Kenya,Ask.Mbatia:tusubiri matokeo kuhusu kifo cha Padre Maina
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Padre John Ndegwa Maina aliyekuwa Paroko wa Kanisa la Mtakatifu Louis huko Igwamiti nchini Kenya hivi karibuni tarehe 15 Mei 2025 alikuf mara tu alipofikishwa Hospitalini baada ya kukutwa ameumizwa vibaya sana, na akiwa hai pembeni mwa barabara kuu ya Nakuru-Nairobi, kilomita chache kutoka katika Parokia yake. Mazishi yake yalifanyika Alhamisi tarehe 22 Mei 2025, kwa kuongoza na Askofu Joseph Ndembu Mbatia, wa Nyahururu. Katika mahubiri yake alisema kuwa: "Kuna uchunguzi unaendelea. Mara baada ya wapelelezi kukamilisha uchunguzi wao wa kifo cha Padre Maina, watatoa mwanga juu ya suala hilo na kujibu maswali ambayo sote tumekuwa tukijiuliza kwa juma moja lililopita." Askofu wa Nyahururu Mbatia alisema hayo kwa kutaka kuwatuliza waamini akiwaalika kuwa watulivu wakati wa mazishi ya Padre Maina.
Misa hiyo ilifanyika katika makaburi ya mapadre wa Kikatoliki yaliyoko katika Kilima kiitwacho Tabor huko Ol Joro Orok, Kaunti ya Nyandarua, mbele ya mamia ya watu, walioshtushwa na kifo hicho katika hali ambayo bado haijafafanuliwa kuhusu Padre huyo. “Niliona kwenye vyombo vya habari wanasema kuwa padre wetu ameuawa nikajiuliza walikuwa wanapata wapi taarifa zao. Bado tunafuatilia suala hilo na Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI, polisi wa makosa ya jinai) ili kujua kilichotokea. Hakuna haja ya kubahatisha. Tunataka kujua ukweli, na ndiyo sababu tunashirikiana na wachunguzi. Lazima tuwe na subira,” alisisitiza Askofu Mbatia.
Kuhusiana na kifo cha Padre huyo kinaelezwa kuwa mnamo tarehe 15 Mei 2025, Padre Maina alipatikana kwenye barabara kuu ya Gilgil-Nairobi akiwa na majeraha mabaya kichwani. Baadaye alifariki dunia alipokuwa akitibiwa katika Hospitali ya Misheni. Inasemekana kuwa Padre huyo alieleza kwamba mwendesha bodaboda aliyempata alikuwa ametekwa nyara huko Nyahururu. DCI ilisema kuwa Padre Maina huenda alilengwa na majambazi wakitaka sehemu ya mchango aliopokea kutoka kwa aliyekuwa Makamu wa Rais Rigathi Gachagua wakati wa ibada ya Misa Katika Kanisa mnamo tarehe 27 Aprili 2025. Inasemekana kwamba Padre huyo alionesha wasiwasi wake kuhusu vitisho kwa usalama wake, lakini hakuripoti rasmi kwa mamlaka. Baba Maina, mtoto wa nne katika familia ya watoto kumi na moja, alizaliwa tarehe 13 Machi 1982, na kupewa daraja la upandew tarehe 24 Machi 2017.
Padre mwingine Bett aliuawa kwa kupigwa risasi tarehe 22 Mei
Na wakati huo huo Padre mwingine mkatoliki nchini Kenya, Padre Alloyce Cheruiyot Bett, aliuawa kwa kupigwa risasi katika eneo la Tot la Kerio Valley, Elgeyo Marakwetm katika Nyanda za Juu Magharibi mwa Kenya. Mauaji hayo yalitokea tarehe 22 Mei 2025, wakati mwishoni mwa misa iliyoadhimishwa katika Jumuiya ndogo ya Kikristo) katika kijiji cha Kakbiken, baadhi ya watu wenye silaha walianza kufyatua risasi, ambayo moja ilimpiga Padre Bett shingoni, na kumuua papo hapo. Polisi wa Kenya walisema kuwa wamewakamata watu sita kuhusiana na mauaji ya Padre huyo.
Ingawa ilidhaniwa kuwa lilikuwa jaribio la wizi lisilofanikiwa, msemaji wa polisi alisema kuwa mauaji ya Padre Bett hayakuhusishwa kwa vyovyote na wizi wa ng'ombe au aina nyingine za ujambazi zinazoathiri eneo hilo. Na taarifa za ndani zimedokeza kuwa wauaji hao walishuku kuwa Padre huyo alikuwa mtoa habari kwa polisi aliyekuwa akisaidia vyombo vya sheria kuhusiana na operesheni ya usalama inayoendelea katika eneo hilo. Padre Tott ndiye Padre wa pili wa Kikatoliki kuuawa nchini Kenya katika kipindi cha Juma moja. Baada ya tarehe 15 Mei 15, Padre John Ndegwa Maina, Paroko wa Kanisa la St Louis Igwamiti, kufariki hospitalini baada ya kupatikana akiwa amejeruhiwa vibaya, lakini bado yuko hai, kando ya barabara kuu ya Nakuru-Nairobi, kilomita kadhaa kutoka parokia yake.