杏MAP导航

Tafuta

Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha (RUCU) kimeadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake huku kikijivunia kukua na kuongeza idadi ya vitivo kutoka viwili hadi kufikia vitivyo 6. Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha (RUCU) kimeadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake huku kikijivunia kukua na kuongeza idadi ya vitivo kutoka viwili hadi kufikia vitivyo 6.  

Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha: Mchango wa Kanisa Katoliki Katika Elimu

Aidha amebainisha kuwa katika kipindi hicho cha miaka 20 chuo kimekuwa na maendeleo makubwa katika nyanja za taaluma, utafiti, huduma kwa jamii na kuongeza programu za taaluma kutoka mbili zilizokuwepo wakati chuo kinaanza mwaka 2005 hadi kufikia programu 24 ambazo zimepelekea ongezeko la idadi ya wanafunzi na wafanyakazi, pamoja na miundombinu ya kufundishia na kujifunzia kama vile madarasa, maabara, maktaba na mabweni." Amesema Pd. Mgeni.

Na Getrude Madembwe, - Iringa, Tanzania

Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro alikazia sana kuhusu umuhimu wa kujenga na kudumisha majadiliano katika elimu kama sehemu ya mchakato unaopania kumwendeleza mtu mzima: kiroho na kimwili pamoja na kutambua kwamba, kila mtu ana haki ya kupata elimu, kwa kuzingatia uhuru wake, lakini Kanisa linatoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo kama chimbuko la maisha, historia na ulimwengu katika ujumla wake. Hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha majadiliano katika sekta ya elimu. Baba Mtakatifu analitaka Baraza la Kipapa la Utamaduni na elimu kuhakikisha kwamba linawaandaa wataalam na mabingwa watakaojisadaka kwa ajili ya: utamaduni na elimu katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi kubwa kwa kutambua kwamba, utoaji wa elimu ni kitendo cha upendo na urithishaji wa maisha. Walimu wawe na ujuzi wa kuweza kuwamegea wanafunzi wao ujuzi na maarifa. Walimu wanaotekeleza dhamana na utume wao katika vyuo na taasisi za elimu zinazomilikiwa na kuoendeshwa na Kanisa Katoliki hawana budi kuwa ni watu: wenye sifa, ujuzi na maarifa; watu wenye utajiri wa tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu, kwani vijana wanatamani kuona ushuhuda wa maisha ya walezi wao. Walimu waendelezwe katika taaluma ili waweze kuchangia kwa hali ya juu kuhusu weledi, imani na fadhila za maisha ya kiroho zilizoko ndani mwao! Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna haja kwa Kanisa kufanya upembuzi yakinifu kuhusu mchango unaotolewa na vyuo vikuu pamoja na taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki sehemu mbalimbali za dunia, kama kielelezo cha uhai wa Injili katika sayansi na tamaduni za watu. Vyuo na Taasisi hizi zioneshe ukomavu na ujasiri wa kushindana na wadau wengine katika sekta ya elumu kwa kujenga utamaduni wa majadiliano pamoja na kutambua kwamba, wao wanamchango mkubwa wanaoweza kuwashirikisha pia walimwengu.

Chuo Kikuu cha Kikatoliki la Ruaha kilianzishwa Mwaka 2005
Chuo Kikuu cha Kikatoliki la Ruaha kilianzishwa Mwaka 2005

Hivi karibuni, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha (RUCU) kimeadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake huku kikijivunia kukua na kuongeza idadi ya vitivo kutoka viwili hadi kufikia vitivyo 6. Hayo yameelezwa na Makamu Mkuu wa chuo hicho Padri Profesa Pius Mgeni wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya chuo hicho yaliyofanyika kwenye viwanja vya chuo hicho na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje Mkoa wa Iringa. Padri Mgeni amesema kuwa miaka 20 ya uwepo wa RUCU ni alama ya kukomaa na kuimarika katika huduma wanazotoa na hilo linadhihirishwa na idadi kubwa ya wahitimu ambao wamepita katika mikono yao ambao baadhi yao wamehudhuria maadhimisho hayo. "Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha kilianzishwa mwaka 2005 kama Chuo kikuu kishiriki cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania (SAUT) kilichopo Jijini Mwanza, wakati huo kilijulikana kwa jina la Ruaha University College (RUCO) kikiwa na programu mbili katika vitivo viwili vya sheria na Tehama pamoja na kozi fupi za kompyuta. Mnamo tarehe 29 Septemba 2014, baada ya kukidhi matakwa ya mamlaka inayosimamia vyuo vikuu Tanzania (TCU) chuo kilipandishwa hadhi na kuwa chuo kikukuu kamili kwa jina la Ruaha Catholic University (RUCU” ameeleza.

Mchango wa Kanisa Katika Sekta ya Elimu ni Mkubwa sana
Mchango wa Kanisa Katika Sekta ya Elimu ni Mkubwa sana

Aidha amebainisha kuwa katika kipindi hicho cha miaka 20 chuo kimekuwa na maendeleo makubwa katika nyanja za taaluma, utafiti, huduma kwa jamii na kuongeza programu za taaluma kutoka mbili zilizokuwepo wakati chuo kinaanza mwaka 2005 hadi kufikia programu 24 ambazo zimepelekea ongezeko la idadi ya wanafunzi na wafanyakazi, pamoja na miundombinu ya kufundishia na kujifunzia kama vile madarasa, maabara, maktaba na mabweni. "Leo hii tunajivunia kuwa na vitivo sita vyenye jumla ya wanafunzi 5,800 wafanyakazi 244 wakiwemo wanataaluma 159, wafanyakazi wa utawala 85" amesema. Aidha Padri Mgeni ametoa shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hasa akikumbuka mchango wa Hayati Benjamin Mkapa kwa kutambua mchango wa sekta binafsi, mchango wa Kanisa Katoliki katika utoaji wa elimu ya Juu Tanzania. "Kwa namna ya pekee tunatambua na kuthamini mchango wa mkubwa wa Rais wa awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Benjamini Mkapa. Mwenyezi Mungu ampe Raha ya Milele. Alihakikisha chuo hiki kinazaliwa kwa manufaa ya Watanzania wote, pia shukrani ziende kwa viongozi walionitangulia katika nafasi ya Makamu Mkuu wa Chuo, wakiwemo Hayati Padri Dkt. Cephas Mgimwa ambaye alikuwa Makamu Mkuu wa Chuo wa kwanza na Hayati Prof. Fulgence Mbunda, walioweka misingi imara ya maendeleo ya chuo chetu" ameeleza.

Askofu Ngalalekumtwa amechangia sana ustawi wa Chuo Kikuu cha RUCU
Askofu Ngalalekumtwa amechangia sana ustawi wa Chuo Kikuu cha RUCU

Akiongea kwenye maadhimisho hayo Askofu wa Jimbo Katoliki Iringa Mhashamu Romanus Mihali amesema kuwa kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) anamshukuru kwa dhati Askofu Mstaafu wa Jimbo la Iringa Mhashamu Askofu Tarcisius J.M. Ngalalekumtwa aliyesimamia hatua kwa hatua uanzishwaji wa chuo hicho. "Ni furaha kwake na kwetu kuona tunaadhimisha miaka 20 ya chuo ndani ya mwaka wa kustaafu kwake tena katika mwaka Mtakatifu wa Jubilei Kuu ya miaka 2025 ya Ukristo Duniani, hakika Mzee wetu anastahili maua yake" amesema Askofu Mihali. Pia Askofu Mihali amesema kwamba mafanikio ya chuo yasingeweza kufikiwa bila michango ya wadau wengine ambao wamekuwa sehemu ya maendeleo ya chuo hususan Serikali ambayo imekuwa ikiwashika mkono kwa namna moja au nyingine na kushirikiana nao kuhakikisha chuo kinapiga hatua. "Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., linapenda kutoa shukrani zake za dhati kwa Serkali yetu pamoja na wadau wengine ambao wamesaidia katika ukamilifu wa mradi wa “Jengo la Science Park.” Waswahili wanasema kushukuru ni kuomba tena, pamoja na kukamilika kwa jengo la kituo cha afya bado tuna uhitaji mkubwa wa vifaa tiba ili kituo kianze kutoa huduma kwa wanafunzi na wanajamii kwa ujumla" ameongeza.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango, amekipongeza chuo hicho kwa maadhimisho ya miaka hiyo pamoja na utoaji wa elimu bora kwa Watanzania. "Serikali inatumbua mchango na kuthamini sana jitihada za Kanisa Katoliki na madhehebu mengine ya dini katika kutoa huduma za jamii mbalimbali hasa sekta ya elimu ili kuwawezesha Watanzania kupata nafasi ya kusoma na kupata maarifa. Nipende pia kumpongeza Mhashamu Baba Askofu Ngalalekumtwa kuwa sehemu ya waasisi wa chuo hicho kwa kazi nzuri ambayo ameifanya" ameeleza. Maadhimisho hayo yamehudhuriwa pia na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Mbeya Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, mapadri, watawa wa kike na kiume, wanafunzi na wafanyakazi wa chuo hicho pamoja na watu wenye mapenzi mema. Maadhimisho hayo yalitanguliwa na maandamano kutoka Kanisa la Parokia ya Bikira Maria Consolata, Mshindo pamoja na maonesho ya kitaaluma kutoka vitivo mbalimbali vya Chuo hicho.

Chuo Kikuu RUCU
20 Mei 2025, 14:00