Tanzania,Kongamano la TYCS Kitaifa:Ask.Mkuu Nkwande,Vijana ni utajiri wa Kanisa,shikeni maadili!
Na Sarah Pelaji - Vatican.
Idara ya Kichungaji ya Vijana Kitaifa ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC)iliratibu Kongamano la Vijana Kitaifa, la Vijana Wakatoliki wa Shule za Sekondari(TYCS) lililofanyika kwa siku nne katika Shule ya Sekondari ya Donbosco-Didia, Jimbo Katoliki Shinyanga, ambapo takribani vijana 1,200 kutoka Majimbo Katoliki 33 walishiriki. Misa ya Ufunguzi ilifanyika tarehe 8 Juni 2025, ikiongozwa na Askofu Mkuu Renatus Nkwande wa Jimbo Kuu Katoliki Mwanza na ambaye katika mahubiri yake alisisitizia vijana kuhusu maadili hasa ya kufanya kazi kwa kujituma, kufanya kazi kwa bidii ili kulijenga taifa na Kanisa. “Vijana ni utajiri wa Kanisa hivyo lazima wawe na maadili na uadilifu huku wakikataa kutumika kisiasa.”
Taifa halijengwi na chawa bali vijana wema na wenye hofu ya Mungu
“Zamani tulikuwa tunashambuliwa na wadudu wanaoitwa chawa ambao waliitesa miili yetu. Tuliwachukia sana, lakini cha ajabu kuna vijana wa sasa wanajiita chawa wa kushabikia mambo maovu. Taifa halijengwi na chawa bali vijana wema na wenye hofu ya Mungu ambao wataingia kwenye siasa na kwenda kupinga mambo maovu,”alisisitiza Askofu Mkuu Nkwande. Akiendelea aliwataka kutumia fursa ya Kongamano hilo “kufanya mabadiliko ya kiroho na kimaadili” huku akiwaonya “juu ya matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo bangi na kubainisha kuwa madhara yake ni makubwa hapo baadaye kiuchumi, kiakili na kiafya.”
Askofu Sangu:ishi maisha ya usafi wa moyo lililo chimbuko la mema na maovu
Hata hivyo katika kuwasilisha mada kuhusu “Vijana na Utakatifu wa moyo,” Askofu Liberatus Sangu wa Jimbo Katoliki Shinyanga, aliwakaribisha vijana hao katika jimbo la Shinyanga huku akihamasisha kuishi maisha ya usafi wa moyo. Chimbuko la mema na maovu ni kutoka ndani mwa moyo wa mtu. Aidha alisema vijana wakue kiimani kama yanavyofundisha mafundisho ya Kanisa Katoliki kwamba “hakuna wokovu nje ya Kristo aliyeteswa, akafa na akafufuka. Vijana ninyi ndiyo tegemeo la Kanisa lazima muelewe kuwa bila Kristo huwezi kufanikiwa chochote. Nyakati hizi watu wamempoteza Yesu kwa kupenda mafanikio ya njia za mkato. Tunampoteza Yesu kwa tamaa za utajiri. Kanisa linafundisha kufanya kazi na kusali kwa bidii. Wewe unatafuta utajiri kwa kuombewa ili unapoingia nyumba iwe imejaa mapesa. Maandiko yanasema asiyefanya kazi na asile. Huwezi kufaulu kwa kuombewa tu, lazima usome. Ukiugua nenda Hospitali, usimjaribu Mungu kwa maombi. Wapo vijana wengi kazi yao ni kucheza kamari na kubeti, huo ni uvivu. Nyinyi ndiyo tegemeo la Kanisa Katoliki na ndiyo wajibu wenu kuiishi na kuitangaza Imani kwa matendo kama linavyoelekeza Kanisa Katoliki,” alisisitiza Askofu Sangu.
Kwa Padre Japhet Nyarubi wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, Tanzania aliwasilisha mada juu ya “Kijana na utandawazi” huku akiwasisitiza kutumia vyema mitandao hiyo kama fursa ya kusambaza upendo na kuchochea moyo na nguvu ya uinjilishaji kwa kueneza upendo wa Kristo ukaenea kwa kasi zaidi. Pia inasaidia kupata taarifa mbalimbali, habari, na kusoma vitabu mbalimbali hivyo kupata elimu ya kidini na kidunia. Katika hili aliwatahadharisha vijana juu ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ambayo inapoteza muda na ari ya maisha kwamba: “Usipokuwa na nidhamu ya kujizuia unaweza ukajikuta unatumia muda mwingi kuliko kazi. Kupoteza nguvu na ari ya kufanya kazi, kuanika maisha yako binafsi ambayo yanaharibu utu wako, kuangalia picha zisizo na maadili hivyo kuvunja usafi wa moyo na kutumia nguvu za ujana wao kiholela,” alisisitiza Padri Nyarubi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Idara ya Utume wa Walei wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC, Askofu Edward Mapunda, aliwasihi vijana kulitumia Kongamano hilo kuwafanya kuwa na nguvu mpya kulishika Neno la Mungu na kutii amri zake.
Misa ya hitimisho 11 Juni 2025: kushika amri za Mungu, kusali Rozari Takatifu na kubaki katika Mapokeo ya Kanisa
Katika hitimisho la kilele cha Kongamano hilo kwa Adhimisho la Misa Takatifu, iliyofanyika tarehe 11 Juni 2025, Mhashamu Askofu Wolfgang Pissa,(OFM Cap), Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), aliwataka vijana kuwa jasiri katika kufanya maamuzi kwa kuwa wamekwisha kua na sio watoto tena, huku akiwahimiza “kuwa tayari kubeba majukumu yanayowakabili katika Kanisa, Jamii na Taifa.” Pia Askofu Pisa alieleza kuwa “baadhi ya nchi na hasa za Ulaya Magharibi na Amerika Kaskazini zinawaandaa watoto kusoma kulingana na karama na vipaji wangali wadogo, hivyo vijana waliopo shuleni watambue vipaji vyao na kufanya maamuzi.”
Hata hivyo alisema kuwa vijana wa sasa wapo kwenye jamii ambayo baadhi ya watu wanaposimama na kuzungumza wanadhani kila mtu ni mtoto, hivyo aliwataka vijana wa Kanisa Katoliki kutambua kwamba “baada ya kupokea sakramenti ya Kipaimara wamekuwa watu wazima.” Aliwataka vijana kushika amri za Mungu, kusali Rozari Takatifu na kubaki katika Mapokeo ya Kanisa, kwani huo ndiyo ukomavu wao wanaoupata katika imani.