Maelfu wakusanyika katika Madhabahu ya Namugongo kuwaenzi Wafiadini wa Uganda
Na Isaac Ojok – Lira na Padre Paul Samasumo – Vatican.
Ufikiaji wa uwanja mkubwa wa Madhabahu ya Namugongo ulianza mapema kama 11:30 alfajiri, Jumanne tarehe 3 Juni 2025, huku mahujaji wakivumilia kwa subira foleni ndefu nyuma ya vizuizi vikali vya usalama na ukaguzi. Wengi walilemewa na heshima kubwa, tafakari ya kiroho, na hisia walipokaribia mahali patakatifu. Wengine walikuwa wametembea kilomita nyingi kufika huko. Mwaka huu, ilikuwa ni zamu ya Jimbo la Lugazi kuongoza na kuhuisha adhimisho la Liturujia ya Misa Takatifu. Kaulimbiu ya mwaka 2025: “Ee Bwana, niruhusu nione tena, mimi mhujaji wako wa matumaini.” Kabla ya Misa Takatifu, kwaya ya jimbo ilijaza anga kwa nyimbo zenye kupendeza za kuwasifu Mashahidi wa Uganda, na kuimarisha urithi wa imani na ujasiri uliosababisha kifo chao.
Namugongo: Mahali patakatifu pa imani na matumaini
Akitoa mahubiri yake, Askofu Christopher Kakooza wa Jimbo la Lugazi, aliwakaribisha mahujaji huko Namugongo, akiwataja nchi baada ya nchi na kueleza Namugongo kuwa ni mahali patakatifu pa imani na matumaini. Alitoa shukrani kwa Mungu kwa zawadi ya wafiadini watakatifu na kuwataka waamini kuungana katika maombi. Pia aliwaomba kusali kwa shukrani kwa zawadi ya Papa mpya, Leo XIV. Askofu Kakooza alisisitiza kwamba, “hija ni safari ya imani na matumaini inayowaimarisha waamini. Hija takatifu inafanywa na mtu mwenye imani akitembea na Yesu kuelekea utakatifu”, alisema.
Kwa sauti moja, tunalia
Mahubiri ya Askofu yalitokana na Simulizi ya Injili ya kipofu Bartimayo, aliyemwita Yesu nje ya mji wa Yeriko. "Kwa sauti moja, tumetoka kumlilia Bwana kwa matumaini. Tumekuja kwa imani ya mashahidi. Mashahidi hawa walitoa maisha yao kwa ajili ya Kristo," Askofu wa Lugazi alisema. "Bwana alichukua imani ndogo ya Karoli Lwanga na wenzake na kuigeuza kuwa kitu kikubwa." Askofu Kakooza aliongeza, “Tunaweza kukabiliana na changamoto, lakini matumaini yetu yanatuita kuvuka vivutio vya dunia. Tunaalikwa kushiriki katika safari hii ya kiroho ya ushirika na Mungu na wengine. Ni safari inayohitaji uthabiti na ustahimilivu. Mapambano yetu hapa duniani ni ya muda mfupi,” Askofu Kakooza alitoa tafakari kwa waamini huko Namugongo iliyojaa.
Sherehe ya mwaka huu ilikuwa ya kusisimua, iliyoadhimishwa na nyimbo za kitamaduni za Kikatoliki na kuimarishwa na idadi inayoongezeka ya mahujaji wa kimataifa kutoka Kenya, Tanzania, Rwanda, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Malawi, Msumbiji, Afrika Kusini, na Zambia. Zaidi ya hayo, mahujaji kutoka Marekani, Ulaya, na Asia walishiriki katika matukio hayo yenye kupendeza. Miongoni mwa waliohudhuria ni viongozi kadhaa wa serikali na wa kimila, akiwemo Makamu wa Rais wa Uganda, Jessica Alupo. Balozi wa Vatican nchini Uganda anayemaliza muda wake, Askofu Mkuu Luigi Bianco, pamoja na Maaskofu kadhaa wa ndani na wageni, mapadre, watawa wa kike na kiume, bila shaka waamini walei watu wa Mungu.
Jaribio la kigaidi lililoshindwa huko Munyonyo
Mapema siku hiyo, shirika la habari la Reuters, likinukuu vyombo vya habari vya Uganda, liliripoti kwamba kitengo cha Kupambana na ugaidi cha Uganda kilinasa na kuzuia kile ambacho kingeweza kuwa shambulio la kigaidi katika kitongoji cha Munyonyo cha jiji la Kampala. Kulingana na ripoti za Uganda, mlipuko uliua watu wawili wanaoshukiwa kuwa magaidi, akiwemo mwanamke wa kujitoa mhanga, ambao huenda walikuwa wakielekea eneo la Munyonyo. Hakuna majeruhi au vifo vingine vilivyoripotiwa. Mamlaka zinaamini kuwa washambuliaji hao wanahusishwa na kundi la Allied Democratic Forces (ADF), kundi la waasi lenye makao yake makuu nchini Congo linaloshirikiana na kundi la kigaidi la Islamic State (IS).
Msemaji wa jeshi la Uganda Chris Magezi alisema kwenye X (zamani Twitter) kwamba kitengo cha kukabiliana na ugaidi " kiliwakamata na kuwaondoa magaidi wawili wenye silaha huko Munyonyo." Mmoja wa washukiwa hao alikuwa mwanamke wa kujitoa mhanga "aliyekuwa na vilipuzi vikali," Magezi aliongeza. Waganda wengi walisema kwenye mitandao ya kijamii kwamba wanaamini shambulio hilo la kigaidi lililozuiwa lilizuiliwa kutokana na uingiliaji kati wa Mungu kupitia maombezi ya Mashahidi wa Uganda, wakithibitisha tena imani yao katika ulinzi wa Mungu. Madhabahu ya Munyonyo ni mahali ambapo Wafiadini wa Uganda walihukumiwa kifo na ambapo baadhi waliuawa, huku Namugongo ikiwa sehemu ya mwisho ya kunyongwa. Umbali kati yake ni kama Kilomita 50.
Ziara ya kihistoria ya Papa Paulo VI nchini Uganda
Wafiadini wa Uganda walitangazwa na Mtakatifu Papa Paulo VI kuwa watakatifu mwaka 1964. Mnamo Julai 1969, Papa Paulo VI akawa Papa mtawala wa kwanza kutembelea Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara aliposafiri hadi Uganda. Ziara hiyo ilijumuisha kuhiji eneo la mauaji ya shahidi huko Namugongo. Mnamo 1993, Papa Yohane Paulo II pia alitembelea Namugongo. Kisha, mnamo 2015, Papa Francisko pia aliadhimisha Misa katika Madhabahu ya Namugongo wakati wa ziara yake nchini Uganda.