杏MAP导航

Tafuta

Kristo Yesu Msalabani ni kielelezo cha upendo usio na kikomo: Upendo kwa Mungu Baba na upendo kwa Jirani. Kristo Yesu Msalabani ni kielelezo cha upendo usio na kikomo: Upendo kwa Mungu Baba na upendo kwa Jirani.   (2021 Getty Images)

Tafakari Dominika Ya Tano Ya Pasaka: Upendo Nguvu ya Ushuhuda!

Yesu alidhihirisha amri hii katika maisha na utume wake, mpaka kufa Msalabani, akishuhudia ni kwa jinsi gani Mungu kwa mapendo makuu aliupenda ulimwengu. Mitume mara baada ya Pentekoste, wanapokea nguvu ya Roho Mtakatifu, wanayakumbuka na kuyaishi mafundisho ya Yesu mintarafu amri kuu ya mapendo. Kwa njia ya Roho Mtakatifu wanaishuhudia Injili, kwa maisha yao, kwa kufundisha, kwa kubatiza, kwa kuwasaidia maskini, na kwa kuvumilia katika magumu.

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Jumapili ya 5 ya Pasaka mwaka C wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii ya tano ya Pasaka yatutafakarisha juu ya, “Amri kuu ya mapendo, nguvu ya ushuhuda na maisha mapya” Bwana wetu Yesu Kristo katika karamu ya mwisho aliwaaga wanafunzi wake, akiwaachia amri kuu ya mapendo (Yn 13:31-33a, 34-35). Kristo Yesu Msalabani ni kielelezo cha upendo usio na kikomo: Upendo kwa Mungu Baba na upendo kwa Jirani. Upendo ni utimilifu wa sheria zote na ni kipimo cha matendo yote ya kibinadamu. Sheria, amri na kanuni zote vinapaswa kutuelekeza kwenye upendo. Anayempenda Mungu anammiliki Mungu ndani yake, alisema Mt. Tomaso wa Akwino. Huu ni mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni vyombo vya huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka! Kristo Yesu alidhihirisha amri hii katika maisha na utume wake, mpaka kufa Msalabani, akishuhudia ni kwa jinsi gani Mungu kwa mapendo makuu aliupenda ulimwengu.  Mitume wa Yesu mara baada ya Pentekoste, wanapokea nguvu ya Roho Mtakatifu, wanayakumbuka na kuyaishi mafundisho ya Yesu mintarafu amri kuu ya mapendo. Kwa njia ya Roho Mtakatifu wanaishuhudia Injili, kwa mfano wa maisha yao, kwa kufundisha, kwa kubatiza, kwa kuwasaidia maskini, na kwa kuvumilia katika magumu na mateso yote ambayo walikutana nayo (Mdo 14:21b-27). Mitume wanatufundisha kuwa ni katika kuvumilia mateso, adha, masumbuko na kifo ndipo tutaupata uzima mpya, tutatawala pamoja na Kristo katika Yerusalemu mpya yaani mbinguni katika uzima wa milele. Shida na mateso ni vya muda na vitapita nasi tutapokea tuzo ya ushindi katika uzima wa milele (Ufu 21:1-2a). Katika Dominika ya tano ya Pasaka, tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha mapya tunayoshirikishwa kwa njia ya Ubatizo wetu. Kwa njia ya Roho Mtakatifu tunapata nguvu ya kuishi maisha ya ushuhuda, tukisukumwa na mapendo ya kweli kwa Mungu yanayotusaidia kuishi upendo wa kweli kwa ndugu na Jirani zetu. Tuombe neema ya kuiishi na kuishuhudia Imani yetu kikamilifu, kwa kuvumilia katika mateso na magumu katika njia yetu ya msalaba tukiwa na tumaini na kuingia katika Yerusalemu yetu mpya yaani mbinguni, ambapo Kristo atayafanya yote kuwa mapya.

Upendo ni nguvu ya ushuhuda na maisha mapya
Upendo ni nguvu ya ushuhuda na maisha mapya   (AFP or licensors)

Somo la Injili: Ni Injili ya Yn 13:31-33a, 34-35. Somo la Injili Takatifu linatoka katika sehemu ya pili ya Injili ya Yohane inayoanzia sura ya 13-21 ijulikanayo kama Kitabu cha Utukufu (The Book of Glory). Mazingira ya Injili hii ni katika Karamu ya mwisho ambapo Yesu anatoa hotuba ndefu takribani sura nne, kuanzia sura ya 13:1-17:26 (farewell discourse) akiwaaga wanafunzi wake kabla ya kuingia katika mateso na kifo chake. Sehemu hii ya Injili ya leo imegawanyika katika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ya Injili hii (Yn 13:31-33a) yafuata baada ya Yuda Iskarioti kuondoka kutoka chakulani (Yn 13:30), aya inayofuta, Yn 13:31, Kristo anazungumza juu ya mateso na kifo chake kama utukufu (suffering and death as Glorification) ambapo Mungu atamtukuza Mwana na naye Mwana atamtukuza Mungu ndani yake. Mwinjili Yohane anasisitiza zaidi mateso na kifo cha Kristo kama Mwanzo wa kuinuliwa kwake katika utukufu, hali kadhalika anamtukuza Baba kwa kuwa kwa mapendo makuu alikubali mateso na kifo ili atimize mapenzi ya Baba kwa ajili ya ukombozi wa wanadamu. Sehemu ya pili ya Injili hii (Yn 13:34-35), Yesu anawapa Mitume wake Amri kuu ya mapendo (the great commandment of love), kwamba walipaswa kupendana wao kwa wao kama vile Kristo mwenyewe alivyowapenda upeo. Upendo ulipaswa kuwa ushuhuda wa maisha na utume wa Mitume. Baada ya Pentekoste Mitume wanapata nguvu ya kumshuhudia Kristo mfufuka kwa maisha na utume wao. Walijulikana na kuwavuta wengi kuwa wafuasi kwa namna walivyoishika na kuiishi amri hii ya mapendo.

Mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili
Mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili

Katika somo hili la Injili Dominika ya leo tuna mafundisho mawili ya kujifunza. Kwanza: Maana ya Mateso kwetu Wakristo (Christian concept of suffering). Katika sehemu ya kwanza ya Injili ya leo, Kristo anazungumza juu ya mateso na kifo chake kama utukufu (suffering and death as Glorification) ambapo Mungu atamtukuza Mwana na naye Mwana atamtukuza Mungu ndani yake. Mwinjili Yohane anasisitiza zaidi mateso na kifo cha Kristo kama Mwanzo wa kuinuliwa kwake katika utukufu, hali kadhalika anamtukuza Baba kwa kuwa kwa mapendo makuu alikubali mateso na kifo ili atimize mapenzi ya Baba kwa ajili ya ukombozi wa wanadamu. Kumbe mateso na kifo kwetu sisi wakristo sio mwisho wa maisha bali ndio namna yetu ya kuinuliwa kwenda kwenya maisha mapya ya utukufu wa milele pamoja na Kristo. Ndugu wapendwa, katika maisha yetu sisi tunapita katika mateso, kila mmoja wetu aweza kueleza uzoefu (experience) yake katika nyakati fulani za mateso na changamoto. Yaweza kuwa changamoto za muda mrefu za afya, yaweza kuwa matatizo ya kifamilia, yaweza kuwa kukosa ajira, dhiki, usaliti, manyanyaso, kudhaniwa vibaya, misiba, ajali, msongo wa Mawazo, hasara katika biashara, kufeli katika mipango yetu mbalimbali na mateso mengine mengi. Haya yote ndio msalaba wangu na wako, ndiyo njia yetu kuelekea utukufu na uzima wa milele. Katika hayo yote tunaalikwa kuyaunganisha mateso yetu na mateso ya Kristo, kuunganisha misalaba yetu na msalaba wa Kristo, ndipo twaweza kuyabeba hayo yote kwa jicho na mtazamo wa kiimani kwamba, hayo ni ya kupita na kwamba kama Kristo alishinda, nasi pia tutashinda. Ndugu mpendwa usijisikie mnyonge pale unapopitia mateso na magumu, bali tuyahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu (Rom 8:18).

Roho Mtakatifu ni chemchemi ya upendo na maisha mapya katika Kristo
Roho Mtakatifu ni chemchemi ya upendo na maisha mapya katika Kristo

Pili: Kristo Yesu anatupa amri mpya kuu ya mapendo (The great commandment of Love). Sehemu ya pili ya Injili ya leo Kristo anatufundisha juu ya Amri kuu ya Mapendo. Ni kwa sababu ya Upendo, Kristo alikubali na kutii mapenzi ya Baba na kutwaa mwili na kukaa kati yetu (Yn 1:14). Kwa maisha na utume wa Kristo alipokuwa angali na wanafunzi wake alilithibitisha hilo, aliwahurumia wenye shida, aliwafariji na kuwaponya wagonjwa, alifufua wafu na matendo mengine mengi. Katika karamu hii ya mwisho anawapa amri mpya wanafunzi wake, amri ya mapendo iliyo amri kuu kuliko zote, upendo kwa Mungu na upendo kwa jirani. Chimbuko au msingi wa amri hii ni Agano la Kale katika kitabu cha Mambo ya Walawi 19:18, ambapo Mwenyezi Mungu mwenyewe anasema, “Usifanye kisasi wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali mpende Jirani yako kama nafsi yako…” Kristo anajengea katika uelewa wa amri ya mapendo iliyojulikana tayari katika sheria ya Musa, lakini anaongeza, “Amri mpya nawapa, mpendane kama nilivyowapenda mimi” (Yn 13:34). Je, Kristo anatutaka tupende kwa namna gani? Amri kuu ya mapendo yapaswa kuwa mtindo wetu mpya wa maisha baada ya ufufuko. Yatualika kuiishi injili kwa matendo. Upendo unatudai kuona na kuguswa na mahitaji ya wengine: Kristo aliona na aliguswa na hitaji ya kutukomboa sisi wanadamu tuliokuwa hapo mwanzo tumekufa kwa sababu ya dhambi. Akatii mapenzi ya Baba na akaja kutupatanisha tena na Mungu. Licha ya hayo Kristo aliona na kuguswa na shida za watu mbalimbali aliokutana nao na aliwasaidia.

Roho Mtakatifu ni chimbuko la upendo na ushuhuda wa maisha
Roho Mtakatifu ni chimbuko la upendo na ushuhuda wa maisha   (ANSA)

Sisi tunaalikwa kuona na kuguswa na shida na mahangaiko ya ndugu zetu. Wapo kati yetu watu wengi wanaoteseka kwa njaa, wajane, yatima, wazee, walemavu, watoto wa mitaani nk. Tukisema tunampenda Kristo twapaswa kufungua macho yetu na kutazama mahitaji ya wenzetu kama Kristo alivyofanya. Tusikae kimya kwa shida za wenzetu. Hata neno la Faraja laweza kumtoa mtu katika hali moja na kumvusha Daraja kwenda hali nyingine. Upendo unatudai kuvumiliana na kupokeana katika madhaifu yetu: Kristo licha ya kuwa ni Mungu alikubali kukaa kati yetu sisi wadhambi. Alitwaa hali yetu ya kibinadamu isipokuwa dhambi ili atushirikishe sisi Umungu wake. Katika familia zetu, katika ndoa, katika jumuiya zetu tunapaswa kupokeana na kuchukuliana kwa upendo na upole. Sisi sote tu dhaifu na mara kadhaa udhaifu wetu unadhihirika katika mahusiano yetu ya kila siku. Je, tunapokeana kwa upendo na kurekebishana kwa upole pale tunapokoseana? Amri ya mapendo yatudai kuvumiliana katika tofauti zetu na kupokeana kama vile Kristo anavyotupokea sisi kila siku licha ya dhambi na udhaifu wetu bado anatuvumilia na kutupa nafasi ya kuanza upya. Upendo unatudai kusahemeheana: Kristo kwa mapendo makubwa alikuja kati yetu ili kutupatanisha tena sisi na Baba wa milele. Kwa njia yake, Mwenyezi Mungu ametusamehe hatia ya kosa la wazazi wetu wa kwanza. Maisha ya Pasaka yatudai kuishi msahama wa kweli. Kristo katika kutimiza mapenzi ya Baba, alisalitiwa, alitemewa mate, alidhihakiwa, alidhalilishwa. Jibu la Yesu lilikuwa, Baba uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo (Lk 23:34). Je, nimefungua moyo wangu kuwasamehe wale wote walionikosea? Je, nipo tayari kusukumwa na upendo kuomba msamaha pale ninapowakwaza na kuwakosea wengine?  Upendo unatudai unyenyekevu katika kutumikiana. Kristo alikuwa mnyenyekevu. Katika karamu hii ya mwisho aliwaonesha kwa mfano wanafunzi wake nini maana ya upendo. Aliwaosha miguu wanafunzi wake ishara ya udogo na unyenyekevu. Upendo unatudai kuwa wanyekevu. Kuwa tayari kujishusha kwa ajili ya faida kwanza ya wengine. Mara nyingi katika maisha tunatazama faida zetu sisi kuliko wengine.

Upendo ni nguvu ya ushuhuda na maisha mapya
Upendo ni nguvu ya ushuhuda na maisha mapya   (@Vatican Media)

Kama viongozi katika familia, katika Kanisa, katika serikali, katika jamii tunakumbushwa kuwa tayari kujishusha kwa ajili ya huduma ya upendo kwa wengine. Mara kadhaa madaraka, fedha, mali vinatufunga macho tunajawa na kiburi na majivuno na kusahau kuwa ni Mungu ameutazima hayo yote kwa muda tu ili kuwasadie wengine kwa niaba yake, na kwamba vyote hivyo vitapita kwa kuwa sisi hapa duniani tu wasafiri. Upendo unatudai utii katika kutimiza mapenzi ya Baba. Kristo alitupenda, akawa mtii katika kutimiza mapenzi ya Baba hata mauti ya msalaba. Maisha ya pasaka ni maisha ya utii katika kushika na kuziishi kiaminifu amri za Mungu. Kwa njia ya Ubatizo wetu sisi pia tunashirikishwa maisha mapya. Kumbe wongofu wetu ni tunda la upendo na utii wa Kristo katika kutii mapenzi ya Baba wa milele. Je, nina utii kiasi gani kwa amri na mapenzi ya Mungu? Ninapokea kwa moyo na imani mapenzi ya Mungu katika maisha yangu hata pale yanapokuwa magumu kueleweka? Tumwombe Kristo atupe nguvu ya kuwa watii kama yeye alivyokuwa mtii hata kifo cha Msalaba.

Kristo Yesu alikuwa Mtii hadi kifo Msalabani
Kristo Yesu alikuwa Mtii hadi kifo Msalabani   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Somo la 1: Ni kitabu cha Matendo ya Mitume Mdo 14:21b-27. Katika kitabu cha Matendo ya Mitume, Mwinjili Luka anatueleza maisha na utume wa Mitume wa Yesu baada ya Pentekoste. Kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, Injili Ilianza kuenea kutoka Yerusalemu hadi miisho ya dunia. Mitume kwa njia ya Roho Mtakatifu wakawa mashahidi wa Injili ya Kristo hadi miisho ya dunia (Mdo 1:8). Ni kwa nguvu hiyo ya Mungu, Paulo na Barnaba walimhubiri Kristo katika safari mbalimbali za kimisionari. Sura hii ya 14, Paulo na Barnaba wapo katika safari yao ya kwanza ya kimisionari ambapo walihubiri huko Asia ndogo (nchi ya uturuki ya sasa). Huko walifundisha, walibatiza na kuanzisha jumuiya za wakristo pamoja na viongozi wa jumuiya hizo waliozoanzisha. Safari hii haikua rahisi, waliteseka, walipigwa kwa mawe na mateso mengine mengi. Somo hili ni Hitimisho la safari yao ya kwanza na wanarejea Antiokia kutoa ripoti ya utume wao kwa Mitume waliowatuma. Katika yote walimtangaza Kristo bila kuchoka. Ndugu zangu katika somo hili la kwanza tuna mambo matatu ya kujifunza. Kwanza: Mitume wanaanzisha maisha mapya kwa watu wa mataifa kwa njia ya utume na umisionari. Mitume Paulo la Barnaba, kwa nguvu ya Mungu mwenyewe walihubiri Injili katika Asia ndogo na huko walipata wakristo wengi. Waliwaimarisha wakristo hawa na wakaanzisha jumuiya mpya za wakristo. Wengi walikua wapagani wakapokea Habari Njema ya Injili na wakamwamini Kristo. Jumuiya hizi zilikua na kuwa makanisa katika sehemu zote walizofanya umisionari. Ndugu wapendwa, mimi na wewe tumepokea habari Njema ya Injili. Tumeacha maisha ya kale na kuanza maisha mapya. Ubatizo umetuondolea maisha ya kale, tunavua utu wetu wa kale na si tunavaa utu mpya (2 Kor 4:16). Injili ya Kristo inahubiriwa kwetu kila siku. Yesu anasema nasi kila siku katika Neno lake, neno linaloendelea kutuunda na kutubadilisha katika hali zetu mbalimbali. Neno la Kristo linatuinua, Neno la Kristo linatubariki, Neno la Kristo linasema na mioyo yetu, linatufariji, linatuinua, linaturekebisha, linapenya ndani kabisa ya mioyo yetu. Neno la Mungu linatupa nguvu ya kuendelea kuamini. Sisi kila mmoja wetu ni mmisionari, kwa njia ya maneno na matendo yetu, tumtangaze Kristo mfufuka. Utume na maisha yetu yawe ushuhuda wa Injili ya Kristo. Maisha yetu yaendane na Injili tunayoihubiri kila siku kwa wengine, watu waguswe kwa namna tunavyopendana sisi kwa sisi. Watu waguswe kwa namna tunavyogushwa na shida za wengine, Kristo aadhimishwe kila siku katika maisha yetu.

Upendo ni nguvu ya ushuhuda wa maisha mapya
Upendo ni nguvu ya ushuhuda wa maisha mapya   (ANSA)

Pili: Mateso ni sehemu ya safari yetu ya maisha. Mitume Paulo na Barnaba walijerejea mpaka Listra na Ikonio na Antiokia, wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile Imani na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi. Mitume Paulo na Barnaba, walipitia katika magumu lakini kwa kuwa walikuwa na nguvu ya Mungu ndani mwao walitambua kuwa hio ndio njia yetu katika kuutafuta uzima wa milele. Ndugu wapendwa, Mitume wa Yesu tukumbuke kuwa hapo Mwanzo walikuwa na hofu, walikuwa na mashaka lakini wakiisha kupokea nguvu ya Roho Mtakatifu walikuwa tayari kushiriki mateso pamoja na Yesu. Walikua na mtazamo mpya kuhus ufuasi wao kwa Kristo, hawakuogopa mateso, hawakuogopa maumivu, hawakuogopa madhulumu wala kifo. Wengi walikufa kifo dini kwa ajili ya Injili ya Kristo. Sisi kwa njia ya Ubatizo na Kipaimara tumempokea Roho Mtakatifu, tumeimarishwa ili tutambue kuwa hakuna njia rahisi katika kumfuasa Kristo. Roho Mtakatifu anatupa nguvu ya kuvumilia katika ufuasi wetu kwa Kristo kila mmoja Kadiri ya wito ambao Mungu amemwitia. Hakuna wito rahisi, hakuna ufuasi lelemama. Kristo anatupa nguvu kwa njia ya Ekaristi Takatifu, anakaa ndani mwetu, anatuimarisha katika Imani, matumaini na mapendo ili tuendelee kumshuhudia hata katikati ya mateso na maumivu.

Upendo ni nguvu ya uinjilishaji mpya: Ushuhuda
Upendo ni nguvu ya uinjilishaji mpya: Ushuhuda   (@Vatican Media)

Tatu: Kwa njia Mitume Kanisa linapanuka na kuwapokea wote. Kwa njia ya Mitume, Kanisa linafungua milango kwa watu wa mataifa. Kristo alivyowatokea mitume katika bahari ya Tiberia, alifanya muujiza kwa mitume wake ambapo walipata samaki wengi, ishara ya ufanisi wa kazi ya mitume ya kuhubiri Injili baada ya Pentekoste. Kanisa limefungua milango kuwapokea wote. Ndugu wapendwa, sisi tupo ndani ya kanisa. Kama mama Kanisa mtakatifu kwa njia ya mitume anavyowapokea watu wote, mimi wewe tulio ndani ya kanisa, tumefungua mioyo yetu kuwapokea watu wote? Utume wangu unawakusanya na kuwaunganisha watu wote au ninawabagua kutokana na kipato, utajiri na mali? Je, ninashiriki katika kuwasaidia wengine kuingika katika kanisa la Kristo? Ninafanya jitihada kuwarudisha kundini wale waliokata tamaa na kuikana imani yao au wale waliorudi nyuma na kuwa waregevu? Yazi ya umisionari inaanza na mimi, ni kazi yetu sote tuliobatizwa.

Upendo ni nguvu ya ushuhuda na mwanzo wa maisha mapya
Upendo ni nguvu ya ushuhuda na mwanzo wa maisha mapya   (@Vatican Media)

Somo la Pili: Ni kitabu cha Ufunuo wa Yohane 21:1-5a. Mwandishi wa Kitabu hiki, Mtume Yohane, aliwaandikia Wakristo waliokuwa wakiteseka katika kisiwa cha Patmos katika Asia ndogo, ili kuwapa moyo na kuwaimarisha Imani yao katika nyakati ngumu utumwa na mateso kutoka kwa watawala wa Kirumi. Somo hili la leo ni sehemu ya mwisho ya kitabu hiki cha ufunuo wa Yohane. Anatueleza matokeo baada ya hukumu ya mwisho ya kwamba taabu zote zitakwisha na viumbe vyote vitafanywa upya. Yerusalemu mpya ni mfano wa ufalme huo mpya wa Kristo ambamo watakatifu wataishi milele pamoja na Mungu. Somo hili latupa moyo kwamba, mateso na magumu ya wakati wa sasa ni ya kupita tu. Hakuna hali inayodumu katika maisha haya yanayopita. Kristo ametuandalia makao mapya, Yerusalemu mpya. Anatuhakikishia kuwa yupo nasi katika nyakati zote, maskani ya Mngu ni pamoja na wanadamu. Ninakuombea ndugu mpendwa, katika Dominika hii ya tano, Kristo aendelee kuweka maskani yake ndani ya moyo wako, kwa njia ya Neno lake na Sakramenti zake. Akafute kila chozi katika macho yako, nyakati ambazo tunapita katika magumu na changamoto mbalimbali katika maisha yetu. Akaanzishe zama mpya ndani mwetu, akatupe moyo nyakati za vilio na maombolezo, nyakati za maumivu. Pasaka yatukumbusha kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita. Ndugu mpendwa, Kristo akafanye yote kuwa mapya kabisa ndani mwako leo na hata milele, amina. Hitimisho: Katika Dominika hii ya tano ya Pasaka, tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha mapya tunayoshirikishwa kwa njia ya Ubatizo wetu. Kwa njia ya Roho Mtakatifu tunapata nguvu ya kuishi maisha ya ushuhuda, tukisukumwa na mapendo ya kweli kwa Mungu yanayotusaidia kuishi upendo wa kweli kwa ndugu na Jirani zetu. Tuombe neema ya kuiishi na kuishuhudia Imani yetu kikamilifu, kwa kuvumilia katika mateso na magumu katika njia yetu ya msalaba tukiwa na tumaini na kuingia katika Yerusalemu yetu mpya yaani mbinguni, ambapo Kristo atayafanya yote kuwa mapya.

D5 Ya Pasaka
17 Mei 2025, 15:51