杏MAP导航

Tafuta

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo; Zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo; Zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani.  

Jimbo Kuu la Dar es Salaam: Jubilei Na Sherehe ya Ekaristi Takatatifu: Ushuhuda

Fumbo la Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo; Zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani. Ni kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha mapendo kwa Mungu na jirani. Ni Sakramenti ya Altare, mahali pa kukutana na Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai, Mwili na Damu yake Azizi. Ekaristi Takatifu ni Fumbo na muhtasari wa imani ya Kanisa; ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Imani katika Kristo Yesu kwenye maumbo ya Mkate na Divai!

Na Sarah Pelaji, -Vatican

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo; Zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani. Ni kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha mapendo kwa Mungu na jirani. Ni Sakramenti ya Altare, mahali pa kukutana na Kristo Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai, Mwili na Damu yake Azizi. Ekaristi Takatifu ni Fumbo na muhtasari wa imani ya Kanisa; ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu Dominika tarehe 22 Juni 2025 yalijikita katika: Ibada ya Misa, Maandamano ya Ekaristi Takatifu na hatimaye fursa ya Kumwabudu Kristo Yesu katika Sakramenti kuu ya Ekaristi Takatifu, ili kuomba neema na baraka kwa ajili ya nyumba, familia na kwa ajili ya binadamu wote. Huu ni mwaliko kwa waamini kila siku wanaposhiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu, kuwa ni alama angavu ya dhamana ya waamini kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli vyombo na mashuhuda wa ushirika, amani, ukarimu na upendo kwa Mungu na kwa jirani zao.

Padre Innocent Bahati akiwahubiri watu wa Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam.
Padre Innocent Bahati akiwahubiri watu wa Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Parokia zinazosimamiwa na Shirika la Ndugu Wadogo wa Francisko Wakonventuali katika Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam zimeungana kuadhimisha Sherehe ya Mwili na Damu Azizi ya Yesu Kristo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025. Parokia hizo ziko saba ambazo ni: Parokia ya Mtakatifu Bonaventura Kinyerezi, Parokia ya Mtakatifu Faustina Kifuru, Parokia ya Mtatakatifu Clara Mongolandege, Parokia ya Roho Mtakatifu Segerea; Parokia Teule ya Kisukuru, Parokia Teule ya King’azi na Parokia Teule ya Manabii. Misa Takatifu ya pamoja iliadhimishwa Dominika tarehe 22 Juni 2025 Katika Parokia ya Mtakatifu Bonaventura Kinyerezi kwenye viwanja vya Kecha huku Mwadhimishaji mkuu akiwa ni Mheshimiwa Padri Jerome Munishi OFM Conv., Muhudumu Mkuu wa Shirika la Ndugu Wadogo wa MFrancisko Wakonventuali Tanzania na kuhudhuriwa na maelfu ya waamini.

Mapadre wakiandamana wakati wa maadhimisho ya "Corpus Domini."
Mapadre wakiandamana wakati wa maadhimisho ya "Corpus Domini."

Katika mahubiri yake kwenye adhimisho hilo, Padri Innocent Bahati alieleza kuwa Kristo ambaye amekuja kwenye maisha ya mwanadamu katika sherehe ya Ekaristi Takatifu wasimwache bali watembee naye katika maisha yao na kupitia yeye atawasaidia katika maisha yao. Padri Innocent, ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Moshi, alisema "Kinachowatofautisha Wakristo wakatoliki na madhehebu mengine ni uwepo wa Ekaristi Takatifu, Kristo ambaye tunamkiri katika maumbo ya Mkate na Divai, hivyo ili uendelee kubaki kuwa Mkristo Mkatoliki kamili lazima kumpokea Yesu kila mara na kuishi katika matendo yanayofanana Naye.” Amewataka wawe jasiri wa kumshuhudia Yesu wa Ekaristi Takatifu hadharani bila kuona aibu ya kumwabudu, kumtangaza na kumshuhudia popote pale.

Waamini wanaalikwa kusali  na kuombea uchaguzi mkuu 2025
Waamini wanaalikwa kusali na kuombea uchaguzi mkuu 2025

Wakati huo huo, Padre Innocent Bahati amewaalika Wakristo waitazame Sherehe ya Ekaristi Takatifu kama siku ya kuzaliwa upya katika neema ya Mungu kwa kutembea na Kristo Yesu katika: Mitaa, familia familia zao na nafsini mwa kila mmoja wao.  Hivyo Wanapofanya Andamano Takatifu la Mwili na Damu ya Yesu Kristo kama Mahujaji wa Matumaini amewasisitiza waamini kuombea Uchaguzi Mkuu ujao. Pia waliombee taifa la Tanzania ili liendelee kudumu katika haki, amani na umoja na mshikamano wa kitaifa. Baada ya Misa Takatifu kila Parokia ilifanya Andamo Takatifu kuelekea parokiani kwake kama Mahujaji wa Matumaini Jambo lililokuwa na mvuto maalumu kwa waamini waliohudhuria na waliokuwa wakishuhudia maandamano hayo yaliyokuwa na maelfu ya waamini. Shirika la Mapadri Ndugu Wadogo Wafrancisko Wakonventuali linafanya utume wake katika majimbo mbalimbali nchini Tanzania katika Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Jimbo Kuu Katoliki Arusha, Jimbo Katoliki Morogoro na Same.

Ekaristi Dar
28 Juni 2025, 16:20