Tafakari Dominika 5 Kipindi cha Pasaka: Upendo Ni Utambulisho wa Kikristo
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 5 ya Pasaka, mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa. Maneno ya wimbo wa mwanzo unaofungua maadhimisho ya dominika hii yanasema hivi; “Mwimbieni Bwana wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu; machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake, aleluya” (Zab 98:1-2). Upendo ni utimilifu wa sheria zote na ni kipimo cha matendo yote ya kibinadamu. Sheria, amri na kanuni zote vinapaswa kutuelekeza kwenye upendo. Anayempenda Mungu anammiliki Mungu ndani yake, alisema Mt. Tomaso wa Akwino. Huu ni mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni vyombo vya huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka! Na ni katika amri ya upendo, iliyo amri kuu ya Bwana, kwamba wakristo wote wahimizwa kutafuta utukufu wa Mungu kwa ujio wa ufalme wake, na uzima wa milele. Ni kweli, Mwenyezi Mungu ametutendea makuu kwa kutukomboa kutoka utumwa wa dhambi na mauti, kwa kifo na ufufuko wa Mwanaye Pekee Bwana wetu Yesu Kristo na kutufanya wanawe wateule. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali akisema; “Ee Mungu, umetuletea ukombozi na kutufanya watoto wako. Tunakuomba utusikilize kwa wema sisi wanao, ili katika kumwamini Kristu tupate uhuru wa kweli na urithi wa milele.”
Somo la kwanza ni la kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 14:21b-27). Somo hili linahusu hitimisho la safari ya kwanza ya kimisionari ya Paulo Mtume na Barnaba katika Asia ndogo, safari iliyochukua takribani miaka 4, wakiongozwa na Roho Mtakatifu. Sehemu hii ya hili simulizi inatupa nafasi ya kujua na kuelewa hali halisi ya Kanisa la wasafiri hapa duniani kuwa limepambwa kwa furaha na mateso. Mtume Paulo akilitambua hili, aliwaimarisha wafuasi wa Kristo, akiwasihi wakae imara katika Imani, licha ya madhulumu na mateso akiwaambia; “Imewapasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi” (Mdo 14:22). Ni katika hali hii Mtume Paulo aliwachagua wazee wa Kanisa kwa maongozi ya Roho Mtakatifu aliyejidhihirisha kwa kusali, kuomba na kufunga. Na kisha kuwachagua aliwawekea mikono ishara ya kumpokea Roho Mtakatifu ili awaongoze katika kuwaimarisha wafuasi wa Kristo na kuwatia moyo wasikate tamaa wakiteswa kwa ajili ya imani yao kwa Kristo. Tendo hili linatufundisha pia kuwa mamlaka na uongozi sio ya kujitwalia, kujichukulia, kujivika na kujitangaza, bali yanatoka kwa Mungu anayewatunukia anaowachagua yeye mwenyewe kwa njia ya watu kwa upendo wake, ili wawaongoze watu wake waishi vizuri maisha ya hapa duniani na mwisho wakaishi naye mbinguni milele yote. Ni katika muktadha huu Zaburi ya wimbo wa katikati inasema hivi; “Ee Mungu wangu, Mfalme, nitakutukuza, nitalihimidi jina lako milele na milele. Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema. Bwana ni mwema kwa watu wote, na rehema zake zi juu ya kazi zake zote. Bwana, kazi zako zote zitakushukuru, na wacha Mungu wako watakuhimidi. Wataunena utukufu wa ufalme wako, na kuuhadithia uweza wako. Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu, na utukufu wa fahari ya ufalme wake. Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote, na mamlaka yako ni ya vizazi vyote (Zab. 145:1, 8-13).
Somo la pili ni la Kitabu cha Ufunuo (Ufu. 21:1-5a). Somo hili linatufunulia uzuri wa Kanisa la washindi huku mbinguni. Ni Kanisa lisilo na dhambi, wala taabu, wala mateso. Mbinguni hakuna dhambi wala madhara yake, ni raha na furaha tu; huzuni na masikitiko havipo. Huko ni maskani ya Mungu pamoja na watu wake, ambapo kila chozi katika macho ya wachamungu yanafutwa. Hivyo hakuna mauti, wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu. Yote yanafanyika kuwa mapya kwa nguvu ya upendo wa Kristo aliyekufa msalabani na kufufuka. Katekesimu ya Kanisa Katoliki inafundisha hivi juu ya hali tatu za Kanisa; “Wakati tunamngoja Bwana arudi katika utukufu akiwa pamoja na Malaika wake wote, akiwa ameshinda mauti, vitu vyote vitakapotiishwa chini yake, baadhi ya wafuasi wake wanaendelea kuhiji duniani. Wengine ambao tayari wamekwisha kufa wangali wanatakaswa, wengine wanafurahi katika utukufu wakimtazama katika nuru timilifu, Mungu huyu mmoja katika nafsi tatu jinsi alivyo” (KKK 954).
Injili ni ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 13:31, 33a, 34-35). Sehemu hii ya Injili inatuambia kuwa amri mapendo ni kitambulisho cha ufuasi wetu kwa Kristo mbele za watu wa mataifa. Kuiishi vyema amri hii kunatustahilisha kuurithishwa uzima wa milele mbinguni. Amri hii ni wosia alioutoa Yesu katika karamu ya mwisho, kabla ya kusalitiwa na Yuda, kukamatwa, kuteswa na kufa msalabani akisema: “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi…Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi”. Wosia huu ndio mwongozo wa maisha yetu ya kikristo na ishara ya utambulisho kuwa kweli tu wafuasi wa Kristo Yesu. Lakini katika Agano la Kale tunasoma hivi; “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa nguvu zako zote na kwa akili zako zote…Mpende na jirani yako kama unavyojipenda?” (Kumb 6:5, Wal 19:18). Kutoka katika maagizo haya ya Agano la Kale ni kama vile hakuna jipya katika amri ya mapendo kwenye wosia wa Yesu. Lakini kiuhalisia upya upo, tena mkubwa sana. Sheria ya Agano la Kale ilisema; “Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe” (Wal 19:18). Lakini Yesu anatuambia; “Pendaneni kama nilivyowapenda mimi.” Upendo wa Yesu Kristo kwetu ndio kipimo cha upendo wetu kwa wengine. Na zaidi sana kwa wayahudi jirani alikwa ni myahudi mwenzao tu, tena asiye kuwa na matatizo. Myahudi aliyekuwa na matatizo hasa magonjwa waliyosadiki yanatokana na laana ya dhambi, hakuthaminika, wala hakupendwa ndio maana wenye ukoma walitengwa na jamii.
Ndiyo maana Yesu anaposema hii ni amri mpya anasisitiza; “Pendaneni kama mimi nilivyowapenda ninyi.” Yeye ni mfano na kipimo cha mapendo kamili yanayodai kujisadaka na kutoa uhai kwa ajili ya wengine. “Hakuna upendo mkubwa zaidi ya huu, kuutoa uhai kwa ajili ya wengine”. Upendo huu hauna vipimo wala vigezo, bali unampenda mtu bila kuangalia undugu, ukabila, mafanikio, utajiri, uwezo au sifa zinazotuvutia. Mtume Paulo anasema kuwa upendo huu unavumilia daima, ni mpole, hauna wivu, haujidai, haujivuni, una adabu, tena hautafuti faida yake binafsi, haufurahii maovu, bali unadumu katika ukweli (1Kor. 4-6). Kumbe upya wa amri hii ni kutokuwa na mipaka wala matabaka, hauangalii taabu, wala dhiki, wala mateso, wala njaa, wala ukosefu wa nguo, wala hatari, wala kifo, wenyewe unadumu daima (Rum. 8:35-39). Mtume Yohane anatuasa hivi; “Yeye asiyependa akaa katika mauti, na kila amchukiaye ndugu yake ni muuaji; nanyi mnajua ya kuwa kila muuaji hana uzima wa milele ukaao ndani yake” (1Yoh 3:14-15). Na upendo huu ndio utakaotufikisha Mbinguni. Ikumbukwe daima kuwa Injili ya Kristo sio Injili ya mafanikio ya kidunia, bali ni Injili ya kuubeba msalaba na kumfuata Yeye aliyetupenda hata kufa msalabani. Hivyo basi taabu tuzipatazo katika kuuishi wosia wa Kristo wa kupendana, visitukatishe tamaa bali vituimarishe kwa maana upendo si lelemama, unagharimu hata uhai. Basi tujipe moyo hata kama tunaishi upendo kwa dhiki, dhiki yetu haitapotea bure. Utafika wakati Mungu atakapofuta kila chozi katika macho yetu na kutujalia uzima wa milele mbinguni. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Mungu, umetushirikisha umungu wako mkuu katika kuishiriki sadaka hii takatifu. Tunakuomba utujalie tuufuate kwa mwenendo mwema ule ukweli wako kama tunavyoujua.” Na katika sala baada ya Komunyo anahitimisha maadhimisho ya dominika hii akisali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba uwe na sisi taifa lako. Na kama ulivyotujalia mafumbo haya ya mbinguni, utufikishe kwenye uzima, utuondoe katika maisha ya zamani na kutuweka katika maisha mapya”. Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo.