杏MAP导航

Tafuta

Upendo ni utimilifu wa sheria zote na ni kipimo cha matendo yote ya kibinadamu. Upendo ni utimilifu wa sheria zote na ni kipimo cha matendo yote ya kibinadamu.  

Tafakari Neno la Mungu Dominika ya Tano Ya Pasaka: Amri Mkuu

Kristo Yesu Msalabani ni kielelezo cha upendo usio na kikomo: Upendo kwa Mungu Baba na upendo kwa Jirani. Upendo ni utimilifu wa sheria zote na ni kipimo cha matendo yote ya kibinadamu. Sheria, amri na kanuni zote vinapaswa kutuelekeza kwenye upendo. Anayempenda Mungu anammiliki Mungu ndani yake, alisema Mt. Tomaso wa Akwino. Huu ni mwaliko kwa waamini kuwa ni vyombo vya huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake!

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican leo, Katika Dominika hii ya Tano ya Kipindi cha Pasaka, tunaendelea kujazwa na tumaini la Ufufuko. Hili ni tumaini si la kinadharia tu, bali linaonekana katika maisha ya kila sikukatika upya wa moyo, huduma, na upendo wa dhati. Kristo Yesu Msalabani ni kielelezo cha upendo usio na kikomo: Upendo kwa Mungu Baba na upendo kwa Jirani. Upendo ni utimilifu wa sheria zote na ni kipimo cha matendo yote ya kibinadamu. Sheria, amri na kanuni zote vinapaswa kutuelekeza kwenye upendo. Anayempenda Mungu anammiliki Mungu ndani yake, alisema Mt. Tomaso wa Akwino. Huu ni mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni vyombo vya huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka! Mwaka huu wa Jubilei ya Matumaini (2025) ni nafasi ya kipekee kwa waamini kuhuisha uhusiano wao na Mungu na jirani. Tunapotafakari masomo ya leo, tunaguswa pia na urithi wa Hayati Papa Francisko, aliyeishi Injili ya matumaini kwa maneno na matendo. Vijana wanao msemo ‘kupishana na gari ya mshahara’… ile unatoka tu mambo mazuri yanaibuliwa, kwamba ungevumilia walau dakika mbili tu zaidi mema yote yangekuwa yako, sasa huna wa kumlaumu, Mungu amekuwekea uwezekano wote lakini umeondoka kwa hiyari yako, umekosa kauvumilivu kadogo tu, nazo fursa zinawaangukia wenzako… Alianza kwa kupokea tonge la chakula kutoka kwa Bwana, tendo la upendo kabisa kwa mtu unayejua hila zake, halafu akaambiwa ‘Uyatendayo yatende upesi’ (13:27.)

Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa nchini Peru: Huduma
Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa nchini Peru: Huduma

Mtoto wa kiume wa Iskariote akajikusanya na kutokomea, alienda wapi huyu bwana mdogo? anajua mwenyewe, lakini alichokifuata kilifungua mchakato wa ukombozi hatua kwa hatua kadiri ya maandiko.. laiti angetubu baadaye! laiti angeiamini na kuitumainia huruma ya Mungu! laiti asingeutoa uhai wake kwa kujinyonga! aliishi na Bwana miaka 3 akimsikia na kumuona anavyopenda na anavyosamehe kwa nini alikata tamaa? Yuda mwana wa Simoni Iskariote. ‘Yuda alipokwisha kutoka’ maneno ya neema yalianza kutoka kinywani mwa Bwana, ni kama alisubiriwa aondoke ndipo Kristo aufunue utukufu wake na kuonyesha namna Mungu Baba anavyotukuzwa ndani ya Mwana. Utukufu wa Mungu na ukombozi wa wanadamu ndilo lengo la uandishi wa Biblia Takatifu, ndilo lengo la ujio wa Kristo, aliyatimiza yote kwa utii kamili ili mapenzi ya Baba yake yatimie na halafu Baba atukuzwe na Mwana katika Roho Mt… Mungu ametukuzwa katika kuzaliwa kwake, utume wake, kifo chake, kufufuka na kupaa kwake mbinguni… nidhamu yake, nguvu zake na hekima yake, hakika amefanya yote vema… tuuone utukufu wa Mungu katika kila hatua ya maisha yetu, katika yote tunayoyapitia, mazuri na changamoto pia, tusijitukuze wenyewe, tusisifu na kuabudu wakubwa, Mungu pekee anastahili… sisi tuheshimiane na kupendana, inatosha! Katika somo la kwanza Paulo na Barnaba wanawatia moyo waamini kwa kusema: “Imetupasa kuingia katika Ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.”Hii ni changamoto kwa ulimwengu unaotafuta mafanikio ya haraka bila uvumilivu. Maisha ya Kikristo yanahitaji ujasiri na uvumilivu. Katika Jubilei hii, tunakumbushwa kwamba matumaini ya kweli hayaepuki mateso, bali yanayapokea kwa imani. Hayati Papa Fransisko aliwahi kusema: “Mateso si mwisho, bali daraja la kuelekea tumaini.” Maisha yake yalikuwa ya ushuhuda huu-alipozungumzia wahamiaji, maskini, mazingira, na waliotengwa, alisimama na waliteseka, si kama msikilizaji tu, bali kama ndugu na shuhuda wa upendo wa kweli wa Kristo na mchungaji wa mfano wa Kristo Yesu.

Amri kuu: Upendo kwa Mungu na Jirani
Amri kuu: Upendo kwa Mungu na Jirani   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

UFAFANUZI: Bwana ni mwenye rehema, mwingi fadhili (zaburi 145), Zaburi hii inatufundisha kuhusu tabia ya Mungu: anatenda kwa rehema, huruma, na wema kwa wote. Hii ni picha ya Mungu tunayemwamini-Mungu wa matumaini. Katika dunia iliyojaa hukumu, mashindano, na majeraha, Mungu wetu anatufundisha uvumilivu na wema. Papa Fransisko alisisitiza sana sura hii ya Mungu. Katika maandiko na hotuba zake, aliendelea kutangaza: “Jina la Mungu ni Huruma.” Ndiyo sababu alifungua Milango ya Huruma mwaka 2016, akisisitiza kuwa kila mtu anaweza kurejea kwa Baba mwenye huruma. ‘Yuda alipokwisha kutoka’ kwenda kwenye giza la nje alipoteza fursa muhimu ya kusikia maneno ya utukufu, akakosa maagano ya baraka “bado kitambo kidogo nipo pamoja nanyi…” (13:33) na agizo muhimu la upendano lililo msingi wa utume uliowangojea baadaye… mimi na wewe pia tunatokatoka sana, tunarudishwa ndani kwa kusamehewa tunatoka tena, sijui tukoje!! Mkristo huwa unatoka kwenda wapi? kwa nani, kufanya nini, saa hizo mbaya za usiku, saa za Iskariote.. wakati mwingine kwa gharama kubwa ya fedha, muda, ajali, ugomvi nk lakini tunatoka tu, huenda kwa ajili ya vitu vya kupita, starehe, raha na faida ya kimwili, ya kidunia kwa majuto ya daima. Mwenzetu alitoka akaenda kumsaliti Bwana wake, mara si haba tumefuata nyayo za mtoto huyu wa Simoni Iskariote tukimuuza Kristo kwa senti chache kwa kusaliti amri yake iliyo mpya nyakati zote “Amri mpya nawapa, mpendane kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo (13:34)… ni katika upendo wa kiagape tunafaulu kuuingia mlango wa imani tuliofunguliwa mataifa yote na Mungu (somo I – Mdo 14:21b-27.

Chakula kwa maskini: kielelezo cha upendo wa dhati
Chakula kwa maskini: kielelezo cha upendo wa dhati   (Vatican Media)

Somo la Pili – Ufu 21:1-5a)…Hili ni mojawapo ya masomo yenye nguvu ya matumaini katika Biblia. Yohane anaona mbingu mpya na dunia mpya, na Mungu akisema: “Tazama, naya fanya mambo yote kuwa mapya.”Ni ahadi ya upyaisho wa maisha yetu, jamii zetu, na ulimwengu. Katika Jubilei hii, Kanisa linatambua kwamba Injili ina nguvu ya kuponya ulimwengu uliovunjika. Papa Francisko, kwa waraka kama Laudato Si' na Fratelli Tutti, alihimiza upyaisho wa dunia kwa msingi wa udugu, mshikamano, na ulinzi wa mazingira. Alisema: “Hatuhitaji dunia mpya, bali mioyo mipya inayoweza kuitazama dunia kwa jicho la huruma.” Kwa njia ya pendo tutaona mbingu mpya na nchi mpya, tutabarizi katika mitaa ya jiji la Yerusalemu mpya, Mungu atafuta kila chozi machoni petu, mauti haitakuwapo tena, wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu… yote yatafanywa upya Ikiwa mambo ndio kama hivi basi tusitoke nje kama Yuda, tutulie, tupendane, upendo watosha, acha huo utawale! Ni upendo wenye kigezo… si tu kusema tunapendana halafu basi, au kuwapenda ndugu zetu tu, kuipenda miili yetu tu, kuwapenda wakubwa, matajiri na wenye uwezo na kuwadharau masikini, sio upendo wa faida, ule wa nipe nikupe… Kigezo cha upendo amekiweka Kristo mwenyewe “… kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo” (13:34). Yesu anatupatia amri mpya ya upendo: “Pendane kama nilivyowapenda ninyi.” Huu ni msingi wa maisha ya Kikristo. Si upendo wa kawaida wa urafiki au hisia, bali wa kujitoa, kusamehe, kuvumilia, na kutumika kwa wengine. Katika ulimwengu uliojaa chuki, upendeleo, na ubinafsi, Yesu anatupatia njia mpya ya kuishi - njia ya upendo hai.

Maskini wakijipanga kutafuta chakula
Maskini wakijipanga kutafuta chakula   (ANSA)

Papa Francisko alikuwa mfano hai wa upendo huu. Alipenda kwa vitendo: aliosha miguu ya wafungwa, aliwahudumia wahamiaji, aliwatembelea wagonjwa. Alisema: “Upendo wa kweli huacha alama, hujinyima, hujitoa bila kutafuta faida.” Katika Jubilei ya Matumaini, tunaitwa kufanya hivyo-kuwa mashahidi wa upendo unaofufua matumaini... hivi tunapaswa kupenda kwa viwango vya Kristo mwenyewe, kiwango cha kuutoa uhai kwa ajili ya mwingine, neno hili ni gumu ila hakuna namna nyingine, ni amri ya Mungu, vinginevyo tuache kuwa wakristo. ‘Yuda alipokwisha kutoka…’ sisi tumekubaliana tusitoke ili tuudhihirishe utukufu wa Mungu kwa pendo lililo kamili… tumpende jirani sababu ameumbwa na Mungu, ana sura na mfano wake, upendo ndio fadhila kuu kuliko zote, Mungu ni Upendo wenyewe… tupende kwa kuwaziana mema, kutakiana matashi mazuri, kwa kubariki na kuombea na zaidi sana kwa matendo ya umoja, undugu na msamaha. Ni mwezi Mei, mwezi wa Mama Bikira tumpe Mungu utukufu na shukrani kwa zawadi ya Pasaka ya Kristo na yetu… tuombe maombezi ya Malkia huyu wa mbingu kwa ajili ya hali njema ya wote. Tusali Rozari (Rose – waridi, Rosarium – bustani ya mawaridi)… Mkristo usitoke kama Yuda Iskariote, usipende nusunusu, chuma mawaridi katika Rozari takatifu yaani katika bustani ya Mungu upate kujipamba kwa maua ya sala, matumaini na upendo,  naye Kristo nuru ya maisha yetu, neno letu la uzima, mkate wetu utokao mbinguni atatujalia Roho wake, alleluia! Dominika hii inatufundisha kuwa Pasaka si tukio la kihistoria tu, bali ni mwaliko wa maisha mapya yenye msingi wa: Uvumilivu katika mateso, Kumtegemea Mungu mwenye huruma, kuamini katika uwezo wa Mungu kufanya upya maisha yetu, kuishi upendo wa kweli unaowatambua wengine kama ndugu. Katika mwaka huu wa Jubilei ya Matumaini, tukimkumbuka hayati Papa Francisko, tujitahidi kufanikisha yale aliyoamini: Kanisa la huruma, dunia ya haki na amani, Na waamini walio hai katika upendo.

Liturujia D5 Mwaka C

 

 

17 Mei 2025, 14:23