AMECEA,ACWECA maandalizi ya kazi ya Hati ya mwisho ya Sinodi imeanza!
Na Dalphina Rubyema - TEC - Dar Es Salaam na Saraha Pelaji- Vatican.
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika Mashariki (AMECEA) kwa kushirikiana na Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Afrika (ACWECA) wameanza kuifanyia kazi Hati ya Mwisho ya Sinodi, kwa kuandaa warsha ya mafunzo ili kuandaa timu ya wawezeshaji ya Ukanda wa AMECEA, ambao watatakiwa kushusha elimu na uelewa juu ya hati hiyo, katika ngazi mbalimbali kwenye nchi zao. Mafunzo hayo ya siku tano kuanzia tarehe 21 hadi 23 Mei 2025 yalifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), lililopo jijini Dar Es Salaaam, ambapo ufunguzi wake ulihudhuriwa na Makatibu Wakuu wa AMECEA, Padre Anthony Makunde na Sr. Bridgita Samba, wa ACWECA, ambao pia waliungana na mwenyeji wao, Padri Chesco Msaga, C.PP.S, Naibu Katibu Mkuu wa TEC.
Naibu Katibu Mkuu wa TEC, Padre Msaga
Katika Neno lake la ukaribisho, Padre Msaga aliwataka washiriki wa mafunzo hayo ambao ni pamoja na maparoko (wajumbe wa sinodi), wawakilishi wa walei, waratibu wa Sinodi katika nchi za AMECEA na ACWECA, kuwa makini katika mafunzo hayo kwa kuzingatia kazi iliyopo mbele yao, ambapo watatakiwa kusambaza elimu watakayoipata, kwa kuunda timu za wawezeshaji katika ngazi mbalimbali kwenye nchi zao. “Ndiyo maana nyie mnaandaliwa kuwa Wawezeshaji wa (TOTs),” alisema.
Hata hivyo Padre Msaga aliwataka kuzitumia Jumuiya Ndogondogo za Kikristo kuwa chombo cha kusambaza ujumbe wa Hati ya Mwisho ya Kisinodi, inayohimiza ushirika, ushiriki na umisionari, huku akiitaja Tanzania kuwa imesonga mbele kwani hadi mwezi Novemba 2024 ilikuwa na Jumuiya ndogondogo zipatano 84,664. “Ndani ya jumuiya ndiko kuliko mizizi ya Kanisa na chimbuko la miito mbalimbali. Sisi tunajivunia kuwa Kanisa la Tanzania linaendelea kukua kwa kasi kubwa mchango mkubwa ukitoka kwenye Jumuiya ndogondogo (JNNK) ambapo hadi Novemba 2024, tulikuwa na jumla ya jumuiya 84,664 na jumla ya parokia 1,440,” alisema Padre Msaga. Zaidi alisema Kanisa la Tanzania limeendelea kukua na kupata neema zaidi kwani hadi sasa lina jumla ya Majimbo 36, maaskofu 50, kati yao maaskofu 10 ni wastaafu na 40 katika utume wa kichungaji.
Katibu Mkuu wa AMECEA, Padre Makunde
Akifungua warsha hiyo, Katibu Mkuu wa AMECEA, Padre Anthony Makunde, alitaka ushiriki hai kutoka kwa washiriki hao, huku kila mmoja akitambua kuwa, ushiriki wake ni utambulisho kwamba anakwenda kuwa balozi, mwalimu na mtangazaji wa matunda ya Sinodi ambayo mchakato wake umeanza tangu mwaka 2021. “Hapa tunatengeza timu ya wawezeshaji watakaosaidia kueneza na kusambaza ujumbe mkuu wa Sinodi katika nchi zenu,” aliwambia washiriki hao.
Katibu Mkuu wa ACWECA, Sr Samba
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa ACWECA, Sr. Bridgita Samba aliwataka washiriki kutambua kuwa, katika mafunzo yao, watapitia kwa pamoja Hati ya Mwisho ya Sinodi inayotoa wito wa kuishi Kisinodi (Final Document of the Synod on Synodality), ambayo uchambuzi wake umefanyika kwa kina kwa kuhusisha mawazo na maoni kutoka ngazi mbalimbali ndani ya Kanisa Mahalia na baadaye kujumuishwa kwenye ngazi ya Bara na hatimaye maoni yote kujumuishwa pamoja na kupata Hati ya Mwisho ya Sinodi katika ngazi ya Kanisa la Kiulimwengu.
“Hati hii sasa ipo mikononi mwetu na ni hati halali iliyoidhinishwa na Kanisa, hivyo tunatakiwa kuipitia na kuangalia kwa pamoja juu ya mbinu tutakazotumia ili kuhakikisha inashushwa katika nchi zetu katika ngazi mbalimbali wakiwemo watu wanaoshi pembezoni,” alisema.
Sinodi ni alama iliyoachwa na Baba Mtakatifu Fransisko
Hata hivyo Katibu Mkuu huyo wa ACWECA alisema huwezi kutaja Sinodi bila kulitaja jina la Baba Mtakatifu Fransisko aliyeaga dunia mnamo tarehe 21 Aprili 2025, kwani wakati wa uhai wake amekuwa akihimiza Kanisa kutembea Kisinodi, kwa pamoja bila kumwacha mwamini yoyote nyuma. “Daima amekuwa akihimiza Kanisa kutafuta njia sahihi ya kuunganisha waamini wote kuanzia ngazi ya Jumuiya ndogondogo, vigango, parokia, jimbo, taifa hadi ngazi ya ulimwengu. Hati hii ni Moyo wa Sinodi, hivyo njia ya pekee ya kumuenzi, ni kuyaishi kwa vitendo yale aliyokuwa akiyahimiza hususani Kanisa kutembea pamoja kwa kuunganisha makundi yote,” alisema na kuongeza: “Hayati Baba Mtakatifu Fransisko amekuwa ni mvuvi mkuu kuhakikisha Kanisa linatembea Kisinodi.”
Kwa mujibu wa Mratibu wa Warsha hiyo, Bwana Bernard Mberere kutoka AMECEA, naye alibainisha kuwa Warsha hiyo “imelenga kuwajengea uwezo viongozi wa Kanisa mahalia kwa kuwapa mbinu za Kitaalimungu na Kichungaji, ili hatimaye waweze kupeleka katika majimbo yao elimu hiyo kwa kuwezesha timu za uwezeshaji watakaosambaza elimu katika ngazi mbalimbali ndani ya Kanisa, hivyo kuwezesha nchi husika kutembea Kisinodi.”
Padre Makunde katika kufafanua 'uelewa wa Kisinodi'
Katika mada iliyohusu ''Uelewa wa Kisinodi: Misingi ya Kitaalimungu na Kanisa la Kisinodi'' iliyotolewa na Padre Anthony Makunde, ambaye kwa kurejea machapisho mbalimbali ya Kisinodi, alisema Mafundisho ya Kanisa juu ya Sinodi, ni mwaliko wa kwenda pamoja na kwamba Sinodi ya Maaskofu ilianzishwa na Mtakatifu Paulo wa VI mwaka 1965 na kwamba katika Kanisa la Mashariki, Sinodi ni Chombo kinachotunga Sheria kwa Kanisa la Magharibi, Sinodi ya Maaskofu ni chombo cha ushauri kwa Kanisa. Kwa kufafanua zaidi alisema, kuwa safari ya Sinodi ya Maaskofu inayotoa mwaliko wa Ushirika, Ushiriki na Umisionari, ilianza tangu mwaka 2021 na utekelezaji wake umepitia awamu nne ukianza nza awamu ya mashauriano (consultative Phase 2021-2022), kufuatia awamu ya utekelezaji katika ngazi ya Ukanda (Continental Phase 2022-2023), ikifatiwa na Kikao cha kwanza cha Sinodi (The 1st Synod Session –October 2023) na Kikao cha Pili cha Sinodi (The 2nd Synod Session- October 2024.”
Padre Makunde kwa kuoneza alisema: Hati ya Mwisho ya Sinodi juu ya kutembea pamoja, ni mkusanyiko wa matunda ya safari ya kukusanya maoni na mapendekezo kutoka ngazi mbalimbali za Kanisa na ina Sura tano ambapo hata hivyo alisisitiza kuwa msingi wa Kanisa ni Ubatizo tena wa maji kwa kuzingatia taratibu zote za Ubatizo wa Kanisa Katoliki. Mambo mengine yanayosisitizwa ni kuzingatia kwa kila wito ndani ya Kanisa unaanzia kwenye familia na msisitizo unawekwa zaidi kwenye Jumuiya Ndogondogo za Kikristo (JNNK) ambazo zinatumika kama mfano hai wa kuishi maisha ya Kisinodi. “Lakini pia msisitizo unawekwa kwenye kuheshimu misingi ya usimamizi wa raslimali fedha za Kanisa ambapo unahitaji uwazi, uwajibikaji huku ikihimizwa pia Sinodi ngazi za majimbo na kuhimiza ushiriki wa waamini walei katika uongozi wa Kanisa,” alisema.
AMECEA
Ikumbukwe kwamba Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika Mashariki (AMECEA) linaundwa na nchi: Tanzania, Kenya, Uganda, Malawi, Ethiopia, Zambia, Sudan, Eritrea na nchi Watazamaji ambao ni Somalia na Djibouti.