Tafakari Neno la Mungu Dominika VI Kipindi Cha Pasaka: Amani, Upendo na Roho Mtakatifu
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya Neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican leo Tunapokaribia mwisho wa kipindi cha Pasaka, Dominika ya Sita ya Pasaka hutualika kutafakari zawadi kuu ambazo Yesu anaziachia Kanisa lake: amani, Roho Mtakatifu, na upendo unaomfanya Mungu akae ndani yetu. Katika mwaka huu wa Jubilei ya Matumaini (2025), ujumbe huu wa kiinjili ni wa muhimu sana kwa ulimwengu wetu unaotamani suluhisho la kweli kwa migawanyiko, hofu, na ukosefu wa mwelekeo wa kiroho. Tukiwa pia tunaukumbuka urithi wa hayati Papa Francisko, tunaona jinsi alivyojitoa kwa dhati kuhakikisha kwamba Kanisa linakuwa mahali pa matumaini, mahali pa amani, na mahali ambapo kila mtu anakaribishwa kwa upendo wa Mungu usio na mipaka. Mazungumzo ya Kristo siku chache kabla ya kupaa mbinguni yalihusu kuondoka kwake. Mitume walihuzunika, anawapa moyo wasihofu sababu atakuja Msaidizi atakayefanya mambo 2, “kufundisha na kukumbusha” naye ana sifa 2, mosi ni ‘Msaidizi’ na halafu ni ‘Roho wa ukweli’. ‘Msaidizi’ katika kiyunani huitwa ‘Paracletos’ mtu anayeitwa kutoa ushahidi kumtetea mtuhumiwa... halafu Paracletos ni ‘advocate – wakili’ anayesimama badala ya mtuhumiwa wa kosa linalompeleka mtu kwenye adhabu. Kadhalika Paracletos ni ‘mtaalamu’ anayeitwa kutoa ushauri katika hali ngumu; mtaalamu huyu anaitwa kuyatia moyo makundi yaliyokata tamaa mf. vikosi vya askari… ni mtu anayeitwa kusaidia wakati wa mahangaiko na taabu, mfariji, mtetezi.
Roho wa Baba ni Msaidizi na ni Roho wa kweli katika maana kwamba yeye atamshuhudia Yesu Kristo kwa maneno ya wafuasi wa Yesu ili watangaze kwa ujasiri na ushujaa kwamba Yesu amefufuka, Yesu yu hai, Yesu ni Kristo, Yeye ni Bwana na Mwana wa Mungu… hilo watalifanya kwa maisha ya upendo, furaha na amani… watayatekeleza hayo kwa ujasiri bila kuwaogopa wapinzani… watakuwa tayari kufa ikibidi ili kutetea ukweli kumhusu Bwana wao. Hili ni tukio muhimu la Mtaguso wa Yerusalemu, ambapo Kanisa la kwanza lilitatua mgogoro mkubwa kuhusu sheria ya Torati kwa waongofu kutoka Mataifa. Kwa hekima ya Roho Mtakatifu, Kanisa lilichagua kuepuka mizigo isiyohitajika, na kuwaalika watu wa mataifa mengine kuishi kwa imani na maadili ya msingi. Katika muktadha wa Jubilei ya Matumaini, somo hili linatufundisha kuwa Kanisa halipaswi kuwa kikwazo, bali daraja la matumaini kwa wote. Tunapaswa kujifunza kusikiliza, kutambua tofauti, na kutafuta muafaka unaojenga. Hayati Papa Fransisko aliyaishi haya kikamilifu. Alisisitiza sinodi, yaani kusikilizana katika roho ya ushirikiano. Alisema: “Kanisa la Kisinodi ni Kanisa linalosikiliza. Ni Kanisa linalojua kuwa kusikiliza ni zaidi ya kusikia: ni kusikiliza kwa moyo.” Hii ni njia ya matumaini: kusikiliza, kuelewa, na kujenga umoja wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa.
UFAFANUZI: Zaburi 65 ni wito wa mataifa yote kumshukuru Mungu kwa wema wake. Ni zaburi ya matumaini ya kimataifa – kwamba baraka za Mungu si za taifa moja tu, bali ni zawadi kwa dunia nzima. Katika kipindi hiki cha Jubilei ya Matumaini, zaburi hii inasisitiza kuwa matumaini tunayohubiri lazima yawe na sura ya ulimwengu mzima – yaani, tujenge ulimwengu wa udugu, mshikamano, na amani. Papa Fransisko aliyaweka haya bayana kupitia waraka wake Fratelli Tutti, akisisitiza kuwa dunia haiwezi kuwa bora bila kutambua kuwa sisi sote ni ndugu, bila kujali tofauti zetu za dini, rangi au utaifa. Huu ni msingi wa matumaini yanayojengwa katika ukweli na haki. Yohane anaoneshwa Yerusalemu mpya – mji mtakatifu usiohitaji jua wala mwezi, kwa kuwa utukufu wa Mungu ndio nuru yake. Huu ni mji wa matumaini, ambapo Mungu yuko katikati ya watu wake, hakuna huzuni tena, na kila kitu kimefanywa kipya. Katika Jubilei hii, Kanisa linakumbushwa kuwa tumaini letu si tumaini la kidunia tu, bali linaelekezwa kwa mji mpya wa milele. Licha ya giza la ulimwengu huu, mwanga wa Mungu bado unaangaza. Papa Fransisko aliwahi kusema: “Mungu hawezi kushindwa na giza la dunia hii. Daima mwanga wake unapenya hata gizani zaidi.” Alisisitiza kwamba hata katika changamoto za leo-vita, umasikini, kupoteza imani – bado Mungu anafanya kazi kuleta upyaisho. Yesu anawaambia wanafunzi wake: “Amani nawaachieni, amani yangu nawapa… Msifadhaike mioyoni mwenu.” Ni amani isiyotegemea hali ya nje, bali uwepo wa Mungu katika maisha yetu. Yesu pia anaahidi Roho Mtakatifu, Msaidizi atakayewafundisha na kuwakumbusha yote. Katika kipindi cha kukata tamaa na sintofahamu, ujumbe huu ni wa thamani sana. Roho Mtakatifu yupo pamoja nasi, na amani ya Kristo bado inapatikana. Hii ni roho ya Jubilei ya Matumaini. Baba Mtakatifu Francisko Francisko alikuwa mtangazaji mkubwa wa amani – alipinga vita mara kwa mara, na kutoa wito wa kutafuta suluhu ya amani kwa mazungumzo na upatanisho. Alisema: “Amani si ukosefu wa vita tu, bali ni kazi ya kila siku ya haki, huruma, na upendo.”
‘Huyo Msaidizi atawafundisha na kuwakumbusha yote niliyowaambia’… Kwa nini atufundishe? Je, yapo mambo ambayo Kristo alisahau? Hapana, Yesu alifundisha yote lakini hakuwa na nafasi ya kutuambia kwa kina mazingira yote na matokeo ya yale aliyotufundisha mintarafu safari ya Kanisa lake katika nyakati mpya, maendeleo ya mwanadamu kijamii, kiuchumi, kisiasa, kisayansi na kiteknolojia… daima kunazuka mambo mapya duniani na kuibuka maswali magumu… Injili ya Kristo ifafanuliwe kulingana na mazingira na majira na Mwalimu mkuu ndiye huyo Msaidizi, Roho wa Mungu… Kwa mfano Roho Mt. anatufundisha namna ya kuitumia Injili ya Kristo ili kuishi kwa amani na maelewano na watu wa imani nyingine na madhehebu mengine... anatufundisha namna ya kukaa na wakana Mungu, wasio na imani, wasioamini kwamba Mungu yupo na maisha baada ya kifo… anatufundisha namna ya kupanga watoto tunaoweza kuwalea ipasavyo bila kumkosea Mungu… anatufundisha tuwe na msimamo gani katikati ya mifumo kandamizi inayonufaisha wachache kiuchumi na kisiasa… anatufundisha tukaaje na jirani mkorofi au na mtu mwenye moyo mgumu, yule kaka/dada mwenye tabia na hulka ya peke yake kabisa… wenzetu wasiosikia, wasiojali wala kuguswa na lolote… Huyo msaidizi, yaani Roho wa Mungu atatufundisha tutumieje Injili ya Yesu katika mazingira ya namna hiyo. Kazi ya pili ya Msaidizi tuliyoambiwa leo na Yesu ni kukukumbusha... mwanadamu ni mwepesi kusahau… tunamfikiria Mungu na kutafakari vema tuwapo Kanisani, tukiisha kutoka mambo yote hubaki humo nasi kubaki walewale, huyo Msaidizi yupo ili kutukumbusha tunapojisahau…
Halafu anakumbusha umuhimu wa vikao na maamuzi ya pamoja (somo I, Mdo 15:1-2, 22-29), Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika hati juu ya Utume wa Walei namba 10 unasema “walei wazoee kufanya kazi Parokiani bega kwa bega na mapadre wao, kuieleza jumuiya ya Kanisa matatizo yao wenyewe na ya ulimwengu na masuala yanayohusu wokovu wa wanadamu, ili yachunguzwe na kutatuliwa kwa mchango wa wote” (Apostolicam Actuositatem 10)… ni lini jamii itajasirika kufungua macho ili kuuishi umoja na kushirikishana mipango, mali na vitu vingine kwa faida ya wote? Ni lini kutakuwa na haki msingi baina ya mwanamume na mwanamke? tajiri na fukara, mwalimu na mfanyabiashara, mganga na muhandisi, Padre na Sheikh… Roho wa Bwana, Msaidizi, anatukumbusha neno hili. Tunapozingatia fadhila ya haki tutafaidi na kufurahia paji la amani tunalopewa na Kristo katika Injili ya leo (Yn 14:23-29 amesema “amani nawaachieni, amani yangu nawapa”. Amani ya Kristo ni tofauti na ile tunayopewa na dunia, amani ya kidunia inatushawishi kuzikimbia changamoto ili kupata raha na starehe… amani ya Kristo ndio utulivu wa roho, wa akili, wa moyo, naam wa nafsi nzima. Mkristo ametulia tulii licha ya misiba, magonjwa, umasikini, uonevu sababu amani ya Kristo mfufuka imo ndani yake, amani inayothibitisha ushindi dhidi ya ulimwengu, dhidi ya shetani na malaika wake. Je mkristo wangu una amani?...
Jenga imani uipate amani yako. Amani atupayo Kristo hakuna awezaye kutunyang’anya, wala shetani, wala misiba, wala magonjwa, wala hatari ya wevi na wanyang’anyi… ni amani ya kweli isiyotegemea lolote kutoka nje yetu sababu chimbuko lake ni Mungu Baba katika Roho Mt kwa njia ya Kristo Bwana wetu… ni amani inayonururisha maisha ya waamini kwa nuru ya Mwanakondoo (somo II, Ufu 21:10-14, 22-23). Dominika hii inatufundisha kwamba matumaini ya Kikristo hayategemei hali za nje, bali yanajengwa kwa: Upendo unaomkaribisha Mungu, Amani ya Kristo isiyoyumbishwa na matatizo, Umoja wa Kanisa unaojengwa kwa hekima na huruma, Roho Mtakatifu anayetuongoza kila siku. Katika Jubilei hii ya Matumaini, tukimkumbuka hayati Papa Fransisko, tujitahidi kuishi urithi wake wa imani hai, huruma ya dhati, na kujitoa kwa ajili ya wanyonge. Tuwe mashhuhuda wa Mungu anayeishi kati yetu na kutufanya sisi kuwa mji mpya unaong’aa kwa mwanga wa tumaini. Tumpende Kristo, tulishike Neno lake, na halafu Baba atatupenda, atakuja kwetu na kufanya makao kwetu, na kutupatia uzima wa milele.