kuanzisha miradi yenye lengo la kuwakwamua WAWATA kiuchumi katika ngazi zote ili kuweza kuchangia kushiriki kikamilifu katika utume wao. Mafunzo/Semina kwa Viongozi wa Halmashauri: Mwezi Desemba 2024 kwa kushirikiana na Baraza la Maaskofu, WAWATA iliandaa mafunzo kwa viongozi wote watano (5) kutoka majimbo yote ambayo ilifahiliwa kwa sehemu na MISSIO na WAWATA Taifa. Lengo ni kuwajengea uwezo viongozi kuweza kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi. Baadhi ya mada zilizofundishwa ni pamoja na: Kusikilizana katika Roho (tunda la Sinodi)– Conversation in Spirit. Namna ya kutembea pamoja Kisinodi. Uongozi katika kanisa – namna ya kuandaa mpango mkakati, kuendesha vikao, namna ya kutatua migogoro na wajibu wa kila mmoja. Biashara haramu ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo ya utumwa mamboleo. Kuwalinda walio katika mazingira hatarishi “Safeguarding.” Mafunzo haya yataendelea kutolewa kila baada ya uchaguzi.

WAWATA wakiwa kwenye maandamano kuingia Kanisani
WAWATA wakiwa kwenye maandamano kuingia Kanisani

Miradi endelevu: Kampeni ya kupanda matumaini kwa kupanda miti miwili kila mwaka – ‘Planting Hope campain’ kwa kipindi cha miaka miwili 2024/25 na 2025/26. Tunawahimiza wanawake wote kushiriki mradi huu katika ngazi za familia, parokia na jimbo. Kampeni ya mlo wa familia bila vifaa vya kielektroniki – ‘Device-free family meal.” Lengo la kampeni hii ni kuzihimiza familia kurejesha uhusiano wa kweli wa familia kwa uwepo, upendo na kuwa na muda wa pamoja ambao wazazi wanawasikiliza watoto na Watoto kuwasikiliza wazazi badala ya simu, tv n.k. Majimbo yameendelea kutekeleza vipaumbele vilivyoanishwa Kitaifa kulingana na mahitaji na hali halisi ya eneo mahalia. Changamoto katika Ulimwengu mamboleo: Kukosekana kwa Katekesi Endelevu kwa Familia. Malezi mengi yameachwa mikononi mwa vyombo vya habari, mitandao, na shinikizo la jamii ya kisasa. Familia nyingi hazina msingi wa mafundisho endelevu ya imani katoliki. Wanandoa wapya hawapati maandalizi ya kutosha kuhusu dhamana na wito wa ya ndoa ya Kikatoliki. Kukosekana kwa elimu ya dini shuleni.Baadhi ya shule hazitoi mafundisho ya dini kwa sababu ya upungufu wa makatekista / walimu wa dini.

WAWATA Chipukizi: Mkazo: Malezi na Makuzi ya Watoto na Vijana
WAWATA Chipukizi: Mkazo: Malezi na Makuzi ya Watoto na Vijana

Mapendekezo ya Kutatua Changamoto za Malezi na Makuzi: Kuanzisha na Kuimarisha Vyuo vya Makatekista. WAWATA inaomba ziwepo jitihada za kanda na majimbo kuwezesha uanzishaji na uimarishaji wa vyuo vya makatekista ili kupata watumishi walioandaliwa kutoa katekesi na elimu ya dini kwa wanafunzi wa komunio na kipaimara, na kufundisha dini mashuleni. Kuboresha maslahi na maendeleo ya makatekista waliopo. Kuwaendeleza makatekista waliopo kuendana na kasi ya maendeleo / Mabadiliko ya sasa ambapo shule nyingi zinafundisha kwa lugha ya Kiingereza. Kuboresha maslahi ya makatekista na kuwapatia nyenzo za kuweza kutekeleza majukumu yao kikamilifu. Kuwatumia Walimu wakatoliki katika shule za serikali na binafsi. Walimu Wakristo, hasa Wakatoliki, wajengewe uwezo na kupewa majukumu ya kufundisha dini mashuleni kwa kushirikiana na Maparoko na WAWATA. Elimu ya Sinodi: Tunawaomba wachungaji kuendelea kutoa elimu kuhusu matunda ya sinodi ili kila mwanakanisa (walei na maklero) kuweza Kushiriki kikamilifu wito wao kama wabatizwa. Kadiri ya maandiko matakatifu, kupitia Ubatizo, wanawake na wanaume wana hadhi sawa kama washirika katika Taifa la Mungu. Hata hivyo, baadhi ya makundi na hasa wanawake bado wanakumbana na vikwazo katika kutambuliwa kikamilifu kwa karama zao, wito wao, na nafasi yao katika maeneo mbalimbali ya maisha na utume wa Kanisa. Kwa niaba ya WAWATA, Mama Evaline Malisa Ntenga Mwenyekiti WAWATA, Taifa; Mwakilishi Mwanamke kwenye Baraza la Viongozi wa Kidini Afrika – Dini kwa ajili ya Amani (SECAM) na Rais wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika.

WAWATA TEC 2025
21 Juni 2025, 15:22