Mkesha wa Pasaka 2025: Mama wa Mikesha Yote ya Kanisa
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni kilele cha siku kuu tatu za Pasaka ambazo tulianza kuadhimisha tangu siku ya Alhamisi kuu, siku ya Ijumaa kuu, na leo tunafikia katika kilele cha siku hizi kuu za pasaka. Baada ya kuadhimisha mateso na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo, leo katika usiku huu mtakatifu, tunaadhimisha ufufuko wake kutoka wafu kama alivyosema. Tunamshangilia, “Kristo Mfufuka, Tumaini la Ufufuko wetu” Ufufuko wa Bwana wetu Yesu ni msingi wa Imani yetu, kama anavyotuambia mtume Paulo, “Kama Kristo asingalifufuka basi imani yenu ni bure” (1 Kor 15:14). Tunamshangilia Kristo aliyetoka mzima kaburi, usiku ambapo Kristo alikata minyororo ya mauti akatoka kuzimu ameshinda (Mbiu ya Pasaka). Ufufuko wa Kristo Yesu ni kilele cha ukweli wa imani ya Kikristo, ambayo jamii ya kwanza ya wakristo iliusadiki na kuuishi kama kiini cha ukweli; waliiendeleza kama msingi kwa njia ya Mapokeo; waliithibitisha kwa njia ya Maandiko ya Agano Jipya; na wakaihubiri kama sehemu muhimu sana ya Fumbo la Pasaka yaani: mateso na kifo cha Kristo Msalabani. Kristo amefufuka kwa wafu, kwa kifo chake alishinda dhambi na mauti na amewakirimia wafu uzima wa milele. Kaburi tupu na vitambaa vilivyolala ni ushuhuda wa Kristo Mfufuka. Kristo Yesu wa kwanza katika wafu ni msingi wa ufufuko wetu, tangu sasa kwa kufanywa haki roho yetu na baadaye kwa kuhuishwa miili yetu. Rej. KKK 638-658. Tunashangilia utimilifu wa ahadi ya Mungu, ahadi ya kuwaletea taifa lake ukombozi wa milele kwa njia ya sadaka ya mwanaye mpenzi Bwana wetu Yesu Kristo, baada ya anguko la wazazi wetu wa kwanza Adamu na Eva. Nasi tunashiriki mateso kifo na ufufuko wa Kristo kwa njia ya ubatizo wetu. tunapokea zawadi kubwa ya ukombozi kutoka katika utumwa wa dhambi na kuanza safari ya mpya ya maisha ndani ya Kristo mfufuka.
Herini nyote kwa sherehe ya Pasaka. Kesha la Pasaka, Mama wa Mikesha Yote ya Kanisa: Siku ya Jumamosi kuu huanza katika ukimya, ni siku Yesu aliyokuwa amelala kaburini. Lakini mambo huanza kubadilika jioni, tunapoingia katika Vijilia hii ya Pasaka. Katika giza, siku inayotangulia ufufuko wa Bwana yaani Jumamosi usiku, Wakristo wanakusanyika katika mkesha, ni vijilia ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, Mama wa vijilia zote. Mtakatifu Agustino aliita Vijilia hii ya Pasaka kuwa “Mama wa vijilia zote” kwa sababu katika usiku huu, kanisa lipo macho kusubiria ufufuko wa Kristo Bwana wetu. Tunatafakari kwa kina historia nzima ya ukombozi wetu, tangu kuumbwa kwa ulimwengu hadi siku hii Takatifu ambapo Kristo anafufuka kutoka wafu, siku ya tatu baada ya mateso na kifo chake. Tunakutanika kusubiria na kushangilia utimilifu wa ahadi ya Yesu kwamba siku ya tatu atafufuka (Mt. 16:21-23; Mk 8:31; Lk 9:21-22). Ni kweli alifufuka kama alivyosema nasi tumekusanyika kushangilia ufufuko wake, ushindi wake dhidi ya kifo na mauti na tunda la ukombozi uliotokana mateso, kifo na ufufuko wake. Tunaposhangilia ufufuko wa Kristo, tunashangilia upya wa maisha si tu kwa Kristo, bali kwetu sisi sote tunaomwamini. Mpango wa Liturujia katika Mkesha wa Sherehe ya Pasaka. Mkesha wa Pasaka unaadhimishwa tofauti kabisa na maadhimisho mengine ya Liturjia. Mkesha huu kwa namna ya pekee umegawanyika katika sehemu kuu nne nazo ni; Liturujia ya Mwanga, Liturujia ya Neno, Liturujia ya Ubatizo na Liturujia ya Ekaristi Takatifu. Katika mkesha huu, siku hii takatifu, ningependa tutafakari kwa kina maana ya adhimisho hili katika maisha yetu ya kila siku. Pasaka ina maana gani katika maisha yetu sisi tunaoiadhimisha kila mwaka na kwa namna ya pekee katika kila adhimisho la Ibada ya misa takatifu? Mgawanyiko wa sehemu hizi nne utatusaidia kuelewa vyema ni nini maana ya Pasaka, adhimisho hili kubwa katika Imani yetu ambalo tunaliadhimisha katika usiku huu Mtakatifu.
Sehemu ya kwanza: Liturujia ya Mwanga/ Mwanzo wa Adhimisho. Mshumaa wa Pasaka: Katika giza mwanzoni kabisa mwa adhimisho la Mkesha huu wa Pasaka, huanza Liturujia ya Mwanga, ambapo Mshumaa wa Pasaka huwashwa. Mshumaa huu ni ishara ya ushindi wa Kristo, ni Mshumaa wa Pasaka, mwanga kwa Kristo uondoao giza la usiku huu, lililo ishara ya dhambi na mauti. Mwanga wa Kristo unakaribishwa katika Kanisa lililo katika giza, na kila mmoja anaalikwa kuwasha mshumaa wake kutoka katika Mshumaa wa Pasaka. Mishumaa yetu inayowaka: Hii ni ishara kwamba kwa dhambi sisi sote tulikua gizani na kwa ufufuko wa Kristo, sisi sote tunatoka katika giza la dhambi na mauti kwa kuupata mwanga wetu kutoka kwa Kristo. Ni kwa njia ya ubatizo sisi sote tunakabidhiwa mwanga huu wa Kristo ili tupate kuulinda na kamwe tusitembee gizani tena, na kwa mwanga huo tuweze mwisho wa maisha yetu kumlaki Bwana. Kwa kuandamana tukiwa tumebeba mishumaa yetu inayowaka, tukiongozwa na mshumaa wa Pasaka nasi, ishara ya mwanga wa Kristo mfufuka, ni mfano wa safari yetu ya maisha mapya, Kristo akiwa mbele yetu, anawasha mwanga wake ndani ya mioyo yetu, anafukuza giza la dhambi, nasi tunatembea katika mwanga huo kueleka Yerusalemu yetu mpya, yaani mbinguni.
Mbiu ya Pasaka: Tukiwa na mishumaa yetu, tukiongozwa na mwanga wa Kristo tunaingia kanisani na kisha huimbwa Mbiu ya Pasaka (Exsultet). Huu ni Wimbo wa Kristo Mfufuka. Wimbo huu watangaza namna dhambi na kosa la Adamu lilivyopeleka ahadi ya Mungu ya kumleta kwetu mkombozi Mkubwa namna hii, yaani Bwana wetu Yesu Kristo. Waeleza utimilifu wa maandiko juu ya ujio wa Masiya, Bwana wetu Yesu Kristo, Njia, ukweli na uzima (Yn 14:6). Inapoimbwa mbiu nasi sote tunamshukuru Mungu kwamba, sasa tumefanywa kuwa huru, usiku ambapo Kristo alikata minyororo ya mauti akatoka kuzimu ameshinda. Kisha hufuata Liturjia ya Neno. Sehemu ya pili: Liturujia ya Neno: Katika Masomo yote ya sherehe hii, kanisa halichoki kutueleza maana ya usiku huu kwamba ni kutoka katika hali ya upotevu na kuingia katika hali ya uzima wa kimungu. Masomo haya yatueleza kwa mpangilio tangu uumbaji, anguko la wazazi wetu wa kwanza, mpango wa Mungu wa kumkomboa tena mwanadamu aliyeanguka na utimilifu wake katika Kristo Bwana wetu. Tunamwona Mungu ambaye kwa mapendo makubwa anamwumba mtu, na kwa mapendo anamkomboa mwanadamu. Somo la Kwanza: (Mwanzo 1:1-2:2). Simulizi la somo hili laelezea Habari nzima ya uumbaji wa Mwanadamu hapo mwanzo. Somo hili latupa picha juu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu: yaani, Baba Mwana na Roho Mtakatifu zadhihirika katika uumbaji, na hivyo hivyo katika safari nzima ya ukombozi wa mwanadamu. Kumbe kazi ya uumbaji ni kazi ya utatu mtakatifu, na kazi ya ukombozi hali kadhalika. Pia latueleza namna Mungu mwema alivyoumba kila kitu chema na kizuri na kilele cha uumbaji huu ni uumbaji wa Mwanadamu, aliye sura na mfano wa Mungu mwenyewe (Mwanzo 1:26). Pasaka yatukumbusha juu ya thamani kubwa ya mwanadamu mbele ya Mwenyezi Mungu kati ya viumbe vingine vyote. Tutunze sura na mfano huu wa Mungu ulio ndani yetu kwa kutamani kuishi daima maisha matakatifu.
Somo la Pili: (Mwanzo 22:1-18): Baada ya anguko la wazazi wetu wa kwanza, uhusiano katika ya Mungu na mwanadamu unaanza kurudishwa tena. Ni Mungu anayeanzisha upya tena historia ya Ukombozi wa Mwanadamu kwa njia maagano mbalimbali, na kisha Agano jipya na la milele kati yake na sisi taifa lake jipya kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ibrahimu anaamriwa kumtoa mwanaye Isaka kama sadaka, ishara ya uaminifu na imani kubwa ya Ibrahimu kwa Agano aliloweka na Mungu. Ni Sadaka ya Ibrahimu ya mwanaye wa Pekee ambaye kwa njia yake ahadi za Mungu alizonena na Ibrahimu zingetimia. Ni mfano wa sadaka ya Kristo ambaye kwa njia yake Mwenyezi Mungu ametimiza kwetu ahadi yake ya ukombozi. Mungu kwa mapendo, anaendelea kudhirisha mpango wake wa ukombozi kwa taifa lake. Somo la tatu: (Kut 14:15-15:1): Somo hili laeleza namna Mungu anavyoendelea kuthibitisha Agano kati yake na watu wake. Taifa la Israeli walikua katika utumwa wa Wamisri kwa muda mrefu. Kwa sababu ya mapendo makubwa kwa watu wake, Mungu anawakumbuka, anamtuma Musa na kwa njia yake anaanzisha safari ya ukombozi kwa watu wake kutoka katika utumwa na mateso kule Misri. Mungu wetu ni Mungu anayeona na kuguswa na shida na maumivu na mahangaiko ya watu wake. Safari hii ya taifa la Israeli inaambatana na matendo makubwa ya Mungu, wanavuka katika bahari ya shamu, na wamisri wanaangamizwa katika kina cha bahari. Kuvuka bahari ya shamu ni ishara ya ubatizo, ambao kwa njia ya maji sisi sote tunavushwa kutoka katika utumwa na kuingia katika uhuru kamili. Mungu anatupenda, anatukumbuka katika mateso yetu, anafanya kitu kwa ajili yetu.
Somo la nne: (Isa 54:5-14): Mwenyezi Mungu ananena na watu wake kwa kinywa cha Manabii. Licha ya taifa lake mara kwa mara kushindwa kuwa waaminifu kwa Agano ambalo alifanya nao, bado Mungu hawaachi. Bado anaendelea kuwapenda na anatamani bado kudumisha ule uhusiano na uaminifu kwa Agano lake kwa kuwa aliahidi kuwa Mungu wao na taifa la Israeli kuwa watu wake, taifa lake teule. Uhusiano huu unafumbatwa katika mahusiano kati ya mume na mke. Vile kama mume na mkewe wanavyopaswa kuwa waaminifu ndiyo yalivyopaswa kuwa mahusiano kati ya Mungu na watu wake. Walipokosa uaminifu, Mwenyezi Mungu aliwapeleka utumwani ili kuwafundisha. Walipokiri na kutambua Makosa yao Mungu, anaahidi kuwakusanya tena watu wake na kuwarehemu tena. Ahadi ya Masiya yatajwa sana katika kitabu cha Nabii Isaya, ndiye Bwana wetu Yesu Kristo. Somo la tano: (Isa 55:1-11): Mwenyezi Mungu anawaalika wale wote wanaotamani uhusiano mwema naye kusahau mambo ya kale, mambo yaliyopita, maisha ya dhambi na kumtafuta Bwana. Mwenyezi Mungu ananena na wale wote walio na hofu na mashaka, njooni! Tumsikilize na kupata daima yale yaliyo mema. Ndio mwaliko wa Kristo mfufuka kwetu sisi sote, anayetualika kuanza maisha mapya, anayefanya yote kuwa mapya kabisa. Pasaka yatukumbusha kuwa, ya kale yamepita, Yesu amefanya yote kuwa mapya kabisa.
Somo la sita: Bar 3:9-15, 32-4:4: Hekima ni zawadi inayotokana na uhusiano mwema kati yetu sisi na Mungu. Inatusaidia pia kuwa na uhusiano mwema na wa karibu zaidi na Mungu. Hekima ni kufahamu yale yote ambayo Mungu ametenda, na ataendelea kutenda kwa ajili yetu sisi taifa lake, watu aliowachagua kuwa urithi wake. Ni katika kutafakari historia ya ukombozi wetu tunaweza kufahamu ni mambo makubwa namna gani Mungu amefanya kwa mapendo makubwa kwetu, na hivyo kutambua wajibu wetu wa kumpa yeye peke yake utukufu kwa kuenenda daima katika maisha ya nuru ndani ya Kristo mfufuka. Somo la saba: Eze 36:16-28: Mwenyezi Mungu anawakumbusha wale wote ambao Mungu aliwachagua na kufanya nao Agano yaani taifa lake teule, kwamba ingawa wamekosa uaminifu, yeye ataendelea kuwahurumia na kuwapenda na kuwa mwamifu kwa Agano alilofanya nao. Mwenyezi Mungu atapyaisha tena Agano alilofanya nao kwa kuwa Mungu ni Mungu anayehusiana na watu wake (Relational God). Atatoa moyo wa jiwe ulio ndani yao naye atawapa moyo wa nyama, atatia roho yake ndani yao na kuwaendesha katika njia yake. Tumepokea Roho huyu ambaye amefanya ndani mwetu uumbaji mpya kwa njia ya ubatizo wetu. Tumepewa moyo mpya na roho mpya kwa njia ya kushiriki mateso, kifo na ufufukowa Kristo katika ubatizo wetu. Baada ya kusikia masomo yote saba ya Agano lake pamoja na sala, tunaimba utukufu kwa Mungu juu mbinguni. Kengele zote zinagongwa, taa zote zinawashwa, maua na mapambo yote ya kanisa sasa yanaonekana wazi. Ni nini maana ya kuimba Utukufu? Utukufu iliyoimbwa juu mbinguni wakati wa kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo, ikiashiria ujio wa Mwanga mkubwa ulimwenguni, masiya na Mkombozi wetu, sasa inaimbwa tena tukishangilia utimilifu wa kazi ya ukombozi kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake. Baada ya utukufu husomwa somo la kwanza katika Agano jipya, somo la waraka. Baada ya somo la Waraka tunaimba Shangilio. Katika shangilio tunamshukuru Mungu kwa kuwa fadhili zake ni za milele. Amedhihirisha hilo katika historia ya ukombozi wa taifa lake, tangu uumbaji hata ukombozi.
Somo la Injili ya Luka 24:1-12: Katika somo la Injili, Mwinjili Luka anaelezea tukio la ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo kutoka wafu likithibishwa na karibu lililo wazi (An empty Tomb). Maria Magdalena na wanawake wengine walikwenda kaburini mapema asubuhi siku ya kwanza ya Juma. Hii ilikua ni siku ya tatu baada ya mateso na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo. Walipofika kaburini wanastaajabu kwa kuwa jiwe lililofunika kaburi la Yesu lilikua limeviringishwa mbali na kaburi. Na hapo wanapewa Habari na Malaika ya kwamba, “Kwa nini mnamtafuta liye hai, hayupo, hapa, amekwisha fufuka” Wanawake ambao hawakua na nafasi katika jamii ya wahahudi wanakuwa mashuhuda wa kwanza wa ufufuko wa Kristo. Yesu alikuja ili kuwainua wale walioonewa, walioonekana hawana thamani. Ndio sababu Injili ya Luka hujuliakana pia kama Injili ya wanawake, kwa kuwa anaonesha nafasi na ushiriki wa wanawake katika maisha na utume wa Yesu. Kumbe ufufuko wa Kristo sio habari ya kutungwa bali ni kweli alifufuka, yu hai, ni mzima, hafi tena. Wakina mama hawa wanafanya kazi kubwa ya kwenda kuwa wamisionari wa kwanza wa ufufuko wa Kristo kwa Mitume wa Yesu. Sisi sote ambapo leo hii tunashuhudia ufufuko wa Kristo tunaalikwa kuwa mashuhuda wa ufufuko wake kwa ushuda wetu wa maisha, kwa maneno na kwa Matendo yetu mema. Kwa kuishi vyema ubatizo wetu na viapo vyetu mbalimbali, tunakuwa mashuhuda wa ufufuko wa Kristo. Kwa kupenda na kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine tunakusa mashuhuda wa ufufuko wa Kristo. Kwa kuishi vyema Imani yetu, kwa kuvumilia katika mateso na magumu na kubeba misalaba yetu kwa uaminifu mpaka mwisho, tunakuwa mashuhuda wa ufufuko wa Kristo. Je, ninapotafakari historia ya ukombozi wetu, ninaona kila mara namna Mungu anavyodhihirisha mpango wake ndani ya maisha yangu? “How do I align my self with the plan of God?” Jinsi gani ninakubali Mpango wa Mungu utimie katika maisha yangu, mpango unaohusisha maumivu, uchungu, hofu, mashaka, mkato wa tamaa, uvumilivu na ustahimilivu na zaidi ya yote upendo usio na miapaka? Tumwombe Mungu daima ili mapenzi yake yatimizwe katika maisha yetu.
Somo la Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi 6:3-11: Mtume Paulo anatupa matokeo ya Fumbo kuu la Pasaka, ambalo kila mmoja tunashirikishwa kwa njia ya ubatizo wetu. Anatufundisha ni nini maana ya kuunganika na Kristo. Tumebatizwa katika mauti ya Kristo, kusudi kama vile Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo nasi sote tuishi katika upya wa uzima. Pasaka inatukumbusha kuwa na sisi pia tulikufa kwa sababu ya dhambi na tunaishi tena pamoja na Kristo. Katika vijilia hii, kanisa linajipatia watoto wapya, wakatekumeni ambao kwa kipindi kirefu walikua wakijiandaa kwa ajili ya ubatizo wao.
Sehemu ya Tatu: Liturujia ya Ubatizo: Baada ya Liturujia ya Neno, hufuata sasa Liturujia ya Ubatizo. Ubatizo wetu ni tunda la ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo kwa kuwa ni kwa njia hiyo sisi sote tunashiriki katika Fumbo la Pasaka, tunakufa na kufufuka pamoja na Kristo kama anavyotufundisha Mtume Paulo. Sehemu hii huanza kwa kubarikiwa maji ya ubatizo na kuwakaribisha wale wanaobatizwa katika jumuiya ya waamini. Maji yana nafasi ya pekee sana katika historia ya ukombozi wetu. Kuanzia wakati wa uumbaji (Mwa 1:1), maji katika gharika ya Nuhu (Mwa 7:12), maji katika Bahari ya Sham (Kut 14:15-15:1), na maji katika mto Yordani (Josh 3:6). Maji yamekuwa ni ishara ya mabadiliko kutoka kifo kwenda katika uzima. Mshumaa wa pasaka unatumbukizwa katika kisima chenye maji ya ubatizo na roho mtakatifu anavuviwa katika maji tukimwomba Kristo mfufuka maji yale yalete uzima mpya kwa wale watakaobatizwa humo. Nasi sote tunapata nafasi ya kukiri tena Imani yetu kwa Kristo Mfufuka kwa kurudia ahadi zetu za ubatizo. Ufufuko wa Kristo ukitumbusha kila mara juu ya ubatizo wetu. Tunakiri nia yetu ya kutorudi tena katika maisha ya kale, maisha ya dhambi na kuahidi kuendelea kuishi katika upya wa maisha. Kanisa hivyo katika usiku huu mtakatifu linajpatia Watoto wapya wanaobatizwa, wakishiriki nao katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Tunaalikwa kuwaombea ili waendelee kuwa imara na kukua katika imani, matumaini na mapendo.
Sehemu ya Nne: Liturujia ya Ekaristi Takatifu. Sehemu ya mwisho katika adhimisho la Mkesha wa Pasaka, Mama wa mikesha yote ni Liturujia ya Ekaristi Takatifu. Ekaristi takatifu ni sadaka ya shukrani kwa Mungu (Eucharistein) kwa zawadi ya ukombozi wetu uliofumbatwa katika Fumbo la Msalaba wa Kristo. Nasi kila tunapoadhimisha sadaka hii ya Kristo tunatoa shukrani kwa Mungu na kukumbuka ukarimu huu mkubwa wa Yesu kutoa uhai wake kwa ajili ya uzima wetu. Pasaka yatukumbusha daima kuwa watu wa shukrani kwa Mungu kwa zawadi hii kubwa ya ukombozi lakini pia kwa neema na baraka zake nyingi anazotujalia katika maisha yetu. Pia tunaposherekea ukarimu huu wa Kimungu nasi tunalikwa kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine. Kukubal kuvunjwa vunjwa, ili kuleta furaha kwa wengine, kukubali kupondwapondwa ili kuleta divai tamu na safi kwa ajil ya furaha kwa watu wote. Kristo alijiota mwili wake kuwa chakula chetu na damu yake kuwa kinywaji chetu nasi tuna uzima wa milele. Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu inatuunganisha na kutuleta pamoja katika ushirika (Communion). Tunapoadhimisha Ekaristi Takaifu, tunaingia katika ushirika na Kristo kwa kuwa tunakutanika pamoja kuadhimisha mauti yake mpaka ajapo, kama alivyowaamuru mitume kufanya kila wakutanapo. Kumbe nasi katika adhimisho hili la Ekaristi Takatifu tunaingia katika ushirika na Kristo. Yupo nasi katika Neno lake, kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu yupo nasi daima katika maumbo ya mkate na divai. Tunapompokea Kristo anakaa ndani mwetu nasi tunakaa ndani mwake, anatupa uzima wa Roho zetu. Hitimisho. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya ukombozi. Tunamshukuru Yesu Kristo kwa kukubali kutimizia mapenzi ya Baba ya kutuletea sisi sote ukombozi wa milele. Tumwombe Kristo atupe nguvu na ujasiri wa kuishi daima maisha ya kipasaka, kwa kumpenda Kristo kama alivyotupenda sisi na kutoa uhai wake kwa ajili yetu, na kupenda sisi kwa sisi tukitimiza amri ya Kristo aliyowaachia wanafunzi wake na ametuachia sisi sote.