杏MAP导航

Tafuta

Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni. Kristo Yesu amepaa kwenda mbinguni kwa nguvu za kimungu zilizoko ndani mwake. Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni. Kristo Yesu amepaa kwenda mbinguni kwa nguvu za kimungu zilizoko ndani mwake. 

Tafakari Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Injili ya Matumaini

Kanisa linasadiki kwamba, Yesu baada ya kusema nao, akachukuliwa mbinguni, akaketi mkono wa kuume wa Mungu. Mwili wa Kristo ulitukuzwa wakati ule ule alipofufuka kama zinavyoshuhudia hali mpya na za kimungu ambazo tokea hapo umebaki nazo daima. Lakini kile kipindi cha siku arobaini ambako alizoea kula na kunywa pamoja na wafuasi wake, na kuwafundisha juu ya Ufalme wa mbinguni, utukufu wake bado ulifunikwa na alama za ubinadamu wa kawaida.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya Neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican leo Dominika ya kupaa Bwana Yesu Mbingu, Hamu hii imo ndani ya wote, hata wasioamini… Mungu ameiweka nafsini mwetu nayo imekuwa sehemu yetu… hivi hata katika kutenda dhambi mwanadamu huyu huwa anatafuta furaha, ukamilifu na hali njema ila kwa namna isiyo sawa… ni hali hii ya kutafuta kupanda mbinguni juu humpelekea mwanadamu kuwa na mahangaiko mengi, akijaribu kushika hili na kuliacha anapogundua kumbe hilo sio ukamilifu wenyewe, roho ya mtu huyu hutulia tu ifikapo katika Mungu aliyeiumba kwa ajili yake (Mt. Augustino) hivi ni dhahiri tupo duniani tumjue Mungu, tumpende, tumtumikie ili hatimaye, tufike kwake. Sherehe hii inaadhimishwa Dominika hii sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 59 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni inayonogeshwa na kauli mbiu: “Shirikisheni kwa upole tumaini lililo mioyoni mwenu.” Rej. 1Pet 3: 15-16. Kristo Yesu anaendelea kujifunua na kuzungumza na wafuasi wake kwa: Neno, neema na baraka zinazobubujika kutoka katika Sakramenti za Kanisa na uzuri wa mbinguni ambapo waamini wanaalikwa kuukumbatia, ili kwa furaha na shangwe waweze kuwa mahali alipo Yeye ambaye ni kichwa cha mwili wake yaani Kanisa. Rej. Kol1:18; 1Kor 12:12-27. Leo kila mmoja wetu aazimie neno hili moyoni mwake ya kuwa iwe iwavyo, katika hali yoyote, sala yetu iwe “Nami nitapanda mbinguni na Kristo…” Kama mahujajiwa matumaini, katika mwaka huu 2025 wa Jubilei unalenga kuinua matumaini ya Wakristo katika dunia yenye changamoto nyingi: vita, migawanyiko, ukosefu wa haki na amani.

Sherehe ya Kupaa Bwana, Kutangazwa kwa Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo
Sherehe ya Kupaa Bwana, Kutangazwa kwa Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa Leo XIV anasisitiza kuwa Kanisa liwe chachu ya upatanisho, amani na tumaini kwa wote katika wajibu wake wa kimisionari wa kuwafika wote wapate kusikia Habari njema ya wokovu bila kumwacha yeyote na bila woga sote tutembee Pamoja kumweleka Kristo Bwana na Mwalimu wetu. Katika somo la kwanza (Matendo 1:1-11) Kupaa kwa Yesu si mwisho wa uwepo wake bali ni mwanzo wa enzi mpya. Malaika wanawaambia mitume: "Mbona mnasimama kutazama juu?" Ni wito wa kuanza kazi ya utume. Katika Jubilei ya Matumaini, tunaitwa kuwa mashahidi hai wa tumaini. Kristo amepaa mbinguni, ni adhimisho la matumaini yetu kwamba kama Yeye alivyoshinda kifo na mauti ushindi huo si wake peke yake bali ni wetu pia. Kwamba tukiyashiriki vema mafumbo tuliyoachiwa kwa moyo mnyofu na utii kamili basi wakati utakapofika nasi ‘tutapaa mbinguni’ na kujipatia furaha isiyo na mwisho… Yesu amepaa mbinguni, Bwana kwa sauti ya baragumu, alleluia… amepaa ili apokee tuzo baada ya utume wake duniani kufanikiwa kwa 100%, amepaa ili ashike kiti cha utawala kama Mkuu wa Kanisa na Bwana wa viumbe vyote, na huko mbinguni amefanyika Mfalme kuume kwa Mungu Baba yake, amepaa ili kutuletea Roho Mtakatifu atuimarishie imani yetu na kutuongoza vema… kadhalika Kristo amepaa mbinguni kwenda kutuandalia makao kwenye nyumba ya Baba [Yn 14:2-3] na nyakati zitakapotimia atarudi kutuchukua ili alipo Yeye nasi tuwepo kwa milele (Yn 14:4).

Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Injili ya matumaini
Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Injili ya matumaini

UFAFANUZI: Somo la pili (Waefeso 1:17-23), Paulo anaombea ili waamini wapate kuona kwa macho ya moyo tumaini la wito wao. Hii ni nguvu ya Kristo aliyepaa, aliye kichwa cha Kanisa. Katika Jubilei hii, tumaini linapaswa kuwa na mvuto na nguvu ya kubadilisha jamii. “Na tupande Mbinguni na Kristo”… ndio, huko alikotutangalia Yeye aliye Kichwa chetu, hili linaanzia hapa hapa nilipo, kwamba moyo wangu, familia yangu na familia nzima ya wanadamu imfuase Kristo na kufanana naye (imitation of Christ)… hili linadai imani ya kweli katika Mwana wa Mungu aliyetupenda na kujitoa kwa ajili yetu… Imani hiyo hujaribiwa na nyakati nyingine hupitishwa katika makaa ya moto ili kama dhahabu katika tanuru inavyochomwa hadi kuyeyuka ili kuwa halisi pasi na uchafu wowote ndivyo imani yetu pia… ndio kusema majaribu na changamoto ni sehemu ya mapito ya Mkristo, Kristo mwenyewe alijaribiwa na zaidi sana aliingia katika utukufu wake kwa mateso (Lk 24:26). Ukweli huu wa Msalaba aliusema wazi kuwa kigezo cha ufuasi (Lk 9:23).. Yesu anapowapokea wanafunzi wake na kuwabariki, anapanda mbinguni. Wanarudi kwa furaha kuu. Kupaa kwake ni hakikisho la uwepo wake wa milele. Ni msingi wa furaha ya Kikristo na utume mpya.

Kristo Yesu Jua la Haki
Kristo Yesu Jua la Haki

Kwa vile katika karne nyingi imani potofu imepigwa vita na ushirikina kutajwa kama jambo baya basi huo umeturudia katika sura nyingine, pale ambapo Kristo anatajwa kwa nguvu na jina lake kuimbwa kwa sauti lakini bila imani yoyote kwake wala uaminifu kwa mafundisho yake… kushabikia na kukumbatia aina mpya ya hirizi, shanga na tunguli zinazotujia katika jina la “upako”, kumtaja zaidi shetani na vitisho vyake kuliko kushuhudia nguvu ya ushindi wa Pasaka ya Bwana na yetu pia, kutozingatia upyaisho wa roho na uhuru utokanao na Sakramenti ya Ubatizo badala yake kujikuta ni wafungwa wa muda wote wa laana, mikosi, kamba na minyororo katika historia ya ulimwengu wa giza kama kwamba hatukupokea nuru yaani mwanga siku ya ubatizo wetu na tukapewa mshumaa na kitambaa cheupe ishara ya nuru na cheo hayo tumeyapuuza kwa kujisajili katika timu mbili kitu ambacho Kristo anakataa, kukataa moyoni mwetu ukweli kuhusu uhalisia na umuhimu wa mateso, dhiki na changamoto za maisha ya mkristo na hivi hata kulilazimisha Kanisa la Mungu kuhubiri kile tu tunachotaka sisi kukisikia hata kama ni kinyume na mafundisho msingi ya imani na kisiposemwa hicho tutaondoka tukilaumu kwamba “hatushibi, hatutosheki” Mzazi anapomzuia mtoto kula udongo na kumpa mkate na kumwambia shida atakayopata akila udongo na faida ya mkate, mtoto akatupa andazi kwa vile yeye anapenda udongo na kuondoka nyumbani akilaumu kwamba hashibi hilo haliwi tatizo la mzazi, vitisho vya mtoto kuondoka nyumbani visimbadilishe mzazi msimamo hivi kwamba anapomuona mtoto anakula udongo amsifie tu  kula mwanangu huo udongo una protini nyingi sana na vitamin  mzazi wa hivi ni changamoto na hata mtoto mwenyewe atamlaumu baadaye atakapodhurika na ulaji wa udongo kwa Bahati mbaya nyakati zetu hizi tuna wazaaji wengi kuliko wazazi wenye mamlaka, upendo na nguvu ya kulea, wengi ni wazazi ruksa kila kitu anachopendekeza mtoto mzazi yeye anamruhusu kwa kile kiitwacho uhuru wa mtoto lakini tukumbuke uhuru bila mipaka ni fujo… tusipozingatia utulivu wa kiimani basi sala hii Na tupande Mbinguni na Kristo itabaki kuwa njozi njema ya mchana…

Sherehe ya Kupaaa Bwana Mbinguni
Sherehe ya Kupaaa Bwana Mbinguni

Katika mahubiri yake ya kuanza huduma kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Papa Leo XIV tarehe 18.05,2025 alisisitiza kuwa Kanisa liwe "ishara ya ushirika" na chachu ya dunia iliyopatanishwa. Kupaa kwa Bwana ni alama ya matumaini mapya. Tumaini halitokani na hali ya nje bali na Kristo aliyeshinda kifo na kutupa zawadi ya amani inayotujaza ujasiri wa kumshuhudia na kuwaalika wengine walio na hofu ambao bado hawajasikia sauti ya Kristo Mfalme na mshindaji wetu. Ikiwa tu nitaishi uhalisia wa maisha yangu na kuzingatia lengo la Mungu katika kuniumba “…enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni?” (Mdo 1:11)… hii ni dalili ya uzubaifu, tamaa ya yasiyowezekana… Tuache kutazama mawingu na turudi kwenye uhalisia wa maisha, tusishangae jua, mwezi na nyota, maisha halisi yapo nyumbani na katika jumuiya… tusiishi maisha bandia, tuchuchumie wito tulioitiwa wa kufanana na kumfuasa Kristo… tusilumbane, tupendane, tusameheane, tujijengee ujasiri na uhodari, kuona tunapita katika katika majira gani na alama za nyakati zinatufunulia nini, kukumbatiana kwa busu takatifu, kuheshimiana, kuwa wakweli, kujitambua sisi ni akina nani na lipi hasa lengo la uwepo wetu duniani… kuzijua karama tulizojaliwa, mapungufu tuliyonayo, uimara na udhaifu wetu, kusali bila kuchoka na kujiunda upya kila wakati… safari ya kiroho inatuelekeza kudumu katika nuru ya Kristo mfufuka… huyo tu tumtafute, huyo tu tumpende, huyo tu tumtumikie na huko alikopaa Bwana “mbinguni nitapanda”… Kupaa kwa Yesu ni: Matarajio ya utukufu wetu, chanzo cha furaha yetu ya Kikristo, Nguvu ya kuendelea na utume wa Injili, Katika Jubilei ya Matumaini Tusitazame tu juu, bali tuwe mashahidi wa tumaini duniani kwa maneno na matendo., Ee Kristo aliyepaa mbinguni, tupe Roho wako ili tuwe mashahidi wa matumaini. Tufanye vyombo vya furaha na upatanisho kwa watu wote. Amina.

Liturujia Kupaa Bwana
31 Mei 2025, 15:41