杏MAP导航

Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Domika ya Sita ya Kipindi cha Pasaka Mwaka C: Ushuhuda wa Injili kwa watu wa Mataifa; Zawadi ya imani inayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa watu wa Mungu Tafakari ya Neno la Mungu Domika ya Sita ya Kipindi cha Pasaka Mwaka C: Ushuhuda wa Injili kwa watu wa Mataifa; Zawadi ya imani inayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa watu wa Mungu 

Tafakari Dominika VI ya Pasaka Mwaka C: Ushuhuda, Upendo na Amani

Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii ya sita ya Kipindi cha Pasaka yatutafakarisha kuwa “Roho Mtakatifu anatusaidia kumshuhudia Kristo Yesu” Bwana wetu Yesu Kristo katika karamu ya mwisho, aliwapa Mitume wake amri kuu ya mapendo. Anawaahidia kuwa wataweza kuiishi amri hii ya mapendo katika ukamilifu wake watakapompokea Roho Mtakatifu. Hapo watayakumbuka, kuyaishi na kuyafundisha yale yote waliyoyaona na kuyasikika kutoka kwa Kristo Yesu

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi. Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya Sita ya Kipindi cha Pasaka, Mwaka C wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii ya sita ya Pasaka yatutafakarisha kuwa “Roho Mtakatifu anatusaidia kumshuhudia Kristo Yesu” Bwana wetu Yesu Kristo katika karamu ya mwisho, aliwapa Mitume wake amri kuu ya mapendo. Anawaahidia kuwa wataweza kuiishi amri hii ya mapendo katika ukamilifu wake watakapompokea Roho Mtakatifu. Hapo watayakumbuka, kuyaishi na kuyafundisha yale yote waliyoyaona na kuyasikika kutoka kwa Kristo. Ni mara baada ya Pentekoste, mitume walipoanza kwa nguvu, kuiishi na kuifundisha Injili, kumshuhudia Kristo Mfufuka kwa watu wa mataifa yote. Kwa njia ya Mitume, milango inafunguliwa kwa watu wa mataifa nao wanaipokea Injili ya Kristo bila vikwazo. Roho Mtakatifu aliwasaida kufanya maamuzi sahihi kuhusu mustakabali wa kanisa changa lilioanza kusambaa hata kwa wa watu wa mataifa. Hii ni ishara ya upendo uliofumbatwa katika utume usio na mipaka. Mpango wa Mungu wa ukombozi ni kwamba sisi sote turejee kwake mbinguni yalipo makao yetu ya kudumu, Yerusalemu yetu mpya. Ni kwa njia ya Mama kanisa ambalo limejengeka juu ya misingi ya Mitume, sisi sote watu wa kila kabila, lugha, jamaa na taifa tunasafiri kuelekea uzima wa milele. Tunaalikwa kuwa hekalu hai la Mungu, kwa kuiishi amri kuu ya mapendo kiaminifu, kumtambulisha Kristo kwa watu wote kwa njia ya maneno na Matendo yetu.

Ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili ni kazi ya Roho Mtakatifu
Ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili ni kazi ya Roho Mtakatifu   (@Vatican Media)

Somo la Injili: Ni Injili ya Yn 14:23-29. Somo la Injili Takatifu linatoka katika sehemu ya pili ya Injili ya Yohane inayoanzia Sura ya 13-21 ijulikanayo kama Kitabu cha Utukufu (The Book of Glory). Mazingira ya Injili hii ni katika Karamu ya mwisho ambapo Yesu anatoa hotuba ndefu takribani sura nne, kuanzia sura ya 13:1-17:26 (farewell discourse) akiwaaga wanafunzi wake kabla ya kuingia katika mateso na kifo chake. Dominika iliyopita Kristo aliwapa wanafunzi wake Amri kuu ya Mapendo, na katika sehemu ya Injili ya leo Kristo anaendelea na fundisho hilo. Anawafundisha kuwa yeyote ampendaye Yesu kwa moyo wote ataweza kuishika amri yake kuu ya mapendo na kwa njia hiyo, moyo wake utajazwa na furaha itokayo kwa Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu, anaposema, “Nasi tutakuja kwake na kufanya makao kwake.” Mitume kwa nguvu yao hawakuyaweza hayo. Kristo anawaahidi Mitume wake zawadi ya Roho Mtakatifu. Ni dhahiri kuwa Mitume bila nguvu ya Roho Mtakatifu wasingeweza kuyakumbuka na kuyaishi yale yote ambayo walifundishwa na Bwana wetu Yesu Kristo. Nasi sote tulio wafuasi wa Kristo tunapata nguvu ya kuiishi amri ya mapendo katika ufuasi wetu kwa Kristo kwa njia ya pendo hili kubwa la Kristo ambalo limekwishamiminwa katika mioyo yetu kwa njia ya Roho Mtakatifu.

Zawadi za Kristo kwa Kanisa: Roho Mtakatifu, Amani na Upendo
Zawadi za Kristo kwa Kanisa: Roho Mtakatifu, Amani na Upendo   (@Vatican Media)

Katika somo hili la Injili Dominika ya Sita ya Kipindi cha Pasaka tuna mafundisho matatu ya kujifunza. Kwanza: Kristo hayupo mbali nasi, Yupo daima kati yetu. Kristo anazungumza kwa kirefu pamoja na wanafunzi wake katika karamu ya mwisho. Anawapa moyo kwamba, bado ataendelea kuwa nao. Ni kwa njia ya kumpenda Kristo, uwepo wa Mungu unaendelea sasa na daima ndani mwetu. Anawaahidi na Mitume na anatuahidi sisi sote pia, kwamba ni kwa njia ya kumpenda Kristo na kulishika kiaminifu Neno lake ndipo naye anafanya makazi ndani mwetu. Kristo yupo nasi katika Neno lake. Ndugu wapendwa Kristo yupo daima kati yetu. Anatufundisha kwa Neno lake takatifu namna tunapaswa kuhusiana naye na kuhusiana sisi kwa sisi. Ni kwa njia ya mependo thabiti kwa Kristo, kulipenda na kulishika Neno lake ndipo anafanya makazi ndani mwetu. Kila mmoja anapata nafasi ya kutafakari upya mapendo yake na uaminifu wake katika amri na mafundisho ya Kristo katika maisha yetu ya kila siku kama wanafunzi wake. Je, nina upendo wa dhati kwa Kristo? Tenga muda kwa ajili ya Neno la Kristo. Je, nina muda wa kutosha wa kumsikiliza Yesu katika Neno lake, ninatenga muda kusoma na kulitafakari Neno lake takatifu, Neno ambalo ni mwanga na taa ya kutuongoza, Neno ambalo ni faraja na kitulizo chetu, Neno linaloturekebisha na kutukumbusa wajibu wetu kila siku kwa Mungu na kwa wenzetu, Neno linalotupa nguvu ya kusonga mbele licha ya changamoto mbalimbali ambazo kila mmoja wetu anapitia katika safari yake ya maisha? Yesu anafanya makazi ndani mwangu/mwako. Ndugu mpendwa, Yesu anaahidi kufanya makazi ndani mwako leo. Hatudai mambo makubwa ili afanye makao ndani mwetu. Anatudai Neno moja tu Upendo. Je ninapenda namna gani? Ninampenda Mungu na kumpa yeye peke yake nafasi ya kwanza? Ninawapenda jirani zangu? Ninaipenda familia yangu? Ninawapenda wanajumuiya wenzangu? Kristo atusaidie kuiishi kweli amri hii ya mapendo ili tuendelee kufurahia uwepo wake ndani mwetu na uwepo wake kweli uyabadili kabisa maisha yetu, uguse hali zetu mbalimbali kila mmoja katika maisha yake ya ufuasi. Kristo yupo nasi katika Ekaristi Takatifu, Sadaka ya Upendo. Ekaristi Takatifu ni sadaka ya shukrani. Tunamshukuru Mungu kwa kutupenda upeo, kwa zawadi ya mwili na damu yake ambayo kwayo sisi sote tumepata ukombozi wa milele. Tunaalikwa kushiriki Ekaristi Takatifu, kuijongea karamu ya upendo na upatanisho. Kisha kupokea Ekaristi Takatifu, tunaalikwa kuushuhudia upendo wa Kristo. Je, ninapopokea Ekaristi takatifu ninaiishi kweli katika uhalisia wa maisha yangu? Ninaiishi imani, ninauishi upendo ambao nimeupokea bure kutoka kwa Kristo, ninauishi upatanisho, ninaushi umoja, ninajitoa sadaka? Kristo atupe nguvu ya kuishi Kiekaristia.

Mashuhuda wa imani ni nguzo imara wa ujenzi wa Kanisa.
Mashuhuda wa imani ni nguzo imara wa ujenzi wa Kanisa.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Pili: Kukataa mafundisho ya Kristo ni kumkataa Mungu. Kristo anawafundisha mitume wake kuwa, “Mtu asinipenda yeye hayashiki maneno yangu, nalo neno mnalolisikia sio langu, ila ni lake Baba aliyenipeleka” Mitume wa Kristo walihubiri Neno la Mungu. Licha ya kwamba Kristo mara kadhaa alieleza kuwa, alihubiri Neno lake yeye aliyemtuma, bado wapo wengi ambao hawakumwamini wala hawakulishika Neno lake. Hawakumkataa Kristo bali walimkata yule aliyemtuma yaani Baba wa mbinguni. Ndugu mpendwa, mara kadhaa huenda nimepuuza kwa namna moja au nyingine mafundisho ya Kristo. Nimepuuza pengine ujumbe wa Kristo unaohubiriwa kwangu. Tunaishi katika ulimwengu ambapo kuna mafundisho mengi, ya kweli na mengine yenye kupotosha. Tunaalikwa kusimamia katika ukweli wa mafundisho ya Kristo. Injili haipaswi kupindishwa wala kuonewa aibu. Ukweli wa mafundisho tanzu ya kanisa kuhusu maadili wapaswa kusimamiwa kwa uaminifu maana ndilo neno la Kristo. Mafundisho msingi juu ya ndoa na familia, juu ya utu na haki, yapaswa kusimamiwa kwa uaminifu. Anayefundisha kinyume na Neno la Kristo mwenyewe, huyo anamkataa Mungu. Pamoja na mambo mengine mengi ambao yapo katika ulimwengu wa sasa, bado Neno la Kristo litasimama. Chagamoto mbalimbali za maisha zisitufanye tulikane na kulipuuza Neno la Kristo, tusitoke katika tumaini letu kwa Neno la Kristo kwa sababu ya starehe na anasa za dunia ambazo ni za muda na za kupita tuu. Tuombe neema ya kuweza kulishika na kuliishi Neno la Kristo na mara zote ambazo tunaliacha na kulipuuza Neno lake, tumwombe Mungu msamaha na tuendelee kutumainia nguvu ya Neno lake katika masha yetu ya kila siku.

Zawadi za Kristo kwa Kanisa: Roho Mtakatifu, Amani na Upendo
Zawadi za Kristo kwa Kanisa: Roho Mtakatifu, Amani na Upendo   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Tatu: Kristo anawaachia Mitume wake zawadi ya Roho Mtakatifu. Kristo Yesu aliwafundisha mitume wake mambo mengi sana alipokuwa angali pamoja nao. Katika karamu hii ya mwisho, anawaahidi kwamba, Roho Mtakatifu, msaidizi ambaye Baba atampelekea atawafundisha na kuwakumbusha yote aliyowaambia. Mitume kweli mara baada ya Pentekoste walipata nguvu ya kuanza upya kumtangaza Kristo, wakivumilia katika shida na taabu zote hata kufa kifo dini kwa ajili ya Injili ya Kristo. Katika sehemu hii Kristo anaeleza kazi kuu nne za Roho Mtakatifu kwa mitume wake. Kwanza: Kuwafundisha. Kristo anawaahidi mitume wake kwamba Roho Mtakatifu atawafundisha yale yote waliyopaswa kutenda, kuamua na kufundisha pia wengine. Nasi sote kwa kumpokea kwa njia ya ubatizo wetu tulipokea Roho Mtakatifu na kisha utimilifu wa mapaji yake katika sakramenti ya kipaimara. Anatufundisha kila siku yale yanayotupasa kwa ajili ya Mungu na kwa ajili ya wengine. Tukubali kuongozwa na kufundishwa na Roho Mtakatifu ili daima tujue na kutenda yale yanayompendeza Mungu. Pili: Atawakumbusha. Kazi ya pili ya Roho Mtakatifu ilikua ni kuwakumbusha mitume yale yote ambayo Kristo aliwafundisha alipokuwa bado angali pamoja nao. Yesu anawahakikishia kuwa, ijapokua atakua mbali nao, hawatamwona ila atakua karibu nao kwa njia ya Roho Mtakatifu. Ndugu wapendwa, kwa njia ya Roho Mtakatifu, Yesu yupo daima karibu nasi. Ni kwa njia ya Roho Mtakafu anakua kati yetu katika maumbo ya mkate na divai katika fumbo la Ekaristi Takatifu akitukumbusha juu ya sadaka yake ya upendo kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Kwa njia ya Roho Mtakatifu anafungua akili na mioyo yetu akitufundisha na kutusaidia katika kuomba kwa kuwa sisi hatujui itupasavyo kuomba. Anatufunulia akili zetu nasi tunaweza kuelewa na kulishika neno lake.

Neno la Mungu liwe ni chachu ya mabadiliko katika maisha
Neno la Mungu liwe ni chachu ya mabadiliko katika maisha   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Katika dominika hii ya sita, Kristo Yesu anatukumbusha kuwa daima hatupo peke yetu na ya kwamba tusitegemee tu nguvu, akili na uelewa wetu ili kuweza kuishi kweli maisha mazuri yenye kumpendeza Mungu. Tunapata ujasiri katika kufundisha Neno la Kristo kama mitume. Tunaishi katika jamii ambapo ukweli unapingwa na kufukiwa na uongo ukipigiwa chapuo na kuenezwa kwa kasi. Tutaweza kutambua mafundisho ya uowongo kwa kumpa roho Mtakatifu nafasi afungue akili na mioyo yetu ili tuweze kukumbuka daima mafundisho ya Kristo katikati ya wimbi la mafundisho mengi yasiyo ya Kristo. Tatu: anawapa Amani: Kristo anawapa Mitume wake amani, anapowaambia “Amani nawaachieni, amani yangu nawapa” Kristo mara baada ya kukamatwa na kufa, mitume walijawa na hofu na mashaka. Kisha kufufuka, neno lake la kwanza anapowatokea Mitume wake anawaambia, “Amani iwe kwenu” Alitambua hali zao wakati ule na itakavyokuwa wakati ujao atakapoondoka kutoka kati yao, anawapa amani. Ndugu mpendwa, Kristo anatambua hali zetu mbalimbali tunazopitia katika maisha yetu kama wafuasi wake. Amani anayowapa mitume wake hatokani na nguvu za kijeshi, wala haitokani na mafanikio yao wenyewe. Amani hii inatokana na muunganiko wa pekee na wa kudumu na Kristo. Mimi na wewe tunaalikwa kuunganika kabisa na Kristo. Tunaalikwa kumweleza hali zetu, hofu na mashaka yetu kila mara anapokutana nasi. Neno lake ni lile lile daima, Amani nawaachieni, amani yangu na nawapa. Maneno haya tunayasikia kila mara tunaposhiriki adhimisho la Misa Takatifu. Wajibu wangu na wako ni kupoke amani hii ya kudumu itokayo kwa Kristo. Tunapmpokea katika Ekaristi Takatifu tunapokea amani yake. Inatusaidia katika kuvumilia hata nyakati, nyakati za kukatisha tamaa, nyakati za kuogofya, nyakati za kushindwa na kuanguka, Kristo anasema na moyo wako, Amani iwe kwako. Pokea amani ya Kristo, amani inayodumu wakati wote, amani isiyotegemea mambo ya nje bali ukaribu wetu na Kristo mwenyewe. Anatuambia maneno ya faraja na kutia moyo, msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.

Roho Mtakatifu na Kanisa; Utume wa Kristo na wa Roho Mtakatifu
Roho Mtakatifu na Kanisa; Utume wa Kristo na wa Roho Mtakatifu   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Nne: Anawahikikisha kuwa atarudi tena. Katika sehemu ya mwisho kabisa ya Injili ya leo Kristo anawapa uhakika Mitume wake kuwa atarejea tena. Ni dhahiri kuwa kama alivyowaahidi mitume ni kwamba atarejea kwanza kwa njia ya Roho Mtakatifu, lakini pia atarejea tena kwa maana ya ujio wake wa pili. Ndugu wapendwa, Hili ni fumbo la imani yetu kwamba, Kristo alikufa, Kristo alifufuka na Kristo atakuja tena. Amekwenda kutuandalia makao na hivi atakuja tena kutukaribisha kwake ili alipo yeye nasi tuwepo. Ndipo mwisho wa nyakati anatuambia mwinjili Yohane katika kitabu cha ufunuo ya kuwa Yerusalemu mpya itashuka kutoka mbinguni, ishara ya kanisa la washindi. Tano: Anawaandaa katika kupokea mambo makubwa ambayo yangetokea muda si mrefu ili yatokeapo wapate kuamini. Kristo anawaandaa Mitume wake kupokea hali ngumu ambayo ingewapata baada ya yeye kuingia katika mateso, kifo na ufufuko wake. Lakini pia anayasema hayo ili yajapo kutokea yawaimarishe zaidi Mitume katika imani yao kwa Kristo. Ndugu mpendwa, Kristo anatuandaa katika kupokea hali mbalimbali katika maisa yetu. Hatupi jaribu liliko kubwa kupita nguvu zetu bali anatupa nguvu ya kuyapokea tujuapo hakika ya kuwa yupo daima pamoja nasi.

Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha
Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha   (@Vatican Media)

Somo la Kwanza: Ni kitabu cha Matendo ya Mitume Mdo 15:1-2, 22-29. Mitume wa Yesu baada ya Pentekoste walianza kwa nguvu kumtangaza Kristo Mfufuka pasi na hofu na mashaka tena. Injili ikaanza kuenea kwa kasi katika Yerusalemu na baadaye hata nje ya Yerusalemu. Hatimaye, Injili ikawafikiwa watu wa mataifa nao wakataka kumpokea na kumwamini Kristo. Tatizo la kuwapokea wapagani katika kanisa changa lilikuwa linaanza kukua na kusambaa lilikuwa kubwa sana. Jibu la tatizo hilo linaamuliwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu katika Mtaguso wa kwanza wa Yerusalemu mwaka 49 A.D. Ni kuanzia hapa kanisa linafungua milango na kuwapokea watu wote wenye ni thabiti ya kuwa wakristo. Sio kwa kufuata tena vigezo kwamba walipaswa kwanza kuwa Wayahudi, wa kutahiriwa na kushika torati yote ya Wayahudi ndipo wawe Wakristo, la hasha.  Injili hii imefika hata kwetu kwa njia ya kazi kubwa walioifanya Mitume wa Kristo. Kristo kwa njia ya fumbo la Pasaka amewaletea wote chini katika kundi moja yeye akiwa mchungaji wa kundi hilo. Ndugu zangu katika Somo hili la kwanza tuna mambo matatu ya kujifunza. Kwanza: Nguvu ya Kristo mfufuka inawaunganisha watu wa mataifa yote. Katika kanisa la Mwanzo, baadhi ya watu waliotoka Uyahudi walihubiri kwamba watu wa mataifa wasipotahiriwa kama desturi ya Musa hawawezi kuokoka. Mitume Paulo na Barnaba walihubiri juu ya nguvu na thamani ya sadaka ya Kristo msalabani, ya kwamba watu wa mataifa yote wamepata wokovu. Anayebatizwa anashiriki hivyo sadaka hii ya Kristo na anahesabiwa haki si kwa matendo ya sheria bali kwa Imani thabiti kwa Kristo mfufuka, kwa kuiamini Injili, kwa kubatizwa na kuishi maisha mapya.

Umoja na ushuhuda wa Kanisa katika Ulimwengu mamboleo.
Umoja na ushuhuda wa Kanisa katika Ulimwengu mamboleo.   (@Vatican Media)

Ndugu wapendwa, Kristo ametuunganisha sote kwa sadaka ya kifo cha Msalabani. Sote tumepokea zawadi hii ya wokovu na hivyo kufunguliwa mlango wa mbinguni. Je, ninapokea na kuthamini zawadi hii kubwa itokanayo na damu ya thamani ya Bwana wetu Yesu Kristo? Ubatizo wetu unatudai kuanza maisha mapya, kuachana mazoea yote ya kale na kuikumbatia habari njema ya Injili. Kila mara tunapata nafasi tena ya kukiri Imani yetu, kutangaza na kurudia tena ile nia yetu ya kuishi kweli kama wana wa Mungu, tuliokombolewa kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti. Tunaalikwa kuwasaidia wengine pia kupokea na kufaidi zawadi hii kubwa ya ukombozi tuliyopewa bure na Kristo mwenyewe. Katika kanisa na katika jumuiya zetu tunapaswa kuwasaida watu wengi zaidi kila siku kupokea mwaliko huu wa ukombozi. Hatupaswi kuweka vikwazo ambavyo kwa namna moja au nyingine vinawazuia watu kuja kwa Kristo na kuikumbatia huruma yake kubwa isiyo na mipaka. Mitume waliondoa vikwazo ambavyo hapo Mwanzo viliwanyima nafasi watu wa mataifa kuipokea habari njema ya Injili. Licha ya hayo waliweka pia mambo ya msingi ambayo yalihusu hasa upya wa maisha kwa yule aliyepokea habari njema na kubatizwa. Ndivyo viapo vyetu vya ubatizo ambao kila anayebatizwa apaswa kuviishi kama mwana wa Mungu.

Zawadi za Kristo kwa Kanisa: Roho Mtakatifu, Amani na Upendo
Zawadi za Kristo kwa Kanisa: Roho Mtakatifu, Amani na Upendo

Pili: Roho Mtakatifu daima analiongoza kanisa la Kristo. Mitume Paulo na Barnaba baada ya kushindana na kuhojiana na watu waliotoka Uyahudi waliokuwa wakifundisha juu ya vigezo na masharti yaliyopaswa kufuatwa na watu wa mataifa waliotaka kuwa wakristo, wanalipeleka swala hilo Yerusalemu katika mtaguso pamoja na mitume wengine. Mtaguso huu wa kwanza kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu, ulileta matunda makubwa ndani ya kanisa la mwanzo. Vivyo hivyo kwa nyakati mbalimbali, Roho Mtakatifu ameliongoza kanisa na hata sasa bado limesimama imara katika misingi ya Mitume. Ndugu wapendwa, Kristo aliwaahidi mitume zawadi ya Roho Mtakatifu. Baada ya Pentekoste, Roho Mtakatifu ameendelea kutembea na kanisa katika nyakati mbalimbali. Kama Mitume walivyomshirikisha Roho Mtakatifu katika maamuzi makubwa yaliyohusu kanisa, tunasali kuliombea bado kanisa ambalo hata hivi leo linapita katika changamoto mbalimbali. Tunamwombea Baba Mtakatifu wetu aliye Khalifa wa Mtume Petro, ili awezae kuliongoza kanisa kwa maongozi ya Roho Mtakatifu. Tunaalikwa pia kumpa Roho Mtakatifu nafasi katika maisha yetu, kuomba nguvu yake katika maamuzi mbalimbali ya maisha yetu, kuomba hekima na busara katika kuwaza na kutenda yale yampendezayo Mungu, kuombe nguvu ya kuwa imara katika imani na kuishudia kweli imani yetu bila kutetereka.

Roho Mtakatifu na Kanisa; Utume wa Kristo na wa Roho Mtakatifu
Roho Mtakatifu na Kanisa; Utume wa Kristo na wa Roho Mtakatifu

Tatu: Umoja katika tofauti zetu. Kristo katika karamu ya mwisho aliomwomba Baba, kwamba wote wawe na umoja. Roho Mtakatifu anawaunganisha pamoja watu wa kila kabila, lugha, jamaa na taifa. Licha ya tofauti zao, nguvu ya Kristo mfufuka imewaleta wote pamoja. Ndugu wapendwa, Roho mtatifu analiunganisha daima kanisa, moja, takatifu, katoliki na la mitume, anatuunganisha nasi sote kuwa wamoja, katika famila zetu, katika jumuiya zetu, katika taifa letu na katika kanisa. Roho Mtakatifu anatusaidia kutambua utajiri uliopo katika tofauti zetu. Kuna tofauti ya karama, na vipaji, tunapovileta pamoja tunajenga jumuiya na kanisa imara. Kanisa limekua imara lenye kuwapokea watu wote na bado litaendelea kuwa imara licha ya tofauti zetu. Je, tofauti zetu katika maisha zinatusaidia katika kukua? Karama na vipaji alivyotupa Mungu vinatusaidia katika kujenga na kukuza upendo na undugu kati yetu au ndio chanzo cha migogoro, chuki, majivuno, dharau na wivu? Je tunapokeana katika madhaifu yetu, kurekebishana na kuchukuliana kwa upole? Roho mtakatifu atupe nguvu ya kuwa wamoja licha tofauti zetu.

Roho Mtakatifu ni chemchemi ya furaha ya familia
Roho Mtakatifu ni chemchemi ya furaha ya familia

Nne: Roho Mtakatifu anatusaidia katika kutofautisha mafundisho ya kweli na yale ya uwongo. Mitume baada ya kusikia habari kwamba watu wa mataifa walipotoshwa kwa habari za uongo ambazo hazikutoka kwao, wanaamua kuwatuma tena Mitume Paulo na Barnaba, sila na Yuda aitwaye Barsaba kuwapelekea ujumbe watu wa kanisa la Antiokia juu ya maamuzi yaliyofikiwa katika mtaguso wa Yerusalemu. Kanisa linatoa na kufundisha mafundisha sahihi juu ya injili ya Kristo kupitia Mitume hawa ambao waliwatuma kwa niaba yao. Ndugu wapendwa, katika nyakati zetu wapo wengi wanaofundisha habari za uwongo tofauti na Injili ya Kristo kwa manufaa yao binafsi. Injili imegeuka kitega uchumi na hivyo kuwahubiria watu yale wanayotaka kuyasikia na wala si Injili ya Kristo. Tumwombe Roho Mtakatifu atusaidie kutambua na kuyakwepa mafundisho yote ambayo ni kinyume na misingi imara ya imani yetu, kinyume na maadili yetu, kinyume na mila na desturi zetu nk. Hatuwezi kuyatambua hayo tusipompa nafasi Roho Mtakatifu ayaongoze daima maisha yetu.

Ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili ni kazi ya Roho Mtakatifu
Ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili ni kazi ya Roho Mtakatifu   (@Vatican Media)

Somo la Pili: Ni kitabu cha Ufunuo wa Yohane 21:10-14, 22-23. Mwandishi wa kitabu hiki, Mtume Yohane, anatueleza maono juu ya Yerusalemu mpya, ikishuka kutoka mbinguni kwa Mwenyezi Mungu, mji wenye utukufu wa Mungu. Ni maono juu ya kanisa la mbinguni ambalo hapo kwanza lilijengwa juu ya misingi ya Mitume kumi na wawili, likazaliwa, taratibu kwa maongozi ya Roho Mtakatifu likakua na kuenea kote, likieleka katika utimilifu wake mbinguni ambapo anaishi Kristo pamoja na malaika na watakatifu wake. Ni baada ya maisha ya hapa duniani, kwa kuishika na kuiishi kiaminifu Imani yetu ndipo tutapata zawadi ya kuingia katika Yerusalemu mpya mbinguni katika uzima wa milele, ndio utimilifu wa kazi ya ukombozi. Ndugu wapendwa, mtume Yohane anawapa moyo wakristo hawa ambao walikua wanapitia mateso na madhulumu mengi kutoka kwa utawala wa kirumi kwamba upo mji udumuo milele. Tunapoishi na kusaifiri katika safari yetu ya maisha ya hapa duniani tuwe na Imani na matumaini kwamba, tunaelekea nyumbani kwetu, kwenye makazi yetu ya kudumu. Milango ya mbinguni ipo wazi, Kristo amekwisha tufungulia njia nasi sote kwa njia ya ubatizo tuna nafasi ya kuingia na kuishi katika uwepo wa Mungu pamoja na Kristo na watakatifu wote milele na milele amina. Hitimisho: Mpango wa Mungu wa ukombozi ni kwamba sisi sote turejee kwake mbinguni yalipo makao yetu ya kudumu, Yerusalemu yetu mpya. Ni kwa njia ya Mama kanisa ambalo limejengeka juu ya misingi ya Mitume, sisi sote watu wa kila kabila, lugha, jamaa na taifa tunasafiri kuelekea uzima wa milele. Tunaalikwa kuwa hekalu hai la Mungu, kwa kuiishi amri kuu ya mapendo kiaminifu, kumtambulisha Kristo kwa watu wote kwa njia ya maneno na Matendo yetu.

D6 Mwaka C

 

 

24 Mei 2025, 11:46