Tafakari Dominika VI Kipindi Cha Pasaka: Kazi za Roho Mtakatifu
Na Padre Pascha Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 6 ya Pasaka mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa. Masomo ya Dominika hii yanasisitiza juu ya umoja wa Kanisa Katoliki. Kanisa ni moja kutokana na chanzo chake, na mwanzilishi wake, na roho yake (KKK 813) – Mwanzilishi wake ni Yesu Kristo, Nafsi ya Pili ya Mungu mmoja katika Utatu Mtakatifu; Kiongozi wake mkuu duniani ni mmoja, Baba Mtakatifu, Khalifa wa Mtume Petro ambaye Kristo alilijenga Kanisa juu yake na wala milango ya kuzimu haitalishinda; mafundisho yake ya kiimani, kimaadili, na kiliturujia, yote ni mamoja. Alama hii ya umoja wa Kanisa inajidhihirisha wazi tangu nyakati za mitume kwa maongozi ya Roho Mtakatifu, atokaye kwa Baba na Mwana, anayeabudiwa na kutukuzwa milele yote, kama tunavyosali katika Kanuni ya Imani. Ni katika muktadha huu wimbo wa mwanzo unaofungua maadhimisho ya dominika hii unasema hivi; “Hubirini kwa sauti ya kuimba, tangazane haya yatamkeni mpaka mwisho wa dunia, semeni, Bwana amelikomboa taifa lake, aleluya” (Isa. 48:20). Na Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali kwa tumaini hili hili akisema; “Ee Mungu Mwenyezi, utuwezeshe kuadhimisha kwa bidii siku hizi za furaha, tunazozitumaini kwa heshima ya Bwana aliyefufuka. Na hayo tunayoyakumbuka sasa, tuyazingatie daima kwa matendo.”
Somo la kwanza ni la Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 15:1-2, 22-29). Somo hili linahusu maamuzi yaliyotolewa na Mitume na wazee wa Kanisa katika mkutano wa Yerusalemu kuwa wapagani wanaoongokea ukristo, sio lazima watahiriwe na kushika Torati ya Musa. Wokovu wao unategemea imani yao kwa Kristo tu. Itakumbukwa kuwa kwa jamii nyingi Jando kwa watoto wa kiume lilifanyika katika umri wa kubalehe kama sehemu ya kumwingiza kijana katika rika la watu wazima wenye nyajibu na haki katika ukoo. Tukio hili liliambatana na mafundisho ya kumuandaa kijana kwa maisha ya ndoa na familia. Kwa Wayahudi, jando lilikuwa ni tendo takatifu la kidini, ishara ya Agano la Mungu na taifa la Israeli (rej. Mwa 17:9-14, 23-27; Lk 2:21). Hivyo kutokutahiriwa kwa Myahudi kulimfanya asishirikishwe ahadi za Agano kati ya Mungu na Ibrahamu na uzao wake wote. Sheria ilidai pia walioongokea dini ya Kiyahudi walipaswa kutahiriwa (rej. Kut 12:48). Katika hali hii, Wayahudi walioongokea ukristo waliwataka Wapagani, watu wa matifa walioongokea Ukristo washike mapokeo na sheria ya Musa ikiwa ni pamoja na kutahiriwa. Hali hii ilileta malumbano na mtafaruku kwa Kanisa la Antiokia. Hivyo wakaamua kutuma wajumbe kwenda Yerusalemu wafikishe jambo hili kwa Mitume nao walilipokea, wakaitisha mkutano, wakajadili, wakatoa suluhisho kuwa mbele za Mungu watu wote, wayahudi na wasio wayahudi, bila ubaguzi, wanaokolewa kwa kuongoka kwao, kutubu dhambi zao na kupokea ubatizo, na kuwa familia moja ya Mungu ndani ya Kristo, tena wanapokea maisha mapya kwa njia ya Roho Mtakatifu, na kufanywa kuwa Wana wa Mungu na ndugu – kaka na dada wa Kristo. Hivyo wapagani hawalazimiki kuzishika Sheria za Musa bali wajiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na dhambi kuachana na maisha ya dhambi.
Petro aling’amua fundisho kwa kuamriwa kula vilivyokatazwa na Sheria ya Musa akiambiwaa; “Vilivyotakaswa na Mungu usiviite wewe najisi (Mdo 10:15), na jinsi Roho Mtakatifu alivyomshukia Kornelio na familia yake hata akasema; “Ni nani awezaye kukataza maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu kama sisi? (Mdo 10:47). Naye Paulo baada ya kushuhudia Roho Mtakatifu akiwashukia watu wa mataifa mengine alisema; “Hakika Mungu hana upendeleo, wote wanakubalika kwake.” Sheria ya Musa ilikuwa muhimu kabla ya ujio wa Kristo. Kwa sasa tunaokolewa na imani kwa Yesu Kristo na kuiishi Amri ya mapendo. Maamuzi haya yalileta maridhiano, furaha, amani na utulivu kwa jumuiya zote. Huu ndio umoja wa Kanisa ulivyo tangu enzi za mitume mpaka sasa unaojidhihirisha katika taabu na raha na ikitokea sintofahamu ya kiimani au kimaadili, maamuzi ya mwisho lazima yatolewa na Baba Mtakatifu na yakishatolewa lazima yafuatwe na Kanisa lote ulimwenguni kwa sababu yanakuwa ni maongozi ya Mungu, Roho Mtakatifu. Ni katika muktadha huu wimbo wa katikati unasema hivi; “Mungu na atufadhili na kutubariki, na kutuangazia uso wake. Njia yake ijulikane duniani, Wokovu wake kati ya mataifa yote. Mataifa na washangilie, naam, waimbe kwa furaha. Maana kwa haki utawahukumu watu, na kuwaongoza mataifa walioko duniani. Watu na wakushukuru, Ee Mungu, watu wote na wakushukuru. Mungu atatubariki sisi; Miisho yote ya dunia itamcha Yeye” (Zab. 67: 1-5, 7).
Somo la pili ni kutoka katika Kitabu cha Ufunuo (Ufu. 21:10-14, 22-23). Somo hili linahusu hatua za Mungu kujifunua kwake na hatua za fumbo la ukombozi tangu kuliteua taifa la Israeli, makabila yake kumi na mawili, na kujidhihirisha kwao kwa njia ya hekalu na baadae kwa njia ya Mitume kumi na wawili aliowachagua Yesu Kristo ambao Imani ya kikristo ikajengwa juu ya misingi yao. Katika maisha ya hapa duniani sisi wakristo tunahitaji bado hekalu, Kanisa - Mwili wa Kristo kama ishara ya uwepo wa Mungu. Lakini baada ya kifo, mwisho wa nyakati, wale watakaofikia maisha ya utakatifu, hawatahitaji tena hekalu kwa sababu watamwona Mungu uso kwa uso katika utukufu wake. Ni katika msingi huu Mtume Yohane alifunuliwa utakatifu wa Kanisa kwa kuoneshwa mji mtakatifu Yerusalemu ambao ni mfano wa Kanisa. Kanisa ni Takatifu kwa sababu: Mwanzilishi wake ni Mtakatifu, Yesu Kristo, linahudumia vitakatifu, linawafanya watu kuwa watakatifu kwa njia ya Neno la Mungu na Sakramenti zake. Mafundisho yake yanaongozwa na Roho Mtakatifu ndiye anayelifundisha kupitia kwa Baba Mtakatifu Khalifa wa mtume Petro. Kanisa ni Katoliki kwa kuwa liko kwa ajili ya wokovu wa watu. Kanisa ni la Mitume kwa kuwa Imani na misingi ya mafundisho yake imejengwa juu ya mitume waliopokea Mafundisho na Imani hiyo moja kwa moja toka kwa Yesu Kristo. Uongozi wa Kanisa nao unafuata mtiririko huo kutoka enzi za Mitume mpaka sasa.
Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 14:23-29). Sehemu hii ya Injili inahusu wosia wa Yesu wa Amri ya Mapendo na ahadi ya Roho Mtakatifu, Msadizi wetu katika kuiishi vyema Amri ya Mapendo, akidhihirisha uwepo wa daima wa Yesu Kristo na Mungu Baba katika maisha yetu. Hivyo anayempenda Yesu kwa moyo wote, atajazwa furaha na amani itokayo kwa Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Huu ndio ukamilisho wa ufunuo wa Utatu Mtakatifu kwamba katika Mungu mmoja kuna nafsi tatu; Mungu Baba – nafsi ya kwanza, muumbaji; Mungu mwana – nafsi ya pili, Mkombozi; na Mungu Roho Mtakatifu – nafsi ya tatu, kiongozi, msimamizi, mwimarishi na mtakatifuzaji. Historia inashuhudia kuwa kuanzia karne ya 16 upinzani wa imani na mafundisho ya mitume, hasa mamlaka ya Baba Mtakatifu Khalfa wa mtume Petro, ulisababisha kuibuka kwa madhehebu ya Kiprotestanti. Mpasuko na mgawanyiko huu umeendelea hadi sasa katika nyakati zetu na unazidi kukua na ongezeko kwa kuibuka kwa wanaojiita mitume na manabii wa Injili ya mafanikio. Chanzo cha mgawanyiko huu ni uchu wa madaraka/uongozi, upinzani dhidi ya mafundisho ya kimaadili, sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayotuelekeza kwenye utakatifu kwa kuubeba msalaba wa Yesu Kristo Mkombozi wetu. Lakini pia matatizo ya kijamii, magonjwa, umaskini, kukosa ajira, zinawafanya watu kutafuta utajiri au umaarufu kwa njia zisizo halali, kwa kufuata Injili ya mafanikio, Pasaka bila Ijumaa kuu, utakatifu bila Msalaba.
Mtume Paulo anaonya akisema; “Lakini wale watu wanaotamani kuwa na mali kwa haraka haraka huanguka kwenye majaribu na wamenaswa na tamaa nyingi za kipumbavu, zenye kudhuru, zinazowazamisha katika uharibifu na maangamizi. Kwa maana kupenda madaraka na fedha ndiyo shina moja la maovu ya kila namna. Baadhi ya watu wakitamani fedha, wameiacha amani na kujichoma wenyewe kwa maumivu mengi mno” (1Tim.6:9-1). Tunaalikwa kushika mafundisho ya imani na maadili yanayotolewa na mamlaka funzi ya Kanisa. Tuzingatie maonyo ya Yesu aliyosema; “Angalieni mtu asiwadanganye. Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu wakisema, mimi ni Kristo, nao watawadanganya wengi” (Mt 24:4-5), “jihadharini na manabii wa uwongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali” Mt 7:15-20. Basi tuwe na sikio sikivu kwa Roho Mtakatifu, tumruhusu atuangaze na kutuongoza ili tuweze kutambua mambo tunayopaswa kufanya katika kuishuhudia imani yetu na tunapaswa kuyaepuka ili tuweze kuwa kweli wafuasi wa Yesu Kristo, ili mwisho tukaurithi uzima wa milele mbinguni. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, sala zetu zipae kwako pamoja na sadaka tunazokutolea; tutakaswe kwa huruma yako, tufae kuzipokea sakramenti za rehema yako kuu”. Na katika sala baada ya Komunio anahitimisha maadhimisho ya dominika hii akisali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, wewe watuponya kwa kufufuka kwake Kristu ili tupate uzima wa milele. Utuzidishie neema za fumbo la Paska, na kutujaza mioyoni mwetu nguvu ya chakula hiki cha wokovu”.