Tafakari Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Mashuhuda wa Fumbo la Pasaka
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, siku arobaini baada ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Kupaa Mbinguni Bwana wetu Yesu Kristo. Baada ya kumaliza kazi aliyotumwa na Baba hapa duniani, kazi ya kuuletea ulimwengu ukombozi wa milele, iliyoanza kwa fumbo Takatifu la umwilisho, kisha utume wa wazi, na kufikia kilele chake katika mateso, kifo na ufufuko wake, Yesu anapaa, anarudi kwa Baba. Mama Kanisa anasadiki na kufundisha kwamba, Kristo Yesu baada ya kusema nao, akachukuliwa mbinguni, akaketi mkono wa kuume wa Mungu. Mwili wa Kristo ulitukuzwa wakati ule ule alipofufuka kama zinavyoshuhudia hali mpya na za kimungu ambazo tokea hapo umebaki nazo daima. Lakini kile kipindi cha siku arobaini ambako alizoea kula na kunywa pamoja na wafuasi wake, na kuwafundisha juu ya Ufalme wa mbinguni, utukufu wake bado ulifunikwa na alama za ubinadamu wa kawaida. Tokeo la mwisho la Yesu linakamilika na kuingia bila kurudi kwa ubinadamu wake katika utukufu wa Mungu uliojionesha katika sura ya wingu na mbingu (Lk 24:51) ambako tangu hapo ameketi kuume kwa Mungu. Kwa namna moja tofauti kabisa na ya pekee atajionesha kwa Paulo “kama mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake” katika tokeo la mwisho lililomfanya kuwa Mtume.
Hali iliyofunikwa ya utukufu wa Kristo Mfufuka kipindi hiki inaonekana katika maneno yake ya fumbo kwa Mariamu Magdalena: “Sijapata kwenda kwa Baba.Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, ninapaa kwenda kwa Baba yangu, naye ni Baba yenu.” Hii inaonesha tofauti ya kujidhihirisha kati ya utukufu wa Kristo Mfufuka na ule wa Kristo aliyetukuzwa kuume kwa Baba. Tukio ambalo kwa upande mmoja ni la kihistoria na bora sana linaloonesha kupita toka upande mmoja kwenda upande mwingine. Lakini yote yanabaki yakiwa yameungana kabisa na lile la kwanza yaani kushuka kutoka mbinguni kulikotekelezwa katika Fumbo la Umwilisho. Ubinadamu ukiachiwa katika nguvu zake za maumbile hauwezi kufika kwenye nyumba ya Baba. Kristo Yesu peke yake ameweza kumfungulia mtu njia hii “ili tukae tukiamini kwamba sisi tulio viungo vyake ametutangulia huko aliko Yeye aliye kichwa chetu na shina letu na kwamba, akiisha inuliwa juu ya nchi atawavuta wote kwake! Maadhimisho ya Siku ya 59 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni inayonogeshwa na kauli mbiu: “Shirikisheni kwa upole tumaini lililo mioyoni mwenu.” Rej. 1Pet 3: 15-16. Kristo Yesu anaendelea kujifunua na kuzungumza na wafuasi wake kwa: Neno, neema na baraka zinazobubujika kutoka katika Sakramenti za Kanisa na uzuri wa mbinguni ambapo waamini wanaalikwa kuukumbatia, ili kwa furaha na shangwe waweze kuwa mahali alipo Yeye ambaye ni kichwa cha mwili wake yaani Kanisa. Rej. Kol1:18; 1Kor 12:12-27.
Kristo anapoondoka kutoka machoni pa Mitume wake anawapa moyo kwamba, “Sitawaacha ninyi yatima, nipo pamoja nanyi” anaahidi kuwapelekea msaidizi, Roho Mtakatifu. Mitume wa Yesu walipaswa kuwa mashuhuda wa mambo yote walioyaona na kuyasikia kutoka kwa Kristo wakati alipokuwa bado pamoja nao. Walipaswa kuwa mashuhuda wa Fumbo la Pasaka kwa watu wa mataifa yote. Kristo anawaahidi kuwaletea msaidizi, Roho Mtakatifu ambaye atawakumbusha na kuwafundisha yote, atawapa nguvu na uwezo wa kuwa mashuhuda kweli wa Ufufuko wake, wakihubiri, wakibatiza na kuwanya watu wa mataifa yote kuwa wanafunzi wa Kristo. Baada ya Pentekoste Mitume walianza kwa nguvu na ari kumshuhudia Kristo Mfufuka. Sisi sote tu mashuhuda wa Fumbo la Pasaka. Kwa njia ya Ubatizo wetu tunakiri fumbo hili kubwa la Imani yetu. Kwa njia ya Roho Mtakatifu, tunapata nguvu ya kuiishi na kuishuhudia Imani yetu. Kristo hajatuacha yatima, amekwenda kutuandalia makao ili alipo yeye nasi tuwepo. Yupo kati yetu, katika nyakati mbalimbali za maisha yetu, tuwapo hapa safarini kuelekea kule alipo yeye.
Somo la Injili. Ni Injili ya Luka 24:46-53. Katika maisha yetu nyakati fulani tunakuwa na haraka, tunaharakisha ili kutimiza lengo au ndoto fulani katika maisha. Huenda tunafanya hivyo kwa sababu shinikizo fulani nyuma yetu, huenda ni jamii inayotutegemea, au ni marafiki, au ni familia, ambao wote hawa wanataka kuona mafanikio yetu ya haraka. Kwa mfano, Vijana wengi wanatamani sana kuwa na maisha mazuri, kutajirika kwa haraka, kuwa maarufu nk. Hali hii yaweza kutokea pia katika maisha yetu ya kiroho. Mara nyingi tunatamani kuona matokeo ya haraka kwa sala na maombi yetu, au majibu ya yale tunayomwomba Mungu bila kufahamu kuwa tunahitaji muda wa kusubiri, kujifunza, kuelewa na kuweza kutenda kwa usahihi yale yatupasayo kwa ajili ya Mungu na kwa ajili ya utume wajibu wetu kwa wengine. Matokeo yake huwa sio mazuri na tunaweza kushindwa kufikia pale ambapo Mungu anataka tufike. Katika somo la Injili Takatifu, Yesu anawaaga mitume wake na anawapa wosia kabla ya kupaa kwamba, wasitoke Yerusalemu bali waingoje ahadi ya Baba ile ambayo walisikia habari zake kwake. Aliwafundisha mambo mengi, walipaswa kusubiria zawadi ya Baba, Roho Mtakatifu ambaye angewafundisha na kuwakumbusha mambo yote waliyosikia na kuyaona kutoka kwa Kristo. Ni dhahiri walikuwa na hofu, ya kuanza maisha mapya bila Bwana wao, lakini Yesu hawaachi Yatima, anawaahidi msaidizi, Roho Mtakatifu. Wakiisha kupokea roho Mtakatifu ndipo wangeweza kuwa mashahidi wa Injili ya Kristo. Mitume walisubiri Yerusalemu mpaka siku ya Pentekoste ambapo walipokea roho Mtakatifu na kuanza kumshuhudia Kristo katika Yerusalemu, Samaria na hata miisho ya dunia.
Somo la Kwanza: Ni kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume 1:1-11. Kitabu cha Matendo ya Mitume chaeleza maisha na utume wa Mitume wa Yesu baada ya Yesu kuteswa, kufa na kupaa kwake mbinguni. Chaeleza Mwanzo wa utume wa Mitume wa Kristo, kama mashuhuda wa Injili ya Kristo. Mwinjili Luka anatuarifu tena kwa mara nyingine wosia wa Kristo kwa Mitume wake kabla ya kupaa kwenda kwa Baba. Mitume walisubiri ahadi ya Kristo kuwapelekea msaidizi, na wakiisha kumpokea, walianza kwa nguvu kupeleka Habari Njema ya ufufuko wa Kristo kuanzia Yerusalemu, Samaria hata miisho ya dunia. Mwinjili Luka anatuandikia sisi sote, tulio wapendwa wa Kristo, kwamba sisi pia tu mashahidi wa Injili ya Kristo kwa njia Roho Mtakatifu tuliyempokea kwa njia ya ubatizo na kipaimara. Katika somo la kwanza katika Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni tuna mafundisho matano ya kujifunza: Kwanza: Tukio la kupaa mbinguni Bwana wetu Yesu Kristo ni ukweli wa Imani yetu. Ndugu wapendwa, katika somo la kwanza na somo la Injili Takatifu, Mwinjili Luka anaelezea tukio la Bwana wetu Yesu Kristo kupaa mbinguni baada ya kuikamilisha kazi aliyotumwa na Baba ya kutuletea ukombozi wa milele. Sio habari ya kutungwa wala hadithi ya kufikirika bali ni tukio kweli liliotokea. Nasi tunapokea ukweli huu wa Imani yetu kwa njia ya Maandiko Matakatifu (Holy Scriptures), Mapokeo ya Kanisa (Tradition) na Mafundisho mbali mbali ya Mababa wa Kanisa (Magisterium). Tunakiri ukweli huu katika kanuni ya Imani yetu kwamba, “Kristo alisulubiwa, akafa, akazikwa, akashukia kuzimu, siku ya tatu akafufuka kadiri ya maandiko, akapaa mbinguni, ameketi kuume kwa Baba, atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu na ufalme wake hautakua na mwisho.”
Ndugu wapendwa, Imani yetu imejengeka katika misingi ya Mitume wa Kristo. Imani hii tunayoikiri kila Dominika kwa kusema Kanuni ya Imani yetu, yatukumbusha wajibu wetu wa kuendelea kuwa na Imani thabiti kwa Kristo. Tumwombee Baba Mtakatifu wetu Leo XIV, tuwaombee Maaskofu, Mapadre nasi sote tulio wapendwa wa Kristo, ili tuendelee kumwamini yeye aliyekuja ulimwenguni kwa ajili yetu, akatwaa mwili akawa sawa na sisi, akaishi kama sisi isipokuwa dhambi, akateswa akafa na akafufuka na anatawala milele mbinguni. Pili: Kila mmoja wetu ni mpendwa wa Kristo “Theophilus”, pokea habari Njema. Mwinjili Luka anamwandikia Theofilo, yaani “Mpendwa wa Bwana” juu ya mambo yote aliyoanza Yesu kuyafanya na kufundisha. Lengo la kuandika habari hizi ni kutupa moyo na kutukumbusha juu ya upendo wa Mungu usio na mipaka kwetu sisi watu wa kila kabila, lugha, jamaa na taifa. Mwinjili Luka anaandika Injili hii kwa watu wa mataifa ambao nao pia kwa njia ya Fumbo la Pasaka, habari Njema ya toba na ondoleo la dhambi iliwafikia. Ndugu mpendwa, ni Bahati iliyoje kuwa mpendwa wa Kristo. Kristo amejitoa sadaka kwa ajili yetu sisi sote. Hakuna tofauti tena kati yetu, sote tuna nafasi katika ufalme wa Mungu kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Tunafurahia ushindi dhidi ya dhambi na mauti, tunafurahia zawadi ya Roho Mtakatifu, Pendo la Mungu ambalo limekwisha kumiminwa kwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Wewe u mwana mpendwa wa Mungu, anakuletea Habari Njema kila siku, kwa Neno lake la Faraja, neno la kutia moyo na matumaini, Neno la kutuimarisha ili tuendelee kumtumaini yeye aliyeutoa uhai wake kwa ajili yetu sisi rafiki zake.
Tatu: Mafanikio ya utume wetu yanatokana na utii wetu kwa Neno la Kristo. Kristo anawaaga wanafunzi wake, anawapa wosia akiwaagiza kwamba, “Wasitoke Yerusalemu bali waingojee ahadi ya Baba ile ambayo mlisikia Habari zake kwangu, kwamba Yohane alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatiza kwa Roho Mtakatifu” Mitume hawakutoka Yerusalemu mpaka siku ya Pentekoste ambapo walipokea zawadi ya Roho Mtakatifu. Ndugu wapendwa, mafanikio ya kweli ya kiroho na katika utume wetu, katika kazi zetu na majukumu yetu mbaimbali, yanatokana na utii wetu kwa Neno la Kristo. Kama vile Kristo alivyowaamuru wanafunzi wake wasiondoke kutoka Yerusalemu mpaka watakapopokea Roho Mtakatifu, ndivyo ilivyo kwetu pia. Twapaswa kujijengea mazoea kwamba, niongozwe daima na Neno la Kristo. Kila ninalowaza na kutenda nimsikilize kwanza Kristo anasema nini na moyo wangu. Kabla ya kuianza siku yangu nimsikilize Kristo anasema nini na moyo wangu, anasema nini nami kuhusu utume wangu, kuhusu Watoto wangu, kuhusu Masomo na biashara zangu, kuhusu hali yangu ya kiimani, kuhusu changamoto mbalimbali ninazokutana nazo katika maisha yangu ya kila siku. Omba neema ya kumsikiliza daima Kristo, kutii Neno lake na amri zake, huo ndio uzima wetu na chanzo cha mafaniko yetu ya kweli.
Nne: Kristo hajatuacha yatima, ametuachia zawadi ya Roho Mtakatifu. Kristo anawaahidi mitume wake kuwa watapokea nguvu ya Mungu akiisha kuwajilia juu yao Roho Mtakatifu. Kristo alikaa na wanafunzi wake kwa muda wa miaka mitatu. Aliwafundisha mambo mengi, alitenda miujiza mingi mbele ya macho yao. Hii yote ilikua na lengo la kuwaandaa ili nao wakawe mashahidi wa Kristo. Mara baada ya kufufuka kwake, Kristo alikaa na wanafunzi wake kwa muda wa siku 40, ishara ya muda wa kutosha. Kisha anapaa kurudi kwa Baba yake mbinguni. Anawapa moyo Mitume kwamba hatawaacha yatima. Anawaahidia zawadi ya Baba kwao yaani Roho Mtakatifu. Anaahidi kuwa pamoja na Mitume wake siku zote hata ukamilifu wa dahari. Ndugu wapendwa, Kristo hajatuacha Yatima. Ametupa zawadi ya Roho wake Mtakatifu kwa njia ubatizo wetu na kipaimara. Roho mtakatifu ni msaidizi, ni mwalimu, anatukumbusha yale yote tuliyosikia kutoka kwa Kristo. Kristo yupo daima katikati yetu katika Neno lake, anasema nasi katika nyakati mbalimbali za maisha yetu. Anasema nasi katika nyakati za furaha, katika nyakati za uchungu, katika nyakati za changamoto, katika nyakati za shida, nyakati za misukosuko ya maisha, Kristo hawezi kutuacha kamwe. Anasema daima na mioyo yetu kila mara tunapopata nafasi ya kusema naye, tunapomshirikisha mambo yetu, tunapotambua nafasi ya Roho Mtakatifu kama mfariji wetu na mwalimu wetu, kisha tunapata nguvu ya kusonga mbele tukiwa na matumaini mapya.
Katika somo la Injili ya Sherehe ya Bwana Kupaa Mbinguni tuna mafundisho matano ya kujifunza. Kwanza: Mateso na kifo vina nafasi ya pekee katika mpango wa Mungu wa ukombozi wetu (Suffering has meaning in God’s redemptive plan). Yesu anapowatokea Mitume wake anawaambia ya kuwa, “Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu” Mateso, kifo na ufufuko wake ulikua ni mpango wa Mungu, kwamba kwa njia hiyo aupatanishe ulimwengu wote na Mungu kama ilivyotabiriwa kuazia Musa na Manabii (rej. Isa 53, Zab 22. Hosea 6:2). Ilifaa au ilimpendeza Mungu (it was fitting to God) kwamba ukombozi wetu utimie kwa njia sadaka ya Kristo msalabani. Ndugu mpendwa sana, nasi katika maisha tutambue kuwa kila mmoja wetu ana msalaba wake, anashiriki kwa namna yake kuteseka pamoja na Kristo ili tuingie nasi katika utukufu pamoja naye. Maisha yetu ya ufuasi si maisha rahisi. Mwenyezi Mungu amemweka mbele yetu Kristo, anayeteseka pamoja nasi kwa ajili ya ukombozi wetu. Ndugu wapendwa, tuone mpango wa Mungu hata katika nyakati ngumu katika kubeba misalaba yetu. Tunaalikwa kumshirikisha Mungu maisha yetu, kumshirikisha misalabba yetu, kujikabidhi daima mikononi mwa Mungu ili tuweze kupokea nyakati zote zinazoambatana na ufuasi wetu. Tusipomshirikisha Mungu hatutaweza kuona maana ya mateso pale yanapotokea. Ilimpendeza Mungu kwamba Kristo ateseke na kufa kwa ajili ya kuuletea ulimwengu uzima. Huenda imempendeza Mungu mimi na wewe kupita katika changamoto hizi kubwa namna hii nyakati fulani katika miito yetu, katika ndoa zetu, katika kazi zetu, katika familia zetu, katika mahusiano yetu, katika masomo yetu, katika mapambano yetu ya maisha, ili atuvushe kwenda kwenye neema na baraka kubwa zaidi alizoandaa kwa ajili yangu mimi na wewe. Huenda msalaba wangu ndio kipimo cha daraja langu kuvuka kwenda ng’ambo ya pili. Kila mmoja wetu amwombe Yesu ampe utulivu pale Mungu anapotimiza kile alichoandika kwa ajili yetu, yaweza isiwe leo wala kesho ila Mungu anatuwazia daima mema, hata katika machungu na mateso, Mungu atakuinua tu.
Pili: Kristo anatuachia wajibu, kuwa mashuhuda Ufufuko wake (we are called to be part of this proclamation). Kristo anawapa Mitume wake wajibu, kwamba haikutosha tu kuwa mashuhuda wa macho juu ya yale aliyoyatenda alipokua pamoja nao, juu ya mateso, kifo na ufufuko wake na hata kupaa kwake Mbinguni, bali walipaswa kwenda kuwa mashuhuda kwa watu wa mataifa yote. Kiini cha ushuhuda wa Mitume wa Kristo ni Injili ya toba na ondoloe la dhambi. Anawaambia, “Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya.” Ndugu wapendwa, sisi sote kwa njia ya ubatizo wetu tumepokea zawadi hii ya Injili ya Kristo ya toba na ondoleo la dhambi. Nasi tunakua mashahidi wa mambo hayo, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kama ilivyokuwa pia kwa Mitume. Tunaitwa kuwa watangazaji wa habari njema ya Injili, kwanza kabisa kuipokea ndani ya mioyo yetu kama tulivyokiri siku ya ubatizo wetu, kukubali kuongozwa na Injili ya Kristo, na kisha matokeo yake yataonekana katika maisha yetu ya kila siku, katika familia zetu, katika jumuiya zetu, katika kanisa, katika nchi yetu nk. Kwa njia ya Mama Kanisa Mtakatifu, tunapokea huruma kuu isiyo na mipaka ya kutoka kwa Bwana wetu Yesu Kristo nasi tukialikwa kuwa channels au vyombo vya huruma ya Mungu kwa watu wote. Kusamehe, kuhurumia, kufariji, kusaidia, kupokeana na kuvumiliana, kuguswa na shida za wengine, ni kuiishi Injili kwa matendo. Je, mimi kweli ni shuhuda wa ufufuko wa Kristo kwanza kabisa kwa njia ya maisha yangu? Kristo mfufuka aendelee kukutukumbusha kwa njia ya Roho wake Mtakatifu kwamba sisi tu mashahidi wake kwa namna sana. Tuishi kweli ushuhuda wa maisha na tuwe sababu ya wongovu kwa wengine.
Tatu: Ili tuwe mashuhuda kweli wa Kristo Yesu, tunahitaji nguvu ya Roho Mtakatifu (Paraclete is the promise of the Father). Kristo alijua kuwa Mitume kwa nguvu na akili zao tu wasingeweza kuwa mashahidi kweli wa Injili. Mara baada ya kuteswa na kufa wengine walikimbia na kujifungia ndani kwa hofu ya wayahudi. Lakini Kristo alipowatokea, aliwapa amani. Na hivi kabla ya kupaa kurudi kwa Baba, anawaahidi kuwaletea msaidizi (Joel 2:28, Mdo 2), Roho Mtakatifu ambaye, atawakumbusha na kuwafundisha yale yote ambayo waliyasikia na kuyaona kutoka kwa Kristo. Kristo anawaambia wasiondoke mjini mpaka watakapovikwa uweza utokao juu. Utume wapaswa kuongozwa na Kristo, walipaswa kutiwa nguvu kwanza kabla ya kuanza kuwa mashahidi wake. Ndugu mpendwa, Mitume walipewa nguvu, walivikwa uweza utokao juu. Roho Mtakatifu aliwabadili Mawazo, fikra na mitazamo yao (transformation), wakawa na utambulisho mpya kama wanafunzi kweli wa Kristo. Petro na Mitume wengine ambao hapo Mwanzo walimkana Kristo wengine kukimbia, sasa wakapata ujasiri wa kusimama ma kumtangaza Kristo mfufuka. Walikua kweli mashahidi (Martyres), hata wengine wengi walikufa kifo dini kwa ajili ya Injili ya Kristo. Ndugu wapendwa, sisi kila siku tunapata nafasi ya kupokea nguvu kutoka kwa Kristo. Kristo Yesu yupo daima nasi katika sakramenti na Neno lake. Anasema nasi kwanza kabla ya kututuma. Anatutia nguvu kwanza kabla hatujatoka na kwenda kuwa mashahidi wake. Kila siku tujitahidi kusema na Kristo kabla ya kuanza mambo yetu. Tumpokee katika Ekaristi Takatifu, atufundishe jinsi gani tunapaswa kuishi katika siku nzima. Uwepo wake ukiwa ndani mwetu, basi sisi hatuna hofu na mashaka yoyote. Tulikwisha mpokea Roho Mtakatifu katika ubatizo na utimilifu wa mapaji yake katika Kipaimara. Tumwombe Roho Mtakatifu afanye kazi daima ndani mwetu ili tuweze kuwa mashuhuda wa Kristo mfufuka. Tusikimbilie kufanya mambo yetu tu, tusubiri Kristo asema na mioyo yetu, atufundishe, atuelekeze.
Nne: Kristo anatutazama kila mara kwa upendo, anatubariki, hatuachi hivi hivi (Jesus’ heart towards us is Blessing). Katika maandiko matakatifu, Bethania ilikua ni nyumbani kwa akina Lazaro na ndugu zake Maria na Martha. Yesu mara kwa mara alikwenda Bethania, na hapo ndipo alimfufua Lazaro (Yn 11:1-44). Bethania kutoka katika Lugha ya kiebrania yamaanisha, “Nyumba ya maumivu” Ni sehemu ambapo waliishi watu waliokuwa na changamoto mbalimbali, wagonjwa, viwete, maskini, wakoma nk. Kristo anakwenda hapo pamoja na wanafunzi wake, na hapo anapaa kurudi kwa Baba akiisha kuwapa Mitume wake ujumbe wa Faraja na matumaini. Ni hapa ndipo alipotoa fundisho kuwa yeye ndiye ufufuo na uzima wakati alipomfufua Lazaro. Kumbe anatukumbusha kuwa nasi kisha kuvumilia taabu na mateso ya dunia hii, tutaenda kule alipo yeye. Ndugu wapendwa, Kristo anatutazama kwa jicho la upendo. Anatupenda upeo na hivyo anatubariki, ishara ya uwepo wake wa daima kati yetu. Anatufikia katika Bethania ya maisha yetu, nyumba ya huzuni anaijaza furaha ya ufufuko wake, nyumba ya mkato wa tamaa anaijaza matumaini mapya, nyumba ya maumivu anaijaza kwa nguvu ya kustahimili na kubeba kwa Imani nyakati ngumu za maisha yetu. Pokea baraka za Kristo, nguvu na mamlaka yake ya kimungu vinatuletea amani na utulivu rohoni mwetu. Ishi chini ya baraka hizi anazokumiminia Kristo, anavyopaa kwenda kwa Baba. Anatuachia baraka hizi tuishi nazo kila siku katika maisha yetu, jenga urafiki na Yesu, atakubariki, atakuinua, nawe ukawe baraka pia kwa wengine.
Tano: Kristo Yesu amepaa, ishara ya nguvu na mamlaka. Tusiwe na hofu (the ascension signifies Enthronement). Tunakiri katika kanuni ya Imani yetu kwamba, Kristo aliteswa, akafa, akashukia kuzima, siku ya tatu akafufuka katika wafu, akapaa mbinguni, ameketi mkono wa kuume wa Mungu, atakuja tena kuwahukumu wazima na watu, nao ufalme wake hautakuwa na mwisho.” Ndugu wapendwa, Kristo ni Mfalme wetu, anatawala milele, mbinguni na duniani. Hatuna hofu, hatuna mashaka kwa kuwa yeye aliyeteseka na kufa sasa anaishi milele katika utukufu pamoja na Baba. Hatuna shaka kwa kuwa alishasema huko ndipo nyumbani kwetu. Alikwenda kutundalia makao na hivi atakuja tena kutukaribisha kwake. Mitume wa Yesu mara baada ya Yesu kupaa, wanarudi Yerusalemu wakiwa wamejawa na furaha kuu tofauti na walivyokuwa hapo mwanzoni. Ndugu wapendwa, Kristo akawe chanzo na sababu ya furaha yetu kila wakati. Tusali na kumwabudu Kristo wakati wote, uwapo na furaha Sali, uwapo na huzuni Sali, uwapo salama sali, uwapo hatarini pia Sali, furaha yetu ijengeke katika Imani na tumaini kwamba Kristo Mfalme wetu anatawala milele.
Somo la Pili: Ni Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso 1:17-23. Katika somo la pili, Mtume Paulo anatufundisha, Kwanza, kuwa ni Mungu alimfufua Kristo kutoka wafu na akamweka mkono wake wa kuume juu sana kuliko ufalme wote na akamweka kuwa kichwa juu ya vitu vyote. Kwa njia hiyo ameshinda kifo na mauti, ametuletea ushindi na ukombozi wa milele sisi tulio viungo vya wmili wake yaani Kanisa. Pili, Tumaini letu sisi sote ni kuwa siku moja nasi tutainuliwa juu na kwenda kuungana na Kristo na kutawala naye milele yote. Ili tuweze kufika alipo Kristo, hatuna budi nasi kila mmoja wetu kutimiza kwa uaminifu utume ambao Mwenyezi Mungu ametukabidhi kila mmoja wetu katika maisha yetu ya ufuasi kwake hapa duniani. Tatu, tunaalikwa kuwa wamisionari wa Habari Njema ya Ufufuko wa Kristo. Mtume Paulo alifanya kazi kubwa ya kumhubiri Kristo mfufuka kwa watu wa mataifa nasi kwa njia ya maneno na matendo yetu, tuwe Injili inayotembea. Maisha yetu yamhubiri Kristo hata pasi na maneno mengi. Hitimisho: Sisi sote tu mashuhuda wa Fumbo la Pasaka. Kwa njia ya Ubatizo wetu tunakiri fumbo hili kubwa la Imani yetu. Kwa njia ya Roho Mtakatifu, tunapata nguvu ya kuiishi na kuishuhudia Imani yetu. Kristo hajatuacha yatima, amekwenda kutuandalia makao ili alipo yeye nasi tuwepo. Yupo kati yetu, katika nyakati mbalimbali za maisha yetu, tuwapo hapa safarini kuelekea kule alipo yeye.