Asia/Bahraini:Askofu Mkuu Berardi:Papa Leo XIV,ishara ya matumaini na umoja
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mwakilishi wa Kitume wa Ghuba ya Falme za Arabia Kaskazini, Askofu Mkuu Aldo Berardi, O.SS.T., alibainisha kwamba: “Kwa Kanisa katika Ghuba ya Arabia, wakati huu unaleta faraja mpya tunapoendelea kuishi na kutoa ushuhuda wa Injili, mara nyingi kwa njia za kimya au siri. Alisema hayo mara baada ya kusikia habari za kuchaguliwa kwa Papa Leo XIV kwenye kiti cha upapa tarehe 8 Mei 2025. Mwakilishi wa kitume huyo alisisitiza kuwa: “Katikati ya uhalisia wetu wa kipekee, kuchaguliwa kwa Baba Mtakatifu ni ishara ya matumaini na ushirika, ambayo inaimarisha umoja wetu na Kanisa la kiulimwengu. Wito wake wa amani, mazungumzo na kukutana unasikika kwa undani mioyoni mwetu, hasa katika eneo hili, ambalo maadili haya hayatakiwi tu, lakini ni muhimu.
Tunaungana na Baba Mtakatifu katika utume wake wa kujenga madaraja, kukuza upatanisho, kuitisha mazungumzo na kutangaza Injili hadi miisho ya dunia. Tunathibitisha kujitolea kwetu kuwa ishara hai ya ushirika, kuchangia utume wa Kanisa kwa ulimwengu wote kutoka kwa Vicariate yetu katikati ya Ghuba ya Arabia. “Kwa kuchaguliwa kwa Papa Leo XIV, tunathibitisha tendo la upole na lenye nguvu la Roho Mtakatifu, ambaye anaendelea kuliongoza Kanisa katika nyakati za kufanywa upya na utume. Wakati huu kwa hakika ni neema kuu kwa Watu wa Mungu, kutukumbusha kwamba Kristo hudumu daima mwaminifu kwa ahadi yake, kwa sababu alisema: “Mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari”(Mt 28:20). Mama Yetu wa Uarabuni, Nyota ya Uinjilishaji Mpya, amwombee, kwa ajili ya Kanisa na kwa watu wote wa Mungu,” alimalizia Mwakilishi wa Kitume.
Ikumbukwe kuwa Askofu Mkuu Aldo Berardi, wa Shirika la Utatu Mtakatifu sana,( O.SS.T) aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 28 Januari 2023 kuwa Mwakilishi wa Kitume wa Arabia ya Kaskasini na Kuwait na kusimikwa kuwa Askofu tarehe 18 Machi 2023.