Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Sala na Mfungo tarehe 23 Agosti 2025: Haki na Amani
Na Sarah Pelaji, - Vatican.
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC limetoa wito wa sala na mafungo kuiombea nchi ya Tanzania ili itawaliwe na haki na amani, pia limetoa sala maalumu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na mwongozo wa maboresho ya Liturujia katika Kanisa Katoliki Nchini Tanzania. Maaskofu hao wametoa wito huo kupitia barua rasmi iliyotolewa tarehe 20 Juni 2025 na kusainiwia kwa niaba ya Maaskofu wote na Askofu Simon Chibuga Masondole wa Jimbo Katoliki la Bunda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Idara ya Liturujia TEC., ikiwa ni mara baada ya Mkutano Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC katika kikao cha 109 uliofanyika Kurasini Jimbo kuu la Dar es Salaam kuanzia tarehe 16-19 Juni 2025. TEC imeeleza kwamba, Taifa la Tanzania linapoendelea na Safari katika Tumaini lisiloisha katika Mwaka huu Mtakatifu wa Jubilei Kuu 2025, Maaskofu wanalialika Taifa zima la Mungu Nchini Tanzania kuwa na siku ya Sala na Mfungo kuombea uwepo wa Haki na Amani nchini Tanzania. “Tunawaomba waamini wote katika Kanisa letu kufanya Sala na Mfungo huo utakaoambatana na kuabudu Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na kufanya kitubio. Kila Jimbo, Parokia, Jumuiya za Kitawa na Taasisi wataweka utaratibu utakaowawezesha watu wote kupata nafasi ya kumwabudu Yesu wa Ekaristi, kusali na kutubu siku nzima kwa masaa 12 au 24 kufuatana na uwezo wa mazingira, tarehe 23 Agosti 2025. Lengo mahususi ni kuliombea Taifa letu la Tanzania lidumu katika Haki na Amani tunapoelekea kufanya Uchaguzi Mkuu mwaka huu wa 2025,” TEC imeeleza katika barua hiyo maalumu iliyotolewa tarehe 20 Juni 2025.
TEC yatoa Sala maalumu kuombea Uchaguzi Mkuu 2025: TEC kupitia Idara ya Liturujia imetoa sala maalumu ya kuombea Uchaguzi Mkuu ujao huku ikielekeza kuwa sala hiyo isaliwe baada ya kusali Sala ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo. Ee Mungu tunakusifu, tunakuheshimu, tunakutukuza, tunakuabudu na kukushukuru sisi Watanzania kwa kutujalia nchi nzuri. Tunakushukuru pia kwa zawadi ya mwaka Mtakatifu wa Jubilei 2025.6.20 Tukiwa Mahujaji katika Matumaini, tunakuomba utuepushe na changamoto zinazoweza kuvuruga Haki na Amani. Jaza nyoyo zetu Mapendo yako ili wote tuwajibike kiaminifu na tuunganishwe ili kuishi kama ndugu wa familia moja. Ee Mwenyezi Mungu, uongozi wa kweli unatoka kwako. Tunakuomba uijalie Nchi yetu viongozi wema na waadilifu, watakaoliongoza Taifa letu kuishi tunu za Upendo, Haki na Amani. Tunaomba Hayo kwa NJia ya Kristo Bwana Wetu, Amina. Bikira Maria Mtakatifu Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mlinzi wa Taifa letu Utuombee.
Maboresho ya Liturujia TEC: Idara ya Liturujia TEC imetoa mwongozo wa maboresho ya Liturujia nchini Tanzania ili kuendeelea kufanya Maadhimisho ya Liturujia kwa heshima na uchaji zaidi katika kuiishi imani Katoliki. Katika barua maalumu iliyosainiwa na Askofu Simon Chibuga Masondole, Mkuu wa Idara ya Liturujia kwa niaba ya Maaskofu wote TEC, Idara hiyo imeeleza kuwa, kila siku Mama Kanisa na Liturujia yake inamwita na kumtaka kuiishi katika kutano la Mungu na watu wake katika hali ya utulivu na uchaji. Hata hivyo kumejengeka tabia ya kuingiza matangazo mengi na hotuba nyingi kwenye maadhimisho mbalimbali ya kiliturujia ambapo jambo hilo likiachwa liendelee litafifisha heshima inayopaswa kutolewa katika Ukuu wa Liturujia mbele ya Mungu. Hivyo katika Mkutano Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC kikao cha 109 uliofanyika Kurasini Jimbo kuu la Dar es Salaam Juni 16-19 mwaka huu 2025, Maaskofu wameagiza maboresho ya Maadhimisho yanayohusu Daraja Takatifu, Nadhiri za Kitawa, Ndoa, Jubilei na Maziko ya Kikristo ambapo jamii inapokusanyika jamii yote ya wana wa Mungu yazingatie utaratibu huo. Mosi ni Mwanzo wa Misa ambapo kuanzia sasa Misa Itaanza mara Moja bila kuketi na kusikiliza utangulizi au maelezo yanayohusu adhimisho na tukio husika. Kama kutakuwa na haja ya katekesi ya Adhimisho husika, mambo hayo yaelezwe kabla ya maandamano ya adhimisho la Misa Takatifu. Adhimisho lenyewe litaadhimishwa kwa kufuata mtiririko wa riti na madhehebu kama yanavyoeleza na kuelezeka.
Mwisho wa Adhimisho (baada ya sala ya Komuniyo), itatolewa mara moja Baraka ya Mwisho. Hakutakuwa na hotuba za kupongezana isipokuwa tu mwadhimishaji (paroko au Padri kama ni tukio la Kiparokia, Askofu wa Jimbo kama ni tukio la kijimbo, Rais wa Baraza la Maaskofu TEC kama ni tukio la kitaifa) ambapo atatambua kwa ufupi uwepo wa wageni wa kidini, kiserikali, kijamii na waalikwa wote bila kuwapa nafasi ya kuzungumza, kutoa hotuba wala kusalimia. Mwadhimishaji Mkuu atawajibika kuwaalika wageni kutoa zawadi zao na bila ya wao kutoa salamu za pongezi. Neno la Mshangwera la Shukrani litatolewa kwa ufupi na Mdarajiwa, Mnadhiri, Mjubilei. Matangazo yatatolewa kwa ufupi kwa ajili ya kuonesha utaratibu wa chakula na yanayofuata. Picha zitachukuliwa chache kwa ajili ya kumbukumbu kisha kutoa heshima kwa Altare na kuondoka. Barua hiyo imeelekeza kwamba utekelezaji wa maagizo hayo unaanza mara moja baada ya ujumbe huo rasmi kutolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.